NCHI YA AHADI - sehemu ya 23

NCHI YA AHADI ILIYOFICHIKA

Karibu katika sehemu ya mwisho ya somo letu la nchi ya ahadi, na leo tunajifunza juu ya nchi ya hadi iliyofichika. Ambayo nayo ni muhimu sana kila mtu aingie. Ni nchi ambayo inayapeleka maisha yako katika umilele mwema usiokoma katika mwisho wowote.

Watu wengi wanaishia katika kujiandaa na maisha haya lakini ni muhimu sana kujiandaa na maisha yanayokuja baada ya kuondoka katika maboksi yaliyotuhifadhi kwa muda tutimize makusudi yetu duniani. Hatuwezi kuishi tukijifurahisha katika dunia ambayo ilikuwa na mwanzo na mwisho tu peke yake, ni bora sana kujiunganisha na huyo Mwanzo na Mwisho.

Mwisho na Mwanzo ndiyo chanzo cha uwepo wetu. Ni lazima tujiungamanishe na Mwanzo na Mwisho huu ambao utatuhakikishia kuwa tutadumu salama katika mwisho wetu hata tukiwa nje ya dunia na maboksi yaliyotuficha sisi au kutuhifadhi.

Kuna wakati maboksi haya yanatudanganya tuone kuwa dunia ndiyo sehemu salama Zaidi ya zote katika umilele. Tukiendekeza maboksi haya kuna mahali yanatupeleka ambako patakuwa pabaya, kumbuka dunia kuna mtu mmoja aliichafua, na maboksi haya hujikuta machafu, ili yawe masafi, ni lazima tujipeleka kwenye Mwanzo na Mwisho. Hakuna kufanya udhuru katika jambo hili nyeti sana kuliko kawaida.

Haya maboksi yaliyotuweka tukiyafanya kipaumbele yatatupeleka pabaya. Maboksi yakiingia maji yanaharibika hata kama yalikuwa na sura nzuri kiasi gani. Hata kama yanavutia kuyatazama kuna wakati yataoza ka kupoteza uhalisia wake. Lakini sisi tulio ndani ya maboksi hatutakiwi kupoteza asili yetu.

Tulio ndani ya maboksi tuna asili yetu. Asili yetu ndiyo ya kuizingatia. Kuna maji machafu yalikuja yakaharibu makazi ya maboksi yetu. Ili tuwe salama ni lazima tujiunganishe na Mwanzo – asili ya uwepo wetu na Mwisho – hatima ya uwepo wetu. Sisi asili yetu iko kwenye Mwanzo na Mwisho. Ni muhimu kutazama katika Mwanzo na Mwisho ili tuishi milele.

Na yamkini katika maisha yetu tumekutana na mambo mengi na tuliruhusu maboksi yatutawale, tukapoteza ukaribu na asili yetu Mwanzo na Mwisho. Iko njia ya kurudi kwenye Mwanzo na Mwisho. Na hiyo njia ilitolewa na Mwanzo na Mwisho, na hiyo njia ndiyo sahihi na ya kweli maana imetoka katika chanzo cha wema wote hata ambao haujawahi kutendeka Mwanzo na Mwisho.

Mwanzo na Mwisho ndiyo chanzo cha wema na uhai wa dunia na vilivyomo. Tunapotaka kukimbia kutoka kwenye Mwanzo na Mwisho ni kuukimbia uhai wetu wenyewe na kuingia katika hatari. Jambo la kushangaza ni kuwa hata mgonjwa aliyepoteza uhai anaweza kuona kachangamka hata wakati anakufa. Baada ya kutoka kwenye maboksi tunatakiwa kurudi kwenye asili yetu. Lakini hauwezi kurudi kwenye asili kama haujaiunganisha na asili baada ya kujitoa katika asili sahihi, kumbuka kama kuna asili sahihi na ya kweli basi kuna asili feki isiyo sahihi.

Ni wakati wa kufanya maamuzi sahihi ili kujiungamanisha na asili sahihi ya uwepo wetu. Kuna wakati tunaona tupo katika asili sahihi za maisha, bahati mbaya ni kuwa kuna wakati unajiona upo mahali sahihi kwa sababu Fulani Fulani zinazopimwa na maboksi yetu. Ukweli ni kuwa tunahitaji kufanya maamuzi sahihi kurudi kwenye chanzo cha uhai wetu. Kumbuka ukikata tawi kwenye mti kwa siku kadhaa waweza kuonekana hai lakini ni ukweli usiopingika kuwa mwisho wa hilo tawi ni mbaya litakauka. Angalia maisha yako.

