NCHI YA AHADI - sehemu ya 20

NAMNA YA KUISHI KWENYE KUSUDI LAKO

Katika sehemu iliyopita tumejifunza namna ya kugundua kusudi lako. Katika sehemu hii tunajifunza namna ya kuishi kwenye kusudi lako. Kumbuka maisha siyo kugundua kusudi bali kuliishi kusudi. Mara zote ni muhimu kufanyia kazi jambo hili. Kuna kugundua kusudi na kuliishi kusudi.

Kuna mambo kadha wa kadha ya kuyazingatia ili kuliishi kusudi lako na kuyafanya maisha yako yawe na maana.  Kumbuka kusudi ndiyo linalotufanya tuendelee kuwa na nafasi ya kuishi. Kila wakati tunaoamka ni kwa sababu Mungu ametupa neema ya kuliishi kusudi letu. Kila siku ni muhimu katika kusudi la uwepo wetu.

Kumbuka katika kila jambo unafanya, kila dakika unayopumua inahesabu katika kusudi lako. Hata kama kuna wakati unasema “ngoja nipoteze muda”. Jua ya kuwa hata hapo kusudi linahesaby mud wake. Na nafasi tunayopewa ya kuishi ni kwa sababu tunatakiwa kuliishi hilo kusudi. Na ipo siku utahukumiwa juu ya namna ulivyoliishi kusudi lako. Hivyo ni muhimu sana kuwa makini hapo.

Vilevile unapopata nafasi ya kuiona siku ni muhimu kuona kuwa kusudi lako bado linahitajika duniani. Kuna namna ambavyo msaada wako unahitajika kuliko unavyoweza kudhani. Hivyo kushindwa kuliishi kusudi lako ni kuikosoa nafasi uliyopewa na kumfanya aliyekupa nafasi amekosea jambo ambalo ni hatari sana kwa ustawi wako na hicho ndicho kiliwafanya Adamu na Hawa kufukuzwa kutoka katika bustani ya Edeni.

Pia unapopata nafasi ya kuwa hai inamaanisha unatakiwa kutatua matatizo ya watu. Usipofanya kitu unafanya watu waingie katika hali mbaya na hatari Zaidi ya uwepo wao kuendelea duniani. Muhimu sana kuchunguza maamuzi yetu tunayoyachukua juu ya makusudi yetu katika kuyaishi kwa sababu kwa sasa yanawaathiri sana wanadamu wenzetu kuwa katika hali mbaya ilhali wanahitaji msaada wetu. Vilevile inatuweka sisi katika hatari kubwa katika wakati ujao.

Ziko njia kuu za msingi nne (4) zitakazokusaidia kuliishi kusudi lako ki-matokeo katika ulimwengu na kuacha alama siku unaondoka. Njia hizo ni kama ifuatavyo:-

1.  KANUNI YA MAARIFA

Hii ni kanuni ya msingi sana. Ya kwanza kabisa itakayokuwezesha kuliishi kusudi lako. Kumbuka aina ya maisha unayoyaishi ni matokeo ya mambo uliyoyapokea (taarifa) na kuyafanya yako na kuamua kuwa wewe na hatima yako.

Maarifa ni jumla ya taarifa zote ambazo umefahamu. Kujenga ufahamu wa taarifa Fulani uliyoipokea. Kujenga dhana mbalimbali na tafsiri tofauti katika mambo kadha wa kadha.

Ni muhimu sana kutafuta maarifa katika maisha yako kuhusu kusudi lako. Lakini kumbuka kuna maarifa sahihi na yasiyo sahihi. Ni muhimu uwa makini hapo. Wakati mwingine ni muhimu kumuomba Mungu akusaidie kupata maarifa sahihi. Lakini maarifa sahihi namba moja yaliyokamilika yanapatikana katika Neno lake, jifunze liweke ndani na ulihifadhi na ulifanye kuwa wewe. Watu wakitafuta hayo maarifa wayaone ni wewe.

Pia kuna maeneo mbalimbali ambayo unaweza kupata maarifa mbalimbali yatakayokusaidia lakini ni muhimu kuwa makini na kila chanzo cha taarifa unazozipokea maana zinaweza kuamua uwe nani. Jiweke katika mazingira sahihi yatakayokupa taarifa sahihi. Kaa na watu sahihi, soma vitabu sahihi, angalia video na hotuba sahihi, tega sikio kwenye vitu vitakavyokusaidia katika kuliishi kusudi lako.

