KANUNI 7 ZA HUDUMA
Katika huduma kuna kanuni saba za kuzingatia ili kutuwezesha kwenda na Mungu vizuri. Hata Yesu alifahamu na kuzifuata kanuni hizi saba zote nah ii ilimsaidia yeye kufikia kusudi la huduma aliyokuja kuifanya. Kanuni hizo ni kama ifuavyo:-
I. Huduma siyo ya mpeleka huduma bali mtoa huduma. Hii ni kanuni ya kwanza ya kuzingatia. Ni lazima ujue kuwa huduma uliyopewa siyo ya kwako ni ya yule aliyekupa uifanye. Hivyo huhitaji kutumia akili yako kuifanya bali maelekezo kutoka kwa aliyekupa. Wengi wanafeli katika huduma kwa sababu wanafanya huduma ya kwao kiasi kwamba Mungu hahusiki kabisa, wanatumia akili, ujuzi na maarifa yao kufanya kazi ambayo siyo ya kwao na matokeo yake wanaishia njiani.
Yesu mwenyewe alijua hili na alilifuata kwa ukamilifu. Soma Yohana sura ya 17 yote, utaona namna ambavyo anamuomba Mungu na kukuambia kuwa lile alilomwambia kulifanya amelifanya kama inavyotakiwa. Maana yake alifanya akiwa anajua alitumwa na kazi siyo yak wake bali ni ya aliyempeleka. Pia soma Yohana 12:44-49. Yesu anawaambia kuwa hakufanya yale yakwake bali ya aliyempeleka kufanya. Ni muhimu kujua kuwa katika huduma tunazofanya kuna mwenye huduma.
Mwenye huduma huyo kuna siku atataka mrejesho wa kazi tuliyopewa kwa namna tulivyoifanya. Wengine wanafanya hawajaelekezwa kufanya wakati huo utajua kuwa ulikosea sana kutokana na adhabu utakayopokea. Huduma siyo ya kwako. Usiringie au kutambia huduma. Kama unajua huduma siyo ya kwako maana yake mwenye nayo akiamua kukupokonya anakupokonya tu na huna cha kufanya. Huduma ni ya Mungu mwenyewe. Anaumia sana tunapoumia na kuteseka bila kumshirikisha kuwa tunataka kufanya naye kazi.
Mungu anatamani kufanya kazi na watu, lakini watu wameona huduma ni za kwao. Hawana mpango wa kufanya na Mungu. Wanaenda kwa akili. Wamejimilikisha na kujipa mamlaka yote kama vile wao ndiyo Roho Makatifu mwenyewe. Hawana hata chembe ya unyenyekevu. Hili siyo jambo zuri na ndiyo linaloharibu utumishi wa wengi. Huduma tulizonazo ni za Mungu na anatamani kufanya kazi na sisi katika huduma hizo.
II. Mpeleka huduma siyo kwa ajili yake bali mpokea huduma ndiyo kwa ajili yake
Pia ufahamu kanuni hii kuwa huduma siyo kwa ajili yako bali ni kwa ajili ya watu wanaopokea huduma. Ubinafsi katika huduma humzuia Roho mtakatifu kufanya kazi na sisi hata kama anatamani kufanya kazi na sisi. Huduma haipo kwa ajili yako, ipo kwa ajili yaw engine. Haijawekwa ili kukufurahisha wewe tu bali wengine. Watu wengi wamekuwa katika tatizo hili na kujikuta wakiweka maslahi mbele kuliko kazi au huduma waliyopewa kupeleka kwa watu.
