MATOKEO 5 YA KUKOSA UFAHAMU WA KIUNGU

 

Zaburi 82:5-8

Kila aliyezaliwa mara ya pili kupitia Kristo ni mwana wa aliye juu, na pia maandiko yanamuita “mungu”. Neno hili Mungu katika lugha ya kiebrania yanamaanisha magistrate/judge au governor yaani hakimu au gavana.

Kwahiyo,

a.    Aliyeokoka ni gavana, anamwakilisha Mfalme Mkuu anayeitwa Mungu duniani. Kwa maneno mengine, gavana anawakilisha uwepo wa mfalme, hivyo uwepo wa aliyeokoka duniani ni uwepo wa Mungu duniani.

b.    Aliyeokoka ni hakimu, maana yake amebeba hukumu ya Mungu juu ya mambo mbalimbali yanayoendelea duniani. Hata kama ni mabaya kiasi gani, yeye amepewa mamlaka ya kushughulikia. Tatizo siyo kuwepo kwa matatizo, tatizo ni kutosimama kwa watatuaji wa matatizo.

c.    Aliyeokoka ni mwana, kwahiyo kama Mungu alijidhihirisha kupitia Mwana yaani Yesu Kristo, anajidhihirisha pia kwa mwana kwa utendaji ule ule au zaidi ya ule aliokuwa nao Yesu.

NINI KINATOKEA HUYU MTU MKUU ANAPOKOSA UFAHAMU

1.    Kutembea gizani; badala yay eye kubeba nuru na kuwafanya watu waje, watu wanamkimbia kwa sababu yuko gizani na hivyo na yeye mwenyewe ni giza. Kumbuka ukiwa na nuru lazima mataifa na wafalme wakujie. Isaya 60. Kinachoamua nani akusikilize na akufuate, ni wewe kuwa nuru au kuwa giza (kutembea kwenye giza).

2.    Kutikisika kwa misingi ya nchi; kila aliyezaliwa mara ya pili ni msingi katika taifa au nchi yake. Yeremia aliwekwa kuwa nguzo (msingi) katika taifa lake (Yeremia 1:18). Misingi ikitikisika jengo lazima lianguke au kupata ufa. Tatizo la nchi kupotea, siyo la viongozi wa nchi, ni tatizo la wana wa aliye juu waliokosa ufahamu wa kubeba nafasi. Kunapotokea sintofahamu ni tatizo la watawala yaani waliozaliwa mara ya pili. Nchi kukosa maendeleo ni matokeo ya kukosekana kwa watu wenye ufahamu wa kiungu kwenye mifumo.

3.    Kufa kama wanadamu; tukumbuke kuwa kila aliyeokoka si mwanadamu wa kawaida. Si mtu kama watu wengine, yeye ni kiumbe kutoka mbinguni. Yeye ametumwa duniani kwa kazi maalumu. Yeye si kama wanadamu wengine, yeye ni mgeni duniani. Yeye hayupo kuongeza namba. Hivyo akikosa ufahamu, ataondoka hapa ugenini bila kuacha alama yoyote ya kukumbukwa kwa mema. Kumbuka, waswahili wanasema mgeni njoo mwenyeji apone. Lakini huyu mgeni na mpitaji akikosa ufahamu, hakuna wenyeji watakaopona. Hatakuwa tofauti na wale ambao hawajaokoka.

4.    Kuanguka kama mmoja wa wakuu; shetani alianguka kwa sababu ya kuharibika kwa ufahamu wake. Mwana aliyekosa ufahamu lazima atakuwa na kiburi na majivuno. Lazima apotee kwenye mstari kwa sababu ufahamu wa neno ndio unaomuwezesha mtu kuendelea kuwa mtu kati ya watu bila kuharibu nafasi yake mbele za Mungu na mbele za wanadamu. Ukitaka kuanguka kama shetani alivyoanguka, njia rahisi sana ni kubeba utukufu wa MUNGU. Na hili ndio tatizo la wengi waitwao watumishi wa Mungu.

5.    Kukosekana kwa hukumu; inafika mahali Mungu anaitwa ahukumu nchi (soma Zaburi 82:8) wakati hii nchi wamepewa wanadamu (Zaburi 115:16). Mungu amewaachia wana waihukumu dunia. Yaani waamue mambo yanayoendelea duniani. Kwa wao kukosa ufahamu kunafanya Mungu aitwe kuja kuhukumu badala yao. Kwa sababu magavana hawajui kilichowaleta hapa duniani.

Kumbuka, namna pekee ya kuwa na ufahamu wa kiungu, ni kulipa nafasi Neno la Mungu. Maandiko yanasema kuwa, kufafanusha maneno yako kwatia nuru na kumfahamisha mjinga (Zaburi 119:130). Tafuta kwa bidii kujifunza Neno la Mungu lisiloghoshiwa na utaona namna ambavyo utakuwa mwana mwenye matokeo kwenye kizazi chako.

Comments