UHUSIANO WA ROHO MTAKATIFU NA HUDUMA - somo la 2, sehemu ya 4

Katika sehemu iliyopita tulijifunza kwanini Roho hadumu na sisi katika huduma zetu, tuliangazia jambo la kwanza juu ya muda, tulijifunza kuwa anahitaji muda na sisi katika maombi, na katika sehemu hii tunaangazia juu ya muda anaohitaji katika kujifunza neno, pia na jambo la pili la uaminifu. 

Karibu

Kujifunza Katiba/Mwongozo Wa Huduma

Watu wengi huwa hawana muda na katiba au mwongozo wa huduma. Roho Mtakatifu anatamani tuwe na muda wa kujifunza katiba ili humo tuyaone aliyoyaficha. Kuna mambo muhimu yamefichwa katika katiba hii ambapo mtu anapoyajua yatakuwa msaada wake. Mambo haya yatakufanya uingie katika maombi na kuendelea kuwa na ushirika na Roho mtakatifu.

Katika hiyo katiba kumejaa haki zako zote kama mfanyakazi wa ofisi ya mbinguni. Kama hausomi katiba hii hutojua haki zako na unaweza kuendelea kuteseka katika huduma kumbe haukutakiwa kuteseka.

Katiba haipo kwa ajili ya dhambi tu bali pia kwa ajili ya haki zako za kimsingi kama mfanyakazi wa mbinguni. Isome katika zijue haki zako na uchukue hatua ya kuzidai. Usikubali kuishi hivyo ulivyo. Unapojifunza katiba utagundua mambo mengi

Katika hiyo katiba yapo majukumu yako yote ambayo unatakiwa kutekeleza. Humo wajibu wako wote umeelezwa kwa undani. Wajibu huu unakusaidia kulinda uhusiano wako na Roho. Anatamani uishi maisha matakatifu. Anatamani usiwe kinyume na Mungu. Hayo hayawezekani kama huijui katiba. Katiba inakuwezesha kujifahamu Zaidi ya vile unavyojifahamu. Katiba imejaa mawazo ya Mungu kwa ajili yako. Roho kama rafiki yako anatamani ujue yote hayo. Mungu hajawahi kukuwazia kushindwa ukiyajua yote hayo hutakubali kuishi nje ya katiba.

Katika katiba mfumo wa malipo ya mshahara kwa wafanyakazi wote wa ofisi ya mbinguni umeelezwa. Humo utagundua nini ufanye ili uupate mshahara wako bila shida yoyote. Humo kuna maelekezo yote pia kuhusu huduma ambayo yanaweza kukusaidia kufanya huduma kwa ufanisi wa kutosha.

Katika katiba kuna elimu ipitayo elimu zote. Elimu hiyo hutolewa na Roho mtakatifu. Katiba ndiyo mwongozo na kitabu cha kujifunzia. Unapoanza kujifunza unaweza kuwa na daftari na kalamu. Na kumuomba mwalimu wako mzuri Roho Mtakatifu aje akufundishe. Yeye anapenda kufundisha kuliko tunavyodhani. Anapokuwa anatufundisha tunazidi kudumisha uhusiano wetu. Anazidi kuwa karibu na sisi. Tunazidi kujifunza kupitia yeye. Ufahamu wetu unazidi kuongezeka. Na kama wafanyakazi tunaweza kufaidi Zaidi kwa kuwa tuna ukaribu na mwalimu ajuaye yote.

Katiba hii au mwongozo huu wa huduma unaitwa BIBLIA TAKATIFU. Hiki ni kitabu cha kipekee sana. Biblia ni katiba ya ufalme wa Mbinguni. Yeyote anayehusika na huu ufalme lazima aitii. Hata Mungu mwenyewe anasema ameikuza ahadi yake kuliko hata jina lake. Inamaanisha kuwa hawezi kwenda kinyume na alichosema. Katiba hii ni maneno ya Mungu mwenyewe ambayo hata yeye hawezi kwenda kinyume nayo. Katika hii katiba hata yeye mwenyewe amejifunua sana kiasi kwamba tunaweza kufahamu jinsi ya kufanya naye kazi.

Kumbuka kuwa wewe ni raia wa mbinguni na mfanyakazi wa mbinguni. Una haki zako kama raia na wajibu kama raia. Una haki kama mfanya kazi na una wajibu kwa mfanyakazi.

 

2.  Uaminifu 1Wakorintho 4:2

Roho mtakatifu anahitaji uaminifu kutoka kwako ili muweze kuwa pamoja. Bila uaminifu hamuwezi kuwa kitu kimoja na yeye. Anatafuta mtu mwaminifu wa kufanya naye kazi.

