4. KUISHI KWENYE USHINDI
Katika hatua hii, unaingia katika mfumo wa kuiendeleza tabia yako ya ushindi hata katika maeneo mengine ya maisha. Unapofanya mambo mengine nayo bado unashinda bila kujali ugumu unaokutana nao katika safari yako. Hapa umefanikiwa kufikia hatua kuu ya mwisho. Umefika kileleni. Hapa unakaa kileleni sasa, unakuwa mwokoaji wa wengine wanaotafuta kufika huko juu kileleni.
Katika hatua hii, unatumia ushindi wa awali kama fimbo ya kuchapia ugumu katika mambo mengine ambayo unatamani kushinda. Unapoingia katika mashindano ule ushindi ulioupata hapo mwanzo unakuwa chachu ya wewe kuendelea katika mapambano na kuubeba ushindi. Unapoingia katika mapambano hauna haja ya kuangalia idadi ya maadui wako ulio nao bali kujiuliza kama uliweza kushinda katika vita iliyopita na ukakamilisha ushindi kwanini hata hii nayo usiweze? Kama vita ijayo ni ngumu, siyo kwamba huwezi kushinda bali kuna njia unazotumia ambazo haziendani na ugumu unaokutana nao. Unaweza kuona una mbinu imara, lakini ukianguka ujue unatakiwa kurekebisha baadhi ya mbinu zako. Katika hatua hii ya nne, jambo hilo ni la msingi sana, yaani kujifunza kubadili gia angani wakati unaendelea na safari.
Hapa unaendelea na maisha ya ushindi. Unasogea hatua za vita kubwa Zaidi ya jana. Mzoefu wa vita haogopi vita ila anaogopa kutoingia kwenye vita. Mshindi haogopi kuanguka katika vita maana anajua kuanguka humpa ishara kuwa kuna mambo hajaweka sawa ambayo hayaendani na aina ya vita anayopigana afanye mabadiliko ili mambo yakae sawa. Katika hatua hii ya nne, ujue jambo moja ya kuwa vita havikomi, ila wewe unaweza kukoma kuwa mshindi. Vita vinaendelea na ni maamuzi yako kuendelea kuwa mshindi au la.
Mfano mtu ambaye ni mpiganaji wa ngumi, ashindapo kwa mara ya kwanza yeye ni mshindi. Basi anakuwa amepanda viwango. Anatafutiwa upinzani Zaidi ya ule aliokuwa nao. Katika hali hii huyu mshindi anatakiwa kuwa mwanafunzi tena. Lazima ajue namna ya upiganaji wa adui yake. Lazima ajue mbinu za adui yake. Lazima awe na taarifa za kutosha kuhusu adui. Kumjua adui yako ni muhimu sana. Unakuwa umemzidi hatua mpinzani wako. Hata hivyo katika mapambano kumbuka hata maadui zako wanaweza kukujua ulivyo, mbinu zako, ndiyo maana unaweza kuanguka katika hatua ya pili ukaacha kuendelea, hivyo unahitaji kufanya kitu kinachoitwa KUJIONGEZA.
Kujiongeza ni kitendo cha kuwa na kitu cha ziada ambacho mpinzani wako hana. Lazima uwe na kitu cha ziada ambapo silaha zote zisipofanikiwa kumuangusha adui basi hiyo ziada inaweza kukusaidia kufanya hivyo. Katika hatua hii ya nne, upo kule kileleni ni lazima uwe makini usije kuporomoka kushuka chini. Wengine wamefika kileleni, wakazembea wakarudi chini kwenye matope sasahivi wanahangaika kujinasua tena. Pambana huko huko usikubali kurudi nyuma. Hatua hii inakudai uwe mbadilisha silaha ili kuendana na maadui walioko huko juu. Kumbuka kipindi upo chini ulipigana na maadui wanaotembea lakini huko juu unapigana na maadui wanaopaa. Unahitaji kuwa makini na utulivu mkubwa sana ili uweze kushinda. Silaha zao hata ukiwa mbali zinaweza kukudungua. Ni wepesi kukukimbia kama usipowawahi. Wanaweza kukuwahi. Usipoinua macho yako, wao wanaangalia chini kukuangamiza. Wengine watakuwa pembeni yako wakikusukuma au kukuvuta ushuke chini. Unahitaji kutulia na kuwa na msimamo thabiti usioyumbishwa kwa namna yoyote ile.
