Ndugu msomaji, hongera kuvuka mwaka 2024 na kuingia 2025. Ninamshukuru Mungu kwa ajili yako. Ametuwezesha wote kuingia mwaka huu mwingine kwa ajili ya kusudi lake maalumu.
Mungu
kuturuhusu kuingia mwaka 2025 ni uhakika kuwa ametuamini, anaona tunaweza
kuleta faida kwa wengine kwenye huu mwaka, anaona tunaweza kuwasaidia wengine
kuwa bora zaidi ya pale walipo, tunaweza kuliishi kusudi na kufanikiwa katika
mwaka huu.
Mungu
ametupa mwaka, maana yake kuna neema ametoa ya kutembea katika haya majira
mapya, ili kutuwezesha kufika. Hatahivyo, kuaminiwa na Mungu kunadai
kuwajibika, na Mungu anahitaji kuona matokeo, na inategemea mtu aliyeaminiwa.
Kuna
mambo ya kuzingatia kwa kila mtu aliyeaminiwa na Mungu ambayo yatamuwezesha
kufanikiwa kwenye huu mwaka, na kumsaidia kutimiza mapenzi ya Mungu kwa majira
haya.
Karibu
tujifunze,
#1. Kaa Kwenye Uwepo wa Mungu
Hili ni
jambo la kwanza kabisa la kuzingatia. Amua kukaa kwenye uwepo wa Mungu. Ni
jambo lisiloepukika, huwezi kufanikiwa bila Mungu, yeye ndiye kila kitu, kama
amekuamini maana yake anataka kukusaidia bila kujali madhaifu uliyonayo.
Ni,
ukweli kuwa tuna maeneo mengi sana ambayo inawezekana yakawa sababu ya
kutofanikiwa mwaka huu, na kwa uwezo wetu inakuwa ngumu kushughulika nayo,
inamhitaji sana Mungu.
Sasa,
Mungu hatafutwi wakati wa uhitaji peke yake, Mungu anatakiwa kutafutwa maisha
yote, na kumtafuta Mungu ni kukaa katika uwepo wa Mungu. Amua kukaa pale. Kuna
faida nyingi sana.
Uwepo wa Mungu unakupa ulinzi wa kiungu
katika mali na afya yako, na tunajua kabisa kuwa hakuna mafanikio
bila usalama na afya nzuri. Ukitaka kuyashinda magonjwa, hatua ya kwanza ni
uwepo wa Mungu. Mimi ni ushuhuda unaoishi, nina miaka mingi siumwi, ni kwa
sababu tu ya uwepo wa Mungu kwenye maisha yangu. Nakutia moyo kuwa afya yako
itakuwa njema moja kwa moja unapokaa kwenye uwepo wa Mungu.
Uwepo wa Mungu unampa Mungu nafasi kwenye
kukuongoza, na tunajua kuwa bila kuongozwa katika njia
sahihi, tunaweza kupita katika njia yoyote na mwisho wa siku tukaishia
kuangukia pua na tusifanikiwe, wengi wanaoamua kuwa wajuaji, huwa hawafiki
mbali. Kwenye maisha kuna njia nyingi sana ambazo unaweza kupita, lakini Mungu
anazo njia sahihi za wewe kupita. Ukikaa na yeye utapita katika njia,
alizoandaa kwa ajili yako ambazo hautapotea hata kama haufahamu sana.
Uwepo wa Mungu unaleta ufunuo wa kiungu, kadri
mtu anavyokaa katika uwepo wa Mungu, kuna aina ya ufahamu anaupata utokao kwa
Mungu, kuna siri anaanza kuzikamata na kuishi nazo, ambazo humfanya moja kwa
moja awe mbele ya wengine na mbele ya muda. Na kwenye maisha hauwezi kufanikiwa
kama hauko mbele ya muda. Pia, maisha tunayoyaishi ni matokeo ya ufahamu tulionao.
Unahitaji sana uwepo wa Mungu.
