NGUVU YA TAARIFA KATIKA MAISHA YAKO - sehemu ya 1

 

TAARIFA

Tunaishi katika kizazi cha taarifa. Tunaishi katika zama za taarifa. Katika zama hizi taarifa ndiyo hutafutwa zaidi kuliko chochote na yeyote mwenye taarifa ndiye mwenye nafasi katika dunia ya sasa.

Kila mahali na katika kila kona ya dunia taarifa ndiyo imekuwa kitu cha muhimu kuliko vyote. Mtu aweza kukubali kukosa vingine lakini hakuna anayetaka kupitwa na taarifa Fulani.

Watu wanaweza kuacha chakula, anaweza kuacha kazi Fulani ili kupata taarifa Fulani ambayo inawezekana kuwa ina umuhimu sana kwake kiasi cha kuacha mengine ili kuipata hiyo taarifa.

Watu wengi wanapata ajira kwa sababu ya taarifa. Watu wanapambana kuhakikisha kuna taarifa zozote zinatolewa mahali Fulani.

MAANA YA TAARIFA

Taarifa ni jumla ya mambo yote ambayo humfikia mwanadamu kutoka katika mazingira yake.

Kitu au jambo lolote ambalo unaweza kupokea kutoka katika mazingira yako hiyo ni taarifa kwako. Na taarifa yoyote ina sababu au athari kwa mhusika anayepokea hiyo taarifa. Na athari hiyo inaweza kuwa hasi au chanya kulingana na mwitikio wa anayepokea hiyo taarifa.

Chochote ambacho unakipokea ndiyo taarifa. Kumbuka kuna taarifa za ana mbili kuna taarifa hasi na taarifa chanya. Taarifa chanya ni ile ambayo inaonekana kumletea matokeo mzuri anayeipokea hiyo taarifa.

Lakini taarifa hasi ni taarifa ambayo huonekana kuleta matokeo mabaya kwa mtu husika anayepokea hiyo taarifa.

Kumbuka pia taarifa kuwa chanya au kuwa hasi inategemeana na mtu husika namna anavyoiona hiyo taarifa. Kuna taarifa ambayo inaweza kuonekana mbaya kwa mtu Fulani na wakati huo huo ikawa njema kwa mtu mwingine. Ndiyo maana akija mtu kutoa kitu Fulani kuna ambao wataenda na wengine hawataenda.

Na kuonekana huko ni matokeo ya mtazamo wa mtu katika wakati Fulani wa maisha yake hapo nyuma. Na hii inamaanisha kuwa taarifa Fulani ambayo imeshapata nafasi ndani yako huweza kukufanya uone kuwa taarifa Fulani ni sahihi au ni mbaya.

Kama ulikuwa na taarifa sahihi ikija mbaya utaona kuwa ni mbaya. Jambo lingine la kuzingatia ni kuwa kuna taarifa inaweza kuwa mbaya lakini kadri inavyopewa muda ndivyo inavyozidi kupata usahihi kwa anayeipokea na mwisho wake anaweza kuona ni sahihi.

Kwa maneno mengine kuna watu ambao walizipa nafasi taarifa mbaya ndani yao na mwisho wake wakaziona kuwa ni sahihi. Endapo ikitokea taarifa sahihi itaonekana kwao kuwa ni taarifa isiyo sahihi. Na hapo pia muda utaamua kama taarifa hii mpya itapata nafasi au la.

 

 

AINA YA WATU KUTOKANA NA TAARIFA INAYOJITOKEZA

Katika taarifa kuna aina tofauti tofauti ya watu kulingana na mwitikio wao kwa taarifa husika. Wakati kuna taarifa yoyote inajitokeza makundi yafutayato hutokea katika kuonesha mwitikio wao kwenye hiyo taarifa;-

·         Kuna watu wanaotoa taarifa

Hili ni kundi la kwanza kabisa katika mwitikio wa taarifa. Taarifa yoyote inapojitokeza wao mwitikio wao ni kuisambaza.

