RASILIMALI 7 AMBAZO KILA MWANADAMU AMEPEWA
1. MUDA
A KUNDI LA WALIOKUFA WANAOWEZA KUAMKA NA KUFANYA KAZI TENA
Hili ni kundi la pili la watu ambao wako nje ya muda. Kundi hili linajumuisha watu ambao wanaweza kufufuka tena. Uwezekano wa wao kubadilika au kuweza kufanya kazi tena ni mkubwa sana. Kundi hili lina afadhali kubwa sana. Na kundi hili bado linaweza kuzinduka na kufanya mambo makubwa sana katika hii dunia. Kundi hili bado lina uwezekano wa kuitikisa dunia kwa mambo makubwa, ya ajabu, tusiyoyajua na ya kutisha na mema sana.
Kundi hili nalo limegawanyika katika sehemu mbili za vifo
· Kifo cha kiroho
· Kifo cha kifikra (nafsi)
KIFO CHA KIROHO
Hiki ni kifo ambacho kinahusisha watu kuwa mbali na Mungu. Mtu anapokuwa hana mahusiano na Mungu anahesabiwa kuwa amekufa. Huyu mtu yupo nje ya muda. Na kuwa nje ya muda kunampa tiketi ya kwenda kwenye umilele mbaya moja kwa moja anapoondoka katika mwili. Kumbuka kuwa na ukaribu na Mungu kunakupa nafasi ya ya umilele mwema baada ya kuondoka duniani. Ni muhimu sana kuwa makini hapa kwa sababu maisha yetu yapo katika maamuzi yetu.
Kifo cha kiroho ni kujitenga na Mungu ambaye ndiye asili ya uhai na uwepo wetu katika dunia hii tuliyomo. Tunapotengwa mbali na Mungu kwa maneno mengine hatuna ushirika au ushirikiano naye kiasi kwamba kama kuna msaada unaotoka kwa Mungu hautakuja kwetu maana hatuko sawasawa nay eye. Sisi ikiwa tumetengwa mbali na Mungu hatuna nguvu ya kuhitaji neema itokayo kwake ambayo ingetuwezesha sisi kufika mahali Fulani sahihi katika maisha yetu.
DALILI ZA KIFO CHA KIROHO
· Kutokuwa mtu wa ibada
Huoni sababu ya kuingia katika ibada. Hauoni maana ya kukutana na wengine ili kusali. Unachukulia ibada ni kitu cha kawaida sana. Hukumbuki kuwa ibada ni mahali ambapo Mungu anakutana na watu ili kuwaponya na kuwasaidia katika mambo mbalimbali. Kutokuwa mtu wa ibada kunamaanisha kuwa wewe uko mbali na uwepo wa Mungu. Na kama haufanyi ibada usitegemee kuuona msaada wa Mungu katika maisha yako.
· Kuishi katika maisha ya dhambi
Mtu yeyote anayeishi maisha ya dhambi hayuko karibu na Mungu. Mtu huyu hana mawasiliano na Mungu. Mtu huyu ambaye anaishi maisha ya dhambi hana hofu ya Mungu. Hali hii inapokithiri anafika mahali pa kuchukulia kuwa dhambi ni sehemu yake ya maisha. Hii inapelekea kuona kuwa maisha yake ni ya kawaida bila kujali anafanya dhambi.
Wengine wanafika mahali kuona kana kwamba Mungu anawaonea huruma kwa sababu wao ni wanadamu. Hivyo kwa kuwa ni wanadamu basi waendelee kufanya dhambi. Mungu atawahurumia kabisa na hawatakutana na adhabu baada ya maisha haya hapa duniani. Ni hatari sana kuwa na mtazamo kama huu. Mungu ni mtakatifu hivyo ambaye anataka kuwa naye karibu lazima awe mtakatifu.
Wengine waamini kuwa kwa kuwa sisi ni wanadamu hatuwezi kushinda dhambi. Lakini ni ukweli kuwa uwezekano wa kushinda dhambi upo kama vile ambavyo uwezekano wa kufanya dhambi upo. Ikiwa kuna jambo baya kuna jambo jema. Mungu mwenyewe anasema mtakuwa watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu. Hii sentensi ni shurutishi, ikiwa na maana ya kuwa, Mungu ni mtakatifu. Na kwa sababu yeye ni mtakatifu sharti uwe mtakatifu. Kumbuka tuliumbwa kwa sura na mfano wake. Hivyo kama yeye ni mtakatifu tunaweza kuwa watakatifu.
Kumbuka Mungu msaada wake bado upo ili tushinde dhambi. Mahali Fulani maandiko yanasema, ninayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. Mungu ndiye anatoa nguvu kama unaona huwezi kuwa na nguvu ya kushinda dhambi. Wewe unaweza. Kumbuka tu maisha ya dhambi ni dalili ya kifo cha kiroho yaani kuwa mbali na Mungu.
· Kukosa moyo wa Kufanya mambo ya Ufalme (Mungu)
Watu wengi ambao wako mbali na Mungu moja kwa moja huwa hawapendi kufanya mapenzi ya Ufalme. Kufanya mambo ya Mungu. Kujitoa ili kazi ya Mungu ikae sawa. Mtu yeyote aliye karibu na Mungu huhakikisha kuwa anakuwa sehemu ya kufanya jambo ili kazi ya Mungu ikae sawa. Anafurahi anapoona kazi ya Mungu inaenda sawasawa na mapenzi ya Mungu.
Unapojitoa kufanya mambo ya Mungu inamaanisha kuwa una ushirika naye na moja kwa moja wewe uko hai. Mtu asiyefanya kazi ya Mungu anahesabika kama mfu. Maana haleti athari yoyote chanya katika ufalme wa Mungu. Ni muhimu sana wewe kibinafsi uhakikishe ukaribu wako na Mungu unakupelekea kufanya mambo ya Mungu yaende na uwe sehemu ya mambo hayo kukaa sawa.
