Karibu katika muendelezo wa YALIYOKO NJIANI, kama haukupata nafasi ya kujifunza sehemu iliyopita, rudi nyuma hapo ujifunze na upate muelekeo wa nini hasa tunajifunza. Mungu akubariki sana kwa kuendelea kujifunza.
Mafunzo haya yapo katika namna (sehemu) mbili kuu. Ambazo ndizo msingi hasa wa mchakato huu. Namna (shemu) hizo ni:-
A Mafunzo juu ya kuondoa mifumo ya nchi ya utumwa
B Mafunzo ya kuleta mifumo ya nchi ya ahadi.
A. MAFUNZO JUU YA KUONDOA MIFUMO YA NCHI
YA UTUMWA
Hii ni sehemu ya kwanza ya mafunzo utakayoyapitia katika mchakato wa kuelekea nchi ya ahadi. Nchi ya uhuru wa kifikra. Nchi ya UWEZEKANO WA KILA KITU.
Katika sehemu hii utajifunza kuachana na mifumo yote ya maisha ya utumwa. Kumbuka hata mtu anapotaka kuwa raia wan chi Fulani, ni lazima akane uraia wa nchi yake kwanza. Huu ndiyo mchakato wa kukana uraia wan chi ya utumwa. Hapa ndipo unaoonesha kuwa hutaki kuwa raia wa nchi ya UKOMO WA UWEZEKANO. Hapa ndipo unapoonesha nia yako ya dhati ya kuachana na utumwa wa kifikra.
Katika sehemu hii utajifunza kuachana na mifumo yako ya kufikiri, kusema na kutenda ambayo ulikuwa nayo katika nchi ya utumwa. Hapa unaachana na vile ulikuwa zamani. Kumbuka huwezi kuwa mtu mpya ikiwa utaendelea kushikamana na mienendo yako ya zamani. Huwezi kuwa mtu mwingine wakati huohuo unaendeshwa na mifumo iliyokuendesha zamani.
Hakuna mabadiliko ikiwa hautaamua kubadilisha mifumo yako ya maisha. Hutabadilika mpaka utakapoamua kubadilika kwa vitendo. Kumbuka mafunzo haya ni kwa vitendo. Hakuna mtu utakayemuona anakuletea vitabu vya kujifunzia. Hakuna mtu atakayekuletea maelezo. Ni wewe unajifunza katika yale yaliyomo njiani. Ni wewe kujifunza katika hayo unayoyaona njiani.
Kumbuka mafunzo hayo yatafanyika kupitia milango mitano ya fahamu, mahitaji yako (haki zako) na wajibu wako. Hapa utakutana na mambo mbalimbali ambayo yapo katika mambo hayo matatu. Kwa hiyo ni jukumu lako sasa kuendana na hali utakayokutana nayo katika mafunzo.
Mawazo yako ya zamani yatatakiwa kuchukuliwa nafasi na mawazo mengine. Maneno yako yatatakiwa kuchukuliwa nafasi na mengine. Matendo yako yatatakiwa kuchukuliwa nafasi na mengine. Kumbuka kuwa unapotaka kuacha kitu Fulani ni lazima nafasi yake ichukuliwe na kitu kingine. Mfano nafasi ya nchi ya utumwa ni lazima ichukuliwe na nchi ya ahadi.
Kupitia mambo mbalimbali utajifunza kuacha mambo yako ya zamani. Kumbuka mtu ambaye unatakiwa kuwa bora Zaidi yake ni yule ambaye ulikuwa jana. Hutakiwi kupambana kumpita mwingine. Bali unatakiwa kupambana kumpita yule ambaye ulikuwa jana. Hivyo ni lazima ujifunze kumuacha yule uliyekuwa jana. Hautakuwa mwingine mpaka umemuacha yule wa jana.
