KANUNI 5 ZA KUISHI VIZURI NA WATU ILI UFANIKIWE

Ndugu msomaji katika wikiendi iliyopita tulijifunza umuhimu wa kuishi vizuri na watu, na ninaamini ulijifunza mambo mengi sana ya kukusaidia. Unapoianza wikiendi hii tutajifunza kanuni 5 za kuishi na watu vizuri.

Ni muhimu kujua kuwa kwenye maisha hauwezi kuishi bila kanuni. Maisha yanaendeshwa na kanuni. Utakapojifunza kuishi kwenye kanuni, utayaweza maisha. Kuna kanuni za kuishi na watu na ufaidike nao.

Hii ni muhimu sana kujua hili, hasa kwa mtu mwenye maono. Kumbuka tunapojifunza kuishi na watu ni kwa sababu tuna maono ambayo tunajua hayawezi kwenda bila kuwa na watu.

Ukiwa na maono ni lazima ujue kuwa unahitaji watu, katika wikiendi iliyopita tulijifunza kuwa watu wana vitu ambavyo huna, wao ni daraja, wanatumiwa na Mungu na kadhalika.

Karibu tujifunze,

 

Kanuni #1. Amini Watu Uliopewa Na Mungu

Mungu akikupa watu waamini hata kama unaona hawafai. Mungu alimpa Yesu kina Petro watu ambao hawana kesho kumkana ili kutetea uhai wao, lakini ndiyo watu hao hao ambao kwao kanisa la watu elfu tatu lilianza.

Hata kama unaona hawana kile unachowaza unakihitaji, hao ni watu muhimu sana ambao wengine wanawatafuta. Waamini utafika mbali.

Sikiliza mawazo yao, kwa sababu kama amekuletea anaweza kupitishia mawazo kwao ili na wao waendelee kuwa sehemu ya mfumo, ukiamini kuwa wewe ndiyo kila kitu kwenye mfumo, hautafika mahali popote.

Wape watu nafasi ya kuongea kile wanachowaza ili kuboresha mambo mbalimbali. Thamini mawazo yao sana, mawazo ni kitu muhimu sana katika kutimiza maono.

Watu wakiwa wengi kuna mawazo mengi, na kwa maana hiyo kuna njia nyingi za kufanya maono yawe halisi, ukiwapa nafasi, maono yatakuwa halisi na utawahudumia wengi kupitia maono yako.

 

Kanuni #2. Jifunze Kuchukuliana Na Watu

Ukiwa na maono utafanya kazi na watu mbalimbali. Na wewe kama mtu ambaye umeanzisha mfumo (maono) unahitaji sana kuchukuliana na watu.

Ni kweli kuwa unataka kuona matokeo na haraka, lakini jambo linalohusisha watu halihitaji haraka uliyonayo.

Unahitaji kuwa mtulivu wa akili. Hata kama unaona hawaendi vile unavyotaka, nenda nao taratibu, hapo unajenga msingi, wakishapata mwendo, utawapenda na hutataka waondoke katika huo mfumo. Ni suala la muda, wape muda na utaona makali yao.

Kuna watu huwa wana tabia mbalimbali, lakini ndio ambao umepewa kufanya nao kazi, acha kulalamika sana, wafundishe taratibu na uende nao pamoja usiwaache nyuma.

Ukiwaacha nyuma, watapotelea vichakani.

 

Kanuni #3. Wajali Watu

Lazima uwajali watu kwa namna yoyote ile. Watu wawe ndiyo kipaumbele chako. Hata kama itagharimu muda wako, fedha yako na akili yako.

Watu ndiyo kitu muhimu kwenye mfumo. Usipowajali, unakusudia kuuharibu mfumo wako.

Jali hisia zao, wape kazi kulingana na uwezo wao, na ukiona wanachoka sana wasaidie kwa sehemu.

Onesha kuwa wao ndiyo kipaumbele chako. Siyo tu unajali maono mliyonayo. Unawajali wao zaidi ya kawaida, mambo yao jitahidi unahusika nayo. Hata kama hauna uwezo katika kila kitu lakini unaweza kutia moyo, kutoa ushauri, na vingine unavyoweza kuwafanyia ambavyo vitaonesha kabisa unawajali.

