MAMBO 10 USIYOYAJUA KUHUSU WATU - Sehemu Ya 1

 Ndugu msomaji karibu tena katika wikiendi nyingine ambayo Mungu ametupa nafasi ya kukutana tena katika Bustani ya Ufahamu mahali ambako tunaongeza thamani zetu kila wikiendi na kuzifanya wikiendi zetu kuwa njema na kuhakikisha kuwa tunaanza wiki nyingine tukiwa na nishati mpya.

Tumekuwa katika mfululizo wa masomo yanayohusu watu, na leo Mungu ametupa jambo jema la kujifunza tena kuhusu watu.

Leo tutajifunza Mambo 10 Usiyoyajua Kuhusu Watu. Mambo haya yatakusaidia kujua namna unavyoweza kuingiliana na watu katika majukumu mbalimbali na pia kufaidika na uwepo wa watu kwenye maisha yako. Kumbuka kuwa Mungu huwa analeta watu kwenye maisha yetu, lakini ni sisi tunaoweza kuamua kubaki na hao watu katika majira husika na kufaidika nao.

Tunapojifunza kuhusu watu, maana yake tunapanua mtazamo wetu kuhusu watu na utu wao ili kutusaidia kujua namna ya kujichukua tukiwa na watu, na namna ya kuteka vilivyomo ndani yao ambavyo ni vya faida maishani mwetu.

Twende pamoja.

 

Jambo La #1. Watu Ni Hazina

Kila mtu unayemuona maishani mwako kuna kitu amebeba hata kama hukioni. Yeyote anaweza kukupa chochote, ni wewe kujua kitu gani unaweza kupata au kuwa na ufahamu kuwa mtu yeyote anaweza kunipa chochote.

Kila mtu ndani yake ni hazina ya kiungu ambayo imebeba mambo mengi ya thamani ambayo ni msaada kwenye maisha yetu.

Kila unayemuona ni hazina ambayo inatembea. Ni bohari yenye mambo mengi ambayo inawezekana hayajulikani lakini yapo. Hata kama anaonekana hana kitu kwa nje, anacho kitu. Ndiyo maana ukisoma Kitabu cha Luka 19:26 inaeleza kuwa mtu asiye na kitu, ananyang’anywa hata kile alichonacho. Uwe na uhakika kuwa hakuna mtu asiye na kitu, kila mtu ana kitu hata kama unamuona si kitu chochote.

Ukijifunza jambo hili kuwa kila mtu ana kitu yaani kila mtu ni hazina, itakusaidia kumheshimu kila unayemuona bila kujali unamuona katika hali gani. Unayemuona si kitu, kama ungepewa nafasi ya kufungua moyo wake yaani ndani yake uone yale aliyonayo, ungebaki umeduwaa kwa sababu ndani yake kuna vitu vingi ambavyo havionekani.

Siku moja wataalamu walikaa wakipanga kujenga lifti ili kupunguza msongamano kwenye hoteli fulani, walipokuwa wamejadili na kujadili, akatokea mlinzi mmoja, akatoa wazo kwamba angekuwa yeye angejenga lifti nje, wakabaki wametazamana na hiyo ikawa ndiyo sababu ya kujengwa kwa lifti ya nje katika Hotel iitwayo El Cortez ya San Diego na kuwa mojawapo ya sababu ya umaarufu wake.

Weka akilini kuwa, watu ni hazina.

 

Jambo La #2. Watu Wanabadilika

Ni muhimu sana ufahamu kuwa watu wanabadilika. Inawezekana haujui, ndiyo maana unapokutana na watu kuna namna unawachukulia; unaweza kuwapuuza au kuwaona kuwa hawawezi kufanya chochote au hawawezi kufika popote.

Mtu anaweza kubadilika na kuwa zaidi ya vile unavyomuona. Haitoshi kusema kuwa unayemuona ndiye halisi aliyekusudiwa kuwa, muda wowote anaweza kubadilika na kuwa yeyote katika namna usiyodhani.

Mtu yeyote anaweza kuwa yeyote kama yatawekwa mazingira ya kumuwezesha kuwa yeyote. Watu wanabadilika, unayemuona leo hawezi kukusaidia kesho anaweza kukusaidia katika jambo ambalo usingeweza kudhani atakusaidia.

