NCHI YA AHADI - sehemu ya 15

       2. KUENDELEA KATIKA USHINDI

Hii ni hatua ya pili katika suala zima la ushindi. Hapa wengi hawafikagi kabisa. Hapa ndipo pale unapoanza kuona uhalisia wa ile njia unayotakiwa kupita. Hapa wengi hukimbia na kutoendelea na kule wanakotaka kushindwa. Hapa wamejaa watu wengi walioingia kanisani wakaacha kuendelea na wokovu wao. Katika hatua hii shetani huitumia sana ili kukuangusha au kukurudisha nyuma au kukudumaza endapo utakubaliana na wewe. Kumbuka shetani hawezi kukurudisha nyuma, kukuangusha au kukudumaza mpaka umpe ruhusu ya kufanya hivyo. Adui yako mkuu wa kwanza ni wewe mwenyewe yaani mwili wako. Huyo ndiye adui wa kwanza, ukimsikiliza sana atakushauri umpe ruhusa shetani aendelee na kazi yake katika maisha yako. Tutajifunza Zaidi kuhusu uadui na namna watu wanavyompa shetani ruhusa hapo mbele.

Katika hatua hii mambo yanaanza kuonekana kuwa hayaendi kama yalivyopangwa. Unaweza kujifunza hili kupitia safari ya wana wa Israel kutoka Misri kuelekea kanaani. Kwanza Musa alitoka usoni pa Mungu akijua hali ni nyepesi, kumbuka aliambiwa na Mungu kuwa Mungu ataufanya Moyo wa Farao kuwa mgumu, Mungu alimpn nafasi ya kujua hatua ya pili katika safari yake ya ushindi ya kuwatoa utumwani Israel. Lakini cha ajabu Musa anaenda tena kwa Mungu kumlalamikia yale ambayo aliambiwa yatatokea. Soma Kutoka 4:21-23 na 5:22-23. Hatua hii siyo nyepesi mpaka pale utakapokubaliana nayo. Wengi inakuwa ngumu kukubaliana nayo kwa sababu wakati wanaanza kuingia katika safari walianza katika namna ambayo fahamu zao zilijenga mtazamo Fulani, sasa wanapokuwa katika hatua hii ya pili wanakataa kukubaliana nayo. Kwa maneno mengine fahamu zao zinagoma kukubaliana na uhalisia wenyewe. Ukweli ni kuwa urahisi utakuja mpaka pale utakapokubaliana na uhalisia na kuona kuwa hata katika huo uhalisia kila kitu kinawezekana. Wana wa Israel walitoka kwa ushindi lakini jiulize kwa nini walikuja kumgeuka Musa.

Wapelelezi kumi na mbili walitumwa kupeleleza nchi ile ambayo Mungu aliwaambia wataingia. Kumi walikuja na uhalisia lakini hawakukualiana nao wakajiona kuwa wao ni panzi na chakula kwa uhalisia wao. Wawili walikuja na uhalisia, wakakubaliana na uhalisia, wakaona kuwa ule uhalisia ni kama panzi na chakula kwao. Hivyo wanaweza kuingia katika nchi ile kabisa. Maandiko yanasema katika hesabu ya kizazi hiki, watu hao wawili tu Yoshua na Kalebu ndiyo walifika katika hiyo nchi iliyojaa maziwa na asali. Kinachosumbua katika hatua hii ya pili ni KUKUBALI UHALISIA NA KUONA KUWA HATA KATIKA HUO UHALISIA MAMBO YOTE YANAWEZEKANA.

Katika hatua hii ya pili ndiyo mtu aliyeamua kushinda anaonekana. Maana haoni uhalisia kuwa ni kitu cha kumrudisha nyuma bali kama sehemu ya kumfikisha kule anakotaka kwenda akiwa na ushuhuda. Hatua hii ndiyo ile inayomfanya mtu awe na kitu cha kumsaidia mwingine anayehitaji kuwa mshindi. Endapo mtu huyu atafika katika hatua ya nne, basi anaweza kuwasaidia na wengine wakamilishe. Katika hatua hii hauhitajiki kukata tamaa bali kuendelea na mchakato wa ushindi huku ukijipa matumaini kuwa unaelekea kwenye nchi iliyojaa maziwa na asali. Unahitaji kuendelea kukusanya silaha bora Zaidi kama zile ulizoanza nazo hazina uwezo wa kukusaidia kuendelea mbele. Hapa unahitaji kuendelea kukusanya maarifa Zaidi kutoka kwa washindi ili uchanganye maarifa hayo kutengeneza mbinu wezeshi kufika kule juu. Unahitaji kuendelea kujifunza Zaidi kwa maneno na vitendo katika hatua hii. Unahitaji kumtazama Mungu na kulitazama kusudi unalotaka kulifikia. Hapa unahitaji kuangalia utapata nini kama utafanikisha kusudi hilo. Hapa hutakiwi kuendeshwa au kuwasikiliza watu wenye maneno yenye mtazamo wa HAIWEZEKANI. Hapa wakati mwingine unapita wewe na Mungu wako tu wengine wanaweza  kukuacha katika hatua ya kwanza, wakaja kuungana na wewe katika hatua ya tatu. Mara nyingi katika hatua hii unajikuta unzungukwa na mazingira mapya tofauti na yale uliyoyazoea. Changamoto ambazo hujawahi kukutana nazo. Uadui ambao hujawahi kukutana nao. Watu ambao hukuwadhania. Watu usiowajua. Vitu usivyovifahamu. Hapa ni sehemu ya mambo mapya ambayo pengine uliyasikia au hata hukuwahi kuyasikia masikioni mwako au kuyaona. Hapa kila kitu kinaweza kuonekana cha ajabu sana kwako kiasi kwamba unaona huwezi maana hujazoea.

