UHUSIANO WA ROHO MTAKATIFU NA HUDUMA - somo la 2, sehemu ya 3

Ndugu msomaji, tumekuwa katika mfululizo wa somo letu linaloangazia juu ya Uhusiano wa Roho Mtakatifu na huduma tunazofanya. Katika sehemu hii tunaendelea kujifunza juu ya:-

Kwanini Hatutembei Au Kudumu Na Roho Mtakatifu Katika Huduma Tunazofanya?

Watu wengi sana wamekuwa wakipitia hii changamoto. Wanapokea uwezeshwaji yaani nguvu za Roho Mtakatifu leo na keshokutwa hawana tena. Wengi wanapitia shida hii. Kwanini sitembei na Roho wa Mungu. Katika sura hii jibu la swali hili litatolewa na utajua kwanini haudumu naye. Kasha chukua hatua stahiki ili uendeleee kudumu naye.

Roho anaweza kukaa na mtu katika maisha yake yote. Mungu hana mpango wa kuachana na mwanadamu. Mungu hataki akuonjeshe uzuri wa kufanya naye kazi halafu akaondoka. Mungu hataki kukutelekeza. Mungu hataki uwe yatima asiye na msaada. Yatima maana yake wazazi wake alikuwa nao lakini kwa sasa wamefariki. Mungu hataki upitie ugumu unaopitia katika huduma. Mungu hafurahishwi na wewe kuumia au kukata tamaa kwa namna yoyote ile. Mungu anaumia sana unapofanya kazi aliyokupa katika upweke na masumbufu mengi.

Shida haipo kwa Mungu. Mungu wakati wote yupo na ana mpango kamilifu na wewe. Kuna vitu ameweka kwa ajili yako. Shida kubwa ipo kwako. Kinachokusumbua siyo kuwa na Roho Mtakatifu bali ni kutembea na Roho Mtakatifu. Watu wengi hawatembei na Roho Mtakatifu japo inawezekana walimpokea. Wao humuita kwao na wao haohao humfukuza kwao. Maandiko yanasema msimhuzunishe Roho wa Mungu. Lakini watu wanamhuzunisha kila wakati. Hivyo inakuwa ngumu kutembea naye katika maisha haya ya utumishi. Hatuwezi kumlaumu Mungu kwa nini hatembei na sisi. Tunatakiwa kujilaumu sisi kwanini hatutembei na Mungu. Yeye ni mwaminifu. Sisi hatujajifunza namna ya kutembea na Roho Mtakatifu.

Yeye maandiko yanamuelezea kama hua yaani mpole. Hivyo tunapenda kumuonea yaani kumfanyia vibaya kwa sababu ya upole wake. Tunautumia upole wake vibaya.Hatuna hata wazo la kutembea naye. Tunasema tunataka kukaa naye huku tunamwambia toka. Hii ni kwa sababu ya kukosa maarifa ya namna ya kuishi naye. Maandiko

yanasema watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa. Tunaangamizwa kwa sababu hatujui jinsi ya kuishi na Roho Mtakatifu.

Hebu tujifunze yale anayohitaji kutoka kwetu ambayo ndiyo yatakayotuwezesha kudumu na kutembea na Roho wa Mungu katika huduma tunazofanya.

 

VITU ANAVYOHITAJI ROHO MTAKATIFU ILI ATEMBEE NA MPELEKA HUDUMA.

Kuna mambo ambayo Roho Mtakatifu anayahitaji kutoka kwetu ili aishi na sisi. Ili atembee na sisi kuna vitu tunatakiwa kuvifanya ilia one fahari kuwa na sisi. Roho anahitaji mambo yafuatayo:-

1. Muda

Roho Mtakatifu anahitaji muda wa kuwa na sisi. Anapenda kuwa karibu na sisi kuliko tunavyodhani. Kwa sababu yeye  ndiye ajuaye yote. Tunahitaji msaada wake. Lakini yeye anahitaji muda wetu. Watu wengi ni wepesi kumuomba aje kwao lakini kutoa muda wao kwa ajili yake limekuwa ni tatizo kubwa sana.