Hivyo unatakiwa kuamua kabisa kupita hatua hii. Amua kuuacha utu wa kale. Utu wa mipaka katika uwezekano wa vitu. Kuona vitu Fulani haviwezekani. Amua kutoka huko. Amua kuona kivingine. Achana na mawazo ya kushindwa shindwa. Achana na mawazo ya kufelifeli. Achana na mawazo kuwa huwezi kuwa na ndoa nzuri. Achana na mawazo kuwa huwezi kufanikiwa katika chochote. Amua kubadilika kabisa na INAWEZEKANA KUBADILIKA UKIAMUA.
B. MAFUNZO JUU YA KULETA MIFUMO YA NCHI
YA AHADI
Hii ni sehemu ya pili ya mafunzo yaliyoko katika mchakato wa kuelekea nchi ya ahadi. Hapa unajifunza mifumo ya maisha ya kule katika nchi ya ahadi. Kumbuka kila nchi ina mifumo yake ya maisha yake. Hauwezi kuishi katika nchi ya ahadi ukiwa na mifumo ya kule utumwani. Hauwezi kuishi katika UWEZEKANO WA KILA KITU ikiwa una mifumo ya maisha ya MIPAKA AU UKOMO WA UWEZEKANO WA VITU.
Katika sehemu hii ndipo unapogeuzwa kikamilifu kuwa mtu mwingine. Hapa unafundishwa kanuni za maisha ya ile nchi unayotaka kwenda kuishi. Hapa unajifunza namna zote zitakazokusaidia.
Hapa utajifunza namna ya kudai na kupata haki zako. Hapa utajifunza kuwajibika. Hapa utajifunza kutawala milango yako mitano ya fahamu kukusaidia kupata taarifa ya habari ya nchi ya ahadi. Milango mitano ya fahamu ndiyo nyenzo za kupata taarifa mbalimbali. Utajifunza namna ya kutawala milango hii.
Pia hapa utajifunza kutawala mfumo wako wa kufikiri. Utajifunza vitu gani unaruhusiwa kufikiria na vitu gani ni marufuku kuvipa nafasi katika ufahamu wako. Kumbuka kuwa nchi hii ya ahadi makazi yake ni katika nafsi zetu. Ipo ndani yetu. Hivyo kama tunataka kuishi huko ni lazima tutawale kufikiri kwetu maana ndiyo hutawala au hutupa nafasi ya kuishi huko. Ukibadilika jinsi unavyofikiri utabadilika jinsi uanvyoishi.
Vilevile, utajifunza kubadili mfumo wako wa maneno na mazungumzo. Kumbuka hata maandiko matakatifu yamesema mambo mawiliya msingi sana. La kwanza mtu huyanena yaujazayo moyo wake. La pili msidanganyike mazungumzo mabaya huharibu tabia njema. Unaweza kuona kuwa ni muhimu sana kuangalia jinsi unavyonena. Pia mahali pengine pameandikwa kuwa mauti na uzima vipo katika uwezo wa kinywa. Ndiyo maana hata Yakobo anasema mtu atakayeweza kutawala kinywa chake basi maisha yake ameyatawala.
Kumbuka maneno unayosema yanatafsiri kile unakiwaza. Pia maneno yana nguvu ya kuumba vitu katika maisha yako. Hata wewe ulivyo ni matokeo ya maneno ambayo umekuwa ukiyatamka siku kwa siku juu yako mwenyewe. Lazima ubadili mfumo wako wa kusema. Kama usipobadili hautaweza kuishi huku. Badili maneno hasi kwa kusema maneno chanya. Mfano kuna tabia hazitaondoka katika maisha yako ikiwa utaendelea kukiri kila siku kuwa ni ngumu na haziwezi kubadilika. Ukibadilisha maneno yako kuna uwezekano wa kubadilisha matendo na maisha yako.
Pia unatakiwa kubadili mifumo yako ya utendaji. Badili matendo mabaya kwa mema. Badili uvivu kwa bidii. Vitu vinawezekana kufanyika. Weka nia ya kufanya. Amua kufanya na chukua hatua ya kufanya. Yale uyawazayo na kuyasema pia kama yasipoonekana katika vitendo hayana maana kuyawaza wala kuyasema. Kumbuka vitendo vinaongea Zaidi ya maneno.
