YALIYOMO NJIANI
Mtu anapokuwa ametoka katika nchi ya utumwa kinachofuata ni mchakato wa kuelekea nchi ya ahadi. Kuelekea nchi ya ahadi ni njiani. Njiani kuna vitu mbalimbali vya kuzingatia. Maana la sivyo unaweza kurudi tena utumwani.Mchakato huu yaani yaliyomo njiani ni muhimu sana kwa kila mtu anayetaka kuwa raia katika nchi ya ahadi, nchi ya UWEZEKANO WA KILA KITU. Ni mchakato muhimu sana. Na yeyote anayetaka kufika nchi ya ahadi. Anayetaka kufika katika uhuru wa kifikra. Anayetaka kufika katika UWEZEKANO WA KILA KITU. Ni muhimu kujua njiani kuna nini???
Huwezi kupita njia yoyote bila kukutana na kitu chochote katika njia hiyo. Kila njia unayopita kuna kitu hapo. Kwa sababu njia ni mchakato unaotutoa katika utumwa na kutupeleka katika uhuru. Hakuna mchakato usiokuwa na kitu. Unaposema mchakato unamaanisha mfuatano wa vitendo kadha wa kadha ili kukamilisha jambo Fulani linalotarajiwa. Hivyo katika njia yaani mchakato kuna mambo kadha wa kadha ya muhimu ili ufike nchi ya ahadi.
Pia kabla ya kuangaliza mambo gani yapo katika njia ya kuelekea nchi ya ahadi, ni muhimu tutazame umuhimu wa haya mambo ambayo yapo katika njia. Ikiwa tutajua umuhimu wake, itakuwa rahisi kufika tunapofika salama na kutorudishwa na chochote nyuma maana tunajua nini tunapata katika huo mchakato.
Faida au umuhimu mkuu katika mchakato wa kuelekea nchi ya ahadi, ni jambo moja, yaani MAFUNZO WEZESHI KWA ATAKAYEISHI KATIKA NCHI YA AHADI. Mchakato huu unakupa mafunzo muhimu yatakayokuwa nyenzo muhimu sana ya maisha katika nchi ya ahadi.
Kumbuka unaenda katika nchi ya UWEZEKANO WA KILA KITU. Hii inamaanisha mchakato huu unashughulika na ufahamu wako kupitia mambo yapatikanayo katika mazingira yako. Mambo mbalimbali yatatumika kama nyenzo ya mafunzo kwako wewe ambaye unatamani kuwa raia wan chi ya UWEZEKANO WA KILA KITU.
Kwa sababu jambo hili ni la kiufahamu linategemea kiwango cha vile unajitoa kujifunza, wepesi wako wa kujifunza na kukubali mafundisho hayo. Kiwango chako cha kuonesha kuwa umebadilika kwa kuanza kuyafanyia kazi yale ambayo umejifunza. Ndiyo maana katika huu mchakato kuna watu watabaki.
Mtu yeyote asipokuwa makini anaweza kurudi katika utumwa. Katika huu mchakato ni rahisi sana kurudi utumwani kwa sababu bado unakuwa na mifumo ya uraia wa utumwani katika maisha yako hivyo katika mchakato umakini ni muhimu sana na haukwepeki.
Mambo ya kuzingatia katika mchakato huu wa mafunzo ya kuelekea uhuru wa kifikra au kuelekea katika UWEZEKANO WA KILA KITU ni kama ifuatavyo:-
· Akili iliyo wazi (open mindset) yaani akili iliyo tayari kupokea mafunzo.
Kama hautakuwa tayari kupokea mafundisho hayo utapinga kila kitu na utarudi nyuma kirahisi. Ikiwa hautaamua kuweka wazi upokeaji wa mafunzo ni rahisi kubaki na yale yaliyo katika ufahamu wako ambayo yamekufanya uishi utumwani na hayo yatakurudisha utumwani.
Akili iliyo wazi ndiyo kitu muhimu hapa. Katika mafunzo utayari wa kupokea ndiyo unaofanya hayo mafunzo yawe na maana au yawe na matokeo kwa mhusika. Mafunzo hayatapata nguvu mpaka utakapoyapa nafasi. Hivyo kujiweka wazi kwa mafundisho kunakuwezesha kufika unapotakiwa kufika.
· Kutojali njia ya mafunzo bali kilichopo ndani ya mafunzo.
Wakati mwingine njia inayotumika katika mafunzo inaweza isiwe rahisi kama unavyotarajia. Kama akili yako ikijikita katika njia ya mafunzo na siyo kusudi la mafunzo ni rahisi kukimbia mapema ikiwa zitatumika njia ambazo zitakusumbua kidogo.
Ndiyo maana wanajeshi wengi wananakimbia jeshini, siyo kwa sababu hawataki kuwa wanajeshi, bali ni kwa sababu hawaangalii nini wanakipata katika mafunzo bali wanaangalia njia zinazotumiwa katika mafunzo. Lakini wale ambao wanaangalia nini ndani ya mafunzo inakuwa rahisi kwao kuendelea kuvumilia.
Kuangalia nini kilichomo katika mafunzo kunakusaidia kuwa mvumilivu. Bila kujali njia gani itatumika, ila wewe unataka kupata kitu chako. Haikusumbui gharama utakayolipa, bali kinakusumbua kile utakachokipata. Ukiwa na mtazamo wa aina hii ni rahisi kutoyumbishwa na chochote hasa maneno ya raia wenzako wa kule utumwani ambao wao wanataka uwe na hali kama zao. Wanaweza kuleta maneno maneno lakini kama utaziba masikio yako utamaliza mafunzo salama na kupata ulichostahili kupata.
