UHUSIANO WA ROHO MTAKATIFU NA HUDUMA - somo la 2, sehemu ya 1

Ndugu msomaji katika somo la kwanza kumhusu Roho Mtakatifu, tulijifunza juu ya uhusiano wake na maombi, katika somo hili la 2 tutajifunza juu ya uhusiano wake na huduma tunazofanya, tutajifunza kupitia mambo mengi ya msingi sana yatakayokusaidia kufika mbali kihuduma.

Watu wengi wamekuwa wakipata shida sana katika huduma walizopewa na Mungu kuzifanya. Wamekuwa na mkanganyiko ndani yao na kuona kuwa hakuna msaada kwa ajili yao katika huduma wanazofanya katika ufalme wa Mungu. Kuna wakati umepita ukaona watu wamekuacha peke yako. Kuna wakati umeona hakuna tumaini. Na kwa kweli katika huduma kuna nyakati ngumu ambazo tunaweza kukutana nazo zinazoweza kutuumiza sana. Hata hivyo iko sababu kuu ambayo imekuwa chanzo cha watu kupata shida Zaidi ya kawaida katika huduma zao. Sababu hiyo ni KUTOTEMBEA NA ROHO MTAKATIFU NA HUDUMA.

Katika somo hili la ROHO MTAKATIFU NA HUDUMA utajifunza kupitia maswali matatu ambayo yatakufanya utoke katika sehemu uliyopo na uzidishe mahusiano yako na Roho Mtakatifu ili kutambea naye katika huduma na uweze kufanikiwa. Hakuna mtu asiyependa kufanikiwa katika huduma anayofanya. Maswali ambayo yatajibiwa katika somo  hili ambayo yawezekana hata wewe umewahi kujiuliza ni:-

1. Kwanini Hakuna Ufanisi Katika Huduma Tunazofanya?

2.Kwanini Hatutembei Au Kudumu Na Roho Mtakatifu Katika Huduma Tunazofanya?

3.Nini Matokeo Ya Kutembea Na Roho Mtakatifu Katika Huduma?

Ni maombi yangu na ni matumaini yangu kuwa somo hili litakuwa Baraka sana kwako na pia utawafundisha na wengine maarifa utakayoyapata katika somo hili.

karibu tujifunze kwa pamoja,

 

Kwanini Hakuna Ufanisi Katika Huduma Tunazofanya?

Huduma ni nini?

Huduma ni jibu la kitu kinachohitajika katika eneo Fulani, kwa watu Fulani katika kipindi Fulani. Huduma ni suluhu ya uhitaji usiokwepeka katika maisha ya mwanadamu. Mungu anajua kuwa mwanadamu lazima kuna nyakati anahitaji jambo Fulani hivyo anahitaji huduma Fulani. Mfano kuna uhaba wa maji, hili ni hitaji, huduma ni jibu, yaani upatikanaji wa maji. Hata hivyo ziko maana nyingi lakini nimetumia hii

Mungu katika kanisa anajua kuna uhitaji mbalimbali hivyo ameweka huduma mbalimbali ndani ya watu ili kuleta majibu ya uhitaji huo. Huduma hulenga kutatua changamoto ambayo isipotatuliwa italeta matokeo mabaya. Mfano watoto wasipopata huduma ya elimu kuna uwezekano mkubwa wa watoto hao kuingia katika hatari kwenye nyakati zijazo. Huduma hizo ni muhimu sana.

Huduma inaathiriwa na mambo makuu mawili ambayo ni muda na mazingira. Huduma yoyote huhitajika kulingana na mazingira husika. Kama watu wanahitaji kuokoka basi huduma ya unjilisti au utume ikahitajika hapo. Kama watu wanahitaji malezi basi huduma ya uchungaji inahitajika hapo. Kila mzingira yanapelekea uhitaji Fulani ambapo ndiyo huduma husika inayohitajika.