Mtu aliye katika Mwanzo na Mwisho anapimwa kwa maisha na mwenendo na matokeo ya kuishi kwake katika hii dunia. Na maisha, mwenendo na matokeo ya uwepo wetu havipimwi kwa maboksi yetu bali vinapimwa na Mwanzo na Mwisho. Mwanzo na Mwisho unaposema jambo hilo ni baya, hata kama boksi linasema ni zuri, uwe na uhakika kuwa unaelekea pabaya. Na tangu mwanadamu alioondoka kwenye asili njema mar azote anajiunganisha na asili mbaya mpaka atakaporudi kwenye asili njema.

Siyo kila njia itakurudisha kwenye asili njema. Kuna njia nyingine ni kujaribu lakini hautafika kwenye asili sahihi. Njia sahihi ilitolewa na Mwanzo na Mwisho na si vinginevyo. Na hiyo njia ni moja tu Yesu Kristo. Anasema katika Yohana 14:6 kuwa “Mimi ndimi NJIA na KWELI na UZIMA, mtu haji kwa Baba (Mwanzo na Mwisho)”. Kuwa makini sana hapo. Njia sahihi ya kurudi kwenye chanzo cha uhai wetu (Baba) ni Yesu Kristo.

Zipo njia nyingi, lakini hakuna njia nyingine ya kurudi kwenye asili. Hakuna njia nyingine ya kuingia katika nchi ya ahadi baada ya maisha haya ya duniani. Njia ni Yesu Kristo. Kumbuka katika nchi ya ahadi ya UWEZEKANO WA KILA KITU uliingia kwa kutumia njia ya MTAZAMO lakini katika nchi ya ahadi iliyofichika (Mbinguni) unaingia kupitia Yesu Kristo.

Hili ni jambo la kufanya uzito kuliko unavyoweza kudhani. Utavuna kile unachopanda. Huwezi kupanda mahindi ukitegemea kupata mananasi. Huwezi kujiunganisha na asili feki (Shetani) kwa matarajio ya kuunganishwa na asili sahihi utakapotoka katika boksi (Mwili). Fanya maamuzi sahihi sasa na uchukue hatua.

Kumbuka Mungu ni mwingi wa rehema Mwenye kurehemu. Kwake kuna msamaha hata kama wanadamu wengine watatutenga. Yeye yupo karibu nasi kuliko hata mavazi yetu, maana anaweza kuingia na kukaa ndani yetu bila kujali ukubwa wake  na matendo yake ya kutisha. Ni suala la kuamua kumuita yeye ili akubadilishe na akupe tiketi ya kuelekea katika nchi ya ahadi. Akupe uraia na kitambulisho cha nchi ya ahadi (Roho Mtakatifu). Akufunze utamaduni wa Mbinguni (Wokovu).

Amua kumpa Mungu maisha yako. Yeye ni mwaminifu anaposema nitakusamehe na kuufuta uovu wako. Yeye ni sahihi katika mambo yake. Kupitia damu ya Yesu Kristo pale msalabani tunaweza kusamehewa na kujiunganisha na asili yetu sahihi. Hatuweze kumchagulia Mungu njia gani tupite tufike kwake. Tutachagua njia ya kwenda  na tutapata matokeo kwa machaguo yetu.

Lakini yeye anashauri tuchague njie njema (Yesu Kristo) ili tuwe na mwisho mwema. Hakuna njia nyingine hata mtu akikupeleka katika sala mia mbili au chochote. Yesu ndiye njia sahihi. Hauna haja ya kutafuta nyingine. Kumbuka kila mtu atawajibika kwa ajili ya maisha yake. Amua kumfuata Mungu. Wajibika kwa ajili ya maisha yako.

Mungu alivyo wa ajabu ni kuwa unaweza kumuomba msamaha kupitia jina la Yesu, na kuomba ile damu iliyomwagika msalabani ikusafishe uovu wako wote. Mungu atakusamehe. Na utapata wepesi hata katika maisha yako katika nchi ya ahadi ya UWEZEKANO WA KILA KITU. Kwa sababu hapo Mungu atazidi kukusaidia kwa kuwa umeona umuhimu wake katika maisha yako. Na unapozidi kuwa karibu naye ndivyo anapozidi kukusaida.

Fanya maamuzi. Mfuate Mungu. Usikubali kurudi nyuma. Watafute watu waliojiunganisha na asili hii njema ya maisha. Epuka watu wanaokurudisha nyuma mpaka utakapofanywa imara na Asili. Mrudie Mungu. Tafuta mahali sahihi pa kusali patakapokujenga kiroho kuwa karibu na Mungu. Kumbuka nchi ya ahadi ya UWEZEKANO WA KILA KITU inakupa uhuru wa Nafsi, lakini nchi ya ahadi iliyofichika inakupa uhuru wa Roho yako dhidi ya utawala wa shetani atakaye kuwapeleka watu kuzimu.

Chukua hatua ya kupambania maisha yako kwa ajili ya wema na Mungu atakuinua sana. Mungu akubariki sana.

Comments