RASILIMALI 7 AMBAZO KILA MWANDAMU AMEPEWA - sehemu ya 9

 

CHANZO CHA HOFU

Sababu kuu ya hofu katika maisha ya wanadamu ni WAKATI ULIOPITA. Fikra zetu zinaendeshwa sana na wakati uliopita kuliko wakati tuliopo na ujao. Watu wengi wanatafsiri uwezo wao na hali zao za sasa kwa wakati uliopita. Na ndivyo adui alivyowashinda wengi. Yeye hukutazamisha katika wakati uliopita. Mungu anakutazamisha wakati ujao. Mungu anautafsiri wakati wako wa sasa kwa wakati ujao na ndiyo maana mawazo yake si kama ya wanadamu wawazavyo.

Tujifunze kwa mfano huu mmoja, Wana wa Israel walipata ujasiri wa kutoka utumwani Misri kwenda nchi ya ahadi. Na ndivyo Mungu alivyowatazama wao. Lakini walipofika bahari ya Shamu, wakaikumbuka Misri, walipogeuka nyuma katika wakati uliopita wakamuona Farao akija na jeshi lake, katika fahamu zao halikuwa lile jeshi bali maisha waliyoyapitia kule yanawapa picha kuwa Farao atawafanya nini na ndiyo maana wanalalamika kuwa wameletwa kufa, na ndiyo maana katika kizazi chao hakuna waliofika katika nchi ya ahadi isipokuwa Yoshua na Kalebu.

Mungu anakuona kwa wakati wako wa kesho na siyo jana yako. Ndiyo maana anasema anautangaza mwisho mwanzoni. Mungu hatishwi na jana yako. Mungu hasumbuliwi na nani ulikuwa jana bali utakuwa nani katika wakati ujao. Na wakati huo huo adui anakuona katika wakati uliopita. Yeye anakutazamisha wakati wako uliopita ili uutumie kutafsiri wakati wako wa sasa na ujao na hapo ndipo hofu huwashika wengi katika maisha yao.

Wakati unataka kufanya kitu, yeye anakumbusha kuwa kule nyuma ulifeli, na utaona huwezi kwa sababu hata jana ulifeli. Unapotaka kutumia uwezo wako katika mambo Fulani Fulani anakuonesha juzi ulishindwa na leo huwezi. Mara unapokubaliana na mawazo yake basi tayari hutachukua hatua yoyote katika maisha yako na kuleta matokeo chanya.

Fikra zilizokufa ni zile ambazo zimejazwa sana na wakati uliopita kuliko wa sasa na ujao. Kumbuka wakati uliopita huwezi kubadilisha yaliyoko ndani yake. Lakini unaweza kubadilisha yaliyoko katika wakati ulio nao.  Kama fikra zako zimejazwa sana na wakati uliopita (hasa mambo Fulani Fulani hasi) jua kabisa uko hatarini na fikra zako zinakwenda kudumaa na kupotea kabisa. Kumbuka wewe umeumbwa kuwa mtu wa mabadiliko kila siku, hivyo jana yako siyo kitu bali leo yako na kesho yako.

Kuipa nafasi jana ni kukaribisha kifo katika maisha yako. Taarifa nyingi za jana hupoteza uwezo wako. Ikiwa marafiki wako ulionao wamejaa jana yako na zao kuliko leo na kesho upo hatarini. Kama mambo unayoyafuatilia yamejaa jana kuliko leo na kesho tena jana yenyewe ni hasi, upo katika hatari kuu maishani.

 

NAMNA YA KUISHINDA HOFU

Namna rahisi ya kuishinda hofu yako ni moja tu, JIACHANISHE NA VILE ULIKUWA JANA. Watu wengi waliofanikiwa ni wale walioamua kuwakataa wao waliokuwa jana. Mkatae yule ambaye ulikuwa jana. Achana naye katika maisha yako hatakufikisha popote. Mtu ambaye unatakiwa kuwa bora zaidi yake ni yule ambaye ulikuwa jana na si vinginevyo. Muepuke wa jana kwa nguvu zako zote.

Na kumbuka tabia huondolewa kwa tabia, hali huondolewa kwa hali, taarifa huondolewa kwa taarifa. Hivyo basi, kama unataka kuondoka katika jana yako, jaa katika leo yako na kesho yako. Itafsiri leo yako kwa ile kesho yako, maana Mungu anakuona kwa ile kesho yako, anakuona upo nchi ya ahadi hata kama upo Misri utumwani. Hatishwi na utumwani uliko bali anakusudia kutoa msaada wake uingie katika nchi ya ahadi.