Muda au kipindi Fulani cha maisha kinapelekea kuwa na uhitaji Fulani. Mfano wakati wa utoto huduma ya malezi inatakiwa kutiliwa mkazo ili kuwaandaa watoto hao kuishi maisha mazuri baadaye. Huduma inategemea muda Fulani. Huduma huitajika kila muda. Lakini muhimu kujua aina za huduma hutofautiana na uhitaji wake hutofautiana au kuwiana kulingana na muda au mazingira.

Katika sura hii tutaangalia kwanini huduma zetu hazina ufanisi. kazi ya Mungu imekuwa ngumu kiasi kwamba watu wamechoka na hata hawana hamu ya kufanya huduma walizopewa kuzifanya.

 

MAMBO YA MSINGI YA KUFAHAMU KATIKA HUDUMA

Katika huduma unayoifanya kama mtumishi wa Mungu kuna mambo manne unatakiwa kuyafahamu ili kuweza kuifanya huduma uliyopewa kwa matokeo. Mambo haya watu wengi hawayatilii uzito na kujikuta wanateseka sana. Kumbuka kuwa siyo kila mateso katika huduma yamekusudiwa na Mungu mengine tunayaleta sisi wenyewe.

Mambo ya kufahamu kuhusu huduma ni yafuatayo:-

   I.        Huduma

Lazima ujue kuwa kuna huduma. Huduma imewekwa ndani yako. Lazima utafute kuijua huduma iliyowekwa ndani yako. Hakuna mtu aliyeokoka bila kuwekewa huduma au kupewa huduma ndani yake. Huduma ndiyo lile jukumu lililowekwa ndani yako kulifanya kwa kanisa ulilopo au eneo ulilopo.

Unapotaka kujua huduma iliyowekwa kwako chukua hatua ya maombi, pia unaweza kujichunguza kitu ambacho unatamani kiwe kinafanyika katika kanisa ulilopo. Unaona kuna kitu kimekosekana na wengine hawakioni wala kama vile hawajali. Kuna jambo halijakaa sawa na linakuumiza moyo sana kila unapoona halichukuliwi hatua. Hiyo inaweza kuwa huduma yako.

 

 II.        Mtoa huduma

Ni muhimu kujua kuwa kila huduma ina mtoa huduma wake. Mfano huduma zote kama elimu hutolewa na serikali husika. Sisi mtoa huduma wetu ni Mungu. Huduma tumepewa na Mungu. Hakuna anayejipa huduma akafika katika kusudi la Mungu. Mungu huwa na mtu yule aliyempa huduma yake. Huduma zote kanisani hutolewa na Mungu kwa kupenda kwake.

Mungu aliona uhitaji Fulani usiokwepeka akaweka huduma kwa watu waifanye au waipeleke kwa kanisa ili kuleta utatuzi wa uhitaji husika.

 

III.        Mpeleka huduma

Wewe ndiye mpeleka huduma iliyowekwa ndani yako na mtoa huduma mwenyewe ambaye ni Mungu aliye juu sana. Kusudi umsaidie kutatua uhitaji wa watu wanaotaka huduma hiyo. Mungu amekuteua kuwa mpeleka huduma kwa watu. Jifunze kwa mfano wa mwalimu aliyejiriwa na serikali ili kuisaidia serikali kutoa huduma ya elimu.

Umeajiriwa na serikali ya mbinguni ili kupeleka huduma kwa watu wa serikali hii. Ofisi ya mbinguni inakujua kwa mwajiriwa na uko duniani na kanisani ili kupeleka huduma unayotakiwa kuipeleka kwa watu humu duniani. Wokovu wako siyo bahati mbaya na Mungu hajakosea kukuchagua amekupa jukumu hilo ili kuleta ustawi katika kanisa na ulimwengu huu. Wewe ni mtumishi wa serikali kupita serikali za dunia hii. Wewe ni mtumishi wa Mungu aliye juu sana na serikali yake na mbingu vyote vinajua hilo. Hata ufalme wa giza unajua kuwa wewe uko na huduma Fulani ya kupeleka kwa watu ndiyo maana wamekuwa na mpango wa kukutumia wewe kujizuia wewe mwenyewe kupeleka huduma hiyo kupitia mwili wako na mazingira yako.

