Ndugu
msomaji, karibu tena katika wikiendi nyingine, ya kuongeza thamani katika
maisha yako. Na tupo katika mfululizo wa masomo yanayohusu umuhimu wa watu
maishani ili ufanikiwa. Na leo tunajifunza kuhusu aina tano za watu unaowahitaji
maishani ili ufanikiwe.
Katikaatika maisha kila mtu anahitaji kufanikiwa katika maeneo fulani fulani. Unaweza kutafuta kufanikiwa katika elimu, au uchumi, au mahusiano, au katika imani na kadhalika. Ni ukweli usiopingika kuwa hakuna mafanikio bila watu.
Kwahiyo,
kwa sababu mafanikio yanahitaji watu, ni muhimu tujifunze ni watu gani
tunaowahitaji maishani ili tufanikiwe katika eneo lolote lile.
Unahitaji aina zifuatazo za watu maishani;
1.
Walezi
Hii ni
aina ya kwanza ya watu ambao unawahitaji maishani ili ufanikiwe. Walezi ni watu
ambao wewe kibinafsi upo chini yao na wao wanakuongoza kwa namna moja au
nyingine ili kukufanya kuwa bora zaidi ya ulivyo sasa katika eneo ambalo
unakusudia kufanikiwa.
Anaweza kuwa
mlezi wa kiroho yaani baba wa kiroho, na walezi wengine wa kawaida katika
maeneo fulani fulani.
Walezi wako
watakuwajibisha, watakushauri, watakufundisha, na kukuongoza, na kukuadhibu
ipasapo ili kukusaidia usirudi nyuma kabisa maishani.
Hakuna mtu
anayeenda mbele ambako huko mbele hakuna watu walioko huko, lazima uwe na watu
ambao wamekutangulia mbele katika eneo fulani. Hao watu watakupa uzoefu muhimu
wa huko unakoenda ili kukusaidia kutopoteza muda, au fedha na rasilimali
nyingine ambako hakuna ulazima. Wengi kwa kukosa walezi, wamekuwa watu wa
kuinuka na kuanguka na kurudi chini kabisa kwa sababu hakuna mtu wa kuwalea.
Hakikisha
unakaa chini ya malezi, hakuna mtu anayetokea kama uyoga, hakuna mtu
anayeaminiwa ambaye hajulikani ametoka kwenye mikono ya nani. Hakikisha unamuomba
Mungu akusaidie kukupitisha katika mikono sahihi, ambapo katika mikono hiyo,
hautabaki kuwa mtu wa kawaida, lazima ubadilike.
Hata kama
una kitu kikubwa, bila walezi, hautakuwa mkubwa, hakikisha unakaa chini ya
malezi.
2.
Washirika
Hii ni
aina ya pili wa watu unaowahitaji maishani katika eneo lolote ili ufanikiwe. Hawa
ni watu ambao mko nao pamoja. Uko nao kiwango (level) moja, na wote mnaenda
mahali.
Kundi hili
ni muhimu sana maishani mwako kwa sababu linakupa joto, hamasa na moto wa
kuendelea mbele katika safari yako ya mafanikio. Hata Daudi alikuwa na watu 400
katika kundi hili, ambapo baadaye alikuja kufanya nao kazi akiwa mfalme.
Katika kundi
hili, wapo watu ambao watafanya kazi na wewe ukiwa katika mafanikio yako. Wako watu
ambao ukikaa nao unapata nguvu ya kuinuka tena, wanakusaidia kujua kuwa hauko
peke yako unayepambana, hivyo usije ukajisahau na kubweteka.
Kundi hili
ukikaa nalo, kazi kubwa ni kubadilishana mawazo, kushirikishana uzoefu
mbalimbali katika hatua ndogondogo ambazo mnapiga, kuulizana changamoto
mbalimbali ambazo zinawasaidia kuchochea hamasa ya kufatuta ufumbuzi na kusonga
mbele.