Wanaipa nguvu taarifa izidi kufika kwa wengi. Na wengine pia katika mwitikio huu wamejitengenezea ajira katika maisha yao kwa sababu watu wengine watawatafuta ili kupata taarifa Fulani ambapo hao inalazimu walipe gharama.

Ndiyo maana katika kizazi cha sasa mtu anaweza kujitengenezea mfumo wake ambapo hatumii nguvu kubwa sana ili kujiingizia fedha lakini anatumia nguvu ya taarifa kutengeneza maisha yake.

Hawa ni watu ambao taarifa yoyote inapojitokeza wanahakikisha wanakuwa wa kwanza kuipata na kuhaikikisha kuwa wao ndiyo wa kwanza kuifikisha popote au kuisambaza kila mahalia au mahali panapokusudiwa.

·         Kuna wanaopokea taarifa

Hili ni kundi la pili wakati taarifa inajitokeza. Watu hawa wenyewe wako wazi ili kupokea taarifa  yoyote inayojitokeza.

Watu hawa wanaweza kulipa gharama kuhakikisha wanapata hiyo taarifa inayojitokeza. Na wanahakikisha hawapitwi na taarifa. Kama kuna taarifa umeikosa kwao ukienda unaipata kwa ukamilifu.

Watu hawa siyo lazima wafanyie kazi taarifa wanayopata lakini wao wanachotaka ni wawe na taarifa tu bila kujali watafanyia kazi au la. Hawana mpango wa kuitumia kazi.

Ndiyo maana unaweza kuwakuta watu wanaonekana kuwa na taarifa nyingi lakini hawajazitumia katika maisha yao kuwaletea faida yoyote isipokuwa wao wamelipa gharama kuipata.

Wao ukikaa nao utaona wana vingi lakini katika maisha yao hautaona hivyo vitu ambavyo unawaisikia wakikuambia.

Kwa maneno mengine taarifa haiwi na faida wala hasara kwao isipokuwa hasara wanayoipata ni kulipa gharama ili kuipata hiyo taarifa.

·         Kuna wanaotekeleza taarifa

Hili ni kundi la tatu linalotoa mwitikio wakati taarifa inatokea ao inapojitokeza kwao. Wao taarifa inapokuja wanaifanyia kazi katika maisha yao.

Hapa napo kuna watu wa aina mbili katika miitikio. Kuna wale ambao wakipokea taarifa mfano mbaya wanapoiitikia wanahakikisha hawaathiriwi na ubaya wa taarifa hiyo. Lakini wengine wanapopokea taarifa hiyo hata kama ni mbaya wanaitekeleza hivyo bila kuichakata na mwisho wake wanapata hasara.

Wanaoifanyia kazi taarifa ndiyo ambao huona matokeo ya taarifa hiyo katika maisha yao. Na miitikio yao ndiyo huamua faida au hasara ya taarifa hiyo kwenye maisha yao.

Wao wanahakikisha kuwa hakuna taarifa ambayo hawajaifanyia kazi. Wao hawajisikii vizuri kuona taarifa inawapita na hawajaifanyia kazi na kuona matokeo yake.

Hawa ndiyo ambao wanaweza kukupa maelezo ya taarifa kwa uhalisia waliokutana nao baada ya kuifanyia kazi taarifa hiyo katika maisha yao na pia unaweza kuona matokeo ya taarifa waliyoipokea katika maisha yao na kuweza kujua ni aina gani ya taarifa waliipokea mpaka wakapata matokeo waliyoyapata.

·         Kuna wanaoikataa taarifa

Hili ni kundi la nne. Katika kundi hili wanapopokea taarifa iliyojitokeza wao lazima waikatae. Mwitikio wao ni kupingana na hiyo taarifa.

Wao taarifa inapokuja kwao inaonekana kuwa ni mbaya na hawataki kitu kibaya kwao. Hawataki kuisikia wala hawataki kuona mtu akiifanyia kazi. Wakiona mtu ameifanyia kazi wanamuonya vikali kuhakikisha na yeye anaiona kuwa ni mbaya.

Hawa wanaona kuwa taarifa inayokuja kwao inaleta athari au matokeo mabaya hivyo ili wasipatwe na mabaya ya taarifa hiyo hawaifanyii kazi wala kutaka kuipokea.