Unapogundua kuwa huduma iliyowekwa kwako siyo kwa ajili yako bali kwa watu wengine inakusaidia kuingia katika mchakato wa kujitoa ili kufanikisha kusudi la huduma hiyo. Watu wengi wanataka ubwana katika ufalme wa Mungu. Hatuwezi kufikia lengo la Mungu ikiwa tunavunja kanuni hii. Hii ni kanuni isiyokwepeka kwa watu wote walio na huduma ya kupeleka kwa watu wengine. Hata Yesu mwenyewe alisema kuwa atakaye kuwa juu ya wote sharti awe mtumwa wa wote. Kupeleka huduma ni kuwatumikia watu. Siyo kuwaangalia watu kukutumikia wewe.
Jifunze kuweka kipaumbele wale unaowapelekea huduma na siyo wewe mwenyewe katika huduma uliyopewa kupeleka kumbuka Mungu hakukupa ili ujinufaishe bali alikupa ili uwasaidie wengine katika uhitaji walio nao. Mungu amekuamini na wewe muoneshe Mungu kuwa alivyokuamini hajakosea.
Usimfanye Mungu ajutie kukuchagua kama alivyojutia kwa Sauli. Usimfanye Mungu muongo kuwa alivyokuamini wewe siyo kweli na wala si sahihi. Onesha kuwa alichokiona Mungu ndani yako ni cha kweli na ni sahihi. Kuwa unaweza kuwaweka wahudumiwa mbele ni kweli na ni sahihi. Kuwa unaweza kupeleka huduma kwa watu ni sahihi na ni kweli.
III. Mtoa huduma ndiye mwezeshaji wa mpeleka huduma kwa wapokea huduma
Hii ni kanuni nyingine muhimu kuzingatia na kufahamu. Unatakiwa kujua kuwa aliyekupa huduma yaani Mungu ndiye anayetakiwa kukuwezesha wewe kupata unachotakiwa kupata ili kufikisha huduma mahali panapohitaji huduma hiyo. Uwezeshaji mkuu hupitia Roho Mtakatifu atoaye maelekezo na kila kitu cha kufanya ili kufanikiwa katika huduma unayopeleka kwa watu kulingana na uhitaji wao.
Roho Mtakatifu ndiye atoaye nguvu wezeshi ya kutusaidia kuwa na ufanisi katika huduma. Watu wengi katika kupeleka huduma wanaweka kipaumbele vitu vingine ambavyo bado haviwezi kuachilia kuwezesha kwako. Unahitaji nguvu itokanayo na Roho ili kukuwezesha kufanya huduma uliyopewa kwa ukamilifu. Hauhitaji kuwa na maelezo mengi. Unachohitaji ni kitu kimoja tu NGUVU YA ROHO MTAKATIFU. Ukipata hiyo nguvu itakusaidia kufanya yote unayotakiwa kufanya bila tashwishi. Huhitaji kwenda peke yako ndiyo maana alisema msitoke humu hata mvikwe uweza utokao juu Luka 24:49. Hutakiwi kufanya kazi bila kuwezeshwa.
Jambo muhimu kujua kuwa uwezesho unapatikana kwa Roho wa Mungu peke yake. Watu wa giza hupewa uwezesho na mwenye giza, hawafanyi wao bali giza ndani yao. Hata kwako siyo wewe, bali ni Roho ya Mungu itende kazi kupitia wewe. Kusudi ni watu wahudumiwe na Mungu kwa viwango halisia.
Kuwezeshwa katika huduma ya Mungu ni kutoka kwa Mungu mwenyewe. Hakuna mwanadamu au chochote kinaweza kukuwezesha isipokuwa kutumiwa na Roho Mtakatifu ili kupitia wao ufike sehemu Fulani iliyokusudiwa.
IV. Mpeleka huduma ni lazima na ni haki yake kudai kuwezeshwa ili kupeleka huduma kwa wapokeaji.
Katika safari ya wana wa Israel Musa kuna mahali alimwambia Mungu, uso wako usipotuchukua hatutoki mahali hapa. Soma Kutoka 33:12-17. Mungu anaamua kukubaliana na Musa kuwa ataenda na yeye. Ni lazima na ni haki yako kuwezeshwa. Usikubali uifanye kazi bila uwezesho. Maana kama utakosa kuwezeshwa kazi itakuwa ngumu kabisa. Kwa maneno mengine unaweza kukimbia huduma.
