MAISHA YA NCHI YA AHADI
Karibu katika nchi ya ahadi. Baada ya kujifunza yaliyomo njiani umejifunza mengi ambayo kwa namna moja ama nyingine yatakuwa nyenzo muhimu katika kuhakikisha unafaidi maisha ya nchi ya ahadi. Pamoja na kuwa umejifunza mengi, na umeingia katika nchi ya ahadi kwa kufaulu mafunzo uliyoyapita kuna vitu unatakiwa kujifunza juu ya maisha ya nchi ya ahadi.
Maisha ya nchi ya ahadi yaani kuishi katika UWEZEKANO WA KILA KITU yanadai jambo moja la msingi sana. Bila kujali kuna uwezekano wa kila kitu, uwezekano huo hautakuwa na matokeo yoyote kama usipojifunza na kufanyia kazi kitu hicho, huo ni msingi wa muhimu sana kujifunza na utakusaidia sana katika kufaidi maisha ya UWEZEKANO WA KILA KITU.
Kitu hicho cha msingi ni KUJUA NA KULIISHI KUSUDI LA UWEPO WAKO katika dunia. Hili ni jambo la muhimu sana la kuzingatia katika nchi ya UWEZEKANO WA KILA KITU. Kusudi lako ndiyo msingi hasa wa kuwepo katika nchi hii ya ahadi.
MAMBO YA MSINGI UNAYOPASWA KUYAFAHAMU KUHUSU KUSUDI
· Kila kitu kipo kwa kusudi
Chochote unachokiona kipo kwa kusudi. Hakipo kwa bahati mbaya. Hakuna kilichopo kwa ajali hata kama kinaonekana kuwa kimetokea kama ajali. Yamkini kuna wengine walipozaliwa waliambiwa kuwa hawakukusudiwa kuzaliwa. Lakini Mungu alijua utazaliwa, na aliwatumia haohao ili uje. Hivyo kwao ni bahati mbaya au ajali lakini kwake yeye aliye chanzo cha uhai wako siyo bahati mbaya au ajali, tazama kile anachowaza Mungu siyo wanachowaza wazazi au watu juu yako. Kile anachowaza, anachosema au anachopanga Mungu juu yako wewe kinahusiana na kusudi lako maana yeye ndiye aliyekusudia uwepo.
· Kusudi ndiyo sababu ya uwepo wa hicho kitu
Kusudi ndiyo sababu ya uwepo wa hicho kitu. Kusudi ndiyo mana hasa ya uwepo wa kitu. Kama hakuna kusudi hakuna maana ya maisha hayo. Uwepo wako au maisha yako yamebebwa na kusudi lako. Kusudi lako ndiyo linalodai wewe uishi. Hivyo kuishi kwako ni muhimu kwa sababu kusudi lako bado linahitajika.
· Kusudi ndiyo suluhu ya tatizo lolote duniani
Jambo la msingi sana kulifahamu. Kila tatizo unaloliona, ujue Mungu aliliona kabla, hivyo kabla halijatokea alishaandaa suluhisho la tatizo hilo, hivyo hata mambo Fulani Fulani yanapotokea tusimlaumu Mungu bali tumuombe atoe msaada wake kwa watu Fulani wenye jukumu la tatizo hilo wajipambanue na kuishi namna sahihi wanayotakiwa kuishi.
Mfano ujio wa Yesu, maandiko yanasema yeye ni mwanakondoo aliyechinjwa tangu misingi ya ulimwengu. Kwa maneno mengine hata kabla mwanadamu hajamuasi, alishaandaa mpango ili mwanadamu akipotea ipatikane namna ya kumsaidia kurudi kwenye mstari. Ndiyo maana walipokuwa wanatoa damu za wanyama hazikutimiza uhitaji hasa bali damu ya Yesu imekuja kutosheleza uhitaji wa mwanadamu katika suala la ukombozi na kurejesha mahusiano na Mungu.
Kila tatizo duniani lina mtu wa kulitatua. Lakini hatari kubwa ni kuwa kama mtu asipojua kusudi lake atatumiwa na adui katika namna hiyohiyo kuleta matatizo Zaidi badala ya kuwa suluhu. Ndiyo maana tuna watu wengi ambao wanafanya mambo makubwa lakini yasiyo na tija hasa kwa mwanadamu bali kupoteza maana halisi ya ubinadamu.
· Kusudi ni siri
Kusudi ni jambo la siri sana, lakini katika ulimwengu wa roho ni jambo linalojulikana sana. Ndiyo maana adui anapoona umuhimu wa kusudi lako anahakikisha unapotea ili tu dunia iharibike. Kumbuka katika ulimwengu wa roho kusudi linajulikana sana, ndiyo maana hata nabii Musa aliona haya, Balaamu aliona hayo akasema, “naona lakini si sasa…..”. hata mamajusi nao waliona ndiyo maana wakaenda kumsujudia, kusudi lako linajulikana katika ulimwengu wa roho. Kusudi katika ulimwengu wa roho linajulikana hasa katika namna ya uwezo uliofichika ndani ya mtu husika.