Uwepo wa Mungu humfanya Mungu aingilie kati
katika vita zako, maisha ni vita na kila mtu anapigana ya kwake,
Mungu amekuamini, haimaanishi kuwa hautakutana na vita, tena inawezekana vita
zikawa kubwa kuliko 2024. Unahitaji sana msaada wa Mungu. Vita nyingi ukipigana
wewe, utaishia kupoteza nguvu, fedha na rasilimali nyingine ambazo zilipaswa
kutumika kukusaidia kufanikiwa kwenye mwaka. Ukikaa kwenye uwepo wa Mungu, kuna
hasara unaziepuka. Kuna vita, lakini uwepo wa Mungu unampa Mungu nafasi ya
kupigana kwa niaba yetu, na mwisho wa siku tunafanikiwa.
Uwepo wa Mungu unazalisha ujasiri ndani
yetu, kadri tunavyozidi kukaa kwenye uwepo wa Mungu, ndivyo ambavyo
ujasiri wetu unaongezeka, uimara wetu unaongezeka, hivyo tunakuwa na uwezo wa
kuziendea harakati mbalimbali za maisha kwa ujasiri, na kushinda bila kujali
vipingamizi vilivyopo. Ukikaa kwenye uwepo wa Mungu, kuna ujasiri wa kiungu,
Mungu hajatupa roho ya woga, bali ya nguvu. Uhodari utakuwa sehemu ya maisha
yako kwa kukaa kwenye uwepo wa Mungu.
Unakaa
kwenye uwepo wa Mungu kwa maombi na mifungo isiyokoma; weka ratiba walau kila
siku uwe na muda wa kuonekana mbele za Mungu kwa maombi, pia uwe na siku
zinazoeleweka za mifungo katika wiki. Jenga tabia ya kujifunza Neno, imarisha
ushirika wako na Roho Mtakatifu, azimia kuwa mtu wa ibada na uhakikishe kuwa
ukienda ibadani hautoki bure. Kama haujaokoka azimia kuokoka, kama umeokoka
lakini haujawa siriazi na Mungu, acha dhambi, amua kuwa siriazi, bila hivyo
hautoboi. Mwaka huu azimia kukaa kwenye uwepo wa Mungu kama unataka kutoboa.
#2. Kuwa Mtu Wa Mipango (Malengo) Na Tathmini
Hauwezi
kufanikiwa bila mipango. Usipopanga chochote utafanya chochote. Kumbuka wewe
haujaruhusiwa kuja huu mwaka ili kufanya kila kitu, au kuwa mtu wa kila kitu.
Kuna kitu maalumu unachopaswa kufanya na si vinginevyo. Kukosa mipango
kutakufanya uwe mtu anayeishi kiholela, hautafika mahali.
Kama
unaishi kiholela bila mipango, hautafika popote, hautakuwa yeyote. Kumbuka muda
haujawahi kukusubiri, unapaswa kuwa na hekima ya kupangilia maisha yako,
uliyopewa ndani ya mwaka mmoja yawe na maana. Weka mipango.
Watu
wengi wanasema wana mipango, lakini hawaiandiki. Huku ni kujidanganya, na Mungu
hawezi kufanya kazi na watu wa aina hii, tafuta watu wote kwenye maandiko, kila
aliyeaminiwa na Mungu alikuwa mtu wa mipango, na Mungu mwenyewe kuna mipango
aliwapa.
Hakikisha
unapata muda, wa kukaa na Mungu, akusaidie kujua maeneo ambayo anahitaji wewe
uwekeze kwa mwaka huu, maeneo ambayo anawaza ufanikiwe, anawaza ufanye vitu vya
maana, omba msaada wa Roho Mtakatifu, kaa chini weka malengo na mikakati.
