KWANINI MUNGU ANAFANYA KAZI NA WATU?

 Ndugu msomaji, karibu katika wikiendi nyingine, ambayo tunajifunza mambo ya kutuongezea thamani na kuyafanya maisha yetu kuwa na matokeo katika dunia yetu na tuishi maisha ya alama isiyofutika.

Wikiendi hii, tunajifunza kuhusiana na sababu 5 za Mungu kufanya kazi na watu. Zipo sababu nyingi, lakini leo tutajifunza sababu 5 ambazo katika hizo, zitatuongezea thamani na kuzaa mabadiliko.

Karibu tujifunze,

 

1.      Watu Wametoka Kwa Mungu

Kila mtu unayemuona duniani ametoka kwa Mungu. Hata awe mbaya kiasi gani, ubaya wake ni matokeo ya hali fulani alizokutana nazo hapa duniani, na asili ya dhambi kwenye maisha ya mwanadamu, lakini yeye mwenyewe ni matokeo ya wazo la Mungu.

Kila mwanadamu unayemuona ni wazo la Mungu. Ametoka kwa Mungu, na kama ametoka kwa Mungu kuna sababu iliyomfanya Mungu amlete huyu mtu ambaye tunamuona katika mwili.

Kwa maneno mengine, tunayemuona katika mwili, si mwili, ni mtu kutoka kwa Mungu ambaye amebeba ajenda fulani ndani yake ya kutekeleza katika dunia ambayo wanadamu wengine wanaishi.

Mungu hajawahi kufanya kazi ya bahati mbaya, kila mwanadamu anayemleta amekuja kwa kusudi. Ni muhimu kujua kuwa wanadamu wametoka kwa Mungu, na kama wametoka kwa Mungu kuna kitu wanacho, wametumwa kufanya kazi fulani.

Mwanadamu ni kiumbe wa rohoni aliyevaa mwili, na kiumbe huyu ametoka kwa Mungu, na amekuja duniani kwa sababu maalumu, yupo kikazi. Ndiyo maana Mungu anafanya naye kazi.

Mungu anaweza kumtumia yeyote, kwa sababu wote wametoka kwake. Hakuna ambaye alijileta mwenyewe, au aliletwa na shetani, kila mwanadamu, ameletwa na Mungu, uwepo wake ni ruhusa kamili ya Mungu Muumbaji wa vyote.

Mungu analazimika kufanya kazi na mwanadamu kwa sababu yeye ndiye amemleta, na kuna vitu amempa ambavyo vinapaswa kuwafikia wanadamu. Yeye ametoka kwake, na amekuja duniani kwa sababu yake (Mungu) na anafanya kazi kwa niaba yake (Mungu) na ndiyo maana lazima afanye naye kazi. Kumbuka kuwa hakuna kinachotoka kwa Mungu kisicho na kazi, kila kinachotoka kwa Mungu kina kazi yake, lazima kitumiwe na Mungu. Kama MBINGU NA NCHI ZINAHUBIRI UTUKUFU WAKE, SEMBUSE MWANADAMU?

 

2.     Watu Wana Asili Ya Mungu (wana baadhi ya tabia za Mungu na wanaweza kuwa na tabia ambazo Mungu anawaruhusu kuwa nazo)

Kila mwanadamu unayemuona ana asili ya Mungu. Kuna tabia za Mungu zimefungwa ndani yake. Mojawapo ya asili ya Mungu ni utashi au kwa lugha nyepesi uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi.

Kila mwanadamu anaweza kufanya maamuzi. Kila mwanadamu anaweza kufikiri. Hata kama anafanya maamuzi mabaya, au kufiriki vibaya, bado yeye anaweza kutumiwa na Mungu, na kama atatengenezewa mazingira mazuri ya kurekebisha uwezo wake wa kufikiri na kuamua, atafanya kazi na Mungu wakati wote.

Mungu amempa mwanadamu baadhi ya tabia zake ili kumuwezesha mwanadamu kufanya naye kazi au kumtumia kwa ajili ya majukumu mbalimbali. Mwanadamu kuwa na asili ya Mungu, kunampa mwanadamu uhalali wa kufanya vitu kwa niaba ya Mungu. Kuna vitu ambavyo Mungu alitakiwa kufanya moja kwa moja kwenye maisha ya watu. Sasa ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu, amewapa  wanadamu tabia zake, ili wafanye kazi kama yeye, kwa niaba yake kwenye maisha ya watu.

