KUONGEZA THAMANI YAKO

 Ndugu msomaji, karibu katika wikiendi nyingine ambayo Mungu ametupa kuwa hai tena na tupate nafasi ya kujifunza vitu vinavyoweza kuongeza thamani ya maisha yetu kama ilivyo ada.

Wikiendi hii tunajifunza juu ya Kuongeza Thamani Yako. Ni muhimu sana kujifunza jambo hili, ili ikusaidie kuwa mtu ambaye unaweza kuwa na nafasi kubwa kati ya watu ili kuwasaidia watu.

Nikukumbushe mambo kadhaa, hakuna mtu asiye na thamani. Kila unayemuona duniani ana thamani, lakini changamoto kubwa sana ambayo inaonekana ni kuwa thamani za wengi hazionekani. Kwahiyo, kuongeza thamani ni mchakato wa mtu kuionesha thamani aliyonayo.

Kumbuka, nafasi yako kati ya maisha ya watu inaamuliwa na thamani uliyonayo kati ya watu. Kwahiyo, kila mtu amebeba ufunguo unaoamua nafasi yake kati ya watu, ukiongeza thamani yako, umetengeneza nafasi kwenye maisha ya watu.

Ukweli ni kuwa, hata kama watu hawakupendi, njia pekee ya kuwafanya wakupe nafasi ni wewe kujiongezea thamani. Hata nafasi mbele za Mungu, ni matokeo ya mtu anayeiongeza thamani yake. Kila mtu ni sawa mbele za Mungu, lakini nani anafanya kazi naye ni matokeo ya thamani ambayo mtu ameitengeneza.

Ukitaka watu wafanye kazi na wewe, Mungu afanye kazi na wewe, kitu bora unachoweza kufanya ni kuhakikisha kuwa unaongeza thamani yako.

Tujifunze zaidi kuhusu namna gani ya kuongeza thamani yako.

 

#1. Kanuni Ya Ufahamu

Hii ni kanuni ya kwanza katika kuongeza thamani yako. Kanuni ya ufahamu ni kanuni nyeti sana. Tofauti ya mtu na mtu ni ufahamu ambao kila mmoja anao. Alivyo mtu ni matokeo ya kile anachofahamu kuhusu yeye, jamii yake na dunia yake kwa ujumla.

Namna pekee ya kuwa mtu anayeenda na wakati, mtu mwenye thamani kubwa zaidi, ni kuhakikisha kuwa unajenga ufahamu wako. Ni lazima ulipe gharama ya kujifunza zaidi mambo ya msingi ili uhakikishe kuwa unakuwa bora zaidi maishani.

Hapa tunaangazia zaidi ni vitu gani unalisha ubongo au akili yako. Na unacholisha akili yako hujumuisha vitu gani unaangalia, unavyosoma na kusikiliza. Wapi unatumia muda wako zaidi. Mtandaoni huwa unajifunza nini, unasoma vitabu gani, unaangalia muvi au aina gani ya vipindi vya televisheni.

Watu wengi wanatamani kuwa bora maishani, lakini hawataki kulipa gharama maishani, na matokeo yake kila siku wanabaki palepale huku wanasingizia wamerogwa. Huwezi kufika mahali ambako akili yako haijafika.

Kwenye maisha, utafanya unachofahamu, utaongea unachofahamu, utatetea unachofahamu, na utalinda unachofahamu. Na mambo hayo huonesha kwa watu wengine una thamani kiasi gani kwao.

Mwenye ufahamu, anaweza kushirikiana na wengine na kuhakikisha wanaona thamani yake kama ipasavyo.

 

#2. Kanuni Ya Maadili

Hii ni kanuni ya pili katika kuongeza thamani yako maishani ili kutengeneza nafasi ya kufanya kazi na Mungu na watu ukiwa hapa duniani na kuacha alama isiyofutika unapoondoka.

Tambua misingi yako ya maisha ya kila siku, ambayo uko tayari hata kugharimu uhai wao kulinda hiyo misingi. Mambo ambayo utayaishi mema maishani, na hautakubali kuyavunja bila kujali itakugharimu nini.

Ni muhimu sana ufahamu kuwa unaweza kuwa na kipaji, lakini maadili ukakosa, na mwisho wa siku hata thamani ya kile ulichonacho yaani kipaji, isionekane tena kwa watu na usisikilizwe popote na yeyote na kushindwa kutimiza wito ulioitiwa na Mungu.

Amua kutengeneza mtindo na mfumo wa maisha ambao utaulinda na kuuishi kila siku uwapo duniani, ambao hauendi kinyume na kanuni za Kiungu, na kuhakikisha kuwa watu wengine wanafaidika na maisha yako hapa duniani.

Jiwekee kanuni zitakazokuongoza, uziandike, uzifuate, na kuziishi. Angalizo, epuka kuweka kitu ambacho hautafanya, uwe mkweli kwenye kile utaenda kufanya lakini usiruhusu kuwa mvivu kwa kuacha kukaza kwenye maadili yako kwa sababu kadha wa kadha.

