UWEPO WA NCHI YA AHADI
Ni vigumu sana mtu kutoka kwenye utumwa na kwenda kwenye nchi ya ahadi kama hajui kuwa hiyo nchi ipo. Watu wengi wameishi maisha ya utumwani ambayo siyo ya kwao kiuhalisia kwa sababu hawajui kuwa kuna nchi ya ahadi kwa ajili yao.
Wanaweza kuendelea kuishi kitumwa japo wana asili ya kifalme na wanatakiwa kuwa wafalme. Wanaweza kuendelea kuteseka tu japokuwa mateso ni jambo la muda wala si maisha ya kila siku. Wanaweza kujiona hawana thamani kabisa kwa sababu hawaijui nchi ya ahadi kwa ajili yao.
Kujua uwepo wa kitu inakuumbia uwezo wa kuamini kukifikia hata kama ni hatua ngumu kuchukuliwa ili kukifikia hicho kitu. Usipojua faida ya kitu huwezi kupambana ili kukipata. Usipojua undani wa jambo huna nguvu ya kulipigania au kulitetea kwa sababu hauna uhakika wa kile unachokifanya au unachokipigania.
Watu wengi wanaishi katika maisha yaliyodumaa kwa sababu hawajui wala kutambua kuwa kuna nchi ya ahadi kwa ajili yao. Usipojua kitu hakuna maana pia ya uwepo wa kitu hicho maana hakitakufaidisha kabisa kwa sababu hutoweza kukishindania hata kidogo kwa kuwa hutokuwa na imani ya kukipata maana hicho ni kitu usichokijua .
Jaribu kutafakari kwa kina, jitazame kwa undani, hali uliyo nayo, maisha unayoyaishi, namna watu wanakutazama, jamii inavyokuchukulia au kukupa nafasi, namna hivyo ulivyo ni kwasababu hujagundua uwepo wa nchi ya ahadi. Utakapoundua uwepo wa nchi ya ahadi hautabaki vile ulivyo. Utapiga hatua zaidi kubadilisha uhalisia wa maisha yako ambao ni makusudi ya Mungu juu ya Maisha yako.
Umeendelea kuwa mtumwa kwa sababu ya kutokujua uwepo wa nchi ya ahadi. Yamkini wapo wanaojua lakini hawakukwambia ndiyo maana unaendelea kuwa vile ulivyo. Unaweza pia kuendelea kuishi maisha ya kitumwa ukijua kuwa hayo ndiyo maisha yako na ndiyo uhalisia wako na ndiyo hasa hatima yako.
Leo nataka nikujuze au nikukumbushe juu ya nchi hii ya ahadi ambayo ni kwa ajili ya kila mwanadamu katika ulimwengu huu. Nchi hii ya ahadi inajulikana kwa jina la:
UWEZEKANO WA KILA KITU
Na jina la nchi hiyo ndiyo hasa humaanisha namna uhalisia wake ulivyo. Ni nchi ambayo wananchi wake wanajua neno moja tu KILA JAMBO LINAWEZEKANA.
Ni watu wachache sana duniani ukilinganisha na watu wote duniani ambao wamefanikiwa kuishi katika nchi hii. Watu wa nchi hii ndiyo wale ambao tunasoma habari zao duniani kuwa walifanya au wamefanya na wanafanya mambo makubwa na ya kushangaza.
Katika nchi hii kila mwananchi nayao nafasi ya kuonesha kile kilichomo ndani yake ambacho kwa hicho Mungu alimuumba na kumfanya awe hai mpaka sasa. Katika nchi hii ya ahadi hakuna mpaka wa kufanya mambo yako. Hakuna neno HAIWEZEKANI. Kutokana na uhuru uliopo katika nchi ya ahadi kila mtu anaweza kufanya jambo la utofauti ambalo linakuja kuonekana duniani.
Jambo lolote unaloliona duniani lenye faida na la kushangaza limetokea katika nchi hii ya ahadi. Nchi hii imejaa wavumbuzi, watoa misaada, watu wenye ushawishi mkubwa n.k. watu wa nchi hii hawaamini kuwa fedha ndiyo kigezo hasa cha mafanikio ya mtu bali wao wanatumia kigezo kimoja tu UWEZEKANO WA KILA JAMBO.
Wanaamini kuwa jambo ambalo wewe unaona kuwa kwako haliwezekani kwao linawezekana. Na kwasababu hii wametatua matatizo mengi sana yanatoisumbua dunia tunayoishi. Wanapambana kuifanya dunia kuwa sehemu bora ya kuishi kama ilivyokusudiwa na Mungu.
Katika nchi hii kuna hazina ya kila kitu chenye faida ya kiroho na kimwili kwa mwanadamu. Mtu yeyote anapofanikiwa kuwa mwananchi wa nchi hii ya ahadi anaweza kuzitumia hazina zote hizo bila matata yoyote. Mtu anayeishi katika nchi hiyo anaweza kuja kufanya jambo lolote kubwa duniani kwa sababu hazina hizo zipo huku.