Ili kujikita katika leo yako na kesho yako, mambo yafuatayo ni muhimu sana

 

Ujue Uhalisia Wako

Ni lazima uujue uhalisia wako ili uishinde hofu. Lazima ujifahamu wewe ni nani hasa. Na ni muhimu kujua kuwa anayejua uhalisia wako ni Mungu pekee. Wanadamu wanaweza kusema mengi kuhusu wewe lakini Mungu aliyekuumba anakujua na alikujua vyema kabisa hata kabla hujazaliwa. Hakuna mahali pengine unaweza kuondoa hofu zako.

Fahamu Mungu anakuonaje wewe hasa. Mungu katika Mwanzo 1:26-28 na katika sura ya 2 anakuona kama:-

·        Mtawala

Kuwa amekuumba ili utawale kila kitu. Amekupa uitawale jana yako, leo yako na kesho yako. Amekuumba ili utawale mazingira yako. Amekuumba ili kila kitu kiwe chini yako ana anatamani sana uwe mtu mkuu sana. Mungu alipokuumba aliiona dunia ndani yako. Mungu aliyaona mataifa kupitia wewe. Mungu anapokuangalia anaona wazo wale ambalo lina sababu Fulani maalumu ya kuwepo duniani.

·        Mtu mwenye kuzaa matunda

Mungu anapokuangalia anaona matokeo na utendaaji katika maisha yako nay a wengine. Anaona kuwa unaweza kuunda vitu na vikatokea. Anaamini kupitia wewe dunia itajazwa wanadamu, itajazwa maarifa, itajazwa hekima, itajazwa ubunifu na mengine mengi.

Mungu anapokuangalia anakuona kama mbegu ambayo ameipanda katika dunia ili izae matunda na matunda hayo yapate kukaa. Na wewe utazaa matunda yenye mbegu ndani yake na kwua na hayo matunda yatatoa mbegu na hizo mbegu zitakuwa matunda na mbegu itatoka na hivyo ndivyo ambavyo Mungu anakusudia kuwa dunia ijazwe na uzuri wa Mungu kupitia wewe.

 

·        Mtu wenye uwezo na nguvu

Mungu anaona uwezo ndani yako ya kutunza vitu mbalimbali katika maisha yako. Mungu anaona uwezo wa kulima bustani. Mungu anaona kuwa una uwezo wa kufanya kazi na ikaleta matunda an ukayafaidi wewe na wengine. Mungu anapokuona anaona uwezo usio wa kawaida. Haoni yake unayoyaona wewe kuwa yatakutesa haoni.

 

Mungu anakuona kuwa wewe unaweza kufanya kazi aliyokupa. Kuwa una weza kufanya vitu vikatokea. Anaona kuwa unaweza kufanya vitu vyenye maana. Mungu anakuona katika namna ya kipekee sana.

 

·        Mtu wa kuaminika

Mungu alipokuumba alikuamini. Na ndiyo maana mpaka sasa bado uko hai. Kwa sababu yeye tu amekuamini. Hivyo anapokuona anaona wewe ni mtu ambaye dunia inaweza kukuamini na ukafanya kitu chenye matokeo katika dunia hii ambayo ina mambo mengi yanayohitaji kuwekwa sawa.

 

Mungu anaona kabisa kuwa wewe unaweza kuwa mwaminifu na unaweza kuaminiwa na kupewa majukumu mazito na ukayatekeleza usipogeuka kwenda upande. Mungu hakuoni kama mtu ambaye hastahili kuaminiwa.

 

·        Mtu wa kuheshimika

Anasema amekuumba kwa sura na kwa mfano wake. Amekuumba na kukupa heshima yake. Bila kujali unaonekana kama hufai. Hofu inazaliwa pale unapijiona kuwa hufai na hapo unaona hauna maana wala thamani yoyote.

 

Mungu anaiona thamani yako hata kama wengine hawaioni. Mungu anaona kabisa wewe unastahili kuheshimiwa kama utakaa katika nafasi yako. Mungu anaona kabisa kuwa wewe heshima ni ya kwako hata kama kuna aibu umepitia hapo jana bado heshima yako hajaiondoa katika maisha yako.