Kumbuka kuwa katika huduma changamoto mbalimbali zinaweza kuinuka. Wakati mwingine wale unaowapelekea huduma wanaweza kuwa kinyume chako hata kama wanaihitaji huduma hiyo. Wakati mwingine unaweza kupitia nyakati za upweke. Huoni mtu akikufariji. Unajihisi uko peke yako. Wakati mwingine unakata tamaa maana huoni msaada wowote kwa ajili yako. Wakati mwingine unaweza kulaumu kuwa watu kama vile hawaoni unachofanya kwa ajili yao. Watu wanaweza kuwa wagumu wa mioyo na wewe ndiyo umepewa kuwafikisha kanaani. Ni wakati mgumu sana unapohisi kuishiwa nguvu za kuendelea.
Katika nyakati hizo zote jambo muhimu ni kuwezeshwa. Unahitaji mfariji wakati wa upweke wakati unapeleka huduma kwa watu. Unahitaji wa kukutia moyo unapoona kukata tamaa katika huduma. Unahitaji mshauri unapoona mambo hayaendi na namna ya kufikia haiwezekani. Unahitaji mwongozaji unapoona giza nene mbele yako. Unahitaji mwalimu unapoona mambo hayaeleweki. Unahitaji msaidizi unapoona msaada kama vile umepotea.
Unahitaji mtoa majibu unapoona majibu yako kuhusu hali ya maisha, afya, uchumi na kadhalika kuwa hayapo. Unamhitaji wa kusimama na wewe katika nyakati ngumu. Unamhitaji anayeweza kuiona kesho kabla yako unapokosa maono kwa ajili ya huduma yako.
Katika hayo yote unamhitaji mmoja tu ambaye amejitosheleza katika maeneo yote unayohitaji kuwezeshwa ili kufikia kusudi husika la huduma uliyonayo. Unamhitaji Roho Mtakatifu tu. Huyu anaweza kukuonesha na kukupa maono yote kuhusu huduma. Huyu anaweza kukupa mpango wote au kile alichokilenga Mungu juu ya huduma aliyoiweka ndani yako maana yeye huyachunguza hata mafumbo ya Mungu. Soma 1Wakorintho 2:10. Yale ambayo Mungu ameyapanga kwa ajili ya huduma aliyokupa, mwisho wote ambao unaonekana kuwa fumbo yeye anajua na anaweza kukuonesha ukajua wapi unakoelekea.
Huyu ni mwalimu ambaye elimu yake imezidi fahamu zote. Anaweza kukufundisha mambo ambayo wengine hawayajui. Alianza kufundisha tangu enzi za kina Petro na kina Paulo na mpaka leo hajachoka kazi yake ya ualimu. Una swali gani gumu ambalo unatamani akufundishe ili iwe rahisi kwako katika huduma. Kama umepewa huduma ya ualimu jua kuwa unaye Mwalimu Mkuu ambaye kama jambo limekushinda unampelekea. Hakuna swali asilowezq kukokotoa. Na kwake hakuna haja ya kikokotozi. Yeye hutoa kila kitu kamili bila utegemezi. Huyu Roho Mtakatifu anatoa mafunzo bora ya hali ya juu kuzidi elimu zote. Unapopokea mafunzo yake, ukiongeza na ule uwezo au ujuzi ulionao katika huduma, basi huduma yako itakwenda vizuri. Kinachofanya huduma yako haiendi sawa ni kwakuwa hauna huyu mwalimu wa kukufundisha nini cha kukufanya.
Zaidi ya hayo huyu ni mshauri na mtiaji moyo mzuri. Hatii moyo katika hewa bali anatia moyo katika uhakika na madhihirisho kwa yule mwenye uhitaji.
