RASILIMALI 7 AMBAZO KILA MWANADAMU AMEPEWA - sehemu ya 7

RASILIMALI 7 AMBAZO KILA MWANADAMU AMEPEWA

1. MUDA

MATOKEO YA KUFA KIROHO

Kila kitu kinachofanywa kina matokeo Fulani katika maisha. Ikiwa tutafanya mambo tukidhani hatutapata athari Fulani basi tunajidanganya. Kumbuka tutawajibika kwa matokeo yote ya sisi kufa kiroho kama vile ambavyo Adam na Hawa walibeba matokeo ya yale waliyoyafanya au ya wao kujitenga na Mungu au kufa kiroho.

Karibu tujifunze mambo haya:-

·        Kutengwa mbali na Mungu

Ukitengwa mbali na Mungu unatengeneza mazingira ya kutopata msaada wa Mungu katika maisha yako. Na unapokosa msaada wa Mungu katika maisha yako ni hatari sana. Kutengwa mbali na Mungu kunayafanya maisha yako yawe na walakini.

Maisha ya mtu aliyetengwa mbali na Mungu kuna namna ambavyo anakosa Amani ndani yake. Ndani yake anakosa kutosheka kwa roho, roho yake itamuendesha kutafuta mahali pa kupata utulivu hata kama siyo utulivu sahihi. Ndiyo hapo mwisho wa siku anajikuta anaingia katika maisha ya uovu.

Kukosa furaha katika maisha kunaleta matokeo mbalimbali hasi ambayo siyo sawa kabisa katika ubinadamu. Watu kunywa pombe na aina zote za ulevi, ni matokeo ya kukosa furaha na kutafuta burudani mahali ambako hakuna burudani sahihi. Kumbuka maandiko yanasema, tubuni basi mrejee, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwepo kwake Bwana. Mungu anapokuwa karibu na wewe ndipo unapopata furaha au burudani ya kweli.

Wakati huo huo vitu ambavyo utavifanya vichukue nafasi ya Mungu katika maisha yako navyo vitakuletea matokeo mabaya. Kumbuka mtoto wa nyoka ni nyoka. Hivyo chochote kinachozaliwa na ubaya ni ubaya. Ndipo unapokuja kuona matokeo ya uasherati, uzinzi, ulevi na yafananayo ambayo wengi huona yatawapa furaha.

Furaha unayopata katika vitu hivyo haitakufanya utosheke, bali utazidi kuwa mtumwa wa vitu hivyo na mwisho wa siku hatari nyingi zaidi zinaweza kujitokeza. Hivyo usijidhanie kuwa unafanya vyema kuondoa nafasi ya Mungu katika maisha yako kwa vitu Fulani Fulani, bado hatari iko palepale na kutotosheka pako palepale.

·        Tiketi ya kuingia Umilele wa uovu

Kufa kiroho ni tiketi inayokupeleka moja kwa moja pabaya. Inayokupeleka kuzimu. Inayokupeleka katika umilele wa ubaya au wa uovu. Na kumbuka katika umilele wa uovu, kama lilivyo jina lake hakuna mambo mema huko. Huko kuna mambo mabaya tu kwako.

Umilele mbaya uliandaliwa kwa ajili ya adui. Na yeyote aliyekufa kiroho ni sehemu yake. Aliyeko mbali na Mungu amejisajili kuwa raia wa ulimwengu wa umilele wa uovu. Na kama umejikatia tiketi, kama hautarudi kwa Mungu tiketi yako bado ina thamani katika ulimwengu huo na mara utakapoondoka katika ulimwengu huu utajikuta moja kwa moja umeingia huko hata kama hautaki.

Watu wengi wanasema hawataki kuingia katika umilele mbaya kwa maneno lakini maisha yao yanawaongoza kwenda katika umilele wa uovu. Kumbuka hata kama uko duniani, siku zote ni lazima utakuwa katika umilele mojawapo uwe mwema au mbaya. Na maisha yako mpaka sasa yanakupa picha ya wapi utaishi.

