Ndugu msomaji katika wikiendi iliyopita tulijifunza umuhimu wa kuishi vizuri na watu, na ninaamini ulijifunza mambo mengi sana ya kukusaidia. Unapoianza wikiendi hii tutajifunza kanuni 5 za kuishi na watu vizuri.
Ni muhimu kujua
kuwa kwenye maisha hauwezi kuishi bila kanuni. Maisha yanaendeshwa na kanuni. Utakapojifunza
kuishi kwenye kanuni, utayaweza maisha. Kuna kanuni za kuishi na watu na
ufaidike nao.
Hii ni muhimu sana kujua
hili, hasa kwa mtu mwenye maono. Kumbuka tunapojifunza kuishi na watu ni kwa
sababu tuna maono ambayo tunajua hayawezi kwenda bila kuwa na watu.
Ukiwa na maono ni
lazima ujue kuwa unahitaji watu, katika wikiendi iliyopita tulijifunza kuwa
watu wana vitu ambavyo huna, wao ni daraja, wanatumiwa na Mungu na kadhalika.
Karibu tujifunze,
Kanuni
#1. Amini Watu Uliopewa Na Mungu
Mungu akikupa watu
waamini hata kama unaona hawafai. Mungu alimpa Yesu kina Petro watu ambao
hawana kesho kumkana ili kutetea uhai wao, lakini ndiyo watu hao hao ambao kwao
kanisa la watu elfu tatu lilianza.
Hata kama unaona
hawana kile unachowaza unakihitaji, hao ni watu muhimu sana ambao wengine
wanawatafuta. Waamini utafika mbali.
Sikiliza mawazo
yao, kwa sababu kama amekuletea anaweza kupitishia mawazo kwao ili na wao
waendelee kuwa sehemu ya mfumo, ukiamini kuwa wewe ndiyo kila kitu kwenye
mfumo, hautafika mahali popote.
Wape watu nafasi ya
kuongea kile wanachowaza ili kuboresha mambo mbalimbali. Thamini mawazo yao
sana, mawazo ni kitu muhimu sana katika kutimiza maono.
Watu wakiwa wengi
kuna mawazo mengi, na kwa maana hiyo kuna njia nyingi za kufanya maono yawe
halisi, ukiwapa nafasi, maono yatakuwa halisi na utawahudumia wengi kupitia
maono yako.
Kanuni
#2. Jifunze Kuchukuliana Na Watu
Ukiwa na maono
utafanya kazi na watu mbalimbali. Na wewe kama mtu ambaye umeanzisha mfumo (maono) unahitaji sana kuchukuliana na watu.
Ni kweli kuwa
unataka kuona matokeo na haraka, lakini jambo linalohusisha watu halihitaji
haraka uliyonayo.
Unahitaji kuwa
mtulivu wa akili. Hata kama unaona hawaendi vile unavyotaka, nenda nao
taratibu, hapo unajenga msingi, wakishapata mwendo, utawapenda na hutataka
waondoke katika huo mfumo. Ni suala la muda, wape muda na utaona makali yao.
Kuna watu huwa wana
tabia mbalimbali, lakini ndio ambao umepewa kufanya nao kazi, acha kulalamika
sana, wafundishe taratibu na uende nao pamoja usiwaache nyuma.
Ukiwaacha nyuma,
watapotelea vichakani.
Kanuni
#3. Wajali Watu
Lazima uwajali watu
kwa namna yoyote ile. Watu wawe ndiyo kipaumbele chako. Hata kama itagharimu
muda wako, fedha yako na akili yako.
Watu ndiyo kitu
muhimu kwenye mfumo. Usipowajali, unakusudia kuuharibu mfumo wako.
Jali hisia zao,
wape kazi kulingana na uwezo wao, na ukiona wanachoka sana wasaidie kwa sehemu.
Onesha kuwa wao
ndiyo kipaumbele chako. Siyo tu unajali maono mliyonayo. Unawajali wao zaidi ya
kawaida, mambo yao jitahidi unahusika nayo. Hata kama hauna uwezo katika kila
kitu lakini unaweza kutia moyo, kutoa ushauri, na vingine unavyoweza kuwafanyia
ambavyo vitaonesha kabisa unawajali.