· Kufumba macho yako au kukaza macho mbele tu.
Hapa namaanisha kuamua liwalo na liwe ila wewe unataka kufika katika nchi ya ahadi. Hujali watu watasemaje. Hujali mafunzo yatakuwaje. Hujali chochote isipokuwa kupambania kumaliza mafunzo na kupata kitu kitakachokusaidia kufika nchi ya ahadi.
Huku ni kuanza kuona uwezekano wa kila kitu. Kwa sababu kuamua liwalo na liwe kunakupa uhakika kuwa unajua uendako na kile utakachokipata. Kama utaanza kuwa na mtazamo wa aina hii ni rahisi kuvuka kila daraja la mafunzo.
Kuna wakati unaweza kukutana na madaraja katika mafunzo yako. Ambayo kazi yake ni kukutoa pale ulipo na kukupeleka hatua nyingine. Madaraja mengine ni marefu na makubwa kiasi kwamba yanaweza kukufanya uhisi kizunguzungu na kujikuta umeanguka. Hivyo kuna maeneo utatakiwa kufumba mamcho nap engine kukaza macho yako ili ufike salama.
Ni suala la maamuzi magumu. Ni suala la kutojali hatari bali kujali matokeo. Ni suala la kuamua kutosumbuliwa na chochote kukurudisha nyuma bali kile unataka kukipata.
· Kuwa mwepesi kujifunza
Hapa tunazungumzia kujijengea uwezo wa kukubali kile unachojifunza kwa haraka. Kumbuka ni rahisi sana kukataa kujifunza kama hujaamua kujifunza. Lakini kuamua kujifunza kunadai kuwa mwepesi. Hii inamaanisha mafunzo yanakutaka uwe na uwezo binafsi wa kupokea na kuyafanya uliyojifunza ya kwako.
Kumbuka muda utakaokaa katika mafunzo unategemeana na vile ambavyo wewe unakuwa active (hai) katika mafunzo hayo. Ikiwa utasimama na kupokea mafunzo kwa na kuyafanya yako kwa wakati itakusaidia kutotumia muda mwingi katika mafunzo.
Kama unataka kutumia muda mchache katika mafunzo amua kufundishika. Kuwa mtiifu katika mafunzo. Kuwa msikilizaji katika mafunzo. Hitaji msaada wa wale waliopitia mafunzo na wakapita kwa ushauri na mawazo yao ambayo yatakusaidia kujifunza kwa haraka. Kama utafanya hivyo itakuwa rahisi kwako. Kama ukifanya hivyo utafika nchi ya ahadi kwa wakati na utafurahia mengi katika nchi ya ahadi. Wengi wetu wanafaidi uzuri wa nchi ya ahadi wakiwa wamezeeka na hii ni mbaya sana. Haitakiwi uzeeke ili ufaidi mema ya nchi ya ahadi. Ila ni maamuzi yako kuingia katika nchi ya ahadi ukiwa umezeeka.
· Utayari wa kufanyia kazi unayojifunza.
Ikiwa utakuwa na utayari wa kufanyia kazi, ni rahisi kuhitimu mafunzo kwa vitendo na kuingia katika nchi ya ahadi kwa wakati. Kumbuka mafunzo yoyote ili yawe na athari katika maisha yako ni muhimu kuzingatia vitendo ili kuonesha pia kuwa umejifunza.
Unapoanza kufanyia kazi yale unayojifunza unaanza kuishi nchi ya ahadi ukiwa njiani. Hii itafanya mafunzo yako kuwa matamu. Kumbuka wale wapelelezi walioenda kupeleleza ile nchi walirudi na matunda ya nchi ile. Kama unajifunza na unafanyia kazi unaanza kula matunda, kunywa maziwa na asali iliyo katika nchi ya ahadi.
Jifunze kujifunza kwa vitendo Zaidi na si kwa maneno kuwa umejifunza. Onesha kuwa umejifunza kwa kubadilika katika mwenendo wa maisha yako. Kubadilika vile unawaza. Kubadilika vile unasema na vile unatenda. Huwezi kusema umejifunza ikiwa utaendelea kusema yale yale uliyozoea kuyasema katika utumwa, kufanya yaleyale ya utumwani.
Ni muhimu sana kuzingatia jambo hilo. Kwani ni kipimo cha mwisho cha kutoa ruhusa kwako kuingia katika nchi ya UWEZEKANO WA KILA KITU. Huwezi kuingia kama ufanisi wako haujaridhisha. Hauwezi kuingia kama bado unafanya yaleyale. Jifunze kuwa mtu wa vitendo. Na kadri unavyokuwa mtu wa vitendo ndivyo ambavyo ufahamu wako unaanza kukubaliana na maisha ya nchi ya UWEZEKANO WA KILA KITU. Na hii inakuwezesha kuishi katika nchi ya ahadi. Hii ndiyo tiketi. Hii ndiyo barua ya kukufanya uwe raia. Hiki ndiyo kigezo kinachotumika kuruhusu watu kuwa raia katika nchi ya UWEZEKANO WA KILA KITU.
Mungu akubariki sana, endelea kufurahia sehemu zijazo na masomo mengine. Uwe na wakati mwema.
Comments
Post a Comment
Thanks for your comment, God bless you!!!