Tambua kuwa mambo yako mengi katika huduma yameharibika kwa kukosa mshauri sahihi. Mimi huyu ndiye mshauri wangu. Wengine wakinishauri kitu, yeye akisema nisifanye napenda kumsikiliza maana yeye ajua kila kitu kuhusu mimi. Washauri wengine yawezekana hawakujui. Lakini huyu anakujua ulivyo tena vyema sana hivyo atakushauri siyo ilimradi tu bali kulingana na vile ulivyo. Unapopoteza Amani ya moyo huyu anakurudishia mapema ili uendelee na kazi uliyopewa. Huyu anakutia moyo kwa vitendo unapopitia katika magumu. Huondoa mizigo yote na uzito wote unaoweza kuuhisi moyoni au ndani yako wakati wa magumu. Anakupa furaha na watu wengine wanaweza kukushangaa umekuwaje. Anakufanya uwe wa tofauti usiyeyumbishwa na mazingira. Mambo yanapokaa vibaya yeye hukusaidia.
Yeye ni msaidizi wetu katika kila kitu. Tunapohitaji msaada yeye anaweza kuwatumia hata wale wasiotupenda au wasiotujua waje kutoa msaada. Siyo wao wanatoa bali ni yeye kupitia wao. Yeye akiamua wa kuzuia hakuna. Akiamua kukusaidia basi hamna mwingine. Yeye anajua yote unayoweza kuhitaji msaada na yuko tayari wakati wote kukusaidia katika jambo lolote endapo utahitaji msaada wake na utamuomba akusaidie. Wengine wakigoma kukusaidia yeye hagomi wala hatakusahau. Anafanya yote haya maana anajua wewe ni mwajiriwa wa ofisi ya mbinguni. Yeye amepewa jukumu la kuwawezesha wafanyakazi wote wa ufalme wa Mbinguni humu duniani. Pia anapenda kutimiza wajibu na ni mwaminifu katika kazi yake. Hivyo unapimhitaji hawezi kukataa maana akikataa atakuwa ameenda kinyume na mpango wake mwenyewe. Atakuwa amejigeuka.
Yeye ni kiongozi mkuu. Ukimpa nafasi atapangilia kila kitu katika mstari. Anajua kila kitu kinatakiwa kikae namna gani.
Anajua hao watu unatakiwa kuwapeleka wapi, lini, kwa usaifiri gani na kwanini. Unapompa nafasi akuongoze unaruhusu atumie ujuzi wake wote kwa ajili yako. Hebu tafakari juu ya maarifa ya Mungu. Na angalia kuwa ukimpa nafasi huyu Gavana wa Mbinguni duniani Roho Mtakatifu unahisi ufanisi utakuwa wa kiwango gani? Nakuhakikishia utaona mambo makubwa. Yeye ni kiongozi anayetaka mambo makubwa. Unapompa nafasi unamlazimisha afanye mambo makubwa katika huduma yako.
Unaweza kuona ni namna gani huyu Mwezeshaji alivyo wa muhimu kwako. Na ukiangalia kila kitu anachokifanya wewe unakihitaji katika huduma unayoipeleka kwa watu. Hivyo basi ni haki yako kuwa naye. Pia vilevile ni lazima kumdai aje kwako. Unaweza kuona namna ambvyo bila yeye huwezi kufanya kitu chochote ukafanikiwa katika huduma. Ajabu kuwa kweli mambo yote yeye anayashikilia. Sasa huyu ni nani hasa mpaka kila kitu ashikilie yeye. Kwa nini yeye.
