Karibu katika sehemu inayofuata katika somo la nchi ya ahadi, na leo tutaangazia juu ya
UHUSIANO WA UWEZEKANO WA KILA KITU NA KUSUDI LA UWEPO WAKO
· Kusudi lako ndiyo linalofanya uwezekano wa kila kitu uwe na maana kwa kuwa uwezekano usiotumiwa mahali sahihi hauna sababu ya kuwa na maana wala kuendelea kuwepo.
· Kusudi ndiyo sababu ya wewe kuendelea kuishi.
Maisha yako na uwepo wako katika nchi ya uwezekano wa kila kitu unadai kusudi liwepo ili uendelee kuwepo la sivyo hakuna chochote kinachokuwepo.
· Uwezekano wa kila kitu unasaidia kuliishi kusudi lako katika kiwango cha juu cha utendaji na ubora.
Kumbuka uwezekano wa vitu ndiyo unaowezesha ubora wa vitu kuwepo.
· Uwezekano wa kila kitu unaondoa mipaka ya utendaji na kupanua uwanja mpana wa watu wengi kufikiwa na kusudi lako ambalo ni suluhu katika tatizo Fulani.
· Uwezekano wa kila kitu unakusaidia kuwavuta watu ambao wanahitajika kuhakikisha unafikia kusudi lako.
Kwa maana ya kuwa siyo kila mtu anayo sehemu kubwa, kila mtu ni kweli ana sehemu yake, ila siyo kila wakati hiyo sehemu yake itahitajika.
· Uwezekano wa kila kitu unakusaidia kuwa na utawala wa muda.
Kumbuka mtu mkuu Zaidi duniani ni yule anaweza kutawala vitu nyeti kama muda.
· Uwezekano wa kila kitu utasaidia kusudi lako likae katika mazingira sahihi ya hilo kusudi kustawi.
Siyo kila mahali kusudi lako litastawi japo lahitajika kila mahali. Hata Yusufu mazingira sahihi ya kusudi lake yalikuwa ni Misri mara alipoona vitu vinayvohusu kusudi lake, vilimfanya akutane na watu sahihi kama yule muokaji, akutane na mazingira sahihi yanayohitajika kwa ajili ya kusudi lake, mpaka aje kuwa waziri mkuu.
UMUHIMU WA KUGUNDUA NA KULIISHI KUSUDI LAKO
· Kusudi limebeba ndani yake neema, uwezo na kibali unachokihitaji ili litimie.
Mara unapoligundua unafungulia kibali, neema na uwezo ambao haukuonekana ukifanya kazi hapo mwanzo. Yamkini umewahi kufanya mambo ambayo wewe unadhani kuwa ni makubwa, lakini utakapoligundua kusudi lako utajua uwezo mkubwa ndani yako kwa sababu kusudi lina vitu muhimu sana kwa ajili ya uwepo wako.
· Kusudi limebeba sababu ya uhai wako.
Wakati mwingine unaweza kuona kuwa maisha yako hayana maana. Maisha yako hamna kitu. Huoni haja ya kuendela kuishi. Utaelewa maana ya kuishi na umuhimu wako katika dunia pale utakapoelewa kusudi lako na namna linahitajika katika dunia. Hii itakusaidia kuachana na fikra hasi, au maamuzi mabaya uliyokuwa unawaza kuyachukua.
· Kusudi limebeba tabia unazotakiwa kuwa nazo katika maisha yako.
Watu wengi wamekuwa na maisha yenye tabia mbalimbali ambazo hata ukiwashauri lakini unaweza kuona mtu habadiliki. Tatizo hapo hajajua kusudi lake. Kusudi lake litaanza kumuumba kwa upya, kuumba tabia zake na matendo yake.
Mabadiliko chanya taratibu utaona yanatokea. Hata kama ulikuwa hauna mpango wa kuachana na vitu Fulani utashangaa unajenga shauku ya kuachana na tabia hizo. Kusudi linakupeleka kwenye utendaji wenye ufanisi. kusudi linakuendesha kufanya mambo Fulani Fulani ambayo ulikuwa unaona hauwezi kuyafanya.
Wakati mwingine namna nzuri ya kuwasaidia watu kubadili tabia Fulani Fulani ni kuwasaidia kujua makusudi ya uwepo wao.
· Kusudi limebeba furaha kuu sana ya maisha yako
Watu wengi wanaishi maisha ya majuto na manung’uniko kwa yale maisha waliyoyaishi hapo nyuma lakini hakuna cha kubadilisha katika yaliyopita. Maisha ya maumivu yasiyopona. Watu wengi hawana furaha katika maisha yao.
Watu wengi wanadhani furaha inapatikana katika fedha au kitu Fulani ajabu ni kuwa fedha haiwezi kukupa furaha unayoihitaji katika maisha. Watu wengi wanadhani mafanikio katika maisha ni kuwa na mali nyingi, ukweli ni kuwa mafanikio makuu katika maisha ni kuwa na furaha katika hayo maisha.
Watu wengi hawajui kuwa mara unapoanza kuliishi kusudi lako taratibu unaanza kupata furaha. Kwa sababu ndani yako kuna mzigo unaoanza kupungua ambao unatakiwa kuumaliza kabisa. Huo mzigo unapoanza kupungua ndipo furaha inapozidi kuongezeka. Kiwango cha furaha kinategemeana na kiwango cha kuliishi kusudi lako. Amua kuliishi kusudi lako ili upate furaha. Furaha itokayo ndani siko zote inatokana na wewe kukiishi kile kilichoko ndani. Furaha ya ndani haitokani na vitu vya nje bali vitokavyo ndani.
· Kusudi linakupeleka karibu na Mungu
Mara unapogundua kusudi lako. Unaweza kuliona ni kubwa. Na ni kweli kuwa ni kubwa. Na kuwa huwezi kulifanya wewe peka yako. Kama unahitaji watu basi unamhitaji Mungu Zaidi ili awe pamoja na wewe ili kulitimiza. Utajifunza kuwa karibu na Mungu ili awe msaada wako namba moja katika kila jambo unafanya kwa habari ya kusudi lako.
Ukaribu na Mungu utakuhakikishia mengi. Kumbuka hata mbinguni hauwezi kuingia kama hauliishi kusudi lako. Kumbuka kazi ya kila mtu itapimwa. Utakatifu unapanda viwango unapoanza kuliishi kusudi na kuona namna ambavyo mambo yasiyofaa uliyokuwa ukiyafanya hayawezi kukusaidia tena.
Ukaribu na Mungu unakuhakikishia uhakika wa kuliishi na kutimiza kusudi lako. Unakuhakikishia usalama wa maisha yako hata katika hatari kuu za maisha. Unapomuona Mungu yupo karibu yako unaanza kuona wepesi maana msaada wake upo na wewe na ndipo unapozidi kufanya makubwa na kushangaza dunia.
Comments
Post a Comment
Thanks for your comment, God bless you!!!