Pia ulimwengu wa roho unaingiliwa kwa vitu viwili tu, fikra na maombi. Mambo hayo mawili ni nyeti sana, Biblia inasema “atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno zaidi ya vile tuombavyo ama tuwazavyo”. Tunaweza kuona kuwa hapo ulimwengu wa roho unaitikia katika kile tunachofikiri au kukiomba. Ndiyo maana maandiko pia yanasema “aonavyo nafsini mwake ndivyo alivyo”. Ikimaanisha kuwa sisi ni matokeo ya fikra zetu. Kumbuka hakuna kitu kinatokea kama hakijapitia ulimwengu wa roho, vilevile hakuna kitu kinachofika ulimwengu kabla ya kutokea mwilini.
Chochote utakachohitaji katika mwili, taarifa inaenda katika ulimwengu wa roho, kisha matokeo ni katika uliwengu wa mwili. Ndiyo maana maandiko pia yanasema “lolote mtakalolifunga duniani, litafungwa na mbinguni na lolote mtakalolifungua duniani limefunguliwa na mbinguni” haisemi kuwa lilifungwa mbinguni litafungwa duniani, bali likifungwa duniani litafungwa na mbinguni kwa maana ya kuwa dunia ni ulimwengu wa mwili ba mbingu ni ulimwengu wa roho, ulimwengu wa roho upo ili kuitikia vinavyohitajika katika ulimwengu wa mwili. Ni mfumo wa kutoa kile ulimwengu wa mwili unahitaji.
Hivyo kama unaweza kuingia katika ulimwengu wa roho unaweza kujua kusudi lako. Kumbuka huko kunaingiliwa kwa maombi na fikra zetu.
· Anayejua makusudi yetu hasa ni yule ambaye ametuumba
Kumbuka anayejua uhalisia na kusudi hasa la gari ni aliyetengeneza gari, ndiyo maana kuna mwongozo wa mzalishaji au mtengenezaji wa hiyo bidhaa. Huo mwongozo ndiyo una kila kitu kuhusu hiyo bidhaa, ndio unaolezea hasa kusudi la hiyo bidhaa. Mungu anajua makusudi ya uwepo wetu. Kwake yapo wazi sana. Na yeye ametoa mwongozo wa kutupeleka katika kuyagundua na kufunua makusudi yetu hasa. Mwongozo alioutoa ni Neno lake, Biblia. Ndani ya mwongozo huu utapata taarifa zote unazozihitaji kuhusu kusudi lako.
Na pia wakati mwingine ni ngumu kutafsiri hasa kile kilichoelezewa kwa haraka. Unapomuomba Mungu anakusaidia kuelewa au kukuletea mtu ambaye yeye atakusaidia kukuweka wazi kuhusu kusudi lako hasa, ndiyo maana hata Paulo alielekezwa na Mungu aende kwa Anania ambaye huyo angempeleka kwenye kusudi lako. Hivyo ukiomba Mungu anakuletea, yamkini hata wewe msomaji umekuwa ukiomba, Mungu ameamua kukuletea mimi ambaye kwa pamoja tutasaidiana ulijue kusudi lako. Mwongozo huo amenifundisha kwa sehemu ambayo ameona naweza kukufikisha katika ile sehemu unatakiwa kufika.
Lakini vilevile kwa kuwa ulimwengu wa roho unaingiliwa kwa maombi na fikra, kuna mahali nitakupeleka kwa maswali kadha wa kadha ambayo yatakudai kufikiri na kutafakari kwa undani hasa kisha tutapa mwafaka unaotakiwa kufikia.
· Ni jukumu la kila mwanadamu kugundua kusudi lake
Ni jukumu lako. Ni wajibu wako. Kila mtu afunue na aweke wazi kusudi lake. Kugundua haimaanishi kuwa kitu ni kipya bali ni kitu ambacho kipo lakini hakijulikani kama kipo. Kusudi lako lipo ndiyo maana upo kama halipo ungeshaondoka duniani. Hivyo maadamu upo, unatakiwa kulitimza, na ni wajibu wako kutafuta kulijua kusudi lako.
Pambana kulijua kusudi lako. Upo ili kutimiza kusudi lako. Pambana, toa muda wako, jitoe, lipa gharama kujua kusudi lako. Na uwe tayari kupambana kulijua kusudi lako.
Kumbuka ili uishi katika UWEZEKANO WA KILA KITU, unatakiwa kujua kusudi lako. Hautatakiwa kuishi nje ya kusudi, uwezekano wa kila kitu unadai kuishi katika sababu ya uwepo wako. UWEZEKANO WA KILA KITU utakuwa na faida kwako kwa sababu utakusaidia kufanya makubwa.Usikose sehemu zijazo na Mungu akubariki sana
Comments
Post a Comment
Thanks for your comment, God bless you!!!