Katika nchi hii hakuna kuamini katika mambo madogo madogo bali kujua kuwa MAMBO YOTE YANAWEZEKANA. Hakuna kikwazo cha ugumu bali ugumu ndiyo daraja la kufanya makubwa.
Nchi hii ipo kabisa na ni kwa ajli ya wanadamu wote ulimwenguni wala siyo watu wa rangi fulani au kabila fulani. Ni kwa ajili yako ndugu msomaji uliyepata nafasi ya kusoma kitabu hiki.
Kwa watu wengi linaweza kuwa jambo la kuchanganya ufahamu, kujua kuwa kuna nchi ambayo yeye haijui iliyojaa hazina zote za maisha yenye furaha. Wanaona ni jambo lisilowezekana kabisa, halipo kabisa ni jambo la kuzusha au uongo tu.
Nataka utambue na kuweka hili akilini kuwa kuna nchi ya ahadi inayojulikana kwa jina la:
UWEZEKANO WA KILA KITU
Ukijua hilo itakusaidia sana kufika mahali ambapo nimekusudia kukufikisha ndugu msomaji. Utakapoanza kuumba ufahamu wa uwepo wa nchi hii utaona namna ambavyo utaona mabadiliko yakitokea katika maisha yako kupitia kitabu hiki.
Kinaweza kuwa kama chakula kigumu kumeza kwako lakini kimeze ili upate afya njema sana kwa ajili ya ustawi wako ndugu msomaji. Lichukue jina hilo kama lilivyo na uamini kuwa lipo. Ukifanya hiyvo itakuwa rahisi sana kwako kuingia katika nchi hiyo.
Unaweza kujiuliza kuwa nchi hii ipo mahali gani duniani ili uende ukaishi huko ukatumie hazina zilizofichika na ufanye mambo makubwa duniani. Unaweza kuanza kuchunguza katika ramani ya dunia kama jina hilo lipo. Unaweza kuutafuta ubalozi wa nchi hiyo ili ufanye utaratibu wa kwenda. Unaweza kutafuta taarifa za nchi hiyo mtandaoni ili ujionee mandhari ya nchi hiyo.
Jambo la ajabu ni kuwa nchi ya ahadi haipo mbali na wewe. Hauhitaji kwenda kutafuta ubalozi wake ulipo. Hihitaji kwenda kuitafuta kwenye ramani ya dunia, huhitaji kuitafuta mitandaoni. Nchi hii ipo na wewe, karibu yako zaidi kuliko unavyodhani. Nchi hii ya ahadi ipo NDANI YAKO.
Nchi hii inapatikana katika ulimwengu wa pili, yaani ndani yako wewe. Unaweza kushangaa hili lakini ni kweli na ufahamu hilo ndugu msomaji.
Nchi hii ipo ndani yako. Haipo mahali pengine. Watu wanaoishi katika nchi hii ni wale ambao wanaishi ndani yao. Kuweka hili sawa hebu tulitazame neno maisha katika lugha ya kingereza na tuchambue kila herufi tuone inaelezaje;
L – Living the
I – Inner to
F – Fill the
E – Earth
Ikiwa na maana ya kuishi kilicho ndani ili kuijaza dunia. Kwa maneno mengine ndani yako kuna mengi unatakiwa kuyaishi ili kuijaza dunia kwayo na ndiyo maana unaishi. Nchi ya ahadi ipo ndani ya kile mtu. UWEZEKANO WA KILA KITU upo ndani ya kila mtu. Nchi hii yeyote anaweza kuiishi kwa kuwa ipo ndani yake. Haiko mbali na yeye lakini anaweza kuwa mbali nayo kwa kutoishi kilichoko ndani yake.
Unaweza kudhani kuwa ni jambo la kushangaza au lisilo la kweli. Ni sawa na wana wa Israel siyo wote waliamini nchi hiyo. Lakini muhimu kujua kuwa wewe kutokuwepo katika nchi hiyo haimaanishi kuwa nchi hiyo haipo bali wewe ndiyo haupo katika nchi hiyo. Na hata kama ni haki yako kuishi lakini kama usipojua kuwa ni haki yako kuishi katika UWEZEKANO WA KILA KITU, unaweza kuishi pengine na ukaendelea kupita katika magumu bila kupata suluhu ya mambo mengi.
Hii ni nchi iliyojaa maziwa na asali. Ni nchi iliyojaa mafanikio yako. Ni nchi iliyobeba hatima ya maisha yako. UWEZEKANO WA KILA KITU umebeba kila kitu kinachokuhusu wewe. Ili kusudi lako litimie lazima uishi kwenye hii nchi. Hii nchi ni kama incubator ya kuatamia mayai ili yatotolewe.
UWEZEKANO WA KILA KITU unaweza kuatamia maono yako, malengo yako, ndoto zako. Unaweza kuhakikisha kuwa unafika kule unakotaka kufika. Nchi ya ahadi ipo kwa ajili yetu na ni muhimu tuishi kwenye hiyo nchi.
MUNGU akubariki, usikose sehemu ijayo.
Comments
Post a Comment
Thanks for your comment, God bless you!!!