Jenga tabia yako, watu wengi wanapewa nafasi, lakini tabia mbaya walizonazo huwaondoa kwenye hizo nafasi, na kumbuka thamani inaamua nafasi yako. Shika maadili yako kama Yusufu, maana kadri unavyokaza kushika maadili unaongeza thamani yako na thamani yako inaamua nafasi yako.

 

#3. Kanuni Ya Ushirika

Hii ni kanuni ya tatu ya msingi, kanuni inayolenga ushirika wako na Mungu. Wekeza katika uhusiano wako na Mungu. Mungu ana maeneo mengi ya kukujenga na kukufanya uwe na thamani zaidi maishani.

Kuna wakati unaona kuna namna haufai lakini ushirika wako na Mungu unalinda thamani yako. Inakuhakikisha kuwa na thamani zaidi. Mungu ni wa thamani, na yeyote anayekuja kwake, huwa na thamani, na ndiyo maana Mungu hufanya kazi na wale ambao wanalinda ushirika wao na MUNGU.

Tenga muda wako wa maombi, muda wa kujifunza Neno la Mungu, jiepushe na dhambi, hudhuria ibada, wekeza muda wako katika ibada, ibada ni maisha na maisha ni ibada.

Unamuhitaji Mungu katika maisha yako zaidi ya unavyodhani, ni muhimu sana kuhakikisha una ushirika naye wa ndani zaidi. Yeyote anayekaa na Mungu anabadilika kufanania thamani itokayo kwa Mungu. Musa alivyokuwa na ushirika na Mungu, alibeba hadi utukufu wa Mungu.

Acha kulala lala, acha kupoteza muda, jenga ushirika wako na Mungu. Na kama unaishi maisha ya dhambi, tubu, mrudie Mungu na Yesu Kristo mwokozi atakusaidia.

 

#4. Kanuni Ya Mipango Na Tathmini

Hakuna maisha isiyo na mipango, ila tunatofautiana kile tunapanga kwenye hayo maisha. Maisha ni matokeo ya mipango yetu, si ajali.

Ukitaka kuongeza thamani yako, hakikisha unakuwa mtu wa malengo au mipaka. Epuka kuishi kiholela. Hakikisha kuwa una malengo yako yam waka, ikiwezekana pia hata miaka mitano au kumi ijayo.

Hakikisha kuwa unaifuata hiyo mipango. Andika mipango, usiwe mtu wa maneno, anza pale ulipo. Fanya vitu vinavyoeleweka. Kila mtu unayemuona mwenye nafasi, hufanya kazi na watu ambao na wao ni kama yeye, mtu wa mipango, hutoa muda wake kwa mtu wa mipango yenye tija na anayefanya kazi katika kile amepanga.

Fanya tathmini kila baada ya miezi mitatu, angalia kama kuna haja ya kuboresha mikakati ya kutekeleza malengo yako au mipango yako. Hakikisha unafanya tathmini ya kweli. Hakikisha kuwa unakuwa mtu anayejua kujichukua, na anayefanya vitu vinavyoeleweka mbele za Mungu hata kama kwa wanadamu bado havijaeleweka. Hakikisha kuwa unaanza kufanya, siyo lazima ufanye kwa ukubwa, anza pale ulipo.

 

#5. Kanuni Ya Uzoefu

Hii ni kanuni ya tano ya kuongeza thamani yako. Amua kukaa chini ya malezi ya watu wenye uzoefu katika eneo ambalo wewe unatamani kuwa bora au unahisi Mungu amekuita kufanya hapo.

Watu wenye uzoefu kwenye maisha ni muhimu sana. Hakikisha una baba wa kiroho, una walezi ambao kwao unawajibika, unatoa taarifa na maelezo ya unachofanya.

Watu hawa ni wa muhimu sana kwa sababu itakusaidia kuwa mwajibikaji, watu wengi wanaojaribu kujiongoza wenyewe mara nyingi huishia kuharibika na kutokuwa na chochote cha maana cha kuwapa watu.

Hakikisha kuwa unakuwa chini ya mtu fulani ambaye Mungu anakupa ili akulee na kukusaidia kuwa bora. Kila mwenye nafasi, ameaminiwa mahali, ni lazima aliwekwa na mtu. Wahenga wanasema, ukimuona kobe juu ya ukuta, ujue amewekwa, hajajiweka.

Wekeza hapo, wewe ni wa muhimu sana, una vitu vingi sana lakini unahitajika kuwa chini ya malezi. Wanaokulea ni kama mafundi seremala au wafinyazi, hukuboresha kadri wanavyokuona kuna shida mahali, na kuboreshwa huku, kunakufanya ubora wako au thamani yako kuongezeka zaidi na kuaminiwa na kumpendeza Mungu na wanadamu.

Ndugu msomaji, naamini kwa wikiendi hii, hayo yatakusaidia sana, anza kuyafanyia kazi, usisahau kuwa, mtu mwenye nafasi ni matokeo ya thamani yake, na thamani ya mtu inaoneshwa kwa kuongeza vitu fulani kwenye maisha yake.

Nakutakia wikiendi njema yenye thamani, tukutane tena wikiendi ijayo kwa ajili yam engine ambayo Mungu atatujalia kujifunza!!

Comments