Kumbuka siyo kila aina ya maarifa au maarifa yoyote unayahitaji. Kuna maarifa maalumu unayahitaji kwa ajili ya kusudi lako. Ukimuweka Mungu kwanza atakuelekeza kwenye mazingira sahihi yatakayokupa maarifa sahihi ambapo itakusaidia kutopoteza muda mwingi kama ambavyo Paulo alipotokewa na Mungu kule Dameski aliongozwa aende kwa mtu sahihi Anania ambaye angemwonyesha njia sahihi.

Kuna watu wamebeba vifurushi kwa ajili yako. Muombe Mungu akuelekeze kwao maana hao watakuelekeza vitu sahihi vinavyolenga moja kwa moja juu ya kusudi lako. Wako watu sahihi kwa ajili yako Mungu amewaandaa ni kujiweka katika mstari wa kiungu ili uambatanishwe nao.

Hatahivyo, ni muhimu kujua kuwa kuna aina ya maarifa ambayo ni ya ujumla kila mtu anatakiwa kuwa nayo. Maarifa hayo ni kama:-

·        Utunzaji wa muda

·        Elimu ya fedha

·        Mawasiliano

·        Mahusiano

·        Upangaji wa mambo katika maisha

·        Na kadhalika

Hayo ni ya kutilia mkazo sana. Jifunze kutunza muda kuliko unavyodhani. Muda ni mali. Kumbuka kila mtu duniani amepewa masaa 24 hakuna aliyezidishiwa lakini tofauti ni vile tunavyoamua juu ya muda. Kuna watu wanasema wako bize sana kiasi kwamba hawana muda lakini utashangaa kuwasikia wakisema “ngoja nifanye hiki ili nipoteze muda”. Ukweli ni kuwa muda tuliopewa unatutosha kabisa kuliishi kusudi letu ila ni sisi na uvivu wetu wa kupanga juu ya muda na kuona kuwa haututoshi. Kwa mengine Zaidi tafuta somo la RASILIMALI 7 AMBAZO KILA MTU AMEPEWA.

Watu wengi hawana elimu ya fedha, hawajajifunza kuwekeza katika makusudi yao, ndiyo maana wanataka fedha ya haraka. Wengine wamekuwa watumwa wa fedha. Badala ya kuitawala fedha wanapelekeshwa na fedha kiasi kwamba hawana tena uhuru juu ya fedha zao wenyewe. Fedha ipo kwa ajili yako na siyo wewe kwa ajili ya fedha ni suala la kutengeneza mifereji ili fedha ikujie kama ambavyo wahenga walisema “maji hufuata mkondo”.  Tafuta maarifa juu ya elimu ya fedha itakusaidia sana.

Wengine hawajui kuwa na mawasiliano mazuri, wengine hawajui kuhusiana na watu, na wao wenyewe, na Mungu, na mazingira na wenzi wao ipasavyo hali ambayo imewapelekea kushindwa kuliishi kusudi. Kumbuka mafanikio yako yapo katika mtandao unaojitengenezea, kwa maana ya kuwa mahusiano yana nafasi kubwa katika kuamua hatima zetu.

Wengine wanaishi bila elimu mipango. Wanaishi tu ilmradi wanapumua ila siyo kwamba wanafanya chochote. Hautakiwi kuwa hivyo, wewe unatakiwa kua mtu wa mipango unayeeleweka na unayefanyia kazi mipango yako. Na maarifa yafananayo na hayo ni muhimu sana kwako na unayahitaji sana.

UELEWA ni kitendo cha kuyafanya yale uliyojifunza kuwa wewe. Ni kuamua kuyasajili mambo Fulani Fulani ndani yako ambayo yataathiri maamuzi yako, mawazo yako, maneno yako, matendo yako, tabia na hatima yako. Kuna mambo ambayo unapoamua yawe wewe ndiyo yanayokufanya uwe hivyo ulivyo hata sasa.

Yale unayojifunza kuna mambo ambayo unahitaji kuyabeba na kuyafanya yako kabisa. Ubunifu unaweza kuzalishwa na kuchanganya mawazo yako na ya mtu mwingine. Uelewa ni uwezo wa kufanya kitu kuwa chako, kuwa na wazo jipya lililozaliwa katika yale uliyojifunza na kulichukulia hatua stahiki na kuleta athari katika jamii na dunia kwa ujumla.

Kusudi lako linaathiriwa sana nay ale unayojifunza. Kila kitu unachofanya kuhusu kusudi lako ni matokeo ya yale uliyoyapokea. Namna unavyolielewa kusudi lako ni matokeo ya vile umejifunza kuhusu kusudi lako.

Utalichukulia uzito kusudi lako kulingana na taarifa ulizozipokea kuhusu kusudi lako. Utaliishi kusudi lako kulingana na namna ulivyojifunza kuhusu wewe. Chochote ulichojifunza huamua wewe utakavyokuwa.

Comments