Sauli aliyekuwa muuaji akawa Paulo Mtume wa yule ambaye watu wake alikuwa akiwaua na kuwatesa. Daudi mchunga kondoo akawa mfalme, au Yusufu mtumwa kuwa mkuu wa nchi ya Misri. Watu wanabadilika, usiwe na tabia ya kudharau watu kwa hali yao ya sasa.

Unaweza kukutana na mtu ukampuuza, ukamfanyia mambo yasiyofaa, baada ya siku ukakutana naye mahali ukaishia kulia na kumuomba msamaha. Mtu wa hovyo, muda wowote anaweza kuwa mtu wa maana ambaye hajawahi kuonekana tangu kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu.

Watu wanakua, wanapitia michakato mbalimbali, hakuna watu wanaokaa palepale walipo, mtu anabadilika kila wakati. Mabadiliko ni sehemu ya maisha ya mtu. Mtu hatabaki pale pale, anaweza kwenda juu zaidi au kurudi nyuma kila baada ya mabadiliko kutokea. Watu wanabadilika.

 

Jambo La #3. Ubora Wa Watu Umefungwa Katika Mazingira.

Kinachokwamisha watu kutokuwa watu hasa, ni kutokuwepo kwa mazingira wezeshi, kwahiyo akiwa tu kwenye mazingira yake hazuiliki, lazima awe bora kuliko vile unamuona leo.

Mfano wake ni samaki, samaki ukimuweka nchi kavu huwezi kumuona kuwa ni bora, lakini samaki huyo huyo ukimuweka kwenye maji, utagundua kuwa siyo kwamba hajui, ni mtaalamu katika mazingira yake. Mfano mwingine ni tai, mazingira ya tai ni juu sana na kwenye kimbunga, ndege mwingine haendi pale, lakini yeye huenda pale, ubora wake huonekana kwenye kimbunga ndiyo maana hatembei na ndege wengine.

Kila mtu ana mazingira yake ya kumfanya awe bora. Kila mtu kuna mahali akikaa, kuna nafasi akipewa, lazima vitu bora vionekane ndani yake. Ukimlazimisha mtu kukaa katika sehemu ambayo si yake halafu ukataka akuletee matokeo mezani ni sawa na kuulazimisha mkuyu ukupe maembe, ni jambo lisilowezekana.

Kila mtu ana mahali pake ambako anaweza kufanya vitu alivyoumbiwa kufanya kwa ubora kuliko vile anafanya kwa sasa. Kadri mazingira yanavyoboreshwa ndivyo na yeye atoa kilicho bora zaidi.

 

Jambo La #4. Watu Wamefungwa Katika Muda

Kila mtu unayemuona amefungwa na muda. Mambo yote yanayoonekana kwenye maisha yake, ni matokeo ya maamuzi yake kwenye muda. Na kitu kikuu anachoweza kujutia katika makosa yake yote ni namna alivyotumia muda wake jana.

Kila leo ya mtu ni matokeo ya matumizi ya muda wake kwenye jana yake. Kila mtu amefungwa katika muda. Hii inamaanisha kuwa, muda ndiyo mpaka unaoamua mtu anafanya nini kwa ubora kiasi gani. Ukweli ni kwamba wanadamu wote wamepewa masaa 24, lakini hali za watu ni matokeo ya maamuzi yao kwa kila saa walilokuwa nalo mkononi au sekunde waliyoaminiwa.

Ifahamike kuwa muda ni zawadi ambayo Mungu amewapa wanadamu ili kuwawezesha kuwa na maisha bora hapa duniani. Hatahivyo, maisha ya mtu yanaamuliwa na mtu kwa namna anavyotumia muda wake. Ukitaka kuiba maisha ya mtu, au kuiba mafanikio ya mtu, iba muda wake. Kadri muda wake unavyopotea ndivyo anavyozidi kudidimia.

Vilevile, ukitaka watu wafanikiwe katika eneo lolote, wasaidie wajue namna nzuri ya kuamua vyema katika muda walionao. Hata wale unaowaona hawana cha maana cha kutoa, watapata cha maana cha kutoa mara baada ya kuanza kuwa na hekima katika matumizi yao ya muda.