Andika
malengo yako. Usijifariji kwa kuyawaza tu, yaandike, na ikiwezekana mpe mlezi
wako, au baba yakow a kiroho, au mtu unayemuamini ambaye atakusaidia kukuwajibisha
katika malengo yako. Acha kuweka malengo ambayo unajidanganya, weka malengo
yanayofikika, acha kujiwekea malengo ambayo hautafanya chochote, na hakikisha
unapoweka malengo yako, unakuwa na Roho Mtakatifu karibu, ili akusaidie maana
hatuweki malengo kwa vile tulivyo nje, bali kwa vile Roho Mtakatifu anatusaidia
kutokea kwenye uwezo wetu wa ndani.
Malengo yatatupa nidhamu ya muda, ukiweka
malengo utagundua kuwa una muda mchache sana wa kufanya mambo yako. Ukiuona
mwisho wako, na kujua kuwa una siku 366 au 365 tu, utagundua hauna tena muda wa
kupoteza. Utajikuta unaacha vitu visivyo vya lazima, kama wewe ni mtu wa
malengo tena yanayoandikwa, utajikuta vitu fulani unalazimika kuacha maana
unagundua kuwa havikuongezei chochote kwenye kutimiza malengo yako bali
vinapoteza muda wako.
Malengo yanatuonesha wapi pa kuongeza nguvu,
mtu
akiweka malengo, atagundua kuwa kuna maeneo mengi sana ambayo anahitaji
kuyashughulikia maana ni ukweli kuwa hatafika mahali. Hii itamsaidia mtu
kushughulika na udhaifu wake wote. Kuna madhaifu yanaendelea kukaa kwenye
maisha yetu kwa sababu hatuna malengo na tunaishi kiholela tu. Kuna vitu
hautashughulika navyo mpaka uwe na malengo. Kuna dhambi hautashughulika nazo
mpaka uwe na malengo, na ukiangalia malengo hayo yanadai utakatifu.
Malengo yanatuonesha vipaumbele, kadri
unavyoyaangalia malengo na kukaza kuyashika, utagundua kuna vitu vinahitaji
muda wako mwingi, vingine mchache, vingine wastani na kadhalika. Ukiona una
shida ya vipaumbele, ujua haujakaza katika eneo la malengo. Kumbuka kama
hatufanyi vitu kwa vipaumbele hatuwezi kufanikiwa hata kidogo, kila mtu
asiyejua vipaumbele, hajawahi kufika mahali, anaweza kubaki alipo na mwisho
wake kupotea kabisa. Ukiwa hujui nini cha kufanya na kwa muda gani, na nini cha
muhimu, nini kianze na kipi kifuate, tiba yake ni malengo. Weka malengo, utaona
mambo yenye uzito zaidi.
Malengo yanaonesha nafasi ya Mungu kwetu, kila
anayeweka malengo, akiyatazama kwa makini, atagundua kuwa ana mzigo mkubwa wa
kubeba ambao unaamua mafanikio yake, na anaona mzigo huo anahitaji msaada
kabisa, na msaada wa kwanza ni Mungu. Kadri unavyozidi kuwa mtu wa malengo,
unaona namna ambavyo unamhitaji Mungu zaidi katika maisha yako. Ukiona hauoni
na hauhitaji zaidi msaada wa Mungu, ni kwa sababu hauna tabia ya kuishi kwa
malengo tena yaliyoandikwa.
Malengo yanatuonesha watu wa kwenda nao
katika kipindi husika, unakwenda na kila mtu ni kwa sababu hauna
malengo. Mara utakapoweka malengo, utaona kuna watu ni kweli unawapenda, lakini
haupaswi kwenda nao, la sivyo hautafika unapotakiwa kufika kwa mwaka huu.
Utagundua kuwa unahitaji aina fulani ya watu, na watu fulani uachane naye. Weka
malengo, utaaanza kuona ni kina nani wa kufanya nao kazi.
Kaa
chini, andika, pangilia. Weka malengo yako ya mwaka huu, usikubali kuishi
kiholela.