Kuna tabia ambazo wanadamu wamezipoteza baada ya dhambi, na nyingine kwa uwezo wao wa kibinadamu hawawezi kuwa nazo, lakini bado Mungu ametoa namna ya kuwasaidia kuwa na tabia hizo ili wazidi kuwa na upana wa kutumiwa na yeye katika dunia yao.

Mwanadamu wa kawaida, ni ngumu kwake kuwa mtakatifu, lakini Mungu mwenyewe ametoa msaada wake kwa njia hii kuwa mtu AMWAMINI YESU KRISTO kuwa alikufa msalabani kwa ajili ya dhambi zake, kisha APOKEE KIPAWA CHA ROHO MTAKATIFU na kuamua kuongozwa naye, na kuamua kuishi maisha ya haki yatokanayo na Neno la Mungu. Hii inamsaidia mtu kuwa mtakatifu.

Na kuna vitu kwa Mungu haviwezi kubebwa bila huyo anayebeba kuwa mtakatifu. Asipokuwa mtakatifu, akibeba tu vitamuua. Kwahiyo, ili avibebe, Mungu anamsaidia kuwa mtakatifu, kumbuka utakatibu ni tabia ya Mungu. Ni tabia inayomtafsiri Mungu na namna anavyotofautishwa na miungu mingine yote, kwahiyo tabia hii mtu akiwa nayo, kuna viwango vya kutumiwa na Mungu vinakuwa vikubwa sana kwa sababu tabia ya kubeba hicho kiwango anayo.

Mfano wa tabia nyingine ni upendo, Mungu ni pendo, hauwezi kumtenga Mungu na upendo. Na mwanadamu wa kawaida upendo wake una walakini, ni jambo dogo sana kuacha kumpenda mtu mwingine kwa sababu fulani fulani. Lakini Mungu ana upendo mkubwa sana hata kwa watenda dhambi, hata kwao ameruhusu mwanae wa pekee afe msalabani kwa ajili ya wote. Huu ni upendo uliovuka mipaka.

Hata Yesu aliuonesha upendo huu kwa ukaribu wake na namna alivyoshughulika na dhambi za makahaba, watoza ushuru na watu wa mataifa. Upendo ni tabia ya Mungu, inayomfanya Mungu afanye vitu vingi kwenye maisha ya wanadamu bila kuchoka. Ili mtu afanye kazi kwa niaba ya Mungu lazima awe na tabia hii ya Upendo. Mungu kwa sababu anajua umuhimu wa tabia hii ya Upendo, anaijenga na kuimimina tabia hii kwa njia ya Roho Mtakatifu ndani ya mtu.

Kwahiyo, mtu anaweza kabisa kutumiwa na Mungu. Anaweza kumsaidia Mungu kugusa maisha ya watu. Anaweza kufanya kazi na Mungu, kwa sababu alivyo yeye Mungu ndivyo na mwanadamu anakuwa. Na haya yote yamewekwa wazi katika maandiko matakatifu ya Biblia katika vitabu mbalimbali.

Unaweza kushiriki tabia ya uungu wa Mungu. Unaweza kubeba tabia za Mungu, ambazo zinakupa uhalali wa kutumiwa na Mungu. Hata kama kuna mtu unamuona hafai, huyo anaweza kutumiwa na Mungu kama kuna baadhi ya tabia ambazo zimeharibiwa ndani yake (kama kufikiri na maamuzi) zitaamshwa na kurudishwa kama awali Mungu alivyokusudia, na kama atawezeshwa kupata asili ambazo zinatokana na utendaji wa Roho Mtakatifu kwenye maisha ya mtu.

 

3.     Watu Wanaweza Kuhusiana Na Watu

Mungu amewaumba watu katika hali ya kutegemeana, watu wanaweza kuhusiana. Ndiyo maana Mungu ana uwezo wa kumtumia mtu ili kumsaidia mtu mwingine hapa duniani. Kila mwanadamu anamtegemea mwanadamu.

Tunawahitaji watu maishani mwetu. Hakuna mtu ambaye hawezi kuwa na uhusiano mzuri na watu. Hata kama aseme yeye ameumbwaje, kila unayemuona ameumbwa na Mungu, amewekewa ndani yake uwezo na asili ya kuhusiana na wengine.