Kumbuka,
aina ya watu ulionao katika kundi hili, inaamua unaenda wapi. Ni kweli kuwa
walezi wana nafasi zaidi, lakini kundi hili linakuwa na muda mwingi zaidi na
wewe maishani kuliko kundi lolote, hivyo kama ukiwa na washirika ambao si
sahihi, uwe na uhakika, bila kujali mafanikio unayopaswa kuwa nayo, hautakuwa
chochote.
Kwahiyo,
ni muhimu uhakikishe kuwa kwa msaada wa Mungu, katika kundi hili unakuwa na
watu ambao ni sahihi, ambao kwa ushirika wenu, utajihakikishia kuwa unafika
mbali.
3.
Wahudumiwa
Wahudumiwa
ni aina ya tatu ya watu unaowahitaji maishani. Kundi hili, ni lile ambalo
linakupa sababu ya kufanikiwa na kuinuka katike eneo fulani maishani.
Hapa sasa
ninaangazia mafanikio yanayoacha alama maishani hata ukiondoka duniani, bado
utakuwa unaishi katika maisha au mioyo ya watu.
Kile ambacho
unafanya, ambacho katika hicho imekusudiwa ufanikiwe, je, watu wanafaidikaje
nacho? Kwa maneno mengine, kundi hili ni watu ambao wanahudumiwa na kitu chako
maishani.
Mfano wake,
ni kama vile ambavyo wewe ndugu msomaji, unapata kitu kupitia mimi, wewe ni
mhudumiwa, mimi ninakutumikia au ninakuhudumia kile nilichonacho. Faida yangu
ni pale ninapokuhudumia, na kadri ninavyokuhudumia kwa uaminifu na kwa ubora
ndivyo ninavyozidi kufanikiwa maishani katika hili eneo.
Mimi nakuwa
mhudumu, wewe unakuwa mhudumiwa, ninachofanya ni huduma. Kwahiyo, ukija kwangu,
unaondoka na huduma ambayo mimi nimekusudiwa kuitoa kwenye maisha yako.
Ndivyo inavyopaswa
kuwa, kuna watu maishani mwako wanahitaji huduma fulani, unapaswa kuwahudumia,
inaweza kuwa ni katika biashara, elimu ya mahusiano, mambo ya elimu, mambo ya
imani na kadhalika. Zote zinakuwa huduma, ambazo wewe unazitoa kwenye maisha ya
mtu.
Sasa,
lazima ujiulize wewe umepewa kitu gani kwa ajili ya watu, ukiboreshe, na
uhakikishe unakitoa kwa ufanisi na ubora kwa watu, na hapo unajitengenezea
nafasi zaidi ya kufanikiwa.
4.
Wanafunzi
Hawa ni
watu ambao wao wanajifunza katika hatua ndogondogo unazofanya. Kundi hili kazi
yake ni kukuangalia, na kukufuatilia na kupata kutiwa moyo na kidogo
unachofanya ili nalo lisogee mahali maishani.
Kundi hili
ni muhimu sana kwako kwa sababu, linakupa chachu ya kuwa bora ziadi ya hapo
ulipo. Linakufanya upige hatua zaidi ya sasa. Linakufanya ukase zaidi bila
kujali magumu. Hakuna mwalimu anayekubali kushindwa kirahisi mbele ya wanafunzi
wake.
Ukiishi huku
ukijua kuwa pamoja na kuwa maisha ni ya kwako, lakini hayo maisha ni kwa ajili
ya wengi, na kuna watu wanajifunza katika namna unaishi na kufanya unachofanya
hata kama ni hatua ndogondogo, utajikuta moja kwa moja unakuwa na hekima ya
kujichukua, unaongeza bidii, na unahakikisha kuwa hauwavunji moyo kwa kuharibu.