Katika kundi hili bila kujali usahihi wa taarifa au ubaya wa taarifa wao hawana mpango nayo. Hii inaweza kuleta athari Fulani kutegemeana na taarifa yenyewe. Mfano taarifa inaweza kuwa sahihi lakini wao wakaikataa na mwisho wa siku wakaendelea kukaa katika hali mbaya.

Wao hawataki kukubaliana na ukweli wa taarifa husika. Hawataki kuruhusu fahamu zao kuona kuwa taarifa waliyoipokea ni ya kweli. Kwa upande mwingine inaweza kuwa faida ikiwa taarifa ni mbaya wataona siyo ya kweli na wataepuka athari zake.

Endapo taarifa ni ya kweli na wao wakaiona ni mbaya hapo ndipo watakapopata hasara katika maisha yao.

·         Kuna wanaoshangazwa na taarifa

Hili ni kundi la tano na la mwisho katika upokeaji wa taarifa. Hawa wanapoipokea taarifa wanashangazwa na hiyo taarifa.

Unaweza kuona mwingine anaweza kupokea taarifa Fulani lakini kama vile haamini na kama vile anaamini yaani yupo katikati hapo na lolote linaweza kutokea kwake.

Wao wanaendelea kufuatilia hiyo taarifa kwa ukaribu ili kutihibitisha kile wanachosikia kuwa ni cha kwelia au la.

Wao wanaweza kuipokea taarifa na pia kuifanyia kazi endapo wataithibitisha kuwa ni kweli.

Pia kwa sababu wao wanaishangaa au wanashangazwa na taarifa waliyoipokea wakati unapoendelea zaidi na wanapotulia zaidi kuna uwezekano wa kuipa nafasi ndani yao na hapo wanaweza kuifanyia kazi.

Wao wanatafuta uthibitisho wa taarifa na utulivu ili taarifa kuwa halisi kwao na wa waweze kuifanyia kazi.

Athari ya taarifa kwao inaweza kuwa hasi chanya kulingana na matokeo ya kutendea kazi taarifa hiyo baada ya kuithibitisha na kutulia.

KUMBUKA

Wewe kuwepo katika kundi Fulani haimaanishi kuwa unatakiwa kuwepo hapo siku zote kuna uwezekano wa kuweka vitu sawa kwa sababu una nafasi ya maamuzi katika maisha yako.

 

MAMBO 7 YA MSINGI KUHUSU TAARIFA

Kuna mambo ya msingi ambayo unapaswa kufahamu kuhusu taarifa na mambo hayo yatakusaidia kwa namna moja ama nyingine katika maamuzi yako unayoyafanya katika mambo yahusuyo taarifa yoyote kwako.s

Yafuatayo ni mambo ya msingi ya kuzingatia sana kuhusu taarifa na unapaswa kuyafahamu na kuyapa uzito katika maisha yako.

·         Kitu chochote kinaweza kuwa taarifa

Kitu chochote kinaweza kuwa taarifa. Ni muhimu kufahamu hili.

Na kama kitu chochote kinaweza kuwa taarifa inamaanisha kuwa na sisi tunaweza kuathiriwa kivyovyote na taarifa husika ikiwa tutaipa nafasi.

Pia inamaanisha kuwa tunaweza kupata taarifa mahali popote. Taarifa hutufikia kutoka mahali popote, kwa mtu yeyote na muda wowote.

Kwa maana huyo hatuwezi kukwepa kupokea taarifa ila tunaweza kuamua juu ya taarifa.

Hatuwezi kuishi bila taarifa kwa sababu tunaishi na vitu, watu, na katika muda Fulani. Na ikiwa tuko hai basi taarifa hutufikia.

·         Taarifa hutufikia kupitia milango mitano ya fahamu

Milango mitano ya fahamu inajumuisha; macho, masikio, pua, ngozi na ulimi.

Chochote ambacho tunaweza kuona kinaweza kuwa taarifa kwetu bila kujali ni kibaya au kizuri.