Vilevile,
unapaswa kuwa mtu wa tathmini. Ukiweka mipango, unaanza kuichukulia hatua,
unapofika kila baada ya kipindi fulani hasa miezi 3, unapaswa kufanya tathmini
ya namna unavyotekeleza malengo yako. Ukifanya hivi, na ukawa mwaminifu, utaona
maeneo unayofanya vizuri, maeneo ambayo haufanyi vyema, na maeneo ambayo
unahitaji marekebisho ili ufanikiwe. Tathmini hutupa nidhamu na ubunifu. Kila
baada ya miezi mitatu, kaa chini, pitia malengo yako, angalia ulivyoyatekeleza,
andika kwenye daftari lako la mwaka, andika changamoto kwa kipindi hicho,
andika maazimio kwa ajili ya robo inayofauata, na uwe mtu wa tabia hiyo kila
wakati. Lazima utafanikiwa.
#3. Jiunganishe Na Watu Sahihi
Kwenye
haya maisha hauhitaji kwenda na kila mtu hata kama unampenda au kuona ni mzuri
sana. Unahitaji kwenda na watu sahihi. Unahitaji kwenda na watu ambao mtafika
wote salama.
Kuna
watu unawahitaji ambao hao ukienda nao tu lazima ufanikiwe. Kuna watu ukienda
nao lazima ufeli tu hata kama una moto kiasi gani. Hata kama una mipango mizuri
kiasi gani, kama hauna watu sahihi wa kwenda nao, hautafika mahali popote.
Watu sahihi wanatupa joto njiani, kwenye
mchakato wa kufanikiwa katika mwaka huu, kuna mambo mengi sana ambayo utakutana
nayo, ambayo utajikuta unahisi kama uko peke yako, au unahisi baridi, watu
sahihi watakuwepo kukutia moyo, na kukupa joto ambalo ni muhimu kwa ajili yako
kufika safari. Ni ukweli kuwa maisha yana vipindi mbalimbali, kuna watu
unawahitaji, ambao wanaenda safari kama ya kwako, ambao mtatiana moyo na
kushikana mkono, itasaidia kurudi nyuma.
Watu sahihi wanatusaidia kushughulika na
madhaifu yetu, kuna watu ukikaa nao, madhaifu yako yatakuwa
fimbo ya kukuchapia, na usifike mahali. Lakini unapokaa na watu sahihi,
wanakusaidia kushughulika na udhaifu wako, watakupa hekima na njia sahihi za
kushughulika nao. Watavumilia udhaifu wako, watakusaidia na kuwa sehemu ya kuwezesha
wewe kutoka kwenye hali uliyonayo. Wao wanaweza kuwa wamepita hapo, au wana
hekima ya eneo hilo, ambayo itakusaidia kuvuka hapo.
Watu sahihi wanatupa mashauri sahihi, kwenye
maisha haya, unahitaji mashauri sahihi katika kuyaendea mambo mbalimbali ili
ufanikiwe. Usipokuwa na watu sahihi hautapata mashauri sahihi. Maandiko
yanasema kwa mashauri ya akili fanya vita, na wokovu huja kwa washauri wengi
(sahihi). Ukikosa hekima mbalimbali za watu, hautafika mahali. Hata Musa pamoja
na kuwa na uwezo wa kuonana na Mungu, kuongea na Mungu kama mtu aongeavyo na
rafiki yake, bado alihitaji mashauri ya Yethro mkwewe kuhusu ugawaji wa
madaraka ambayo mwisho wa siku ikamrahisishia utekelezaji wa malengo. Wewe na
mimi hatujui kila kitu, tunahitaji watu wa kutushauri katika maeneo mbalimbali.
Watu sahihi wanatuunganisha na Mungu, ukikaa
na watu sahihi, watakusaidia kumuona Mungu na kuona ubora wa Mungu na namna
ambavyo ni wa muhimu sana kwenye maisha yetu. Watu sahihi wanaijua nafasi ya
Mungu, na wanaiheshimu na hakika watakuchagiza na kukuchochea wewe kuwa karibu
na Mungu, maana hata wao wanafahamu siri ya kufanikiwa kwao, ni kuwa karibu na
Mungu.
