NCHI YA AHADI - sehemu ya 14

 Karibu tena katika sehemu nyingine ya somo letu, kumbuka kila sehemu ina umuhimu wake, hivyo hakikisha umejifunza sehemu iliyopita kabla ya inayofuata ili upate kitu kamili.

Baada ya kujifunza umuhimu wa mafunzo hayo, na mambo ambayo yatakuwepo katika mafunzo. Ni vizuri pia tuangalie ni njia gani ambazo zinaweza kutumika kwako wewe ili kujifunza. Hapa tutaangalia njia ambazo mara nyingi zinatumika katika mafunzo.

Lakini hata hivyo, njia hizo zimewekwa katika jambo kuu moja tu, MITIHANI.

Mafunzo haya yapo katika mfumo wa mitihani na changamoto. Zingatia kuwa kama maisha yetu ni tofauti hivyo kila mtu atakuwa na karatasi yake ya maswali. Hautakiwi kuiga majibu ya mtu. Lakini unatakiwa kujifunza njia akiyotumia kupata majibu yake.

Ikiwa kuna mitihani, kuna majibu. Mitihani inaweza kuja kwa namna mbalimbali ambazo hutofautiana baina ya mtu na mtu, lakini itabaki kuwa mitihani. Mwingine anaweza kukutana na changamoto ya ndoa, mwingne uchumi, mwingine magonjwa, mwingine elimu na kadhalika. Katika magumu yote hayo ni muhimu kupambana tu na kuendelea. Na katika eneo hili tutajifunza kanuni kuu moja ya msingi sana isiyokwepeka ikiwa tunataka kufika tunaotaka kufika

Kanuni hiyo ni:-

KANUNI YA USHINDI

Hii ni Kanuni ya muhimu sana ambayo kila mtu aliyepo katika mitihani ni lazima ajifunze. Kumbuka kanuni hii unatakiwa uitumie  ili kukupa nafasi ya kumaliza mafunzo salama na kuingia katika nchi ya ahadi. Mungu alikuumba uwe juu ya vyote hivyo inamaanisha uwe mshindi katika kila kitu. Biblia inaposema katika Mwanzo 1:28 kuwa mkaitiishe na katika lugha ya kiebrania neno hili linasomeka hivi radad likiwa na maana ya to conquer  yaani kushinda kwa lugha ya Kiswahili. Hivyo basi Mungu alituumba ili tushinde juu ya kila kitu.

 

Ushindi ni kuwa juu ya upinzani wote. Kuufanya upinzani ukose nguvu yoyote. Kuondoa mamlaka iliyopo na kuchukua hatamu. Kumuangusha adui. Hii inamaanisha kuwa hakuna kitu kinaweza kusimama mbele yako kikaendelea kusimama. Isipokuwa ukikiruhusu kiendelee kusimama mbele yako. Kwa maneno mengine ushindi katika maisha unaamuliwa na mwandamu bila kujali mazingira yanasemaje.

Ushindi ni wazo, ushindi ni fikra zako wewe. Vile unavyojiona mbele ya adui yako. Vile unavyojitazma mbele ya jambo linalokusumbua. Haukuumbwa kushindwa lakini unaweza kushindwa ukiamua kushindwa ni wewe tu. Ni maamuzi yako kushindwa au kushinda katika jambo lolote lile maishani. Hakuna jambo lisilowezekana isipokuwa wewe uwe hauwezekani mambo utayaona hayawezekani. Hakuna kitu cha kukung’oa katika madaraka yako mpaka umeamua kikung’oe.

Hii ni kanuni muhimu sana ambayo lazima uitambue na uishi nayo maana kama usipojua wewe ni mshindi utasumbuliwa katika maisha yako na kushindwa kufika katikanchi ya ahadi. Unaweza kuishi maisha ya kinyonge sana japokuwa si ya kwako. Watu wengi hawafanyi vitu vikubwa au hata kujaribu kwa sababu wamejiona wao ni wa kushindwa tu. Kuwa hawawezi kushinda. Ujue jambo hili kuwa katika hali yoyote ile, au vita katika maisha yako, changamoto yoyote, anayetakiwa kuwa mshindi ni wewe lakini unaweza kuamua kumpa adui yako ushindi. Timu ya mpira inaweza kuwa na uwezo mkubwa wa kushinda lakini kama haitafanya chochote uwanjani kushinda hakutakuwepo kwao hata kama ilitakiwa washinde. Hivyo kushindwa ni pale tunapoacha kuchukua hatua. Mtu aliyechukua hatua hajashindwa ila ameanguka.

Kuanguka maana yake ni kutofikia viwango au kutoendelea katika kusimama. Huyu mtu aliyeanguka kwa maneno mengine bado hajakamilisha ushindi wake. Anahitaji kuongeza viwango ili ushindi wake uwe kamilifu. Kwa maneno mengine kuna vitu anatakiwa kuvifanya ili akamilishe ushindi wake. Ushindi pia unamaanisha kuendelea kufanya mpaka ufike mwisho na ufikie kusudi lako. Unapoanza kuchukua hatua, basi umeingia katika mchakato wa ushindi, unapozidi kusonga unaelekea kukamilisha ushindi wako, unapomaliza kabisa na kufikia kusudi basi umekamilisha ushindi wako.

Kwa uwazi Zaidi ushindi una hatua nne

1.  kuingia kwenye ushindi

2.  kuendelea katika ushindi

3.  kukamilisha ushindi

4.  kuishi kwenye ushindi

 

1. KUINGIA KWENYE USHINDI

Hatua hii ni ya kwanza kabisa. Hapa ndipo mtu anapoanza kuchukua hatua. Hapa mtu anaweza kuwa na shauku inayochoma kuhusu kule anakoelekea. Jambo analotaka kulitimiza. Kusudi au ndoto aliyonayo inakuwa na moto ndani yake. Matamanio yake na shauku yake ni kulifikia kusudio lake. Hapa mtu haoni kama kuna changamoto yoyote. Anaona mambo yote kama vile yako mteremko tu. Haoni makorongo. Haoni milima. Yeye anajua jambo moja tu kuwa kuna jambo anatakiwa kulitimiza. Hatua hii wengi wanaichungulia, wengine wanaingia kabisa na kupata uzoefu wake kidogo. Ndiyo maana unaweza kunielewa ninachokimaanisha kwa kuwa yawezekana umeshaingia katika hatua hii ya ushindi. Kwa wengine hapa wanaweza wasiingie kabisa. Hawa ndiyo wale wanaoitwa walioshindwa. Mtu anaweza kuwa na mipango lakini asipoingia katika vitendo huyo tunamuita ameshindwa. Lakini mtu akiingia katika hatua hii akaishia hapa huyu hajashindwa bali ameanguka. Mtu aliyeanguka anaweza kuinuka na kuendelea na safari yake ya ushindi. 

Mtu huyu anaweza kama ni wewe, kuinuka na kuendelea na hatua ya pili ambayo tutaendelea nayo katika sehemu inayofuata Mungu akubariki.

 

Comments