Ndugu msomaji, karibu katika wikiendi nyingine ambayo tunaendelea na somo letu kuhusu, Mambo 10 Usiyoajua Kuhusu Watu.
Katika wiki iliyopita, tuliishia katika jambo la tao, karibu tuendelee na jambo la sita na kuzidi kuongeza thamani ya maisha yetu.
Jambo La #6. Watu Wana Udhaifu
Bila kujali mtu ni mkuu kiasi
gani katika ulimwengu, bado kuna udhaifu anao. Udhaifu huo ni muhimu kwa sababu
unamsaidia kuona haja ya kuhitaji msaada kwenye maisha yake kutoka kwa Mungu na
wengine.
Hata Paulo alikuwa na udhaifu
ambao ulimfanya awe mnyenyekevu na kuhitaji msaada wa Mungu kila wakati. Ukijua
kuwa watu wana madhaifu, hautajiona kuwa wewe peke yako ni sahihi na pia
wanapoharibu utajifunza kuwasaidia na kuwarejeza katika upendo bila kuathiri
kanuni zilizowekwa zinazoendesha maisha ya watu hapa duniani.
Kila mtu kuna mahali ana udhaifu
fulania ambao anahitaji msaada. Hata mimi kuna udhaifu ambao unanifanya niwe
mwanadamu kamili, na udhaifu huu zaidi sana unanifanya kuwa karibu na Mungu,
kwa sababu bila msaada wa Mungu siwezi kushinda udhaifu ambao wakati mwingine unaweza
kuleta mateso maishani.
Udhaifu wa mtu haupaswi kumfanya
mtu aubebe na kushindwa kuchukua hatua sahihi za kumsaidia. Udhaifu wowote
unaomshinda mwanadamu, unahitaji msaada wa Mungu wa Mbinguni. Kwahiyo, kama
kuna mtu unamuona ana udhaifu, au wewe una udhaifu, kitu muhimu zaidi
unachoweza kufanya ni kumrudia Mungu na kumpa nafasi ya kukusaidia katika huo
udhaifu.
Hakuna mjanja zaidi ya mwingine
maishani. Kila mtu anapambana vita yake dhidi ya udhaifu fulani, lakini wale
wanaoonekana kushinda ni matokeo ya msaada wa Mungu maishani mwao.
Ukijua kuwa watu wana udhaifu,
hautashangaa kumuona mtu akija kwako kukueleza namna anavyotesekea, na
hautatumia nafasi hiyo ili kuyaharibu maisha yake, badala yake utamsaidia
kumuonesha njia sahihi na bora ya kuvuka hapo anapoteseka.
Kuna madhaifu ambayo yanaondoka,
na kuna madhaifu ambayo yapo tu. Na hayo yote yapo kwa watu unaokutana nao kila
siku, unaoshirikiana nao kila siku pale kazini. Wanahitaji msaada, wanahitaji
kutegemeana ili wazidi kuwa bora kuliko hapo walipo kwa sasa. Usimdharau wala
kumcheka mtu, au kumpuuzia kwa sababu ya udhaifu wake, siku moja ataota nywele
zake na atawaangusha wafilisti. Udhaifu wa mtu, ni sehemu ya Mungu kudhihirisha
nguvu zake kwa wanadamu.
Jambo La #7. Watu Wanahitaji Watu
Hili ni jambo lingine, ambalo
unapaswa kulifahamu kwa undani sana kwenye maisha yako. Kila mtu kuna mtu
anamhitaji maishani mwake. Huyu anahitaji mume, yule anahitaji mtoto, yule
anahitaji mke, na yule anahitaji mfanyakazi, huku mwingine anahitaji mwalimu,
mwingine anahitaji kiongozi na kadhalika.
Maisha ni mfumo wa utegemezi wa
watu na watu. Tunategemeana watu wote. Kila mtu ana sehemu yake duniani. Hakuna
mtu ambaye dunia ni yake peke yake, dunia ni yetu sote.
Kuna watu wanajihisi wao ndiyo
wanaopaswa kuwepo duniani, wengine waondoke tu, hawana faida. Hatuwezi kuzuia
mfumo aliouweka Mungu usifanye kazi, kila mtu anamhitaji mwingine. Unahitaji
watu ili ufanikiwe.
Kama wewe ni mfanyabiashara basi
utahitaji wateja. Hakuna mwalimu bila wanafunzi, hakuna mchungaji bila washirika,
hakuna kiongozi bila washirika. Hakuna mtu bila watu. Tunahitajiana kuliko
kawaida.