Watu sahihi wanajitoa sana kwa ajili yetu, kuna
vitu ambavyo hauna uwezo wa kufanya, hali yako ya kifedha hairuhusu, ni kweli
kabisa, huwa inatokea, lakini Mungu anafanya kazi na watu. Ukiwa na watu
sahihi, una uhakika wa Mungu kukusaidia kupitia wao. Hawa watu huwa wanajitoa
kwenye kiwango ambacho hata wewe hauwezi kurudisha walichofanya, na si hivyo tu,
hautawaona wakiutumia msaada waliokupa kama fimbo ya kukuchapia na kukuendesha.
Hawa watu wanajitoa sana, lakini wanaheshimu, wanathamini, na kulinda utu wako.
Hata wakikusaidia, utu wako kwao ni kitu muhimu sana.
Watu
sahihi ni muhimu sana lakini ni vigumu sana kuwaona, inahitaji jicho la
utambuzi wa kiungu kuwaona. Hivyo, tafuta msaada wa Mungu wa kukuunganisha na
hawa watu sahihi, na Mungu atawaleta kwako, na utawaona, na hao watu watakuwa
baraka sana kwako. Mwaka huu azimia kuachana
na watu mbalimbali, amua kumuomba Mungu akuunganishe na watu sahihi, na
muombe MUNGU awaondoe watu wasio sahihi, na akutie nguvu ya kuachana nao.
#4. Kuwa Mtu Wa Misingi
Ni
muhimu uwe na misingi ambayo utaiishi katika mwaka huu. Uwe na mambo ambayo
utayathamini sana, na utahakikisha kuwa hauyavunji. Misingi ni misimamo yako.
Misingi yako ni maisha yako. Mtu akivunja misingi yako, ameyavunja maisha yako.
Misingi yako ni kila kitu.
Maisha yetu yanajengwa kwenye misingi yetu, Samsoni
alipoangusha nguzo (misingi) ya jengo ndivyo alivyoangusha jengo zima. Mfano,
mimi mojawapo ya msingi wangu ni UWAZI. Maisha yangu yamejengwa kwenye uwazi,
nikiacha kuwa muwazi, nimeharibu maisha yangu, ninaanguka. Ndiyo maana niko
muwazi kila siku, na ndivyo maana nashiriki na wewe siri hizi, kwa sababu uwazi
ni msingi wa maisha yangu.
Misingi inaamua tutafanya nini, msingi
ndiyo mwanzo wa kila kitu na mwongozo wa ufanyaji wa kila kitu. Jinsi
tunavyofanya mambo yetu ni matokeo ya misingi tuliyojiwekea ambayo tunaishi
katika hiyo. Kama hauna msingi katika lolote, hautafanya chochote. Na mwisho wa
siku hautakuwa chochote katika huo wakati wako wa maisha.
Misingi inaamua utambulisho wako, ukiona
mtu anaonekana ni muongo, ni kwa sababu ameweka maisha yake kwenye msingi wa
uongo. Uongo ni msingi wa maisha yake. Jinsi watu watakavyokuona, na kukuchukua
ni matokeo ya misingi yako ya maisha. Mimi niliamua kuwa na msingi wa UTU,
hivyo watu wakikutana na mimi lazima watakutana na msingi huu, watanitambua kama
mtu anayethamini utu wa mtu. Nimeamua huu uwe utambulisho wangu.
Misingi inaamua mwisho wako kwenye jambo, ukiona watu
hawadumu kwenye jambo wanalolifanya, ni kwa sababu hawana misingi ya maisha.