Chochote tunachosikia kinaweza kuwa taarifa kuwa kwetu bila kujali unachokisikia kuwa ni chema au la.

Chochote unachoweza kukigusa, kukinusa au kukihisi kwako kinaweza kuwa taarifa.

Kwa kusema hivyo inamaanisha kuwa sisi wenyewe miili yetu ndiyo tunaohusika na taarifa duniani na siyo taarifa yenyewe kwetu.

Kwa maneno mengine tunaweza kuamua chochote kiwe taarifa kwetu ikiwa tutaruhusu mojawapo ya milango mitano ya fahamu ifanye kazi katika hicho.

Na pia ikiwa kuna taarifa kutoka katika ulimwengu basi kutakuwa na uhusiano wa karibu sana na milango mitano ya fahamu ili kuhakikisha kuwa hiyo taarifa inakuwa taarifa.

Matokeo yoyote katika taarifa yoyote kupitia milango mitano ya fahamu hayaepukiki kwa mwenye hiyo milango mitano ya fahamu.

·         Usahihi wa taarifa hutegemeana na mtu husika japo haithiri uhalisia wa taarifa yenyewe.

Yeyote anayeipokea taarifa ndiye atakayeona kuwa ni sahihi ama siyo sahihi.

Bila kuathiri ukweli kuwa wakati taarifa inakuwa ina uhalisia wake ndani yake kuwa ni sahihi au la.

Unaweza kuitafsiri taarifa yoyote kuwa sahihi au kuwa siyo sahihi. Hilo lipo katika uwezo wako japo haubadilishi taarifa bali kuitazama kwako hiyo taarifa ndiko kutakakokuathiri wewe mwenye kuipokea hiyo taarifa.

Na pia mtu anaweza kuifanya taarifa ionekane kuwa ni sahihi au siyo sahihi jinsi atakavyoamua kuitikia huyo taarifa na jinsi atakavyoifikisha kwa wengine.

Hii pia inamaanisha kuwa taarifa ya kweli inaweza kupotoshwa kwa watu japo hitaiathiri taarifa yenyewe kuwa iwe ya uongo bali itaonekana ya uongo kwa wanaopokea.

 

 

·         Taarifa hutengeneza mazingira ya taarifa inayofanana kukufikia kupokelewa kwa urahisi.

Hili ni jambo la muhimu unalopaswa kufahamu kuhusu taarifa.

Unapoipoeka taarifa Fulani na ikapata nafasi ndani yako kuna uwezekano mkubwa wa maisha yako kupokea taarifa zinazoendana na hiyo iliiyoko ndani yako.

Ukweli ni kuwa ikiwa taarifa moja inafanana na nyingine iliyoko ndani yako inakosa upinzani ndani na inakaribishwa kwa wepesi kwa sababu ile taarifa ina mazingira sahihi ya hii mpya kuingia ndani.

Ndiyo maana ni rahisi kumkuta kahaba ni mlevi kwa sababu ulevi unakuta mazingira yanatengenezwa na ukahaba huo. Hii ni kwa sababu mazingira ambako taarifa ya ukahaba imepetikana ndiko ambako kuna uwezekano mkubwa wa taarifa ya ulevi kupatikana pia.

Hii inamaanisha kuwa taarifa Fulani iliyoko ndani yako itakusababisha kutafuta mazingira yanayoendana na taarifa hiyo na ikitokea kuna taarifa nyingine zinazotoka katika mazingira hayo zinapata nafasi kwa wepesi.

Ndiyo maana ni muhimu sana kuwa makini na taarifa tunazozipokea.

·         Muda ambao taarifa inapewa huamua nafasi ya hiyo taarifa ndani yako na katika maisha yako.

Kinachoamua nafasi ya taarifa Fulani ndani yako na katika maisha yako ni muda unaoutoa kwenye hiyo taarifa.

Bila kujali usahihi wa taarifa yoyote unayoipata muda huamua nafasi ya hiyo taarifa kwako.