Hizo ni baadhi ya sifa au namna ambavyo Mungu anakuona wewe na ndiyo maana alikuwa radhi kumtoa mwana wake wa pekee msalabani ili uokolewe. Thamani yako ni sawa na thamani ya damu ya Yesu msalabani. Kama usingekuwa wa thamani kwako basi ule mfumo wa damu za wanyama ungeendelea mpaka leo kwa utakaso na mengine.

Mpe Mungu nafasi ya kwanza maana yeye anakujua vizuri. Wakati Gideon amejificha, Mungu anaagiza malaika akamuite shujaa asiogope maana yeye ni shujaa hata kama amehjificha. Ni kweli maadui zao walishinda jana lakini bado yeye ni shujaa kiasi cha kuwaongoza wengine kuwashinda hao maadui waliokuwa wakiwashinda katika wakati uliopita.

Mungu anavyokuona ni tofauti na vile unavyotafsiriwa na jana yako. Yeye bado anakuwazia mema. Hakuna hofu yoyote ya kukuendesha. Hakuna hatari yoyote ya kukutisha kiasi cha kushindwa kuchukua hatua katika maisha yako. Daudi anasema Mungu ni Mwamba wa wokovu wake je mwanadamu atamtenda nini, nini cha kumtisha nini cha kumuogopesha ni nini?

Jifunze kujiona Mungu anavyokuona.

 

Ione kesho yako kwa uhalisia

Nii ni namna ya pili (hatua ya pili katika kushinda hofu). Ni muhimu kuhakikisha kuwa kesho yako unaiona sasa. Vile Mungu alivyokuona tangu anakuumba ndivyo unatakiwa ujione. Si hivyo tu unajiweka kimkakati kwa ajili ya hiyo kesho yako. Kesho yako ione ipo mikononi mwako. Usiangalie nini unapitia au nini ulipitia angalia wapi unaelekea. Paulo anasema anahesabu mambo yaliyopita kama kinyesi (mavi), akiyachuchumilia yale yajayo. Yajayo yanafurahisha ni mazuri sana.

Weka maono, weka kesho yako katika maandishi. Ione kesho yako. Hakikisha unaandika maono yako. Mungu anamuagiza aandike maono kwenye ubao kuhusu kama ubao yasomeke kama maji. Andika maono yako na uwe unayapitia mara kwa mara. Kila wakati unavyotafakari maono yako ndivyo ujasiri na uhakika wa hayo mambo kutokea unauona ndani yako na hapo ndipo unapoweza kuchukua hatua.

Kiri yale unayoyaona kesho. Weka kaulimbiu, tiwa moyo na kesho yako. Kaulimbiu yako uitamke mara kwa mara. Weka mahali ambapo inaweza kusomeka na kuwa unaweza kufanya kitu Fulani cha maana katika maisha yako.

Jifunze kuandika mipango yako na malengo yako. Yaandike, yasome, yakiri kila wakati na utaona namna ambavyo unaanza kupata ujasiri wa kuchukua hatua.

 

Tafuta taarifa sahihi

Toa nafasi kwa taarifa sahihi zinazokuhusu wewe.  Epuka taarifa zinazoficha uwezo wako. Hata kama kuna watu wanasema wewe huwezi na kukuambia mambo hasi tu kila wakati, waondoe na uweke mambo chanya kuhusu hatima yako. Waza vile Mungu anakuwazia, vile Mungu amekukusudia uwe katika maisha yako.

Fuatilia hotuba za kujenga. Fuatilia mambo yanayoweza kukusaidia kuvuka ng;ambo na siyo kukubakisha pale ulipo.  Epuka kuangalia video zisizo na faida kwako bali zinaua uwezo wako wa utendaji na kukufanya uwe na hofu. Epuka mazingira hasi yanayoharibu utu wako katika eneo la ujasiri.

Soma vitabu. Sikiliza mafundisho sahihi. Jifunze Neno la Mungu kwa usahihi. Marafiki wasio na faida aachana nao kabisa. Watu ambao wanakufanya utende na kufikiria uovu epukana nao, jijenge kisha uje uwajenge na wao, kama hawataki kubadilika, usibadilike wewe kufuata mambo hasi tena.

Kumbuka uwezo wako wa kutafsiri mambo, kufanya maamuzi na kuchukua hatua unaathiriwa sana na taarifa zilizoko ndani yako. Kama umejaza taarifa chanya kuhusu mambo mbalimbali moja kwa moja unakwenda kufanya maamuzi sahihi na kuchukua hatua sahihi na utakuwa na ujasiri na siku zote maamuzi yako utaayaamini na utavuka ng’ambo kuelekea kule ulikokusudiwa na Mungu uwepo.