Dunia yetu, au jamii yetu, au
nchi yetu iwe salama, inahitaji watu waje pamoja. Watu wanahitajiana katika
maeneo mbalimbali. Hatahivyo, watu ili waje pamoja na watu, inahitaji kanuni
mbalimbali za kuwaweka pamoja la sivyo uharibifu hautaepukika. Popote walipo
watu kuna hatari ya uharibifu kama hakuna kanuni zinazoongoza ushirika wao.
Ni muhimu ujue kuwa unahitaji
watu kwenye maisha yako ili ufike mahali. Usidharau watu, usijione umefika,
hakuna mtu aliye peke yake akafika popote. Hata Adamu alihitaji uwepo wa Hawa.
Tena ni Mungu mwenyewe aliona kuwa Adamu hapaswi kuwa peke yake. Mungu
ameshaona kuwa haupaswi kuwa peke yako, kaa na watu. Kila mtu ana kitu cha
thamani. Ishi na watu vizuri.
Kilichokushinda wewe kuna watu
wanakiweza, usichofanya wewe kuna watu wanafanya, usichojua wewe kuna watu
wanajua. Unahitaji watu maishani mwako kuliko unavyodhani. Lakini inamhitaji
Mungu zaidi ili kupata watu sahihi maishani mwako.
Jambo La #8. Watu Wamefungwa Na Ibada
Kila mtu anaabudu. Iwe ni Mungu
wa Kweli au mungu mwingine wa uongo. Kila mtu kuna anachoabudu, hakuna mtu
ambaye anakwambia haabudu. Swali gumu la kujiuliza ni hili, je, anaachoabudu au
anayemuabudu ndiye anayepaswa kuabudiwa?
Kila mwanadamu anahitaji ibada.
Ndiyo maana popote linapotokea janga fulani lazima watu waambiane kuwa tutakuwa
tumemkosea Mungu, tukatubu, Mungu atatusaidia.
Kila mtu anamhitaji Mungu.
Mojawapo ya mambo ambayo unaweza kumsaidia mwanadamu, ni kumsaidia
kumshirikisha juu ya ibada na Mungu wa kweli anayepaswa kuabudiwa na watu wote
kwa ajili ya faida ya maisha yake.
Huwezi kujitenga na ibada, ila
unaweza kuamua unaabudu nini? Kuna anayeabudu Mungu wa kweli, kuna anayeabudu
milima na miti au mizimu, au fedha na vingine vingi, ni ibada. Lakini ifahamike
kuwa kuna Mungu mmoja anayepaswa kuabudiwa, na siyo kila anayeabudiwa ni sahihi
kuabudiwa hata kama anaabudiwa na watu wengi au wachache na kusifiwa kuwa anafanya
kazi.
Muhimu sana kuwa na uhakika na
unakoabudu kuwa je, ni mahali sahihi? Ushauri wangu kwako ni huu, kama unaona
kuna namna ibada yako haikusaidii, basi kuna mahali pana shida, tafuta namna
mrudie Mungu wa kweli akusaidie.
Ndugu msomaji, fanya toba ya
kweli, kama haumwabudu Mungu wa Kweli, mrudie Mungu. Au kama kuna mtu unamuona
hafanyi ibada ya kweli, msaidie amrudie Mungu wa kweli, maana ili ibada iwe ya
kweli na sahihi, lazima mtu amuabudu Mungu wa kweli katika ibada yake. Mungu wa
kweli, anapatikana kupitia njia moja, nayo ni njia ya Yesu Kristo. Watu wana
njia (dini) nyingi za kumtafuta Mungu wa Kweli, lakini njia sahihi zaidi ni
kupitia Yesu Kristo. Ukiweza kuijua njia hiyo, utagundua mengi ambayo huyajui
kuhusu maisha yako na Mungu katika ibada yako.
Jambo La #9. Watu Wana Maswali
Kila mtu kuna swali analotafuta
jibu lake. Ndiyo maana tasnia ya habari inazidi kushika kasi ulimwenguni,
ulimwengu tulionao unaitwa ulimwengu au zama za taarifa. Hii ni kwa sababu,
taarifa hizo zinalenga kujibu maswali ya watu ya kila siku.
Ukitafuta kujua maswali ya watu,
na kuja na majibu sahihi, hakika utafaidika na uwepo wa watu duniani. Kila mtu
mwenye soko duniani, ni matokeo ya kuuza taarifa au kitu fulani ambacho
kinajibu maswali ya watu duniani.
Kuna watu wana maswali katika
ndoa, malezi, uchumi, fedha, uongozi, elimu na kadhalika, wanahitaji majibu.
Kila siku maswali yanajitokeza na yanahitaji majibu.
