RASILIMALI 7 AMBAZO KILA MWANADAMU AMEPEWA - sehemu ya 5

 

RASILIMALI 7 AMBAZO KILA MWANADAMU AMEPEWA

1. MUDA

AINA ZA WATU WALIOKO NJE YA MUDA

Kuna makundi matatu ya watu ambao wako nje ya muda. Makundi mawili ni ya watu ambao wako duniani lakini sehemu yao kama haipo duniani. Wapo kwa sababu wameamka ila siyo kwamba wana sehemu ya kufanya katika dunia. Siyo kwamba hawana hiyo sehemu bali wenyewe hawajiweka katika namna ya kufanya kitu katika dunia bila kujali wameletwa na Mungu kuja kufanya mambo Fulani nyeti na makubwa sana. Kundi la tatu halipo kabisa duniani, uwezekano wa kuendelea kutekeleza majukumu yake umeondolewa.

Makundi haya ni matatu kama nilivyosema hapo awali. Makundi hayo yamejumuishwa katika namna moja kuu ambayo ni KIFO. Watu wote walioko nje ya muda kwa maneno mengine wanahesabiwa kama watu waliokufa. Mtu yeyote aliyeko nje ya wakati haishi tena hapa duniani kwa kuwa wakati unafanya kazi katika dunia. Wamekufa kwa sababu hawafanyi jambo lolote duniani. Unaweza kushangaa wengi wao ndio wale wanaosababisha matatizo duniani badala ya kuleta majibu ya Mungu katika maisha ya watu.

Kifo ni kushindwa kufanya kazi. Mfano, unapoambiwa mashine imekufa maana yake  haifanyi kazi. Kama haifanyi kazi ni sawa na kusema haina umuhimu tena. Umuhimu wake hauonekani. Ili umuhimu wake uonekane ni lazima iwe hai. Ifanye kazi.  Ndiyo maana mtu asiyefanya chochote umuhimu wake hauonekani mahali alipo. Hiyo siyo ajabu ni kanuni ya asili tu kuwa kama hufanyi kazi umuhimu wako hauonekani. Hivyo ni muhimu kuwa hai ili thamani yako iwepo duniani. Ndiyo maana Mungu anasema watakatifu walioko duniani ndiyo bora, ni kwa sababu wanaweza kufanya kazi. Wanaweza kuleta athari katika hii dunia.

Makundi haya matatu ya watu walioko nje ya muda, yamegawanywa katika makundi makuu mawili:-

1.     Kundi la waliokufa na hawana uwezekano wa kufanya kazi (Isipokuwa kwa sababu maalumu tu)

2.     Kundi la waliokufa wanaoweza kuamka na kufanya kazi tena

 

                              A            KUNDI LA WALIOKUFA NA HAWANA UWEZEKANO WA KUFANYA KAZI TENA (isipokuwa kwa sababu maalumu)

Hili ni kundi la kwanza la watu walioko nje ya muda. Kundi hili linajumuisha watu wote ambao wanakufa kimwili. Kwa kweli watu hawa kama watafufuka ni kwa sababu ya Utukufu wa Mungu. Lakini katika namna iliyo ya kwetu ni kuwa wakifa hesabu yao imeisha kabisa. Watu hawa hatunao.

Mtu anapokufa kimwili anaingia katika ulimwengu mwingine. Roho yake inahama kuingia katika umilele. Mwili hautafanya kazi yake tena. Maandiko yanasema Baada ya kifo ni hukumu. Mtu anapokufa tu ni hukumu.

Hakuna mjadala wa wewe unaenda wapi baada ya kifo, kumbuka maisha unayoishi leo ndiyo tiketi yako ya kuingia katika umilele mwema au umilele wa uovu. Maamuzi bado yanabaki kwetu kumrudia Mungu ili kuingia katika umilele mwema au tukubaliane na adui tuingie pabaya.

Mtu aliyeko katika kundi hili hana nafasi tena ya kufanya chochote. Habari yake imeisha. Mtu huyu ameondoka katika muda. Ameingia katika ulimwengu ulio nje ya muda. Huko hakuna usiku na mchana. Huko kuna sehemu ambako ni nuru milele na kuna sehemu ambako ni giza milele. Kama uko nje ya muda ni muda wa kupokea majibu ya milele ya maisha yako ulipokuwa ndani ya muda au katika ulimwengu ambao una muda na matokeo ya matumizi yako katika huo muda.

MASWALI YA KUJIULIZA KUHUSU AINA HII YA KIFO

Yafuatayo ni maswali yanayokupeleka katika tafakuri ya maisha yako unayaoyaishi sasa. Kumbuka dhumuni la maswali haya ni kukuelekeza na kukuonesha mahali ulipo sasa. Kumbuka pia hutakiwi kujibu maswali haya ili tu kujifurahisha, usisahau kuwa utu uzima ni kujiambia ukweli na kuchukua hatua. Usijibu tu ilimradi umejibu, ikiwezekana uwe na kalamu na daftari ambapo utaandika maswali na majibu yako.

Yatumie majibu yako kuona hali yako ya sasa. Unapoona hali yako ya sasa, iko nafasi ya kufanya maamuzi. Kumbuka unaweza kuamua kuacha vitu vibaki kama vilivyo au kubadilisha vitu. Kumbuka mwenye maamuzi na maisha yako ni wewe mwenyewe. Hakuna mtu wa kukuamulia. Amua kufanya maamuzi kwa ajili ya maisha yako.

Kisha ni muhimu kuchukua hatua sahihi, kipimo cha ufahamu kamili ni kuchukua maamuzi sahihi na hatua sahihi. Kama utajua hali uliyonayo na usichukue hatua stahiki ni dalili ya ufahamu dhaifu au shida ya kiufahamu ambayo nayo unatakiwa kushughulika nayo sawasawa. Chukua hatua kujenga maisha ambayo yatakuwa na athari chanya sasa na baadaye baada ya dunia hii.

·        Umejiandaaje juu ya kifo hiki (je una hofu)?

·        Je maisha yako yanakuonesha utaingia katika umilele gani (mwema au wa uovu)? Kumbuka Mungu haamui uingie wapi, amekupa nafasi ya uchaguzi

·        Je utapewa thawabu gani ya namna ulivyotumia muda wako hapa duniani?

·        Je kusudi lako uliliishi hapa duniani? Na utalipwa malipo gani? Mema au mabaya? Kumbuka utavuna ulichokipanda

·        Je maisha yako kabla ya kifo yanamfurahisha Mungu na kumfanya ajivunie uwepo wako duniani?

·        Je ni alama gani yenye maana utaiacha utakapoondoka duniani?

Je nani atasoma wasifu wako?

MUNGU akubariki, usikose sehemu inayofuata.

Comments