Kumbuka hakuna kuwa katikati. Ukiwa katikati tu Mungu mwenyewe atakutema (atakutapika). Hapo hakuna mjadala ni suala la maamuzi ambayo yapo kwako. Kama hautaki kuingia katika umilele wa uovu amua kukata tiketi  ya maisha ya umilele mwema ambao unatokana na kuwa karibu na Mungu au kuwa hai kiroho.

·        Kuwa chanzo cha migogoro na matatizo

Yeyote aliyekufa na kiroho, hutumiwa na adui ili kuendelea kuleta mabaya katika dunia yetu. Badala ya kuleta mambo mema ambayo Mungu anataka ulete unakuwa wakala wa giza (ulimwengu wa uovu). Iwe unataka au hutaki,  kama utakuwa umekufa kiroho ni lazima uwe wakala wa giza. Kumbuka Paulo anasema lile nisilolitaka nalifanya, kwa sababu Yesu hakuwepo katika maisha yangu, lakini sasa yuko nafanya lile nalotakiwa kufanya ambalo ni sahihi.

Watu wengi wanasema hawataki kuwa chanzo cha migogoro. Lakini maisha yao kama hayana Mungu wamejipa uwakala wa migogoro na matatizo. Kumbuka Mungu alipoumba dunia aliona ni vema. Kama ni vema basi hakuna matatizo. Matatizo yamesababishwa na watu kuwa mbali na Mungu. Adui anatumia nafasi ya wao kujitenga na MUNGU ili watumie kufanya maovu yake. Huji kumuona adui mtaani anazurula ili kuwafanya watu wafanye maovu, bali atawatumia watu ambao wamejitenga mbali na Mungu ili wafanye maovu.

Kumbuka dhumuni la kuubwa kwako ni ili uwe sehemu ya waleta mambo mema duniani. Kama siyo sehemu ya mema  basi ni sehemu ya mabaya. Kama uko mbali na Mungu unakuwa karibu na adui na kuwa wakala wake hapa duniani. Kumbuka adui hajawahi kuiwazia mema dunia. Hata kama hayo mabaya huonekana mema, kumbuka hujivika sura ya malaika ili watu wamkubali. Lakini matokeo ya mambo hayo ni mbaya. Siku zote usifanye kitu bila kufikiri, fikiri matokeo yake ni nini?

Matokeo ya uovu siku zote ni mabaya na matokeo haya ndiyo yanaoigharimu dunia. Kila jambo baya unaloliona ni matokeo ya watu ambao waliamua kujitenga mbali na Mungu na kuamua kuwa wakala wa adui. Yamkini hata mimi na wewe kuna mambo ambayo tumeyasababisha ambayo kwa kweli ni mabaya sana. Ni wakati wetu wa kufanya maamuzi mazuri ili kuwa sehemu ya mema duniani.

NAMNA GANI TUNAWEZA KUFUFUKA NA KUWA HAI KIROHO

Yafuatayo ni mambo ya kuyazingatia ambayo tukiyafuata yatatusaidia kuwa hai tena rohoni. Yatatusaidia kuwa karibu na Mungu tena. Kumbuka mambo haya si ya kuyasoma tu, bali kuyachukulia hatua katika maisha yetu, na nani ajuaye kuwa umepata nafasi hii ya kujifunza haya kwa sababu maalumu ya kurudi kwa Mungu.

Karibu tujifunze:-                                   

·        Kukubali ukweli

Siku zote katika maisha ili ufanye mabadiliko ni lazima ifike mahali uone ukweli na uukubali. Hakuna mabadiliko kama hakuna kukubali ukweli. Ukweli siku zote haubadiliki bali sisi tunatakiwa kubadilika na kuukubali na kuufuata. Kama hatutaukubali siyo kwamba utabadilika na kuwa uongo. Ukweli utabaki kuwa kweli. Ni sisi ndio wa kuamua katika huo ukweli, japo maamuzi yetu hayatauathiri kweli bai sisi wenyewe kwa namna chanya au hasi kulingana na maamuzi yenyewe.