Wewe ni mtu wa thamani sana machoni pa Mungu. Maana huduma yake haiwezi kuwafikia wahusika bila uwepo wako ndiyo maana amekutafuta kwa gharama kubwa ili uje umsaidie kupeleka huduma. Mungu ni roho, hivyo anatakiwa kutumia mwili wako kuwafikia watu katika uhitaji wao. Hii ni kanuni ya kifalme. Dunia inatawaliwa na wenye mwili. Shetani anatumia miili ya watu kutimiza matakwa yake. Wakati huo huo Mungu na yeye anatumia miili yetu kupeleka msaada kwa wanadamu walio katika uhitaji ambao kwa namna moja ama nyingine haukwepeki.

Usiishi kama mtu asiye na kazi, huhitaji kazi za dunia kuthibitisha kuwa una kazi, mbingu ipo kuthibitisha kazi uliyopewa, unaposimama katika hilo jukumu, utaona kuthibitishwa na mbingu. Ajira yako haiwezi kulipwa kwa mishahara ya kibinadamu, malipo yako yanalipwa na ofisi ya mbinguni hata kupitia wanadamu wengine. Unahitaji kujua kuwa wewe siyo bahati mbaya. Usiwaze kuwa mnyonge mnyonge. Jua kuwa Mungu anakuhitaji kuliko vile unvyoweza kudhania. Usibweteke ukajua Mungu peke yake atakamilisha kusudi bila kukutumia wewe. Hapana huo mtazamo wa kuwa Mungu atasimama tu na kuipigania kazi yake bila wewe kusimama ufute kabisa. Mungu anakuhitaji wewe usimtupie jukumu la kupeleka huduma kwa watu ni suala la aibu kuwa mvivu na kumkabidhi Mungu wajibu wako.

 

IV.        Mpokea huduma

Pia ni muhimu kufahamu kuwa kuna watu unaowapelekea huduma. Lazima uwajue unaowapelekea huduma ni akina nani. Lazima ujue tabia zao na vitu vingi kuhusu wao. Mchungaji lazima afahamu kondoo zake. Mwalimu bora ni lazima awajue wanafunzi wake. Jua historia, tabia, tamaduni, umri, na mambo fungamano ili kujua na kuwa na wepesi wa kupeleka huduma uliyopewa na Mungu. Kuwa na huduma uliyopewa haitoshi tu bali unahitaji kuwajua wale unaowapelekea huduma ni akina nani kwa undani Zaidi. Mungu anaweza kukwambia juu ya watu hao. Pia unaweza kuwafahamu wewe mwenyewe kupitia uwezo uliowekezwa na Mungu juu yako.

Wapokea huduma ndiyo watu wanaohitaji kitu Fulani. Wanasubiria kupewa huduma ili maisha yao yastawi. Wewe umewekwa na Mungu ili kuleta huduma hiyo. Mungu anataka watu wastawi ndiyo maana amekuweka. Peleka huduma unayotakiwa kupeleka mahali sahihi. Mwambie aliyekupa huduma akufahamishe watu wanaotakiwa kupelekewa huduma uliyopewa.Kisha ukienda nenda kajifunze kuhusu hao watu ili uweze kuendana nao na kufikia lengo kuu la ustawi wao.

 

  V.        Uwezeshwaji wa mpeleka huduma

Kama mpeleka huduma unatakiwa kufahamu kuwa unahitaji kuwezeshwa kupeleka huduma hiyo kwa watu husika. Mungu ndiye anayetoa uwezesho huo  kwako. Uwezesho huo upo kwa ajili yako. Uwezesho huo unatolewa na  ROHO MTAKATIFU. Ni muhimu kujua kuwa Roho Mtakatifu  hutoa nguvu inayotusaidia kuwa na ufanisi katika kupeleka huduma tuliyopewa. Ukisoma katika Matendo ya Mitume 1:8 maandiko yanasema ……mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu nanyi mtakuwa mashahidi wangu……. Hivyo hatuwezi kuwa mashahidi yaani wapeleka huduma bila huo uwezesho.