Muda ni kipimo kizuri sana cha kuthamini mtu au kitu. Tunapotoa muda kwa ajili yake tunamaanisha yeye ni wa thamani sana kwetu na tunamuonesha yeye ni wa thamani sana kwetu basi hawezi kutuangusha anahakikisha kiwango kile kile tulichomthamini anafanya kazi ili tuendelee kumthamini. Pia inaonesha kuwa tumemuamini, Mungu anampenda mtu anayemuamini, anamlazimisha kufanya kazi ili Imani yake isiwe bure.

Roho anahitaji muda katika maeneo mawili

 

Maombi  Waefeso 6:18-19

Roho mtakatifu anatamani kuwa na muda na sisi. Tupige stori naye. Tunabadilishana naye mawazo. Anatuelekeza nini cha kufanya pia anatusaidia hata katika kuomba. Maombi ni kitu muhimu sana katika kudumisha ushirika wako na Roho Mtakatifu. Wengi hawapendi kuomba nah ii inawafanya wasitembee na Roho Mtakatifu. Maombi ni muhimu sana.

Maombi ni kitendo cha kumpa Roho ruhusa kufanya kazi na wewe. Kumbuka dunia inatawaliwa na wanadamu. Viumbe wenye miili ndiyo wenye haki na dunia. Kiumbe kingine kinachoingia duniani siyo haki yake. Ndiyo maana tunayo haki ya kukemea mapepo maana siyo haki yao duniani. Hata Roho hana ruhusa ya kufanya kazi duniani maana hana mwili. Hata Kristo ilimlazimu kuvaa mwili wa Yesu ili akamilishe kazi. Roho anahitaji mtu atakayekuwa anamruhusu kuja kufanya kazi duniani ya kuuthibitisha ufalme wa Mungu. Tunapoacha kuomba tunamaanisha Mungu asifanye kazi. Na kama asifanye kazi maana yake tupo kinyume naye. Roho anapoona kuwa hatutaki afanye kazi na sisi au katika ulimwengu huu, anatuacha na kwenda kutafuta ruhusa kwa wengine wanaoweza kukubaliana naye na kumpa ruhusa.

Mungu anataka tumruhusu achukue hatamu kutusaidia katika kazi maana tukae tukijua kuwa humu duniani kuna ufalme wa giza utendao kazi, bila nguvu za nuru hatuwezi kushinda. Ndiyo maana Mungu amemtoa Roho wake ilia je kutusaidia kuwa washindi. Tunapomnyima nafasi tutashindwa na tutazikimbia huduma maana shetani hataki huduma tunazofanya zifanikiwe. Magumu utakayokutana nayo yatakufanya uachane kabisa na kazi ya kupeleka huduma na kujikuta katika hatari ya mateso Zaidi ya kugoma kufanya kazi ya Mungu.

Mungu anahitaji kutumia mwili wako kufanya kazi zake duniani. Kama vile alivyomtaka Mariamu kupitia yeye Kristo Yesu aje vivyo hivyo anakuhitaji kupitia wewe Roho wake aendeleze mapambano ili kuleta USHINDI katika ufalme wa nuru. Mungu anamtafuta mtu atakayekuwa anatoa ruhusa kutumiwa nay eye ili huduma iwe na ufanisi. huwezi kutembea na Mungu bila maombi.

Yesu mwenyewe alikuwa anatumia muda mwingi katika kuomba ili amruhusu kwa wingi Roho aje afanye kazi kupitia yeye. Ndiyo maana alikuwa anatumia muda mchache katika huduma na anakuwa na matokeo makubwa. Wengi wetu tunatumia muda mwingi na wanadamu au kuhudumu na matokeo madogo kwa sababu hatuna muda wa kumruhusu Roho afanye kazi na sisi. Tukumbuke kuwa huduma tulizonazo siyo mali yetu. Huduma zina mwenyewe. Tunapoomba tunamruhusu mwenye huduma afanye kazi mwenyewe na tuone matendo makuu ya Mungu. Roho anapenda kuona tunampa kazi yake yeye mwenyewe ili sisi tutumike kukamilisha kazi kwa sehemu ndogo isiyotuumiza. Anataka kubeba majukumu yote ili atutumie kufanya makubwa na tuwe na ushuhuda hapo mbeleni. Shida iko kwetu hatuna muda wa kuomba. Hatuna muda wa kumpa ruhusa ya kufanya kazi na sisi. Tunaweza kuomba tumpokee na tukampokea lakini kama hatutoendelea na tabia ya kuomba na kumpa ruhusa ya kututumia kufanya huduma aliyotupa, kamwe hatuwezi kuendelea au kudumu naye.