Hatua hii inakudai kuyafanya maisha yako kuwa maisha ya ushindi. Mshindi haogopi kupigana anaogopa kutopigana maana asipopigana makali yake yanapungua na anazidi kuwa dhaifu. Vita vya huko kileleni vinataka kukunoa Zaidi na Zaidi. Huku unakuwa na makali kuliko wembe. Makali yako ni muhimu katika kuondoa maadui zako mbele yako. Maadui ni zile changamoto au vikwazo vinavyojitokeza mbele zako. Lakini kumbuka una maadui wakuu watatu ambao ni
· Wewe mwenyewe
Yaani mwili wako unaweza kuwa adui. Na ndiyo adui namba moja. Ukiuendekeza mwili kuna mambo hutaweza kuyafanya duniani. Mwili mar azote hautaki shuruba. Hautaki mambo magumu. Hautaki uchukue hatari. Endapo kuna hatari, basi mwili utakushauri uache kupambana maana utaangamia au utakufa kabisa. Huyu ni adui asiyetaka maendeleo yako. Mwili umekuwa adui baada ya dhambi kuingia ulimwenguni. Homoni zinazofanya kazi sasa zinafanya kazi katika namna isiyosaidia kama hutakuwa makini. Nafsi ikikubaliana na mwili woga na mashaka vitakuendesha. Uvivu uliokithiri utakutawala na hutakuwa na uwezo wa kutimiza makusudi makuu katika maisha yako yaani huwezi kuwa mshindi maana hata kujaribu unaogopa.
· Mazingira yako
Mazingira tunayoishi kwa sasa siyo yale yaliyokukusudiwa katika uumbaji. Tunaishi katika mazingira yaliyozidi kuharibiwa . huyu ni adui wa pili. Hapa unaweza kuziona changamoto kuwa ni kubwa kuliko hata uwezo wako bila kukumbuka kuwa mpaka changamoto inakuja kwako mbingu zinajua kuwa unaweza kuzishinda. Mazingira haya ambayo yanakuwa adui yaani mazingira hasi, au mabaya au yasiyofaa yakiungana na mwili ndiyo huzidi kuwa imara Zaidi na kukufanya uogope kabisa. Mwili utayakuza mazingira uyaone mambo kuwa ni mazito sana yasiyobebeka na utajikuta unashindwa yaani huchukui hatua yoyote. Na kama uliingia katika mchakato wa ushindi unajikuta unaanguka au kuishia njiani.
· Shetani
Huyu ni adui wa tatu na wa mwisho. Watu wengi hupenda kumuweka adui huyu kama wa kwanza. Kila siku katika maombi yao ni kumkemea mtindo mmoja. Sizuii watu wasimkemee bali wakati mwingine huwa ni woga na upuuzi. Badala ya kupeleka mahitaji yetu kwa Mungu tunaishia kukemea tu. Hatupati majibu halafu shetani anatucheka akiwa amekaa pembeni. Anaona namna ambavyo tunampa mamlaka kiulaini. Huu mtazamo kuwa shetani ndiye adui mkuu naomba uue kabisa kwenye maisha yako. Jiulize hivi ukiingiaga kwenye maombi huwa unaomba au unakemea. Maana watu wengi wemejikuta wakimkemea Mungu kama shetani badala ya kumuomba. Hii ni kwa sababu fahamu zao zilishaathiriwa na tabia ya kukemea kemea bila utaratibu. Mungu ni wa utaratibu.
Adui huyu ana tabia ya kujikuza aonekane mkubwa hivyo watu wanajikuta katika hali ya woga usio wa kawaida wa kukemea tu wakati wote. Wakati mwingine hata hayupo ni sisi wenyewe tumeamua lakini bado tunamkemea shetani badala ya kuukubali ukweli na kuchukua hatua stahiki. Wachanga wengi wa kiroho wamejaa makanisani bila kujali wana miaka mingapi kanisani. Mtu mchanga anapimwa viwango vya Imani yake. Imani kubwa siyo kumkemea shetani bali Imani kubwa ni vile ulivyo na ujasiri na utaratibu kwa Mungu wako.