Mojawapo ya vitu vinavyionifanya niwe mtu wa kudumu katika mambo yangu, ni
msingi wa UAMINIFU. Nimejikuta nadumu kwenye mambo yangu, sipotei njiani, kwa
sababu nalinda uaminifu wangu. Kadri ninavyolinda uaminifu, ndivyo ninavyodumu
katika jambo husika. Ukiona mtu anatokea mbele za watu akawa na kipawa,
kikakubalika, na baadaye akapotea ghafla, uwe na uhakika hakuwa na misingi
nyuma inayomuwezesha yeye kudumu, misingi aliiyokuwa nayo, ilikuwa inamsapoti
kuanguka na kupotea.
Misingi inaamua aina ya watu wakaokaa na
sisi, kuna watu hata ufanye vipi hawatakaa na wewe kama misingi
yako haiendani sana na kile unachosimamia, hii ni kawaida kwa maisha ya
wanadamu, ndege wanaofanana huruka pamoja. Kama hauko tayari kuingalia misingi
yako, na kuiishi kikamilifu, kuna watu hawatakaa na wewe hata kama una kitu
kizuri. Kuna watu wana vitu vizuri, vya kuwafanikisha kabisa kwenye mwaka 2025,
lakini hakuna mtu anayetaka kukaa naye kwa sababu ya misingi yake mibovu. Siyo
kwamba una laana, ni kwamba misingi yako ni mibovu, na misingi ikiharibika
mwenye haki atafanya nini?
Ndugu
msomaji, sasa unaweza kujiuliza, je, wewe una misingi gani? Maisha yako
yamejengwa katika misingi gani? Mimi ambaye ninakuletea siri hizi, maisha yangu
yamejengwa katika misingi hii UTU, USAFI, UKWELI, UWAZI, UAMINIFU, MATOKEO na UFANISI.
Misingi hii, ndiyo inayonifanya, niwe radhi kushiriki na wewe mambo haya,
ambayo wengi hatuyajui, ninatamani na wewe ufike mahali fulani ambako watu
watajifunza kupitia wewe. Mwaka huu azimia kuwa mtu wa misingi.
#5. Jilishe Chakula Sahihi
Hakikisha
unakula chakula sahihi cha mwili. Usile hovyohovyo, kula chakula kwa utaratibu.
Jali afya yako ya mwili, kujali afya ya mwili, siyo lazima uwe na fedha, ni
maamuzi ya kujizatiti kula chakula bora katika hali hiyo hiyo uliyonayo. Pia,
kujali afya, wakati mwingine ni kuacha chakula, siyo lazima ule kila siku, pata
muda wa kufunga.
Pata
chakula sahihi cha akili na roho. Soma vitabu, sikiliza mafundisho. Kaa na Roho
Mtakatifu, hudhuria ibada ujifunze. Mimi kila mwaka ninasoma vitabu
visivyopungua 50, na kusikiliza mafundisho mengi lakini ambayo ni sahihi.
Unacholisha ufahamu wako kinaamua umbali
utakaoenda, Eliya alikula chakula kilichompa stamina ya
kusafiri siku arobaini. Wewe unalisha nini ufahamu wako. Hauwezi kwenda mahali
ambako ufahamu wako haujaenda, kadri ambavyo unasafiri kiufahamu, ndivyo
ambavyo unaweza kwenda kimwili. Kadri unavyopanua ufahamu wako, ndivyo
unavyojihakikisha kuwa utafika mbali. Hatufiki mbali kwa maneno, tunafika mbali
kwa kiwango tunacholisha ufahamu wetu.
Unacholisha ufahamu wako kinaamua njia gani
utatumia kufanikisha mambo, kadri unavyokuwa finyu
kiufahamu, ndivyo unavyozidi kuwa njia finyu za kufanikisha mambo yako.
Unahitaji ufahamu mpana ili kuwa na njia nyingi za kufanya mambo kwa usahihi.
Mungu mwenyewe huwa anafundisha watu ili wapate faida, na hatimaye wapite
katika njia iwapasayo kupita. Kuna njia ukipata lazima ufanikiwe, na hili ni
zao la ufahamu wako. Kuna wakati hauoni njia, siyo kwa sababu hamna njia, ni
kwa sababu ufahamu wako ni mdogo.
