NCHI YA AHADI - sehemu ya 4

 

NCHI YA UTUMWA

Katika sehemu iliyopita tumejifunza sana juu ya uwepo wa nchi ya ahadi. Pia ni muhimu tujifunze juu ya nchi ya utumwa. Nchi hii ni hatari sana. Unaweza kujiuliza maswali mengi kidogo kuhusu hili, ni nchi gani? Ikoje? Kina nani wapo? Hayo yote tutajifunza katika sehemu hii na utapata mambo ya msingi sana.

Kwanza kabisa ili tujenge msingi hebu tuangalie wana wa Israel walipotoka Misri kwenda Kanaani. Wengi walikufa njiani, unafikiri kwanini, japo walitolewa utumwani kimwili, bado katika nafsi zao walikuwa utumwani, bado katika fikra zao walikuwa Misri. Ndiyo maana katika kizazi chao ni wawili tu walioingia katika nchi ya ahadi ambao ni Yoshua na Kalebu. Hawa walipotoka utumwani waliuacha na utumwa wa nafsi.

Nchi hii ya utumwa kama vile ambavyo tumeangazia katika nchi ya ahadi, inahusika moja kwa moja na nafsi na fikra zetu. Wengi sana katika dunia yetu wapo katika nchi ya utumwa. Nchii hii ni mbaya sana. Lakini kabla hatujaangalia athari za nchi hii, tutazame nchi hii inaitwaje.

Nchi hii ya utumwa inajulikana kwa jina la

UKOMO WA UWEZEKANO

Nchi hii ni nchi ambayo imejaa watu wenye kuona ukomo katika uwezekano kama lilivyo jina lenyewe. Jina lake lasadifu yaliyoko katika nchi hiyo. Watu wa hii nchi wanaamini kuna mambo yanayowezekana na mambo yasiyowezekana. Watu hawa wana shida kubwa sana. Katika nchi hii unakosa mambo mengi sana mazuri ambayo mtu angeyapata katika nchi ya ahadi. Kuna mambo mengi na ni sharti la mtu kuamua kukubali kutolewa katika nchi hii. Na unatoka katika nchi hii kupitia maarifa ya Mungu kama haya unayojifunza. Kwa kweli wakati mwingine ni huruma sana kuona watu wakiendelea kuteseka katika hii nchi wakati uwezekano wa wao kutoka upo.

Na bahati mbaya mtu asipokuwa makini akiwa katika nchi hii ya UKOMO WA UWEZEKANO anaweza kuridhika na hali aliyonayo na mwisho wa siku akafa katika utumwa. Utumwa huu ni hatari, unaona kuwa wewe ni huru, wewe ni mzima lakini kumbe umeshatekwa muda sana. Na hapa mtu anaweza kufa kabisa wakati sisi tunamuona anatembea.

Hatari ni kuwa mtu anakuwa mtumwa ilhali anaonekana huru. Mtu anakuwa amekufa ilhali anaonekana yuko hai. Mtu akiendelea kudumu katika nchi hii anaweza kufa na akaendelea kutembea mtaani. Ndiyo maana kuna watu wamekufa wakiwa na miaka 21 au 25 na kuzikwa wakiwa na miaka 65 hadi 80 au hata 90. Ajabu sana mtu asipokuwa makini hawezi kujua kuwa yeye amekufa.

Hakuna jambo baya sana kama kuona kuwa kuna mambo hayawezekani. Kuona kuwa kuna mambo ni magumu tu hayawezi fanyika . Kumbuka kuwa kama kuna jambo ambalo mwanadamu amelitenda basi kuna mwanadamu mwingine anayeweza kulitenda pia. Unaona kuwa, kuwa na kitu Fulani haiwezekani, kuna watu wanatakiwa kuwa na hivyo vitu, wewe haustahili. Hayo ni mambo mabaya sana na yanamkera Mungu sana. Amemuumba mwanadamu akijua kuwa anaweza kufanya vitu bila kujali ni magumu au la. Ni muhimu kujua kuwa siyo kwa kwamba mambo hayawezekani bali hatujui namna ya kufanya. Ugumu wa kitu ni kikwazo sana kwa raia wa nchi hii.

Na raia wa nchi hii wana tabia yao moja ambayo ni ya kipekee kwao. Tabia hiyo ni KUJIHURUMIA na kupenda KUHURUMIWA. Watu hawa wanapenda uwaone kuwa wapo mahali pagumu ili uwahurumie vya kutosha. Wanapenda kujihurumia. Hawataki kuichukua hatari.

Hebu tuzichangue kwa sehemu sifa za raia hawa

·        Kupenda kuhurumiwa na kujihurumia

Kama ambavyo tumeangalia hapo juu. Kuwa hawa watu wanapenda kuwahurumia. Ikitokea ukiwahurumi hurumia watakuona kuwa wewe ni mtu wa maana sana kwao bila kujua kuwa wanapotea. Maneno yao ni ya kutia tia huruma utafikiri kuwa wao ni viumbe dhaifu sana kuliko wengine hapa duniani. Utadhani wao ni viumbe wengine siyo wanadamu kama sisi, na kuwa mambo tunayoyafanya sisi wao hawajaumbwa kuyafanya.

·        Kuendeshwa na hofu

Raia hawa wanatawaliwa sana na hofu. Hasa hofu ya kuchukua hatua ya kwanza na hofu isiyojulikana. Watu hawa ni watu wa ajabu sana. Kila kitu wanaogopa. Wakianza kitu chao ni rahisi kukiacha maana wanaogopa hasara au hatari. Ukiona mtu anafanya biashara na anaogopa hasara ujue ni raia wa nchi hii na itakuwa kazi ngumu kwake kufanikiwa katika biashara yake. Hofu ni kuona kuwa jambo unalolifanya ni hatari. Wakidhani kuwa kule wanakobaki ni salama kumbe ndiyo hatari Zaidi.

·        Kukuza mambo

Raia wa nchi hii wanapenda sana kukuza mambo. Ukiwasikiliza sana unaweza kuona wanachosema ni kweli na ni kikubwa sana. Kuna wakati usipokuwa makini unaweza kuchukuliwa na ufahamu wao hatari. Mambo madogo madogo wanayaona ni makubwa sana. Inafika mahali hawataki hata kuchukua hatu kisa mambo wanasema ni magumu.  Hizo ni baadhi ya tabia zao za msingi au kuu. 

Usikose sehemu ijayo na Mungu akubariki sana.

Comments