Watu wengi wanazidi kudidimia maishani kwa sababu wapo watu wanaowaibia muda kwa mitandao ya kijamii, tamthiliya na vitu vingine vingi, ili wakati wewe unapoteza muda huko, wao wanakaa chini na kuandaa vitu vingine, mwisho wa siku unabaki kuwa mteja wao kila siku, na hakuna unakoenda. Kwahiyo, kama unataka kuwasaidia watu au kuwadidimiza watu, jambo hilo limefungwa katika muda.

Ukitaka kumpa mtu msaada wa thamani zaidi kama utapewa nafasi mara moja, msaidie kujua kutumia muda wake kwa hekima. Hakika dunia itajivunia uwepo wake siku moja kama ataendelea kubaki katika tabia hiyo ya kutumia vyema muda wake.

Pia, hata ukitaka kuwafanya wanadamu wakupe fedha wewe tafuta kuwa na bidhaa ambayo inarahisisha wao kutotoa muda mwingi kwa ajili ya kupata bidhaa hizo. Ndiyo maana kina Mama N’tilie kila siku wanaongezekana na wanapata wateja, wanahakikisha kuwa wanawasaidia watu ule muda ambao wangepika, wao wanapika, wanaenda kwao kuchukua chakula, hivyo kilichotumika hapo ni muda. Watu wamenunua muda wake. Wanaweza kupika, ila tatizo ni muda, hivyo wanahitaji kununua muda, mtu yeyote anayelipia bidhaa analipia muda wa mtu aliokaa kununua hiyo bidhaa.

Vilevile, ukitaka watu wakupe vitu vya thamani, au wafanye kazi na wewe kwa uhakika na uhuru na kujiamini, hakikisha unakuwa na moyo wa kweli wa kujali muda wao

 

Jambo La #5. Watu Wana Nguvu

Kila mtu kuna nguvu anazo, kuna vitu anaweza kufanya. Watu wengi wanawaona kuwa ni dhaifu tu, hawana chochote cha kufanya, si kitu si lolote. Ni matokeo ya kutojua wanaweza kufanya vitu gani.

Watu wengi hawawapi watu nafasi kwa sababu wanaona madhaifu ya watu tu, hawaoni kingine. Ni kawaida ya watu kuona madhaifu ya watu, na hiyo inawafanya washindwe kupata mazuri kutoka kwa watu.

Ukijifunza jambo hili kwenye maisha yako, watu watafunguka na kukupa vitu vya thamani ambavyo wengine hawajavipata kutoka kwao. Unayemuona hana thamani, ni kwa sababu mtazamo wako ni eneo la udhaifu tu.

Ukikaa na watu, wasaidie kujua mambo mema wanayoweza kufanya, hata kama wao wenyewe wamejikatia tamaa maishani, wanaona hawawezi kufanya. Unaweza kulipa gharama ya kuwatia moyo na kuwawezesha kufanya kitu mpaka pale wanapoweza kujisimamia kabisa kikamilifu. Thawabu yako ni kubwa kwa Mungu, lakini pia utakuwa umetoa mchango mkubwa sana wa kuzuia watu kadhaa kuondoka na vitu vyao vya thamani, au kuzuia dunia kukosa mambo ambayo inapaswa kuyapata kutoka kwa huyo mtu.

Kila unayemuona ni dhaifu, ana nguvu, hata kama hauioni, akisaidiwa kujua uwezo wake, na kuwezeshwa na kutiwa moyo wa kufanyia kazi uwezo wake, dunia itashangaa uwepo wake, maana atakuwa mtu mwenye tija katika dunia yake.

Ndugu msomaji, ni matumaini yangu kuwa umepata mambo mengi ya kujifunza. Ninaamini kuwa kuna hatua za msingi unazichukua kwa kujifunza somo hili. Ni furaha yangu kuwa hautabaki nalo peke yako, utashirikisha na wengine Bustani hii inayokuongezea thamani maishani mwako.

Wewe ni mtu wa thamani sana hapa duniani na mbele za Mungu, uwe na wikiendi njema yenye baraka za Mungu. Tukutane tena wikiendi inayofuata kwa muendelezo wa somo letu.


Comments