UMUHIMU WA KUJIFUNZA KUISHI NA WATU VIZURI

Ndugu msomaji karibu katika siku nyingine ambayo tunajifunza somo zuri sana ambalo litatusaidia kufika sehemu fulani katika maisha.

Lengo la somo hili ni kukuonesha umuhimu wa kujifunza kuishi na watu vizuri. Kujua umuhimu wa kuishi na watu kwa namna inavyotakiwa, itakujengea ufahamu utakaokuonesha ulazima wa kutafuta hekima za kuishi vizuri na watu.

Zifuatazo ni sababu za kujifunza kuishi na watu vizuri.

 

1.      Watu wana vitu (vinavyoshikika) ambavyo wewe hauna.

Na kumbuka kwenye maisha kuna vitu vingi sana unavihitaji ili ufike mbali. Na vitu hivyo wanavyo watu, kwahiyo, ili uvipate kwa watu lazima ujifunze kuishi nao.

Hakuna mtu atakupa kitu chake kama hauoni thamani yake, kama haujali utu wake, kama haujali hisia zake na maeneo mengine kuhusu maisha yake. Mtu akiona utu wako kwake, ni rahisi kutoa kitu chake ambacho kitakusaidia wewe maishani mwako.

 

2.     Watu wanatumiwa na Mungu kama daraja

Ni muhimu sana kujua kuwa Mungu anafanya kazi na watu. Kwahiyo, ukijifunza kuishi vizuri na watu, inamrahisishia Mungu kuwatumia watu kama daraja ili wewe ufike unapotakiwa kufika.

Kuna mahali hauwezi kufika bila watu, hata kama unajihisi una kila kitu na unajua vingi, utahitaji madaraja ili uvuke. Kuna watu Mungu alishawafanya kuwa daraja kwa ajili yako, ukijua kuishi nao vizuri utafika.

Mahali fulani, Yesu anawaambia watu kuwa alikuja kwa walio wake na walio wake hawakumpokea. Maana yake walishindwa kuishi naye vizuri na kumbe yeye ndiye daraja la kuwafikisha kwenye wokovu.

Kuna watu unawachukulia poa, lakini ni daraja la Mungu kukufikisha mahali.


3.     Watu wana ufahamu (mtazamo) unaoweza kukusaidia

Siku moja Mkwe wake Musa alikuja, akamkuta Musa anachoka kwa sababu ya majukumu aliyonayo, ikamlazimu kumpa ufahamu fulani wa kugawa majukumu na kuwapa watu nafasi ili yeye abaki kwenye mambo fulani makubwa.

Mwisho wa siku, Musa akafanyia kazi na akapata msaada kutoka kwenye changamoto ambazo hazikuwa na ulazima. Kuna watu wana mawazo yanayoweza kukuinua na kukufanikisha kutoka hapo ulipo.

Kuna watu wanajua usichokijua. Ukijifunza kuishi nao vizuri, itakusaidia kupata wanachofahamu ili ufanikiwe maishani.

Usijaribu kuwa mjuaji, wewe haujui kila kitu, hata kama una mawazo mengi, bado kuna watu wana mawazo ya kukusaidia kufika unapotakiwa kufika.

 

4.     Watu ni rasilimali

Watu ni rasilimali muhimu sana maishani. Kila taifa chini ya jua linathamini sana rasilimali watu. Kila taifa linajua kuwa watu ni nguvukazi muhimu ya kusaidia kufanikisha mambo mengi kwenye taifa.

Kuna vitu unataka kufanya maishani. Hautaweza kufanya mwenyewe, unahitaji kufanya kazi na watu.

Hauwezi kufanya kila kitu peke yako maishani. Unahitaji msaada wa watu, unahitaji kufanya kazi na watu. Unaweza kuanzisha mradi fulani au taasisi fulani ukidhani kuwa utafanya mwenyewe lakini mbeleni utajikuta unahitaji watu.

Kadri unavyoendelea utagundua kuwa unahitaji watu zaidi ili ufike mbali zaidi kwenye kile unachokifanya. Kuna msemo unaosema kuwa “ukitaka kufika haraka, tembea mwenyewe, ukitaka kufika mbali tembea na watu”. Wewe unataka kufika mbali au unataka kufika haraka? Kumbuka harakaharaka haina baraka.

 

5.     Watu ni soko

Kila bidhaa inayozalishwa duniani soko lake ni watu. Kama hakuna watu hakuna soko. Kama haujajifunza kujali na kuishi na watu vizuri, utashindwa kutoa kilicho bora na utashindwa kupata wateja wa bidhaa yako.

Hata kama una kitu kizuri kiasi gani, hata kama una bidhaa kubwa na zinazohitajika kiasi gani, kama haujajifunza kuishi na watu na namna ya kuwahudumia watu katika namna ifaayo lazima watakukimbia.

Unapotaka soko lako lipanuke, walenge watu, yaani watu ndiyo kitu muhimu unachohitaji ili kufika mbali.

Ndugu msomaji, natumaini kupitia mambo haya matano, yamekujengea msingi unaokuonesha ulazima wa kuishi na watu vizuri. Wakati mwingine tutajifunza kanuzi au namna ya kuishi vizuri na watu. Mungu akubariki uwe na wakati mwema, tukutane tena wikiendi ijayo.

Comments