Na namna nyingine
za kujali nyingi unaweza kujifunza hasa mawasiliano na kadhalika.
Kanuni
#4. Wafanye Kuwa Bora Zaidi Ya Walivyokuja
Watu wengi
wanashindwa kwenda na watu kwenye maono yao kwa sababu hawataki kuwafanya watu
kuwa bora zaidi ya walivyokuja.
Watu wengi
wanaoanzisha maono wanapenda kuwatumia watu kutimiza maono yao. Hapo hautapa
hata mtu wa kufanya kazi na wewe, wote watakukimbia.
Kama kuna maarifa
unayo ambayo unadhani hawana jenga tabia ya kukutana nao na kuwashirikisha hayo
maarifa.
Kama unajua kuwa
watu huwa wana vitu mbalimbali, unaweza kuomba kukutana nao na kuwapa nafasi ya
kuongea au kutoa maarifa katika eneo husika.
Wape kazi ambazo
zinaenda kuamsha nia ya kujifunza na kutaka kuwa bora zaidi. Wape majukumu
ambayo si ya wa kuwatumia kwa faida, bali wao kujinoa zaidi.
Hakikisha kwako
wanakuwa bora zaidi ya walivyowahi kuwa. Itawafanya kukuamini na kukaa katika hayo
maono. Kumbuka unatakiwa kukaa na watu kwenye maono, lakini watu wanaokaa
wanatakiwa kuwa bora.
Wafanye kuwa bora
hata wakiondoka wanaweza kukuletea watu kwa sababu wanajua wewe una nia ya
kuwafanya watu kuwa bora zaidi kupitia maono ambayo umepewa kuyaanzisha.
Kwa gharama yoyote hakikisha
unawafanya kuwa bora zaidi. Watu hawatafuti watu wa kuwatumia kwa faida zao,
wanahitaji watu wa kuwasaidia kuwa bora zaidi ya walivyo sasa, ukiamua kuwa
huyo mtu utaenda nao pamoja na usiogope kama ukiwafanya kuwa bora wataondoka,
bado wapo watu ambao watakuja tena kwako.
Kanuni
#5. Hakikisha Wanatimiza Maono Yao Kupitia Maono Yako
Kwa sababu maono
yako yanakuwa mfumo maana yake unawasaidia hao watu watimize maono yao katika
maono yako.
Utawasaidia
kutimiza na utawafundisha namna ya kuweka maono yao kimkakati ili kufanya yawe
halisi.
Wawezeshe kuwa na
maono na tengeneza mazingira katika mfumo kwa ajili ya wao kuishi maono yao.
Na wewe uwe sehemu
ya kuhakikisha maono yao yanatimia.
Mfumo sasa unakuwa
wenye maana kwa sababu kila mmoja anamtegemea mwingine ili kutimiza maono yake,
na hii itajenga uimara mkubwa sana.
Kama itafika mahali
kila mtu anamtegemea mwenzake ili maono yake yatimie, kila mtu atamhesabu
mwenzake kuwa bora, na hivyo kuheshimiana, na hapo itakusaidia kulinda mfumo
dhidi ya mpasuko na migongano ambayo haina ulazima na ni hatarishi.
Nasisitiza tena
hakikisha mfumo unaotengeneza kwa ajili ya maono yako, unakuwa ni mfumo wa wao
kutimiza maono yao.
Kama ukiweza
kuyafanyia kazi mambo hayo matano ninakuhakikishia kupata matokeo mazuri.
Unaweza pia kupata maarifa mengine kutoka kwa wengine ambao na wao wana hii
mifumo, jifunze kwao.
Ndugu msomaji,
ninaamini kuwa umejifunza mambo muhimu na hakika yatakuwa msaada kwenye maisha
yako. Uwe na wikiendi njema, nakukaribisha tena wikiendi ijayo, wewe ni mtu wa
thamani. Mungu akubariki sana.
Barikiwa kwa somo zuri
ReplyDelete