Kuna wanafunzi
wako nyuma yako, hata kama wewe unajiona ni mwanafunzi, kuna wengine wanakuona
ni mwalimu. Ukiishi kwa mtazamo huo, utahakikisha kuwa hauharibu maisha yako,
kwa sababu kuna uwezekano wa wengi kuanguka.
Hii itakupa
nidhamu ya kuishi, na hakuna mafanikio bila nidhamu, si tu kwamba unafanya kwa
sababu kuna watu wanakuangalia, ila ni kwa sababu unajua Mungu amekuamini
maisha yako kwa ajili ya watu wengi, hivyo hauwezi kukwepa nidhamu. Na mafanikio
yanachochewa na nidhamu, kila aliyefanikiwa alikuwa na bado ana nidhamu fulani
zinazotafsiri na kujenga mwendelezo wake katika eneo lolote.
5.
Wapinzani
Hii ni
aina ya tano ya watu unaowahitaji maishani. Unahitaji kuwa na wapinzani katika
safari yako. Ieleweke kuwa ninaposema wapinzani, simaanishi wewe unapingana
nao, bali wao ndio wanaopingana na wewe hata kama haujui.
Kila mtu
lazima awe na upinzani ili afanikiwe, lakini usitafute upinzani maishani. Kwa kila
mtu anayeelekea mahali, upinzani huwa unakuja hata bila kuitwa.
Kazi ya
upinzani ni kukuhakikisha kuwa, haujapendelewa kuwa hapo. Japo unaweza kuona
kama wanataka kukuangusha, lakini ni wajibu wao, ili kukuthibitisha katika
nafasi ambayo umeaminiwa na Mungu katika maisha yako.
Upinzani
upo, ili kutusaidia kujifunza vitu ambavyo, kama tungeambiwa kwa maneno ya
kawaida, tusingeweza kupokea au kuelewa. Kwahiyo, upinzani ni njia rahisi zaidi
ya kutusaidia kuelewa na kukuza ufahamu wetu katika eneo husika.
Nikukumbushe,
hakuna mafanikio nje ya ufahamu wako, kiwango ambacho unafanikiwa katika
ufahamu, huamua kiwango cha mafanikio ya maishani.
Usizikimbie
changamoto, na upinzani au wanaokuletea changamoto na upinzani, tafuta msaada
wa Mungu, uwe mbunifu, ili uweze kutoka hapo na vitu vya thamani.
Kazi ya
moto kwa dhahabu siyo kuiangamiza dhahabu, ni kuonesha ubora wa dhahabu ambao
wengine hawauoni kwa kawaida, ndivyo ulivyo upinzani kwenye maisha
yako,unafunua ubora ambao wengine hawauoni.
Ukiona kuna
upinzani maishani mwako, ujue kuna kilicho bora kinatafutwa ili kitoke nje,
kionekane na kiwe msaada kwa wengine, kazi yako ni kuhakikisha kuwa hicho
kilicho bora kinaonekana. Usiishie na kukaa kila siku kulaumu watu
wanaokupinga, jitahidi kutafuta kujua kile wanachokupinga, na kile bora
kinachotafutwa, jinoe hapo, na uhakikishe kuwa unafunua huo ubora ambao wengine
hawajawahi kuuona.
Upinzani
wa kina Sanbalati na Tobia, ulifunua ubora wa uongozi wa Nehemia ambao haukuwa
unaonekana akiwa mnyweshaji wa mfalme. Na kumfanya kuaminiwa kuwa liwali ya
Yuda.
Ndugu msomaji, ni imani yangu kuwa, unazidi kujijenga kiufahamu katika eneo hili, una unazidi kujiongezea thamani, ninakuombea uwe na wikiendi njema, na uendelee kufaidi thamani zilizoko humu. ukiweza kumshirikisha na mwingine, utakuwa umesaidia kuwaongezea wengine thamani, hakikisha una marafiki wanaojua chimbo ambalo linakuongezea thamani kila siku.
Mungu akubariki!!
Comments
Post a Comment
Thanks for your comment, God bless you!!!