Kuna watu ambao wanapenda kujihesabia haki. Hawataki kuuona ukweli na kuukubali. Wanajiona wako sahihi sana. Ukweli ni kuwa endapo ukiona hatari, na usikubali kuwa hatari inakuja na usichukue hatua, hatari hiyo haitaondoka bali itakukumba na kukufanya majeruhi.  Kama umekosea kubali ukweli. Kama umekufa kiroho na unaona kabisa katika dalili zile tulizojifunza, hakuna haja ya kujifanya huoni kubali ukweli.

Kuna wengine waswahili wanasemaga wanakaza fuvu yaani hawataki kuelewa kitu. Wameamua maamuzi yao, hawasikii lolote.  Wako sawa lakini hawako sahihi ikiwa walichoshikilia kitawaletea matokeo mabaya. Usilazimishe unachokishikilia kiwe ukweli, kama ukikutana na ukweli wenyewe basi ukubali na uchukue hatua.

Kumbuka siku zote maamuzi bado yapo kwako.

·        Kufanya maamuzi sahihi na chukua hatua sahihi

Ukikubali ukweli amua kuamua. Amua kufanya maamuzi sahihi. Usiseme umeukubali ukweli na huku umebaki pale pale hapo hujaukubali ukweli bali umejifariji tu ili kujidanya. Fanya maamuzi sahihi. Chukua hatua sahihi. Maamuzi sahihi ni kuamua kumrudia Mungu wa kweli. Kuna miungu wengi yamkini hata wewe umejifanya mungu wako mwenyewe. Lakini ukweli uliosimama imara ni kuwa MUNGU WA KWELI NI MMOJA. Yeye pekee ndiye wa kweli.

Maamuzi sahihi ni kumrudia Mungu wa kweli. Kumbuka hatua nyingi wamechukua wanadamu ili kumrudia Mungu. Lakini Mungu ameweka njia au hatua sahihi na ya kweli ya watu kumrudia yeye. Njia sahihi ni Yesu Kristo. Huyu alitolewa na Mungu kuwa sadaka ya dhambi zetu. Alitolewa kuwa njia ya sisi kufika kwa Mungu. Kupitia Yesu Kristo unapatikana wokovu wa kweli. Kunapatikana uhakika wa kuwa na Mungu na ushindi juu ya dhambi ambazo watu huona haiwezekani.

Kama mtu akimkubali Yesu Kristo moja kwa moja anajiungamanisha na Mungu na kumrudia yeye. Hatua sahihi ni kumkubali yeye kama mwokozi wa maisha yetu. Kukubali kuwa Mungu amemleta Yesu Kristo ili atuunganishe na Mungu. Na kama mtu akikubali moja kwa moja anamaanisha kuwa Mungu yuko sahihi.

Unapotafuta njia yako kumrudia Mungu, unamaanisha njia ya Mungu siyo sahihi. Na kama unaonesha hivyo basi hatakuwa karibu na wewe. Ikiwa unamuona siyo sahihi huwezi kuhitaji msaada wake. Hivyo hata Mungu mwenyewe hatakurudia wewe. Ukimpokea Yesu Kristo unampokea Mungu mwenyewe.

·        Kutubu na Kurejea kwa Mungu

Hili ni jambo la tatu la kuzingatia ikiwa unataka kuwa karibu na Mungu. Amua kumuomba Mungu msamaha. Muombe akusamehe. Yeye ni Mwingi wa rehema Mwenye Kurehemu. Yeyey si mgumu kiasi kwamba mtu kwa wa moyo wa kweli akiomba msamaha kwake. Mungu atamkaribisha kwake.