Mungu hakuona kuwa ni vyema kumuacha Adamu peke yake, lakini ajabu ni kuwa Hawa alitoka kwa Adamu, maana yake  kuna kitu ambacho Adamu atakipata kwa Hawa ndiyo maana ikalazimu uwepo wa Hawa.

Mtu ambaye haheshimu uwepo wa watu wengine, anayejiona anajua vyote, ambaye hajali wengine wala kuonesha upendo kwa walio dhaifu, anajaribu kumkosoa Mungu aliyeweka asili ya kutegemeana baina ya mtu na mtu. Na ukweli ni kwamba hatafika popote maishani.

Kuna watu maishani wamepewa vitu ambavyo vitakusaidia wewe. Usipojua kuwa wana vitu, unaweza kukaa kwenye maombi unasubiri vije, kumbe tayari vipo, ni kumuomba Mungu hekima ya kuwajua watu na kuhusiana nao vyema.

Sauli (Paulo) alitokewa na Yesu, lakini ajabu ni kuwa Yesu mwenyewe akamwambia aende kwa Eleazari, na wakati Yesu mwenyewe angeweza kumwambia yote. Sasa kwanini amwambie aende kwa mtu? Yesu hawezi kuvunja kanuni ambayo aliiweka tangu mwanzo ili kuongoza maisha ya mwanadamu. Ameshaweka asili na kanuni ya kuhusiana, hatafanya kazi na mtu mmoja, atafanya kazi na kila mtu, kwahiyo, mtu asije akadhani peke yake ndiye anamjua Mungu kuliko wengine.

Hata Paulo mwenyewe pamoja na kazi yake yote, lakini bado kuna vitu alienda kuuliza kwa kina Petro. Hii ni asili ya wanadamu, haiwezi kukwepeka. Hata kama utaenda maombi na kukaa milimani, kuna vitu tu utalazimika (kulazimishwa) kuja kutafuta watu hata kama ulikuwa unawadharau na kuwaona kuwa hawafai.

Kuna vitu Mungu huwa anawapa watu, na akishawapa watu, ni wajibu wa watu kwenda kwa hao watu, na wanapaswa kwenda kwa msaada wa Mungu, kwa sababu kila mtu ambaye kuna kitu amepewa kwa ajili yako, kuna majira yake kukipata kwake. Na kuna hekima pia ya kupata hicho kitu kwake, hauendi kichwakichwa.

Mungu anatumia watu kwa sababu ametengeneza uumbaji wote katika hali ya kutegemeana, na hali hiyo haiwezi kuondoka. Ukielewa hili, itakusaidia sana kuona watu namna ambavyo kuna vitu vingi wamebeba vya thamani sana kwa ajili yako, ni wewe tu kukosa hekima ya kuhusiana nao.

Kila mtu anamtegemea mtu mwingine. Hakuna kukwepa hili. Ukiona jambo hata Mungu mwenyewe hakwepi jambo fulani, ni lazima ujue kuwa lina uzito kwake usio wa kawaida, na ukitaka kutoboa unapaswa kulichukulia jambo hilo uzito ambao na yeye anauchukulia.

Wakati mwingine inahitaji kufunguliwa ufahamu kwa maombi, au kwa taarifa kama hizi, ili kuelewa ulazima wa kuhusiana vizuri na watu maishani mwako. Siyo lazima aletwe malaika Gabrieli, na wakati mwingine hata akija, bado atakuelekeza kwa watu kama Mariamu alivyoelekezwa kwa Elizabeti.

 

4.     Watu Wamepewa Mamlaka Juu Ya Nchi

Mara baada ya Mungu kuiumba dunia (nchi), kisha akamweka mwanadamu, ni mwanadamu pekee mwenye mamlaka na dunia. Ndiyo maana hata shetani alipotaka kuitawala dunia, alienda kwanza kwa mwanadamu.

Duniani hauruhisiwi kufanya chochote bila kuwepo kwa mwanadamu. Mwanadamu ndiye mwenye maamuzi na dunia. Ni kweli kuwa Mungu ni muumbaji wa vyote, na anatawala vyote, lakini akimpa mtu nafasi, haingilii nafasi hiyo mpaka huyo mtu amtengenezee nafasi au kumpa nafasi Mungu aingilie kati katika jambo husika.

Inamlazimu Mungu kufanya kazi na watu au kutumia watu kwa sababu hawezi kuvunja mfumo aliouweka mwenyewe na akauainisha kwenye Neno lake. Yeye akiainisha kitu, hakika anakilinda na kukiheshimu kwa sababu ya uaminifu wake. Inahitaji nafasi ya watu kumpa Mungu nafasi ili afanye kazi duniani. Ndiyo maana Mungu anafanya kazi na watu.