Sababu ni kuwa Roho Mtakatifu ni Gavana mkuu wa Ufalme wa Mbinguni Duniani. Yupo ili kuusimamia ufalme wote wa Mungu. Yupo kuhakikisha wafanyakazi katika ufalme huu wanahudumia watu katika mazingira wezeshi. Huyu ndiye anayehusika na kila kitu ufalme huu. Yeye pekee ndiye mwenye mamlaka ya mwisho huku duniani katika usimamizi wa ufalme wa Mungu. Kusudi la uwepo wake ni kuunganisha utawala wa mwanadamu na utawala wa nuru kuwa kitu kimoja na shetani aanguke. Na kwakuwa anahitaji watu wa kufanya naye kazi ndiyo maana amebeba jukumu la kuwawezesha ili wafanye kazi kwa ufanisi ili kusudi la kuwarudisha na kuwafanya watu waishi katika ufalme kwa raha bila ubaya.
Kwa maneno mengine ni haki yako akuwezeshe. Ni haki yako kuwa na ukaribu naye ili awe anakuelekeza hatua kwa hatua nini cha kufanya.
Unahitaji akuwezeshe wewe mwenyewe usiishi tena katika ufalme wa giza, na uwafanye wale walio katika giza waje katika nuru, na wale walio katika nuru wakae katika nuru. Roho Mtakatifu ni haki yako kuwa naye. Kama ni haki yako, nakushauri usikubali haki yako ipotee. Yeye ni mwaminifu, unapoomba haki yako anakupa. Fanya bidii kuwa naye. Hakikisha unampata ili akusaidie. Unaweza kuchukua hatua ya maombi yasiyokoma mpaka umepata na unaishi naye. Usikubali kufanya huduma bila yeye ni haki yako. Hata wewe unaweza kumpokea, kuvikwa na kujiliwa na Roho Mtakatifu. Hayupo tu kwa ajili ya wale unaowaona wako naye bali hata wewe unaweza kuwa naye.
Unahitaji kuumba shauku inayochoma, mfanye aone ukweli huu kuwa bila yeye huwezi. Kuwa wazi kwake kuwa unamhitaji na umueleze umuhimu wake kwako. Muombe akupe nguvu. Omba kujaze, akuvike uweza utokao juu, akujilie juu yako na akujalie kunena kwa lugha mpya kama ishara mojawapo ya kuwa unaye tayari. Fanya bidii, omba kwa bidii, usikubali kutulia mpaka umepokea nguvu yake. Yeye anaweza kukupa lakini anahitaji utayari wako. Anataka kuona kama unamhitaji kweli au la. Wengine wameridhika na hali walizonazo katika huduma zao, na yeye ameamua kuwasubiri waje kwake awape nguvu. Usikubali kuridhika na hali uliyonayo. Ni haki yako kuwa naye. Mng’ang’anie mpaka awe na wewe.
Endelea kuwa na ushirika naye. Usikubali kumpoteza katika maisha yako yote ya huduma. Utamtumia katika majukumu yako yote na utaona wepesi katika huduma. Hutatamani kuacha huduma bali utatamani kuongezewa huduma za kupeleka kwa watu maana mzigo siyo wa kwako tena ni wa Gavana mwenye dhamana.
V. Mpeleka huduma ni wajibu wake kujua kusudi la huduma anayoipeleka kwa mpokea huduma.
Unatakiwa kujua kusudi la huduma unayofanya.
Wengi kwa kutokujua kusudi la huduma wanazozifanya wamejikuta hawachukulii uzito wa huduma hiyo na kutoifanya kwa ufanisi. wengine wamejikuta hata kutafuta uwezesho ni kama kumsumbua mwezeshaji. Ni kwa sababu hawajui uzito wa huduma walizopewa kuzifanya kwa wakati huo.
Ni muhimu kujua umuhimu wa huduma uliyopewa. Fahamu kupitia Roho Mtakatifu na Neno la Mungu juu ya kusudi la huduma uliyonayo. Unapoujua umuhimu au kusudi la huduma iliyowekwa ndani yako inakusaidia kuchukua hatua stahiki ili kutafuta uwezesho na kuingia katika utendaji wenye ufanisi. tafuta kujua kwanini hiyo huduma ipo, kwanini huduma hiyo imewekwa ndani yako. Maana Mungu hawezi kuweka huduma bila kusudi au sababu maalumu.