Hata kama taarifa ni mbaya lakini ukiipa muda katika maisha yako basi taratibu itageuka kutoka kwenye kuwa mbaya hata kuonekana kuwa sahihi kwako na hapo itakapoonekana sahihi basi inapata nafasi.

Kumbuka kuwa taarifa yoyote inayoonekana sahihi ndani yako ndiyo inayopewa nafasi kubwa kuliko taarifa nyingine zote. Hii ni kwa sababu mwanadamu siku zote anapenda kuwa katika sehemu salama (comfort zote). Hataki mahali pasipo na usalama.

Ndiyo maana kama jambo ni jipya siyo rahisi mwanadamu kulifanyia kazi ni mpaka pale atakapoona kuwa ni sahihi. Na ndiyo maana imekuwa ngumu kwa wengi kuacha baadhi ya mambo katika maisha yao. Kwa sababu wanaona yako sahihi hata kama ni mabaya na yanaathiri maisha yao iwe kwa kujua au kutokujua.

 

·         Maisha yetu yalivyo ni matokeo ya taarifa tulizozipa nafasi ndani yetu.

Hii inamaanisha kuwa kila kitu katika maisha yetu ni matokeo ya taarifa Fulani ambayo tuliiona ni sahihi na tukaipa nafasi bila kujali usahihi wake hasa.

Hii inamaanisha kuwa maisha yetu yanategemea taarifa. Na kila kitu tunachoamua katika maisha yetu ni matokeo ya taarifa zilizoko ndani yetu ambazo zimepeta nafasi.

Siku zote maamuzi tunayoyafanya katika maisha yetu juu ya mambo ni matokeo ya machaguo yetu katika baadhi ya taarifa zilizoko ndani yetu.

Hii inamaanisha kuwa tabia zetu, mienendo yetu na hatima za maisha yetu zinaamuliwa na taarifa zipi tunazozipa nafasi katika maisha yetu.

Kwahiyo, kwa maneno mengine hakuna mtu wa kumpa lawama juu ya maisha yetu. Kwa sababu hata kama tunaona wao wametuathiri kwa namna moja ama nyingine bado iko nafasi ya kubadilisha taarifa zilizoko ndani yetu ili maisha yetu yawe tunavyotaka yawe. HAKUNA WA KUMLAUMU JUU YA MAISHA YETU, SISI NDIYO WENYE MAISHA YETU NA NDIYO TUNAOTAKIWA KUYABEBA NA KUYAAMULIA NA SI VINGINEVYO.

·         Taarifa yoyote ndani yetu huondolewa pale tunapoipa nafasi taarifa nyingine iliyo kinyume na taarifa iliyoko ndani.

Hatuwezi kuondoa taarifa Fulani kwa taarifa inayoendana nayo isipokuwa nyingine ambayo ipo kinyume nayo kwa sababu kuna ukinzano wa taarifa.

Na ili kuondokana na taarifa mbaya ndani yetu lazima tujiweke katika taarifa sahihi. Kumbuka hata maandiko yanasema nanyi mgeuzwe kwa kufanywa upya nia (akili) zenu na pia msidanganyike, mazungumzo mabaya huharibu tabia njema.

Hapo tunaona kuwa ili tugeuzwe lazima tufanywe upya nia zetu na ili kufanya upya nia zetu yaani akili zetu kuna ulazima wa kuleta taarifa mpya zilizo tofauti au kinyume na zile zilizoko ndani.

Pia ni muhimu kujua kuwa mchakato huu wa kubadilisha taarifa siyo mwepesi na kuwa kunahitajika gharama na maamuzi magumu ambapo inakulazimisha kuweka mkakati wa makusudi kabisa kubadilisha taarifa zako kwa gharama yoyote.

Kadri ambavyo tutazidi kujiweka katika taarifa tofauti na zile zilizoko ndani yetu au zilizo kinyume na zilizoko ndani yetu ndivyo tunavyojiweka katika mazingira ya kubadilisha taarifa zilizoko ndani yetu na maisha yetu kwa ujumla. MAAMUZI YAKO KATIKA MIKONO YETU ILI KULIPA GHARAMA JUU YA MAISHA YETU NA SI MTU MWINGINE.

Comments