NCHI YA AHADI - sehemu ya 22

 Tunaendelea na kanuni ya tatu na ya nne katika somo letu zuri la NAMNA YA KULIISHI KUSUDI LAKO. Kama hujajifunza kanuni ya 1 na ya 2 rudi nyuma katika masomo yaliyopita ili upate kitu kamili. Mungu akubariki sana kwa kuendelea kujifunza.

                 3.  KANUNI YA UTENDAJI

Kila jambo linalopangiwa lazima lichukuliwe hatua. Ni kweli umeweka mipango lakini hiyo mipango haitajikamilisha yenyewe tu bali inakuhitaji wewe uifanye iwe halisi kutoka kwenye fikra zako au kutoka kwenye maandishi. Ni kweli Mungu amekupa maono hayo lakini anakuhitaji wewe ufanye naye kazi ili yatimie.

Utendaji ni muhimu sana. Utendaji una nguvu Zaidi ya maneno. Jifunze kuepuka kusema kuwa unaweza tu kila siku, ifike mahali uoneshe kwa vitendo kuwa unaweza. Uwe mtu wa vitendo siyo wa maneno.

Jiwekee ratiba, weka vipaumbele na uchukue hatua. Kila kitu kinawezekana kama utachukua hatua. Kuna mambo katika maisha yanaonekana kuwa ni magumu na hayawezekani. Lakini endapo utachukua hatua ndipo utakapojua kuwa inawezakana.

Mara nyingi katika kuelekea kusudi lako hatua ya kwanza huonekana ngumu sana. Kuchukua hatua ya kwanza kulifuatia kusudi lako. Mara nyingi watu wanaendeshwa na hofu isiyojulikama. Mtu anaogopa kisichojulikana. Yeye anaweza dharura zake na kuona kuwa zina nguvu kuliko kusudi lake jambo ambalo siyo kweli kabisa.

Hofu haina nafasi katika maisha yako. Usiku bali hofu ikutoe katika mpango wako. Kuna njia kadhaa za kushinda hofu, ambazo kwa sehemu ni kama ifuatavyo:-

·        Muweke Mungu namba moja

Wengi wanahofu ni kwa sababu Mungu hana nafasi ya kwanza katika maisha yao. Mungu alikuumbia ujasiri. Hakuna hofu. Hofu ya nini. Katika maandiko kuna usiogope takribani 365 na hii ni kwa sababu kila siku Mungu anakuambia usiogope kwa sababu tangu mwanadamu wa kwanza alipojitoa karibu na Mungu alianza kuendeshwa na hofu

Katika maisha yako unatakiwa kuwa na aina moja tu ya hofu. Hofu ya Mungu. Hofu ambayo itakusaidia kuwa na hekima, heshika, kuwa karibu na Mungu, kupata maarifa na kadhalika. Kuwa na hofu ya Mungu na si kitu chochote.

Mwamini MUNGU katika maono yako na katika kusudi lako. Mwamini kuwa anaweza  kukufikisha pale ulipopaona. Ondoa hofu na mashaka.

Weka Neno la Mungu moyoni mwako. Neno likijaa ndani linakupa ujasiri ambao utakufanya kufika pale unapotakiwa kufika. Walio wa Mungu ni majasiri kama samba. Hakuna hofu, yeye alishashinda kila kitu pale msalabani. Tunayaweza mambo yote katika yeye atutiaye nguvu, nini cha kuhofu. Muombe atakupa ujasiri.

Kuna wakati unatamani kuchukua hatua lakini unaona ugumu. Muombe Mungu akupe neema na msaada wake. Maana tunashinda na Zaidi ya kushinda katika yeye aliyetupenda. Mambo yote yanawezekana kwake yeye aaminiye. Ninayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. Yeye ndiye mwenye uwezo wote hakuna cha kumzuia. Ndiyo yake ni amina na kweli, akisema unaweza unaweza kweli hakuna wa kupinga, hakuna kizuizi cha kukurudisha nyuma hata kikisimama kama nini, kumbuka bahari ya Shamu iligeuzwa kuwa barabara, mto Yordani uligeuzwa njia kwa Neno lake ni nini cha kumshinda.

·        Uwe na shauku inayochoma

Hata maandiko yanasema utawezaje kutulia ikiwa Bwana amekupa agizo. Ndani yako kukiwa na kitu kinachokuchoma hautatulia. Hautaogopa chochote. Muombe Mungu aweke mzigo ndani yako kwa habari ya kusudi lako.

Hiyo shauku itakulazimisha kufanya mambo makubwa sawasawa na mapenzi ya Baba. Maana yeye mapenzi yake ni mema katika yale atuagizayo kuyatenda na Baraka yake imo humo.

Weka shauku, ona hitaji la dunia katika kusudi lako. Angalia je hiyo hofu inayokusumbua inapimana na ukubwa wa kusudi na uhitaji wake katika dunia.

·        Uwe na kaulimbiu yako

Kuna nguvu kubwa sana katika kaulimbiu. Mara nyingi hii inaeleweka sana jeshini. Kauli zao zinawapa motisha ya kuingia vitani ambako kuna hatari kabisa ya kifo.

Weka kaulimbiu na itakusaidia sana. Iandike. Itamke mara kwa mara. Iwe wimbo wako. Utaona namna ambavyo ule uwezo uliowekwa na Mungu ndani yako ukiamka na kukupelekea kufanya kazi yenye matokeo katika dunia.

CHUKUA HATUA KWA AJILI YA KUSUDI LAKO.

2.  KANUNI YA TATHMINI

Maisha yasiyotafakarika hayana maana kuyaishi. Katika kila utendaji kuna tathmini. Fanya tathmini ya vile umefanya. Pima kazi yako kama itasimama mbele za Mungu bila kujali unaona ni kubwa kiasi gani.

Yagawe maono, malengo na mikakati yako katika vipindi. Fanya tathmini ikiwezekana kila baada ya miezi 3, angalia utendaji wako ili kuangaliza hatua stahiki kulingana na utendaji katika wakti huo.

Tathmini itakusaidia kuona unahitaji msaada wa Mungu kiasi gani, ni nini unahitaji zaidia na hatua gani unahitaji kuzichukua ili kufika pale unapotakiwa kufika. Kumbuka hata mbinguni tathmini itafanyika. Kazi ya kila mtu itapimwa.

Hata Mungu katika uumbaji alifanya tathmini. Siku ya saba aliona kazi yake ni njema. Ipime kazi yako. Angalia yale umefanya yamekuwa na matokeo gani. Kumbuka matokeo yako lazima yake katika usawa wa vile Mungu anaona na siyo wewe unaona.

Andika ukweli wa utendaji wako. Mara zote utu uzima ni kujiambia ukweli na kuchukua hatua. Hakuna namna ambavyo utakwepa umuhimu wa kujipima vile umefanya. Tathmini itakusaidia kufanya maboresho Fulani Fulani ambayo yatasaidia kuleta ufanisi Zaidi. Na kumbuka ufanisi ndiyo muhimu katika kazi yoyote.

Chochote unachofanya kipimwe na uone kama kuna sehemu ya kurekebisha, wapi pa kuacha kama palivyo, wapi pa kupatilia mkazo. Kumbuka tumepewa akili katika mambo yote.

Nashauri uwe na daftari lako ambalo humo unafanya tathmini ya utendaji wako. Hata kama ni kila siku. Unatakiwa kuweka utendaji wako katika maandishi ili uwe unaona namna maendeleo yako yalivyo.

TUJIFUNZE KUZIPIMA KAZI ZETU WENYEWE.

Comments