Unacholisha ufahamu wako kinaamua nani aje
kwako, ukiwa na ufahamu dhaifu, utakuwa ni sumaku inayovuta watu
dhaifu kama wewe. Kwa sababu ufahamu ulivyo ndivyo mtu alivyo. Kumbuka, hata
kama unatamani kuwa na watu wa aina fulani, kama hauna ufahamu kama wa kwao,
hautakaa nao meza moja. Yeyote anayetaka kufanikiwa, lazima awe na ufahamu kama
wa wale waliofanikiwa katika hilo eneo.
Unacholisha ufahamu wako kinaamua mitazamo
yako, mitazamo yako inajumuisha namna unavyoyaona mambo, kuyapokea
na kuyaitikia. Kuna vitu unaviona ni muhimu, kwa sababau tu ya ufahamu wako,
siku ufahamu wako ukibadilika, utagundua kuwa hivyo vitu siyo vya muhimu, na
haupaswi kuendelea navyo. Kumbuka pia, ukiwa na ufahamu fulani, utautetea,
utausambaza, kuulinda na kuuthamini. Sasa kama hauna ufahamu mzuri, utakuwa na
mtazamo mbaya, ambao utaulinda, utautetea, utausambaza, na kuuthamini katika
kila unalofanya. Unaweza kuona sasa maisha yako yatakuwaje.
Unacholisha ufahamu wako kinaamua Mungu
atafanya kazi na wewe kwa kiwango gani, ni kweli kuwa Mungu ana nguvu
nyingi sana lakini ufahamu wetu huwa kipimo cha yeye kufanya kazi na sisi. Kuna
vitu akiruhusu kulingana na ufahamu wetu, hatutabaki salama. Ndiyo maana Mungu
akitaka kufanya mambo kwenye maisha ya mtu, kitu muhimu cha kwanza ni kumletea
ufahamu sahihi, ambao unaweka mazingira ya yeye kufanya vitu kwenye maisha
yake. Ndiyo maana kabla Yesu hajazaliwa, alikuja malaika kuleta taarifa
(chakula) kwa mariamu, na vilevile hata kuzaliwa kwa Yohana mbatizaji. Na
mahali pengine anasema, umuite, naye ataitika, kisha atakuonesha mambo magumu,
makubwa, usiyoyajua. Kwanini akuoneshe hayo? Ni kwa sababu akili yako
ikiyashika, inamruhusu yeye kufanya kazi kwa kiwango hicho kwenye maisha yako.
Amua
kusoma vitabu, amua kulisha ufahamu wako chakula sahihi, na chakula sahihi
zaidi ni Neno la Mungu, hakikisha unaathiriwa na Neno la Mungu. Pata muda wa
kujifunza, peke yako, wewe na Roho Mtakatifu na pia na wale wenye ufahamu wa
kiungu. Soma Makala na mafundisho mbalimbali, msaidie na mwingine ajifunze.
Mwaka huu, azimia kujifunza. Azimia kupanua ufahamu wako.
#6. Shughulika Na Udhaifu Wako
Hauwezi
kufanikiwa bila kushughulika na udhaifu wako. Shughulika na udhaifu wako.
Unahitaji kujiboresha katika maeneo hayo, ili ufike mahali kwenye maisha yako.
Usiulee ubovu wako, usiizoeleee dhambi, usipuuzie ubaya unaouishi, usiufanye
kuwa sehemu ya maisha yako.
Udhaifu wako ni mlango wa adui kukupoteza, shetani
huwa anatafuta kuona mahali ambako una udhaifu ili akupoteze. Alienda kwa Hawa,
akagundua hajayashika vizuri maelekeo waliyopewa na Mungu. Mungu amesema msile,
yeye akaongeza na msiguse, na mwisho wa siku Adamu na Hawa wakaingia mkenge.