Yeye anajua kila kitu kuhusu huduma, hivyo kama tutakuwa na tabia ya maombi yeye anatupa maelekezo yote kuhusu huduma. Yeye anatuambia nini cha kufanya. Yeye hutoa maarifa yote kamilifu ambapo kama tutayaunganisha na ya kwetu tunajiweka katika mazingira ya utendaji wenye ufanisi Zaidi. Tunafanya huduma ambayo siyo ya kwetu bila kuwa na maelekezo kutoka kwa mwenye huduma. Tumeajiriwa lakini hatuna muda na mwajiri wetu ili atuelekeze Zaidi kuhusu utumishi wetu. Tunahitaji maombi endelevu yatatusaidia kupata maelekezo. Pata muda wa kuomba. Pata muda wa kuwa na Roho mtakatifu. Tafuta muda. Muda wa kuwa na Roho usiwe muda wa nyongeza au dharura bali uwe muda kamilifu.

Kupitia maombi unayaona yote hata mwisho wa huduma yako. Kila jambo linalokusumbua  linamfikia kupitia maombi. Kupitia maombi unamwambia Mungu juu ya mahitaji yako yote na uhakikishe hutoki mpakan amekuambia nini kitatokea. Maombi ni utulivu binafsi wa kuongea na Roho juu ya huduma ili kupokea maono mapya, njia na mbinu mpya za kufanya huduma hiyo. Kubadilishana mawazo ili kuhakikisha lengo lililokusudiwa kupitia hiyo huduma linakamilika.

Wengi wanachanganya kati ya maombi na kukemea. Watu wengi hii imekuwa ni changamoto kubwa sana. Wanapoingia katika maombi wanaishia kumkemea shetani na wakati mwingine hata Mungu halafu wanaondoka bila kuongea na Mungu Roho Mtakatifu juu ya huduma walizopewa. Kukemea siyo sababu pekee ya kumfukuza shetani bali jambo kuu ni kuwa na ushirika na Roho. Usitumie muda wako mwingi kukemea. Ni ishara ya hofu na mashaka zinazotawala maisha yako. Kama unataka kuwa kuwa na ushirika na Roho kuwa na muda mwingi Zaidi wa kuomba yaani kuzungumza na Mungu. Kumueleza yaliyokusumbua au kukusibu, kumueleza unachohitaji.

Hauhitaji muda mwingi Zaidi na wake unaowahudumia. Unahitaji muda mwingi Zaidi na yule mwenye huduma. Ukiwa na muda mwingi sana na unaowahudumia utaishia kuwafahamu wao tu. Muda mwingi uwe katika kuomba. Muda mwingi katika ushirika na Roho. Fanya bidii Roho awe kipaumbele chako. Kadri unavyozidi kutoa muda kwake, na yeye ndivyo anavyozidi kutoa muda kwako katika huduma unayofanya. Utakuwa muda wako unauwekeza kwake ili yeye afanye katika utumishi wako. Hivyo ndivyo wale waliotembea na Roho walivyofanya. Waliomba. Hawakuishi maisha ya kukemea. 

Maombi ya Imani, maombi yenye nguvu, yenye matokeo yako katika ushirika na Roho. Na hapo ndipo siri ya kudumu na Roho ilipo. Wengi hawaombi ndiyo maana huduma hazina ufanisi. 

Mungu akubariki usikose sehemu ijayo, mshirikishe na mwingine.

Comments