Adui huyu anatabia ya kutengeneza muunganiko wake na mazingira na kushirikiana na mwili ili kukuharibu. Mwili kwa kuwa nao una tabia ya kukuza mambo unakufanya ujione panzi na chakula kwa hiyo changamoto. Unapokubali wewe ni chakula basi unakuwa chakula kweli. Kazi ya mwili hapa ni kukuondoa katika ukweli. Mazingira nayo huonesha ugumu na shetani huanza kukupigisha stori za huo ugumu na namna ambavyo huwezi. Kusudi ni kuwa ubadilishe mtazamo wako. Ukibadili mtazamo wako tayari amekuweza. Hata katika mpango wake wa Kumuangusha Hawa alikuwa anapambana jambo moja tu kubadilisha mtazamo wa Hawa ili afanye vile anvyotaka yeye. Kuwa makini sana. Katika maisha yako ujue jambo moja tu SHETANI ANAPAMBANA ILI WEWE UBADILISHE MTAZAMO WAKO ILI AWEZE KUKUTAWALA NA KUKUENDESHA VILE ATAKAVYO.
Hivyo makali hayo yatakusaidia kuvuka hao maadui watatu ambao ndiyo sababu ya wewe kuwa hapo ulipo. Makali hayo yatakusaidia kulinda mtazamo wako wa kiushindi. Makali hayo yatakufanya usiyumbishwe na ushawishi wa mwili au mazingira au shetani. Maana katika ushindi fikra zinapogeuzwa kuwa hasi yaani kutoka katika fikra za kuweza na kwenda katika kutokuweza, kutoka katika nguvu kwenda katika udhaifu basi ujue unaenda kuanguka na usiinuke.
Hakuna jambo baya la aibu kama kuwahi kushinda halafu usiendelee kuwa mshindi. Hii ni fedheha nzito kuliko fedheha nyingine. Timu za mipira na wanamichezo wengine wanalijua hili. Ukimshinda mpinzani usikubali aje akushinde tena ni aibu tena akija kukushinda na yeye ataamini kuwa kumbe hata wewe huwa unashindwaga basi atakugeuza nyama yake. Usikubali kushindwa. Yaani ingia katika vita, endelea mpaka tone la mwisho na utoke na ushindi. Usikubali kuanguka kwako kuwe sababu ya kuacha kufuatia ushindi mwingine tena. Maana unatakiwa kuwa mshindi katika mweneo yote. Ukiwa kileleni hapo ndiyo mahali pa kutengeneza nafasi ya kushinda kila mahali bila kujali vizingiti vilivyoko mbele yako. Kumbuka unapoishi katika maisha ya ushindi kuna watu nyuma yako wanajifunza na unawasaidia na wao kuwa washindi kama wewe. Mungu atakuinua kabisa.
Na kwa namna moja ama nyingine ikiwa utawasaidia kuwa washindi basi unawasaidia kuingia katika nchi ya ahadi. Na hivyo ndivyo unavyozidi kubarikiwa na Mungu. Mungu anakupa kusogea mbele Zaidi na kuwa mkuu kati ya watu.
Ikiwa tutajifunza na kuchukua hatua ya kuwa washindi, tutaingia katika nchi ya ahadi bila shida. Kumbuka ushindi unakufanya uone UWEZEKANO WA KILA KITU katika uwazi halisi. Na hii itapanua uwezo wako wa kuona uwezekano wa vitu na utajikuta unafanya mambo makubwa sana katika maisha yako. Na hiyo ndiyo siri ya kuingia katika nchi ya ahadi.
Kumbuka haijalishi nini kipo njiani, haijalishi ni njia gani ya mafunzo. Haijalishi nini bali ushindi ni lazima. Kuingia katika nchi ya ahadi ni lazima. Kuingia katika UWEZEKANO WA KILA KITU ni lazima. Inawezekana kuingia huku na kufaidi maisha mazuri na kuwa na furaha katika maisha yako. INAWEZEKANA.
Mungu akubariki. Mambo haya yaendelee kukusaidia. Na yakusaidie katika kufikia UWEZEKANO WA KILA KITU. Usikose sehemu zijazo.
Comments
Post a Comment
Thanks for your comment, God bless you!!!