Hapa ndipo penye changamoto kubwa sana. Watu wanafanya huduma au wanapeleka huduma kwa watu bila kuwezeshwa. Ndiyo maana huduma inazidi kuwa ngumu. Roho Mtakatifu ndiye anayetoa uwezesho. Ndiye anayetoa nguvu itakayokufanya uwe na ufanisi katika kupeleka huduma hiyo. Wengi  wamempa mipaka Roho mtakatifu kwa kuona kuwa kuna kazi kama vile hastahili kuzifanya kwa ajili yako.

Unapokuwa mwajiriwa jambo muhimu la kujua ni kuwa mshahara unalipwa na mwajiri wako. Pia anayekuwezesha katika utendaji ni mwajiri wako. Anayekupa nyumba ni mwajiri wako. Kwa mwajiri wako uatapata kila kitu unachohitaji katika kupeleka huduma yako. Wengi wanaona kuna vitu Roho mtakatifu hawezi kufanya. Roho Mtakatifu anajua mifumo yote wezeshi kwa ajili yako. Anajua mifumo ya kifedha unayohitaji ili kupeleka huduma aliyokupa. Anajua namna bora ya wewe kupata fedha ambako hakutaathiri upelekaji wa huduma kwa watu.

Wengi huwa wanaharibu huduma walizoambiwa kupeleka kwa sababu ya kutojua kuwa Roho Mtakatifu anajua mifumo yote na anao mfumo sahihi wa kifedha kwa ajili yako kulingana na huduma aliyokupa kupeleka kwa watu.

Wengine wanahangaika na maarifa tu bila kushirikiana na Roho Mtakatifu na mambo yanaharibika. Tambua kuwa Roho ndiye ajuaye watu wanachohitaji kwa wakati huo na siyo kwa kutazama kwako. Usimsaidie nini cha kufanya bali yeye akuelekeze nini cha kufanya. Kituo cha kwanza cha maarifa sahihi katika huduma unayoipeleka ni Roho Mtakatifu. Kama ni Mwalimu wa Neno la Mungu kama hupewi maarifa na yeye na unaishia na vitabu vingine tu ujue maarifa yako hayana uvuvio na hutafikia lengo la Mungu.

Mifumo ya maisha kwa ujumla ule nini, uvae nini,ulale wapi ni jukumu la aliye kuajiri. Usiposimama na yeye aliyekuajiri iliakuoneshe nini ufanye. Hii haimaanishi kuwa usifanye kazi zako binafsi bali fanya chini ya maongozi yake. Fanya kile anachosema. Roho mtakatifu anajua yote hata mafumbo ya Mungu. Anajua kile Mungu alichopanga kwa ajili ya huduma unayopeleka kwa watu. Anajua malipo ambayo yameandaliwa kwa ajili yako. Anajua kila kitu.

Ndiyo maana Yesu alisema hatatuacha sisi yatima katika Yohana 14:15-21. Anaposema atarudi tena anamaanisha kuwa atafufuka, anapofufuka kusudi lake limekamilika, linabaki la kwetu, la kwetu haliwezi kukamilika bila uwezesho wa Roho Mtakatifu. Hata Yesu alipokea Roho ili amuwezeshe kukamilisha huduma aliyokuja kuileta ya ukombozi wa mwanadamu. Uko umuhimu wa kuwa na uwezesho katika huduma tulizopewa kama tunataka zilete ufanisi.

Mwisho,

HAKUNA UFANISI KATIKA HUDUMA KAMA HAKUNA ROHO MTAKATIFU.

usikose sehemu ijayo na Mungu akubariki sana, mshirikishe na mwingine


 

Comments

Post a Comment

Thanks for your comment, God bless you!!!