· Kutokuwa mtu wa maombi
Maombi yanasaidia sana katika kujenga ukaribu na Mungu. Kumbuka maombi ni mawasiliano baina yako na Mungu. Pia maombi ni mchakato wa kumruhusu Mungu afanye kazi katika maisha yako au kupitia wewe. Mtu yeyote mwenye utayari wa kumruhusu Mungu afanye kazi kupitia yeye (kazi yoyote njema ya ufalme), Mungu mwenyewe atahakikisha anakuwa karibu naye. Maana Mungu anawatafuta watu kama hao.
Kama wewe ni mvivu wa maombi moja kwa moja unazidi kupotea na kuwa uko mbali na ufalme wa Mungu. Ni jukumu lako kurudi kwa Mungu ili akusaidie. Kuwa mwombaji. Kama siyo mwombaji inamaanisha (kwa msisitizo) umekufa. Na kama umekufa sehemu yako haipo, kumbuka Mungu ni Mungu wa walio hai (kiroho).
· Kutokuwa na mtazamo wa kifalme (Mtazamo wa kiungu)
Mtu yeyote mwenye mtazamo tofauti na ule Mungu anaoutaka hayuko karibu na Mungu. Kumbuka mitazamo yetu ni matokeo ya watu na vitu ambavyo tumekuwa karibu navyo kwa muda mrefu. Kama tungekuwa na ukaribu na Mungu tungekuwa na mtazamo wa kwake Mungu.
Kumbuka sehemu kuu ya kupata mtazamo wa Mungu ni kupitia Neno lake. Neno lake limekamilika, ni amina na kweli. Neno lake limebeba mawazo yake na mipango yake na kusudi la kila kitu kilichoko duniani. Neno lake ni mwongozo wa namna viumbe vyote vinavyofanya kazi. Ikiwa na maana kuwa kama uko na ukaribu na Mungu uko na mtazamo wake. Na kama uko na mtazamo wake moja kwa moja utafanya mambo ambayo ni vile Mungu amekusudia.
Kama hauna mtazamo wa kiungu ni ishara tosha kuwa uko mbali na Mungu ndiyo maana unafanya kulingana na mitazamo matokeo ya adui na watu wengine ambao yamkini hawana mitazamo mema. Kumbuka hakuna mtazamo kamili na bora kama alionao Mungu juu ya maisha yako.
· Kutoongozwa na Roho Mtakatifu
Hii nayo ni dalili nyingine ambayo huonesha kifo cha kiroho. Kama hauna roho mtakatifu katika maisha yako na hauongozwi naye moja kwa moja uko mbali na Mungu. Umetengwa na Mungu. Roho Mtakatifu ni muhimu sana kwa yeyote aliye karibu na Mungu. Roho Mtakatifu hujua hadi mafumbo ya Mungu, maana yeye ndiye Mungu mwenyewe. Hivyo anajua mambo yote unayotakiwa kuyafanya.
Maandiko yanasema, wanaoongozwa na Roho wa Mungu hao ndio wana wa Mungu. Kipimo kikuu cha wewe kuwa mwana wa Mungu ni kuongozwa na Roho Mtakatifu. Kumbuka kuongozwa na Roho Mtakatifu ni kumpa nafasi yeye akuongoze katika njia ikupasayo kuifuata. Yeyote aliye hai rohoni anaongozwa na Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu anakusaidia kuwa vile Mungu anataka nje ya hapo hauwezi kuwa karibu na Mungu.
· Kumheshimu Mungu na Watumishi wake
Mtu yeyote anayemheshimu Mungu yupo karibu na Mungu na anajua thamani ya Mungu. Kama haumheshimu Mungu basi hauna ukaribu naye. Kama haufuati mapenzi ya Mungu, haumheshimu Mungu. Kama haumheshimu kwa mali zako, bado uko mbali naye. Kuna watu ambao kwa maisha yao na mali zao hawaoneshi kumheshimu Mungu na hii ni hatari sana. Unapogoma kumpa Mungu nafasi ya kwanza katika mambo yako na maisha yako kwa ujumla, unatengeneza mazingira ya yeye kuwa mbali na wewe. Kumbuka yeye anatafuta watu ambao watampa nafasi ya kwanza. Mungu atakuwa kipaumbele kwao katika vitu vyao vyote. Katika muda wao, katika mali zao na katika familia na yafananayo.
Kumbuka pia maandiko yanasema, mtu akinitumikia Baba (Mungu) atamheshimu. Hivyo kutomheshimu mtumishi wake ni sawa na kutomheshimu huyo aliyempa heshima ya kuwa hapo. Ukiwa karibu na Mungu utaelewa thamani ya watumishi na umuhimu wao kwako na namna wanavyoweza kukusaidia wewe kufika mahali Mungu anataka. Unapoona wewe una vingi kuliko mtumishi anayekulea bado una nafasi ya kumheshimu ili Mungu akuinue zaidi ufike mahali anataka ufike.
Yeyote anayeheshimu, hujua thamani ya yule anayemheshimu, na thamani ya mtu hujulikana pale ambapo kuna ukaribu. Na siku zote unapoheshimu unatengeneza mazingira ya kuheshimiwa. Na unapoheshimiwa unatengeneza nafasi ya kufanya makubwa katika maisha yako maana Mungu atakuwa tayari kukupigania, watu watakuwa na wewe ufike na watumishi wa Mungu watakubeba ufike.Mungu akubariki sana
Comments
Post a Comment
Thanks for your comment, God bless you!!!