Unapovuka hatua hii ya pili ambayo ni muhimu sana katika ushindi, hatua inayokutofautisha na wengine, unaenda kwenye hatua ya tatu inayoitwa:

 

                     3. KUKAMILISHA USHINDI

Karibu katika hatua ya tatu na muhimu katika ushindi. Katika hatua hii, ukifika hapa ni pale ambapo umeanza kuzoea ile hali uliyokutana nayo katika hatua ya pili. Hapa unaona hakuna ugumu, hata ule ugumu uliokuwa unaonekana kwako katika hatua ya pili kama vile haupo. Hii ni kwa sababu fahamu zako zinakuwa zimemezwa na hali iliyopo na kuchukuliana nayo kama ilivyo. Fahamu zako zimechukua hali zote na kuvaana nazo, zimekubaliana na kufanya mapatano. Fahamu zako nimefanya urafiki hivyo changamoto za katika hatua ya pili siyo maadui zako tena hugeuka kuwa marafiki.

Katika hatua hii wale waliokuacha katika hatua ya kwanza, ukaingia ya pili peke yako, wanaweza kurudi na kukutia moyo mnaendelea tena. Vitu vinakuwa kama vile viko kawaida hakuna kipya. Mambo mapya unayazoea, wale watu wapya unawazoea hakuna kitu cha kukusumbua sana hapa. Hata ule ugumu ukiwepo bado huoni kama upo. Fahamu zako zinakuwa siyo zile za huko nyuma. Kufikiri kwako kunabadilika. Huwi tena mtu asiyejua bali unaanza kuwa mzoefu unayeweza kushiriki na wengine yale uliyojifunza kwa sehemu katika safari yako ya ushindi. Hapa unajikuta katika hali ya mtu mpya kabisa. Watu wanaweza kukushangaa na kusema umekuwa tofauti na kadhalika. Unaweza kuanza kuonekana kwa watu katika ule upekee wako halisi ambao kwa huo uliumbwa uwe. Hapa hata wewe mwenyewe unajiona tofauti na kuanza kujivunia jitihada ulizofanya katika ule ugumu wa hatua ya pili.

Hapa unaelekea kukamilisha ushindi wako. Hapa lile jambo ulilokusudia linakuwa katika kushikika kabisa. Kama ilikuwa unataka kurekodi nyimbo katika hatua hii tayari umerekodi. Hapa unakuwa umetimiza kile ulichokusudia. Upo kwenye lengo lako hapa. Hakuna sehemu ya furaha kama hii. Hii sehemu unaona sasa uhalisia wenyewe kwa mapana yake ya kuwa hakuna jambo gumu duniani ambalo haliwezekani isipokuwa mtu awe ameamua lisiwezekane.

Muhimu: hatua hii ina maeneo mawili ya msingi sana kuzingatia. Eneo la kwanza ni kuwa kile ulichokusudia kinaanza kuingia katika mikono yako. Unakiona kinatimia. Eneo la pili ni kuwa kile ulichokusudia kimekamilika. Ulichotarajia kimeenea kama uvyotaka. Kwa maneno mengine unaweza kuanza kutimiza kusudi. Kama usipoendelea utajikuta hili eneo la pili haulifikii yaani kukamilika kabisa. Inamaanisha kuwa utakuwa umetimiza lengo lakini bado hujakamilisha. Unahitaji kuendelea kufanya ili ukamilishe kabisa. Usiishie kutimiza kitu hakikisha umekikamilisha. Huna unachodaiwa katika hilo jambo. Umehakikisha umetumia jitihada zako kufikia kiwango cha juu kabisa cha kusudi kuu.

Unapomaliza hatua hii ya tatu, unaingia katika hatua ya nne na ya mwisho ambayo ipo katika sehemu inayofuata usikose na Mungu akubariki.

Comments