Watu wana shida mbalimbali
wanhitaji msaada, watu wana changamoto wanazopitia, watu wana mambo yanayowayumbisha
na kuwaumiza vichwa, wanatafuta kujua wanatokaje hapo. Akitokea mtu mwenye
majibu, lazima apate soko, lazima apate nafasi kwenye maisha yao.
Unaweza usijue wanajiuliza
maswali gani na majibu gani sahihi, lakini ukipata muda wa kutulia mbele za
Mungu, na kushiriki mambo mbalimbali ya wanadamu, utasemeshwa mambo ambayo
Mungu anatarajia kuona yakiwa majibu kwenye maisha ya watu na maswali ambayo
watu wanajiuliza na bado hawajapata msaada.
Hii dunia haitakuja iishe
maswali mpaka mwisho wake. Lazima uweke hili kichwani. Hivyo, kitu pekee
unachoweza kufanya, ni kujua maswali gani yanaulizwa, na Mungu anakupa kujibu
swali gani. Ukipata majibu ya hata swali moja tu, lazima usikilizwe na watu, lazima
utapewa kipaumbele.
Mwenye majibu, hata awe na
mwonekano usiowapendeza watu, au asipendwe na watu, bado atakuwa na nafasi kati
ya watu. Kinachompa nafasi ni majibu aliyobeba. Siyo lazima ujipendekeze kwa
watu ili upate nafasi ya kusikilizwa, jipendekeze kwa Mungu, akupe majibu ya
maswali fulani, uje nayo, uone kama hautasikilizwa. Itafika mahali unatamani
kupumzika lakini hamna muda, watu wanakutafuta kama lulu, wanatafuta majibu
yao, wanaamini unayo wewe, inawezekana ni Mungu anayewaelekeza waje kwako.
Jambo La #10. Watu Wapo Safarini
Maisha ni gari iliyowabeba watu
kuelekea mahali fulani. Watu wapo safarini. Hapa duniani kila mtu ana safari
yake, kuna mtu anaelekea pale juu serikalini, kuna mtu anaelekea pale kwenye
zile fedha, mwingine anaelekea kule kwenye umasikini. Na suala la mwisho wa
safari yako ni wapi, ni matokeo ya maamuzi ya mtu akiwa ndani ya gari la
maisha.
Vilevile, watu wapo safarini,
hawaishii hapa tu duniani. Kila mtu kuna mahali anaenda, kuna wanaojiandaa
kwenda Jehanamu, kuna wanaojiandaa kwenda Paradiso, kila mtu kuna mahali
anaenda.
Ndugu msomaji, hakuna mtu ambaye
ataishia hapa duniani. Hili ni jambo unalopaswa kufahamu, hata wewe upo
safarini, na utaishia wapi ni matokeo ya umepanda gari gani hapa. Kuna gari
(maisha) inayowapeleka watu pabaya, na wengine wapo kwenye gari (maisha)
inayowapeleka watu uzimani.
Umewahi kuwaza utakuwa wapi
baada ya kuondoka hapa duniani? Asikudanganye mtu kuwa ukiondoka duniani, kila
kitu kimeisha, bado kuna mengi yanaendelea huko unakoenda, ambayo hata ya
duniani huku hayafiki hata nusu. Huko ni milele, hakuna miaka 100 au 60, ni
milele.
Hebu waza, mtu kwa maisha ya
hapa tu duniani ambayo anaishi miaka 100 au 60 lakini analalamika kila siku kwa
magumu yake, sasa itakuwaje siku atakapoingia kule jehanamu ambako ataishi
milele kwa maisha mabovu anayoishi leo?
Umewahi kuwaza namna ambavyo
watu wanajidanganya kwa kujifariji kuwa watasamehewa kwa maombi ya watu fulani
fulani hapa duniani? Umewahi kuwaza namna ambavyo watu wanawazaga juu ya yale
maombi ya Mungu mlaze mahali pema peponi? Hakuna hata mojawapo linalofanyiwa
kazi, kila mtu atakula matunda ya maamuzi yake kwenye miaka michache aliyopewa
duniani. Kitu muhimu mtu anachoweza kufanya ni kuamua sasa ataishi wapi baada
ya maisha ya hapa duniani.
Kila mtu yupo safarini, kuna
mahali anaenda. Hakuna ambaye ataishia duniani. Hilo likae ndani kabisa ya moyo
wako. Kinachozikwaga pale kaburini ni mwili, na ndiyo maana unaitwa mwili wa
marehemu, na siyo marehemu mwenyewe, marehemu mwenyewe hayupo, ameenda kula
matunda ya kazi na maisha yake hapa duniani.
Comments
Post a Comment
Thanks for your comment, God bless you!!!