Kinachokupoteza ni udhaifu wako.
Udhaifu unakuchelewesha katika hatima yako, kadri
ambavyo unaulea udhaifu, ndivyo unavyopoteza muda wako na kujichelewesha. Hata
kama unaonekana kuwa unafaa kuwa mtu fulani, udhaifu wako unakuchelewesha
kuaminiwa kuwa mtu fulani katika eneo fulani. Hata Mungu, anataka kwanza
ashughulike na udhaifu wako ndiyo akuamini.
Udhaifu unakufanya usiaminike, kadri
watu wanvyozidi kujua kuwa una udhaifu fulani, ndivyo ambayo hauaminiki kwao.
Mfano uwe mchungaji, halafu washirika wajue kuwa wewe ni mzinzi, uwe na uhakika
kuwa kule kukuamini kwao, kutaondoka ghafla. Sauli alipoung’ang’ania udhaifu
wake, Mungu hakumuamini, akatafuta mtu mwingine. Bila kujali kuwa eneo
ulilopewa linafaa, kama una udhaifu, hautaaminika.
Udhaifu wako ndiyo anguko lako, watu
wanaonekanaga bora kwenye vipawa vyao, lakini baada ya muda, kwa sababu ya
udhaifu, hasa ule wa siri, ile dhambi ya siri, unashangaa mtu kaanguka ghafla.
Kuna udhaifu alikuwa anaulea ndani yake, alipaswa kushughulika nao mapema kabla
hajapewa nafasi lakini alipuuzia.
Udhaifu hukuzuia kufanya vitu, huwezi
kufanya kazi ya kuwahudumia watu huku unafanya uzinzi, utasikia hukumu,
utajikuta tu hauwezi kufanya huduma. Hata ukijilazimisha, huduma yako haitakuwa
na matokeo. Kuna vitu hautafanya kwa sababu wewe ni dhaifu katika eneo fulani,
kama wewe ni dhaifu katika matumizi ya fedha, kuna baadhi ya malengo
hautayafanikisha kwa sababu unatumia fedha hovyohovyo. Kuna dhambi, inamfanya
Mungu asikutumie, inakuwa kizuizi cha yeye kukupa nafasi ya kufanya makubwa.
Dhamiria
kushughulika na udhaifu wako. Na udhaifu lazima ukasirike kwanini uko nao, na
sehemu ya kwanza ya kuanza ni kwa Mungu, unamueleza Mungu namna ambavyo udhaifu
huo unakutesa na unahitaji kutoka hapo. Kuna madhaifu mengine ni zao la vifungo
fulani fulani, hivyo ukianza na Mungu itakuwa rahisi kutoka hapo.
Wakati
mwingine inaweza kukulazimu kuwashirisha watu wa muhimu kama walezi, baba wa
kiroho na wengine, ambao wanaaminika. Mungu huwa amewaamini na nguvu ya
uponyaji katika madhaifu. Gharama ambayo wewe ungelipa miaka, yeye anatoa tamko
tu au wana hekima ya kukutoa hapo. Hatahivyo, kuna madhaifu lazima tushughulike
nayo wenyewe.
Baada ya
kusaidiwa lazima uchuke wajibu wako, unaposhughulika na udhaifu wako, kuna
mazingira utajitenga nayo, kuna watu utaachana nao, kuna vitu utaachana navyo.
Kuna vitu pia utaanza kufanya. Utaanza kujenga ufahamu wako na kudumu hapo.
Udhaifu
wako unaweza kuwa ni dhambi, ugonjwa, tabia, ujinga fulani na kadhalika. Shughulika
nao. Mwaka huu amua kushughulika na maeneo ambayo ni dhaifu.
Ndugu
msomaji, Mungu akubariki sana, ninakuombea mwaka wa mafanikio. Mungu akuongoze,
na atembee pamoja na wewe, asikusahau kamwe.
Comments
Post a Comment
Thanks for your comment, God bless you!!!