 

Jifunze kuomba msaada wa Mungu

Mungu siku zote huwatia nguvu watu hata katika nyakati ngumu. Na watu wote ndani yao kuna namna wanapata ujasiri baada ya kumuomba Mungu. Hivyo kadri unavyozidi kumshirikisha yeye aliyekuumba na akujuaye vyema atakusaidia sana kuyashinda mazingira na mambo yanayokufanya uwe na hofu na kushindwa kuchukua hatua katika maisha yako.

Tenga muda wa kuwa na ibada na wengine, huko utakutana na mambo ya kujenga na yatakayokusaidia kufika mbali. Jifunze kuomba na wengine, hapo utajenga umoja na mazingira ya kukusaidia kupata sapoti zaidi ili kufika juu zaidi. Upate watu waminifu ambao unaweza kushirikishana maono yako na wakakubeba kufika pale na kufanikisha kile Mungu amekusudia. Na kimsingi kadri unavyomuomba Mungu na kujiungamanisha na watu wake ndivyo anavyokuunganisha na watu sahihi ili kukusaidia kufika pale.

Watu wengi wanakuwaga na hofu kwa sababu wanaona hakuna watu wanaowatia moyo au wanaowabeba kwa namna moja ama nyingine kufika pale juu. Lakini unapojifunza kuomba msaada wa Mungu na kuwa mtu wa ibada anakuunganisha na watu sahihi. Siyo lazima ujipendekeze kwa watu, lakini Mungu mwenyewe anaweza kuwaleta kwako ili wakufikishe mahali sahihi kama vile ambavyo Mungu alimwita Anania ili amfikishe Paulo Mtume mahali Mungu anataka.

Watu unaowatafuta ili wakufikishe mahali Fulani, Mungu anawajua nayeye ndiye aliyewaandaa. Jifunze kumuomba Mungu ili akusaidie kukutana nao katika nyakati sahihi alizokusudia. Pia akusaidia kuwatambua maana wanaweza kuja kisha ukawaona sio. Dhumuni ni kuhakikisha unashinda hofu na kuchukua hatua kwa ajili ya maisha yako na maisha ya wengine.

 

Jijenge kitabia

Yafanye yale unayoyaona kesho kuwa tabia yako ya leo. Ijenge tabia yako kwa maono yako. Hofu ni tabia na inatakiwa kuondolewa kwa tabia nyingine. Kama hukuwa na tabia Fulani Fulani anza kuchukua hatua maana kama umemuomba Mungu na umejua vile ambavyo yeye anakujua ni kitu gani cha kukuzuia kuchukua hatua?

Kadri ambavyo unazidi kujifunza kubadili yale maandishi ya maono yako na mipango yako kuwa vitendo ndivyo ambavyo unaona kuwa unaweza zaidi. Usianze pakubwa Sanaa bali pale ulipo. Watu wengi wanasubiri mpaka vitu waone vimekamilika. Na ndiyo maana hawafanyi chochote. Usisubiri, chukua hatua kwa maelekezo sahihi na msaada wa Mungu sawasawa na mapenzi yake mema kwa ajili yako.

Fanya kitu Fulani. Fanya vitu. Usiishie kuomba. Maandiko yanasema, ombeni nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtaona, bisheni nanyi mtafunguliwa. Kuna haja ya kuchukua hatua hata kama siyo kubwa sana ilimradi ni hatua kuelekea kule Mungu anataka ufike. Kwa sababu hofu siku zote hukufanya ushindwe kuchukua hatua kwa ajili ya kehso yako. Unapofika katika hatua hii, jambo moja tu unatakiwa kuliogopa….. hofu yenyewe… iogope hofu. Ikimbie hofu maana huyo si rafiki mwema kwako hata kama anakufanya wakati mwingine ujone uko salama.

Kila hatua unayopiga inakupa motisha kwa ajili ya hatua nyingine kubwa zaidi ya jana. Maono yako ukiwa umeyavunja vunja katika hatua zinazofikika, hakika utayafikia na kesho yako itakuwa ni njema sana. Kumbuka muda ni rasilimali uliyopewa na Mungu ili ufike kule alikotaka ufike. Na kama umeishinda hofu unaweza kuutumia muda wako vizuri na ukafika kule unakotakiwa kufika.

Comments