Badili matendo yako. Badili yale uliyokuwa ukiyafanya katika nchi ya utumwa kwa yale unayotakiwa kuyafanya katika nchi ya ahadi. Inawezekana kabisa kufanya hivyo. Badili matendo yako. Badili mienendo yako hasi kwa mienendo chanya. Kama uliweza kuwa na mwenendo mbaya basi unaweza kuwa na mwenendo mzuri. Unaweza kubadilika na wewe ndiyo mwenye jukumu la kubadilika ili mambo yabadilike.
Hii ndiyo hatua ya kuukubali uraia wa nchi unayotaka kuishi. Ikiwa katika sehemu ya 1 ya mafunzo ni kuukata uraia wa nchi ya utumwa basi katika sehemu hii unaukubali uraia wa nchi ya ahadi. Unakubali uraia huu kwa fikra zako, usemi wako na mwenendo wako. Ndiyo maana Paulo anamuasa Timotheo kuwa kielelezo katika Usemi na Mwenendo. Kila nchi ina usemi wake. Kila nchi ina mwenendo wake.
Pamoja na kwamba nchi ya ahadi ipo katika nafsi zetu. Ipo ndani yetu. Na maisha yake yanaanzia katika fikra zetu. Lazima katika ulimwengu wetu wa kawaida zitokee athari Fulani. Lazima maisha yako ya mwilini yaathiriwe na maisha ya nchi ya ahadi iliyoko ndani yako. Hapo ndipo utakapotofautishwa na raia wa nchi ya utumwa. Kumbuka tunaoishi mwilini, tuna uraia labda wa utumwani au wa nchi ya ahadi. Hivyo maisha yetu yataakisi uraia wetu na hilo ndilo jambo la msingi la kuzingatia.
Tumejifunza sehemu mbili za mafunzo. Na tumejifunza kuwa mafunzo hayo yamelenga kubadili maeneo matatu ya msingi
· Fikra zetu
Hapa tutajifunza kufikiri kama raia wa nchi ahadi. Na ni muhimu kwa sababu pia nchi ya ahadi tunayojifunza hapa ipo katika nafsi zetu. Hivyo tutapitia mafunzo yatakayotufanya tuwe raia halali wa nchi ya UWEZEKANO WA KILA KITU
· Usemi wetu
Hapa tutajifunza kubadili mazungumzo yetu na maneno yanayotawala vinywa vyetu. Tutajifunza ustaarabu wa kuzungumza wa nchi ya ahadi. Tutajifunza namna ambavyo raia wa nchi ya ahadi anatakiwa kukiri juu ya maisha yake. Tutajifunza kuondokana na usemi hasi ambao huharibu tabia na mwenendo wetu. Tutajifunza jinsi itupasavyo kunena na kuwa na hekima ya nchi ya ahadi.
· Mwenendo wetu
Hapa tutajifunza tabia mbalimbali zitakazotuwezesha kuishi katika nchi ya ahadi. Kanuni mbalimbali zisizokwepeka ili kuishi katika UWEZEKANO WA KILA KTIU. Tutajifunza kanuni mbalimbali kama vile, kanuni ya utoaji, bidii, uvumilivu, ujasiri, upendo na nyingine nyingi za muhimu.
Tabia na mienendo yetu hutupa nafasi muhimu za kufaidika na nchi ya ahadi. Tutajifunza kuwajibika. Tutajifunza namna bora ya kupata haki zetu kama raia. Tutajifunza namna bora ya kufanikiwa na katika hali hiyo tutaanza kufurahia maisha ya kuwa katika nchi ya UWEZEKANO WA KILA KITU.
usikose sehemu ijayo
Comments
Post a Comment
Thanks for your comment, God bless you!!!