NCHI YA AHADI - sehemu ya 5

 

ATHARI ZA NCHI YA UTUMWA

Nchi hii ya utumwa imeleta athari mbaya sana kwa maisha ya watu hasa wale raia wa nchi hii. Nchi ya utumwa ni hatari sana katika maisha ya ujumla ya mwanadamu. Hebu tuzitazame athari au matokeo ya kuishi katika hii nchi, ambayo kwa namna moja ama nyingine kama wewe ni raia wa nchi hii ni dhahiri kuwa hautakubali kuendelea kubaki.

·        Kushuka kwa mamlaka ya mwanadamu

Mungu aliumba watu ili watawale kama ambavyo tumejifunza katika somo la ASILI 7 ZA MWANADAMU. Lakini nchi hii inaondoa mamlaka ya mwanadamu. Nchi hii inakufanya uwe tegemezi na kuamuliwa na mazingira hasi yatakayoleta mambo mabaya katika maisha yako. Mamlaka ya mwanadamu yanaposhuka uwezo wa maamuzi juu ya mazingira unahama kutoka kwenye upande chanya kwenda hasi, kwa sababu kutofanya maamuzi sahihi nayo ni maamuzi pia. Mamlaka yanapoondoka yanakufanya upoteze uhalisia wa uwepo wako.

·        Kutotimiza kusudi la uwepo wako

Ni muhimu kujua kuwa haupo kwa bahati mbaya au kama ajali. Katika nchi hii ya utumwa inakupelekea kutotimiza kusudi la uwepo wako. Itakupa mipaka ya utekelezaji wa mambo makubwa Mungu anayaotaka uyafanye katika maisha yako.  Unapoacha kutimiza kusudi la uwepo wako ni hatari sana na jambo baya. Kwa sababu inakufanya kumkosoa Mungu kuwa alikosoa kukupa kusudi alilokupa uje ulifanye.  Ni hatari sana kumfanya Mungu muongo.

Hii ni kwa sababu utakuwa na woga wa kufanya maamuzi magumu na kufanya mambo makubwa katika maisha yako. Kuogopa kuchukua hatua ya kwanza. Kutotaka kuwa na nia ya kufanya vitu chanya.

·        Kukwamisha mabadiliko chanya

Ikiwa utaogopa kufanya vitu kutokana na kuwa waoga ni raia wa nchi hii utajikuta unakwamisha mabadiliko chanya. Hii ni kwa sababu kama unaogopa kufanya vitu chanya moja kwa moja unajipeleka kufanya vitu hasi. Hivyo utajikuta unaruhusu kuleta mabadiliko mabaya na kuwa adui wa mapenzi ya Mungu Anayetaka watu wafanye mambo mazuri ya kimaendeleo katika dunia yetu.

Watu wenye hofu ya kuchukua hatua katika mambo yao, wanapelekea kutofanya mambo sahihi, kwa nyakati sahihi na kadhalika. Hii itadumaza maisha na kuharibu kabisa maisha ya mwanadamu.

·        Kupoteza Imani kwa Mungu

Unapoogopa kufanya vitu chanya vya kimaendeleo kama matokeo ya kuwa raia wa nchi ya utumwa, unajikuta katika mazingira ya kukosa Imani kwa Mungu. Mungu anataka tufanye mambo mazuri, na sisi tunaogopa kuyafanya kwa kuogopa vikwazo tunavyokutana navyo. Hii ni kumaanisha kuwa Mungu aliyeona tunaweza kufanya mambo hayo yote mema ni muongo. Ikiwa tunamfanya yeye muongo tunaamini kuwa adui ni sahihi. Hii inatufanya kupoteza nafasi ya kusaidiwa na Mungu katika maisha yetu na kujikuta katika maisha magumu nyakati zote za maisha yetu.

Mambo ili yatokee katika maisha ya mwanadamu yanadai Imani, inapokosekana Imani katika Mungu, msaada wa Mungu hautapatikana kwake. Na msaada wa Mungu ukikosekana maisha ni mabaya, hayafai hata kuyaishi.

·        Kukwamisha ustawi wa maisha ya mwanadamu

Mtu anapoishi katika nchi hii, inayotawaliwa na hofu, anapata wakati mgumu sana. Ni ngumu kwake yeye kustawi katika jambo lolote. Maisha yatakuwa magumu sana. Maisha yenye huzuni na masikitiko. Maisha ya majuto. Wazee wengi wanaumia na kujutia maisha waliyoyaishi wakiwa vijana na kukubali kuendeshwa na hofu na kujikuta katika nchi ya utumwa. Hakutakuwa na hali nzuri katika maisha ya mwanadamu. Kila jambo litakuwa chungu. Muda wote ni manung’uniko tu na kulaumu wengine kwa makosa yako binafsi.

·        Kuharibu mahusiano baina ya Mungu na mwanadamu

Mtu anayeishi katika nchi hii, yanapotokea mambo mabaya kila nyakati na kutoona namna ya kutatua tatizo hilo. Katika mazingira haya mwanadamu anaweza kuona kuwa Mungu ni mbaya. Kuona kuwa kwanini hamsaidii. Hiyo yote inapelekea uvivu wa maombi au kuwa mtakatifu na kuwa karibu na Mungu.

Mahusiano yetu na Mungu yanajengwa na maombi na utakatifu. Kama tukiona Mungu kuwa hafanyi kitu, na kwa kuwa uvivu unatawala katika hii nchi ya utumwa unajikuta kukwepa majukumu yako na kumsingizia yeye kuwa hakufanyii na kutotaka hata kumsikiliza Mungu. Kukosa uhusiano na Mungu inakwenda kuharibu mtiririko wa msaada na wa Baraka kutoka kwa Mungu.

·        Kukwepa majukumu na kukosa haki za msingi

Watu wenye hofu ni rahisi sana kutotimiza majukumu yao. Wanapenda kujihurumia na wanatafuta kuhurumiwa. Watu hawa wanakwepa majukumu yao. Mfano mtu kila siku hana kitu cha kutoa kwa wengine. Anakwepa majukumu. Anapokwepa majukumu moja kwa moja unajikuta katika mazingira ya kukosa haki zako kwa Mungu.

Mungu atakupa haki zako, ikiwa utajitahidi kutimiza majukumu yake. Ni muhimu kujua kuwa hautapata haki zako ikiwa utakwepa majukumu yako. Kuishi katika nchi ya utumwa kunakufanya uone kuwa kuna mambo usiyoweza kufanya. Na huku kuona vitu haviwezekani itasababisha kutotimiza majukumu yako. Na hii itakupelekea kukosa msaada na haki zako kutoka kwa Mungu.

Mwisho,

Kutotimiza majukumu itapelekea utegemezi kwa watu. Siyo lazima kutegemea watu mpaka kupita kiasi lakini kama usipotimiza wajibu wako itakuwa rahisi kuwa tegemezi kwa watu wengine. Hii itapelekea kuharibu uhusiano wako na wengine. Kwa sababu kuna wengine wakikuona tu wanatafuta kona za kukimbia.

Usikose sehemu inayofuata shirikisha na wengine na Mungu akubariki sana.

Comments