VI. Mpeleka huduma ana maamuzi juu ya kupeleka au kutopeleka huduma
Mungu ameweka uamuzi ndani yako. Unaweza kuamua kupeleka au kutopeleka huduma. Unaweza kuacha kuhudumu kama ukiona ni sahihi. Hakuna wa kukuzuia katika kutofanya huduma isipokuwa wewe mwenyewe. Wengine wameacha huduma kwa kuwalaumu wengine kuwa wamekuwa sababu. Siyo kweli kabisa, kuacha huduma umeamua wewe mwenyewe. Hakuna wa kukufanya uache huduma. Wewe ndiyo kizuizi cha huduma yako.
Watu wengine unaowasingizia wapo ili kusapoti maamuzi yako. Unapowaza kuacha huduma wako watakaokupa ushauri wa kuacha na kukuonesha kuwa uko sahihi katika maamuzi yako. Unapowaza kufanya huduma wako watakaokuambia kuwa umewaza kitu sahihi na ukifanya huduma utakuwa umefanya maamuzi sahihi. Hawajakuamulia bali wako nyuma ya maamuzi yako mwenyewe.
VII. Kila maamuzi ya mpeleka huduma yana matokeo yatakayoathiri maisha yake
Maamuzi unayoyafanya yoyote yale yana matokeo.
Hakuna maamuzi yasiyoleta matokeo duniani hakuna. Usimlaumu mtu juu ya mambo yanayokutokea ni matokeo ya maamuzi yako tu hakuna wa kumlaumu. Hakuna aliyekosea ni wewe mwenyewe. Hakuna aliyekupeleka shimoni ni wewe mwenyewe umajipeleka. Usiendeshwe na roho au tabia ya malalamiko kwa makosa yako mwenyewe.
Ukiamua kupeleka huduma utaona msaada wa Mungu juu ya maisha yako. Utaona namna ambavyo Mungu akiwa na wewe katika huduma. Mara zote Mungu anapokutaka kufanya huduma hakulazimishia kwanza bali anatafuta maamuzi yako. Unapokubaliana na wazo lake jua jambo moja kuwa utafaidi mambo mengi kutoka kwake maana mnaendana. Mmekubaliana na yeye atakusaidia katika maisha yako kwa sababu umemsaidia katika kupeleka huduma.
Endapo utakataa nayo ni maamuzi. Kukataa huduma unayopewa moja kwa moja na Mungu unamaanisha kuwa wewe upo kinyume na Mungu. Na kama upo kinyume na Mungu utakutana na mkono wake katika sura nyingine na utaangukia katika matokeo ya maamuzi yako.
Kama akiona kuwa unakataa kwa sababu ya hofu. Ujue kuwa atakupitisha katika majaribu mpaka uingie katika huduma. Akiona kuna kitu kinakusababisha usifanye kazi basi atashughulika nacho ili wewe uisaidia dunia katika uhitaji wake.
Wakati wote maisha tuliyonayo ni matokeo ya vile tulivyoamua katika kupeleka huduma kwa watu. Kama tutaamua kupeleka lakini kwa ulegevu maandiko yanasema alaaniwe afanyaye kazi ya BWANA kwa ulegevu. Hivyo kama hatutaamua kufanya kwa bidii ile kazi tuliyopewa tutajikuta bado hatufaidi kawa wafanyakazi bila kujali tunafanya kazi katika ufalme na serikali ya Mbinguni. Tuamue kufanya huduma kwa bidii zote na tutarajie kuuona uwezesho wa Mungu kwa kuamua kuomba huo uwezesho ambao upo kwa ajili yetu kama wafanyakazi.
Usikose sehemu ijayo, mshirikishe na mwingine na Mungu akubariki.
Comments
Post a Comment
Thanks for your comment, God bless you!!!