NAMNA YA KUGUNDUA KUSUDI LAKO
Tumejifunza juu ya umuhimu wa kugundua na kuliishi kusudi lako. Hapa tutajifunza namna gani tunaweza kugundua makusudi yetu katika namna iliyo rahisi Zaidi lakini ya kutafakarisha Zaidi. Kumbuka hapa tunaingia katika ulimwengu wa roho ili kugundua makusudi yetu.
Kama tunaingia katika ulimwengu war oho tunahitaji fungua sahihi ili kufungua milango sahihi tupate tunachokitaka. Hivyo ni muhimu kuhakikisha tunatafakari kwa usahihi Zaidi na kwa undani ili kupata undani wa makusudi yetu.
Pia mtu aliyegundua kusudi lake ni yule ambaye ameweza kulielewa kusudi lake kiasi cha kuweza kulitamka kwa neno moja tu, mfano Neno YESU lilikuwa lina maana ya UKOMBOZI. Hivyo yeye kuitwa Yesu, ni msamiati uliotumika kusema ukombozi. Hata mimi na wewe makusudi yetu yanaweza kutamkwa katika neno moja tu.
Mtu ambaye anatoa maelezo mengi kuhusu kusudi lake bado hajalielewa kusudi lake kwa undani. Kitu ambacho una ufahamu nacho unaweza kukieleza kwa ufupi kwa sababu unakielewa kwa undani. Ukiweza kutaja kusudi lako kwa neno moja tu au msamiati mmoja, basi umelielewa kusudi lako.
Unawezaje kujua kuwa neno hilo ndilo hasa limebeba au ndiyo kusudi lako lenyewe hasa? Ni swali ambalo unaweza kujiuliza sana, yafutayo ni mambo ya kuzingatia juu ya kusudi hilo kwa neno utakaloliweka,
Ø Neno hilo liwe moja, lakini pan asana kiasi kwamba litabeba majibu ya maswali utakayoyajibu hapo chini. Lazima lijumuishe yote na lisibakize hata moja.
Ø Neno hilo lazima linapotamkwa liwe linadai maelezo ambayo ni mapana. Wewe unalielewa kwa mapana lakini wengine hawalielewi katika upana unaohitajika hata kama wanajua matumizi ya hilo neno. Wao watatafsiri hilo neno kulingana na matumizi yao siyo kusudi lako.
Ø Neno hilo lazima liwe jepesi kutamkwa yamkini hata limezoeleka lakini lina kina sana, mfano USHAWISHI, UKOMBOZI, MAANDALIZI, SULUHU na kadhalika.
Ø Hata kama hilo neno linafanana na kusudi la mtu mwingine uhalisia ni kuwa kila moja limebeba maelezo na uhalisia tofauti na lingine, mfano neno Yesu na Yoshua yote yana maana moja UKOMBOZI lakini kawasome watu hawa wawili na utajifunza tofauti zao.
Angalizo:
Unapojibu maswali haya
· Hakikisha unakuwa katika hali ya utulivu isiyo na masumbufu.
· Hakikisha unakuwa na utulivu wa akili, hakikisha unafikiria kujibu maswali tu
· Hakikisha una daftari utakaloandika majibu ya hayo maswali.
· Hakikisha unajiambia ukweli na kutoa majibu sahihi, usikubali kujidanganya mwenyewe.
· Hakikisha unajibu kama mtu ambaye ana uchungu na kile kilichowekwa ndani yake akifanyie kazi. Hii inamaanisha hautajibu kwa haraka, wala kiwepesi wepesi.
· Baada ya kujua kazi yako, usiishie hapo, nenda hatua moja Zaidi katika vitendo vyenye tija.
· Hakikisha unamuomba Mungu akusaidie kufika kwenye utambuzi wa kazi yako, na akuwezeshe uitimize.
A. Ni jambo gani ambalo ukilifanya unakuwa na furaha sana, Amani na utulivu wa nafsi?
Hapa unatazama kwa umakini sana, kuna vitu ambavyo wengi wanapofanya wanajisikia furaha lakini siyo kwamba vinaendana na kusudi lao. Hapa namaanisha kuwa ujitazame ndani kabisa ya moyo wako. Kisha jiulize hili swali. Ukishajiuliza kwa nia ya kutaka kujua ukweli kuhusu wewe, utapata majibu sahihi, kisha yaandike.
B. Ni jambo gani unapenda kulifanya kuliko mambo yote?
Hapa unatazama vitu ambavyo wewe unapenda sana kuvifanya. Mfano unapenda sana kuimba, hii inamaanisha kuwa una kazi ya uimbaji. Tazama kile ukipendacho sana. Tahadhari ni kuwa usipende kujijibu haraka haraka, wakati mwingine inakulazimu kutulia kabisa. Jijibu kwa uhakika kitu gani unapenda, labda kifanyike kwenye jamii ili iwe na ustawi.
C. Pia unaweza kujiuliza ni vitu gani ukiwafanyia wengine wanafurahia Zaidi kuliko ukiwafanyia kitu kingine?
Hapa napo
unaweza kujua kazi yako. Japo siyo muhimu sana lakini ni muhimu. Unaweza
kuangalia kitu ambacho ukikifanya katika jamii kinakutofautisha na wengine.
Hata kama wengi wanafanya kitu kimoja, lakini watu wanafurahi Zaidi unapofanya
wewe. Hicho kitu kinaweza kukutambulisha kwa watu kipekee sana na inaweza kuwa
ndiyo kazi yako. Kitu gani wengi wanatamani uwasaidie. Kuna kitu ambacho watu
wanakutafuta ili uwasaidie kikiwa ni kitu kinachojirudia rudia, kitazame kwa
umakini hicho kitu.
D. Kitu gani ambacho unaona ni cha kipekee ulichonacho ambacho wengine hawawezi kukifanya kama wewe utakavyoweza kukifanya?
Tazama ule uwezo wako wa asili na kipaji chako. Tazama uwezo wako ambao hata usipotafuta ujuzi unaweza kukifanya hata kama si katika ubora sana. Kitu hicho kikiungana na ujuzi unaweza kufanya makubwa. Tazama kitu kilichoko ndani yako ambacho unaweza kukifanya kipekee Zaidi kuliko wengine.
E. Kitu gani unapenda kukifanya kwa ubora Zaidi?
Kuna kitu ambacho wewe unapenda kukifanya kwa ubora kuliko vyote. Kitu ambacho hupendi kukifanya kiholela holela. Hicho kitu kinaweza kuwa kazi yako uliyoumbwa kuja kuifanya.
F. Kitu gani hukipendi kuliko vyote kwenye jamii na mazingira yako, au kiwatokee watu wengine?
Kitu hicho ndiyo kile umeletwa kuja kushughulika nacho. Umeitwa kushughulika na changamoto hiyo. Ndiyo maana wewe unakichukia lakini wengine wanakichukulia kawaida tu. Hilo ni jukumu lako.
KUMBUKA
Ukishapata majibu, yaunganishe yote kupata neno moja lililobeba yote, hapo umafanikiwa kugundua kusudi lako. Mshukuru Mungu na anza kuliishi. Pia nakushauri kutafuta somo langu linaloitwa KUGUNDUA SIRI KUHUSU ASILI YAKO na ASILI SABA (7) ZA MWANADAMU, hapo utajifunza mengi yatakayokusaidia kupanua ufahamu wako juu ya kusudi na kulitimiza kwa upana ambao Mungu amekusudia.
Comments
Post a Comment
Thanks for your comment, God bless you!!!