Karibu tena katika muendelezo wa kanuni 4 zitakazotusaidia kusihi katika makusudi yetu.
2 . KANUNI YA MIPANGO
Hii ni kanuni ya pili na ya muhimu sana. Ni kweli kuwa umejifunza lakini nini umepanga kuhusu kusudi lako?????. Kumbuka ukishindwa kupanga, umepanga kushindwa. Ni suala la maamuzi tu hapo. Na muhimu sana kuamua lililo jema. Kumbuka mipango inategemea kiasi cha maarifa yako, maana hapo utachagua njia, namna na wapi uende nini ufanye n.k
Maisha yasiyo na mipango ni hatari sana na bora kutoyaishi kabisa maana yanapoteza uhalisia wa uwepo wa mwanadamu katika dunia. Mungu mwenyewe ni wa mipango ndiyo maana aliumba dunia na vitu vyote kabla ya kumuumba Adamu. Bila mipango hufiki popote.
Mipango huhusisha; maono, malengo, mikakati na kalenda. Mambo hayo ni ya msingi sana kuyazingatia ili kuliishi kusudi lako na liwe na matokeo katika dunia yetu.
Maono ni uwezo wa kuona picha Fulani kuhusu kusudi lako. Kumbuka maono yako ndani ya muda. Hivyo unaweza kuwa na maono Fulani kwa muda Fulani kuhusu kusudi lako ambayo yatakusaidia kuliishi kusudi lako katika hicho kipindi. Maono ni kuona mwisho wa jambo katika kusudi kwa kipindi Fulani cha maisha.
Maandiko yanasema pasipo maono watu hushindwa kujizuia. Maono ni nyeti sana katika suala zima la upangaji kuhusu kusudi lako. Mtu aonavyo nafsini mwake ndivyo alivyo. Kumbuka unaposema nafsi unamaanisha ndani yako wewe, mazingira ya ndani, hivyo bado tunaona maarifa yanaathiri hadi uwezo wetu wa kuwa na maono juu ya makusudi yetu ya maisha.
Pia Mungu ana maono sahihi kuhusu kusudi lako na upangaji wake katika nyakati tofauti tofauti za maisha. Unatakiwa kuwa karibu naye na kumuomba ili akupe mwongozo sahihi ili ufike mahali sahihi. Kumbuka kiongozi kipofu akimuongoza kipofu wote huangukia shimoni. Mungu siyo kipofu yeye anautangaza mwisho mwanzoni. Kumbuka maono ni kuuona mwisho wa jambo kabla ya kuufikia. Kama utajiweka karibu na Mungu, atakuwezesha kuona picha sahihi ya wakati ujao au mahali unapotakiwa kufika bila kujali itagharimu nini kufika.
Maisha yasiyo na maono ni sawa na kuongoza ndege bila dira, unadhani nini kitatokea hapo?. Ni hatari sana kuishi bila maono ndiyo maana katika kitabu cha Ufunuo Mungu anasema twende kwake tukapate dawa ya macho ili tuone jinsi itupapsavyo kuona.
Kuna namna wewe unatakiwa kuona. Mungu anajua unavyotakiwa kuona. Wale wana wa Israel walipowaona wenyeji wa nchi ya ahadi ni majitu, na kuwa wao ni chakula tu kwao walikufan jangwani kwa sababu wameona nje ya vile Mungu ameona. Umewahi kujiuliza ni kwanini kuna vitu vingi hujavifikia? Ni kwa sababu hukuona vile Mungu anaona, anasema anaangalia Neno lake apate kulitimiza. Ukiona sawa na vile Mungu anaona kuna mahali pazuri unaelekea.
Hakikisha unakuwa mtu wa maono. Na unaandika maono yako. Yaweke maono katika maandishi. Pia nashauri kila unapoanza mwaka muombe Mungu akupe maono halisi ya mwaka huo ili usije kuwa na mipango mingi isiyofikika ambayo itakufanya unyong’onyee tu na kudumaza utendaji wako katika ulimwengu. Kama haujafanya hivyo unaweza kufanya hata wakati huu kwa wakati uliobaki upate mwongozo wa Mungu katika kile anakiona juu ya kusudi lako katika wakatu huo na ujionee namna ambavyo utafika pale vyema maana yeye huachilia neema ili anachokiona kitimie.
Zingatia sana mambo hayo yatakusaidia sana. Ni muhimu sana kuwa na maono. Weka maono ikiwezekana kila mwaka na inawezekana. Kama unaweza hata ya miaka kumi ilmradi yawe ni mwongozo wa kiungu. Kumbuka hata ukipanga wewe mwenyewe unaweza kufika, lakini utafika ukiwa umechoka sana, ndiyo maana anasema “usizitegemee akili zako mwenyewe”.
Malengo, ni zile shabaha unaweka katika yale unayoyaona. Ni kwanini unaona kile unachokiona. Kama umepata maono hayo kwa Mungu ni muhimu kujua kwanini huo mwaka Mungu amekupa maono hayo, nini hasa shabaha husika ya kuona jambo hilo. Yaandike. Yatakuwa motisha kwako kuendelea kupambana na kushinda vizuizi vyote vinavyokurudisha nyuma na utashinda tu.
Mikakati ni kwa namna gani utafika pale unapopaona au utafikaje katika ile shabaha uliyoweka. Weka mikakati inayofikika chini ya msaada wa Mungu. Inuka ukafanye makubwa inawezekana.
Uwe mtu wa mipango. Mipango ni muhimu sana. Inakusaidia kulivunja vunja kusudi lako katika namna ambayo itakusaidia kuliishi kwa urahisi na kufika pale unapotakiwa hata kama kuna vikwazo. Mipango inakupa namna ya kuvishinda chini ya msaada wa Mungu.
Mipango itakusaidia kufika salama. Itakusaidia kurekebisha mambo bila kuathiri kusudi, maono au shabaha. Itakufanya usitoke nje ya kusudi lako. Itakupa mipaka ya utendaji wa mambo. Itakupa kujimiliki na kufanya sawasawa na mapenzi ya Mungu.
USIKOSE KANUNI ZILIZOBAKI, MUNGU AKUBARIKI SANA
Comments
Post a Comment
Thanks for your comment, God bless you!!!