Na namna nyingine za kujali nyingi unaweza kujifunza hasa mawasiliano na kadhalika.

 

Kanuni #4. Wafanye Kuwa Bora Zaidi Ya Walivyokuja

Watu wengi wanashindwa kwenda na watu kwenye maono yao kwa sababu hawataki kuwafanya watu kuwa bora zaidi ya walivyokuja.

Watu wengi wanaoanzisha maono wanapenda kuwatumia watu kutimiza maono yao. Hapo hautapa hata mtu wa kufanya kazi na wewe, wote watakukimbia.

Kama kuna maarifa unayo ambayo unadhani hawana jenga tabia ya kukutana nao na kuwashirikisha hayo maarifa.

Kama unajua kuwa watu huwa wana vitu mbalimbali, unaweza kuomba kukutana nao na kuwapa nafasi ya kuongea au kutoa maarifa katika eneo husika.

Wape kazi ambazo zinaenda kuamsha nia ya kujifunza na kutaka kuwa bora zaidi. Wape majukumu ambayo si ya wa kuwatumia kwa faida, bali wao kujinoa zaidi.

Hakikisha kwako wanakuwa bora zaidi ya walivyowahi kuwa. Itawafanya kukuamini na kukaa katika hayo maono. Kumbuka unatakiwa kukaa na watu kwenye maono, lakini watu wanaokaa wanatakiwa kuwa bora.

Wafanye kuwa bora hata wakiondoka wanaweza kukuletea watu kwa sababu wanajua wewe una nia ya kuwafanya watu kuwa bora zaidi kupitia maono ambayo umepewa kuyaanzisha.

Kwa gharama yoyote hakikisha unawafanya kuwa bora zaidi. Watu hawatafuti watu wa kuwatumia kwa faida zao, wanahitaji watu wa kuwasaidia kuwa bora zaidi ya walivyo sasa, ukiamua kuwa huyo mtu utaenda nao pamoja na usiogope kama ukiwafanya kuwa bora wataondoka, bado wapo watu ambao watakuja tena kwako.

 

Kanuni #5. Hakikisha Wanatimiza Maono Yao Kupitia Maono Yako

Kwa sababu maono yako yanakuwa mfumo maana yake unawasaidia hao watu watimize maono yao katika maono yako.

Utawasaidia kutimiza na utawafundisha namna ya kuweka maono yao kimkakati ili kufanya yawe halisi.

Wawezeshe kuwa na maono na tengeneza mazingira katika mfumo kwa ajili ya wao kuishi maono yao.

Na wewe uwe sehemu ya kuhakikisha maono yao yanatimia.

Mfumo sasa unakuwa wenye maana kwa sababu kila mmoja anamtegemea mwingine ili kutimiza maono yake, na hii itajenga uimara mkubwa sana.

Kama itafika mahali kila mtu anamtegemea mwenzake ili maono yake yatimie, kila mtu atamhesabu mwenzake kuwa bora, na hivyo kuheshimiana, na hapo itakusaidia kulinda mfumo dhidi ya mpasuko na migongano ambayo haina ulazima na ni hatarishi.

Nasisitiza tena hakikisha mfumo unaotengeneza kwa ajili ya maono yako, unakuwa ni mfumo wa wao kutimiza maono yao.

Kama ukiweza kuyafanyia kazi mambo hayo matano ninakuhakikishia kupata matokeo mazuri. Unaweza pia kupata maarifa mengine kutoka kwa wengine ambao na wao wana hii mifumo, jifunze kwao.

Ndugu msomaji, ninaamini kuwa umejifunza mambo muhimu na hakika yatakuwa msaada kwenye maisha yako. Uwe na wikiendi njema, nakukaribisha tena wikiendi ijayo, wewe ni mtu wa thamani. Mungu akubariki sana.

 

Comments

Post a Comment

Thanks for your comment, God bless you!!!