Kumbuka njia sahihi ya kumrudia Mungu, ni kuomba msamaha kupitia jina la Yesu Kristo. Jina lake ndiyo kibali cha maombi yako kupata nafasi kwa Mungu. Hakuna kupata kurudi kwa Mungu kupitia njia nyingine isipokuwa kwa kupitia jina la Yesu Kristo. Yeye ndiye aliyeidhinishwa kuwaunganisha watu na Mungu wa kweli.

Rejea kwa Mungu. Omba toba. Omba kwa mzigo Mungu akusamehe. Na kwa kuwa utatumia jina la Yesu Kristo, yeye atakusamehe kabisa, atazisamehe dhambi zako. Na atakufanya kuwa mtoto wake. Na hapo utaanza kuona msaada wake katika maisha yako.

·        Kuishi katika maagizo yake

Jambo la nne muhimu sana ni kufuata maagizo ya Mungu. Kumbuka kama utajaribu kufuata maagizo ya Mungu kabla ya kuomba toba kwa Mungu kupitia Yesu Kristo kazi yako ni bure. Hii ni kwa sababu Mungu anaanza kuhesabu maisha yako na matendo yako baada ya wewe kuingia katika ufalme wake. Mungu hapo anakuhesabu kuwa mtu mwingine na maisha yako yataanza mahesabu mengine.

Amua kufuata maagizo ya Mungu. Jifunze maagizo yake. Kumbuka yeye ametoa maagizo ambayo yamebeba Baraka zako. Fuata maagizo upate Baraka. Pia vilevile, kutii kanuni zake kunamfanya awe karibu yako zaidi.

Kumbuka kuwa karibu naye kutakusaidia kutimiza mambo uliyopewa kuyafanya katika hii dunia katika muda uliopewa. Na utafanya sawa sawa na mapenzi yake. Tafuta kuongozwa na Roho Mtakatifu. Tafuta kufanya yale anayoyataka Mungu.

Endelea kuwa na bidii ya kumpendeza Mungu. Endelea kupambana vita sahihi ya upande wa Mungu. Endelea kumtafuta Mungu na kuwa karibu naye ili uendelee kufaidi mazuri kutoka kwake.

Tafuta mahali ambapo watu wanamwabudu Mungu halisi katika roho na kweli. Watu ambao wameokoka. Tafuta watu hao na uwe karibu nao. Tafuta mtumishi wa kukulea kiroho na kukupa miongozo mbalimbali. Endelea kukaa kwa Mungu. Unaweza kuona kama wakati mwinginekuna ugumu lakini ni jambo la kawaida. Ukikumbuka kuwa kuna mambo ambayo ya thamani ni lazima yalipiwe gharama kubwa zaidi ya yale yasiyo ya lazima.

·        Furahia uwepo wa MUNGU katika maisha yako

Hii ni sehemu ya mwisho. Hakikisha unafurahia kuwa karibu na Mungu. Mtazamo wako juu ya Mungu uendane na mtazamo wa Mungu juu yako na hapo ndipo utakapofaidi maisha yako.

Hakikisha unakuwa mahali ambapo Mungu amekuweka. Hakikisha unapokuwa na uhitaji unampelekea Mungu. Jifunze kuwe na ushirika wako binafsi na Mungu. Usitafute kumwambia kila mtu juu ya jambo unalopitia, unaweza kukutana na mambo magumu kwa kuwaambia watu mambo yanayokusumbua (isipokuwa watu unaowaamini na wa kuaminika kweli) na mwisho wa siku ukajikuta katika hali mbaya. Muhimu ni kujua kuwa MUNGU anatakiwa kuwa wa kwanza katika maisha yako, mambo yakienda sawa awe wa kwanza, yasipokaa sawa, awe wa kwanza. Awe wa kwanza kujua mambo yote yanayokusibu. Yeye anasema, NJOONI KWANGU NINYI NYOTE MSUMBUKAO NA WENYE KULEMEWA NA MIZIGO NAMI NITAWAPUMZISHA.

Barikiwa sana!!!!1

Comments