Uaminifu  ni tabia ya kufanya jambo katika wakati sahihi, mazingira sahihi, kwa mtu sahihi, kwa ubora na mwitikio chanya ndani yako.

Uaminifu unadai kufanya jambo kwa wakati sahihi. Roho anataka mtu anayejali muda. Anayethamini muda. Anapokuambia fanya jambo Fulani kwa wakati Fulani basi unafanya hilo jambo kwa wakati huo. Hapendi kufanya kazi na mtu anayetaka kufanya kwa muda wake yeye na siyo muda anaomuelekeza. Kama unahitaji kutembea na kudumu na Roho wa Mungu basi hakikisha unafanya huduma au kile alichokuagiza kwa wakati. Uwe na tabia ya kujali muda wa Roho Mtakatifu. Fanya anachokuambia kwa wakati huo huo uliombiwa  siyo nje ya. Ukifanya kwa muda wako anatamfuta mtu wa kufanya naye anayejali muda wake.

Uaminifu unataka ufanye jambo katika mazingira sahihi. Mfano wewe ni mwonyaji au muonaji, umeona jambo baya kuhusu mtu au uovu anaoufanya, hutakiwi kwenda katikati ya watu na kuanza kumwambia jambo alilofanya isipokuwa umeambiwa kufanya hivyo. Ni kweli umepewa ujumbe, unaupeleka kwa wakati lakini mazingira siyo sahihi. Unatakiwa kuwa makini sana. Mungu anakuambia fanya kitu Fulani, lakini hufanyi katika sehemu amekuambia. Siku moja kina Paulo walikuwa katika safari zao za injili, kuna sehemu walikusudia kwenda, kwa kweli walikuwa wameambiwa wakahubiri injili na walienda katika wakati, lakini walikuwa wanaenda mazingira ambayo siyo sahihi.

Mungu akawaambia katika ndoto waelekee Makedonia mahali ambapo ndiyo mazingira sahihi. Kuna maeneo walitaka kuhubiri lakini Roho hakuwaruhusu maana siyo mazingira sahihi kwa wakati huo. Ukiambiwa peleka kitu Fulani mahali Fulani fanya hivyo. Kwa kujali mazingira unayoambiwa kupeleka unajiweka katika nafasi ya kuwa na ushirika na Roho wa Mungu na kuweza kutembea naye.

Uaminifu ni kufanya jambo kwa mtu sahihi. Huduma uliyopewa ina watu wake maalumu wa kuwapelekea. Mungu anataka upeleke kwa watu hao. Wakati mwingine inakuwa vigumu kukubaliana na Mungu maana tayari huwa kunawatu wetu ambao tumewakusudia kumbe siyo hao. Ikiwa Mungu amekupa huduma ya ualimu wa watoto usilazimishe kwa wakubwa huwezi kufika popote. Nenda kwa wale ulioambiwa uende kwao. Msikilize Mungu akuoneshe ni akina nai unatakiwa kuwahudumia na uende ukawahudumie hao watu. Kwa kufanya hivyo unaweka uhusiano wako na Roho vizuri na utadumu naye siku zote.

Pia uaminifu ni kufanya jambo kama inavyotakiwa au kwa ubora. Watu wengi wanapopewa kazi wanafanya ilimradi tu. Ili wakija kuulizwa waseme wamefanya kazi. Suala siyo kufanya kazi suala ni kuwa je umefanya kazi katika viwango unaavyotakiwa? Unafuata maelekezo ya kazi uliyopewa? Je una maandalizi ya kutosha kuhusu kazi yako unayotakiwa kuifanya. Umejiandaaje kimaombi, umejiandaaje kimazingira, umejiandaaje kifikra?  Tathminii ya kazi au huduma na utendaji wake unavyoendelea ikoje? Umeipima inaendaje? Marekebisho gani unayafanya kulingana na uhitaji wa watu na utendaji wako? Je umeridhika ka viwango ulivyonavyo vya utendaji? Je umechukua hatua gani?

Mwisho; 

uaminifu unamaanisha uwe na mwitikio chanya ndani yako kuhusu huduma unayoifanya. Wengi wanapenda kujiinua katika huduma. Ukifanya hivyo anakuacha na ataenda kwa wengine ambao wao watamrudishia utukufu yeye. Usifanye kitu ili wakuone fanya kwa sababu ni jukumu lako kufanya. Msikilize Gavana na fuata maelekezo yote anayosema. Fanya kulingana na maelekezo yake siyo ya kwako tu. Hatuwezi kufika kama tunamuweka Roho Mtakatifu mifukoni na kwenye pochi zetu, halafu tunataka atuongoze. Lazima tumuachie yeye, na yeye aongoze katika safari yetu ya huduma.

 Mungu akubariki sana kwa kuendelea kujifunza Neno lake, mshirikishe na mwingine.

Comments