Kinachoruhusiwa kufanya kazi kwenye dunia ni chenye mwili, ndiyo maana ililazimu hata shetani aingie ndani ya nyoka, Mungu aongee kupitia punda ili kumjulisha vitu Balaamu. Sasa hawa viumbe wengine wanatumika kwa dharura sana, asilimia kubwa sana wanaotumika hapa ni wanadamu kwa sababu wanadamu ndio wenye mamlaka juu ya viumbe wengine wote na kila kitu kinachofanyika.

Ni ukweli kuwa ukimpata mwanadamu umeipata dunia. Mungu akimpata mwanadamu mmoja, anaweza kuipata dunia nzima na kuisaidia katika jambo husika. Kutokana na mamlaka aliyonayo mwanadamu, Mungu hakwepi umuhimu wa mwanadamu kwenye kufanya kazi zake hapa duniani.

Ukielewa hii utajifunza kuwa, hautatumika wewe peke yako. Mungu anamtumia mwanadamu yeyote ambaye amempa yeye [Mungu] nafasi. Kwahiyo, ukiamua kumtengenezea Mungu nafasi, ataonekana kwenye maisha ya watu na dunia nzima kupitia yeye.

Ndiyo maana mahali fulani pameandikwa kuwa Mungu hafanyi jambo bila kuwajulisha watumishi wake. Kwanini anawajulisha, ni kwa sababu anatafuta mlango, na wao wakifungua, Mungu anaingia kazini kusaidia wanadamu.

Hata wewe unaweza kumtengenezea Mungu nafasi ya kusaidia kizazi chako. Unaweza kuanza hili kwa kuwekeza kwenye maombi na mifungo ya kumwambia Mungu kuwa unahitaji kutumiwa na yeye kwa ajili ya utukufu wake, kuwekeza kwenye ufahamu ambao unaamua upana ambao Mungu atafanya kazi na wewe, kutafuta kujua eneo gani ambalo Mungu amekusudia kufanya kazi na wewe na kuwekeza hapo, na pia kukaa chini ya watu wenye uzoefu wa maeneo mbalimbali ambayo Mungu amefanya nao kazi.

Ndugu msomaji, usikubali kutokuwa sehemu ya watu ambao wanafungua mlango kwa yeye kufanya kazi kupitia wao maishani. Amua leo, na chukua hatua madhubuti, na maisha yako yatakuwa yenye tija. Na itakuwa vyema sana kama utawaisadia wengine, kufungua mlango ili nao pia watumiwe na Mungu, maisha ya watu Yazidi kujengwa katika wema kwa mapenzi ya Mungu mwenyewe.

 

5.     Ni Furaha Ya Mungu Kufanya Kazi Na Wanadamu.

Mungu anafurahia sana kufanya kazi na wanadamu. Mungu anajivunia sana kufanya kazi na wanadamu. Ni fahari ya Mungu kufanya kazi na uumbaji wake kwa ajili ya uumbaji wake. Inampa sana yeye utukufu.

Mungu anafurahia kufanya kazi na wewe ili watu wengine wasaidike na maisha yao yajengwe. Mungu anatamani sana kufanya kazi na wewe ili maisha ya watu yawe na tija hapa duniani.

ni furaha kwa sababu, hii inaonesha namna ambavyo uumbaji wake umekuwa na tija mbele zake. Unaleta matokeo aliyokusudia huo uumbaji ulete. Mungu anafurahia kufanya kazi na wewe kwa matokeo unayomletea.

Mungu ni furaha yake kukupa ufalme, ili uende nao popote, na ulete matunda yanayoeleweka mbele zake. Mungu anafurahi sana anapokuona unakuwa mtu mwenye tija kwenye kizazi chako.

Jifunze hili, Mungu hatafanya kazi na mtu mmoja tu peke yake, wakiwepo wengine, watafanya naye kazi pia, maana wote ni uumbaji wa Mungu, na ni kawaida na furaha ya Mungu kufanya kazi na uumbaji wake.

Mungu anafurahi anapokuona amekutuma mahali, amekupa maelekezo, unaenda pale, unafanya kama ulivyotakiwa kufanya, na unaleta mezani matokeo yaliyopangwa. Ni jambo dogo sana yeye kukuamini katika yaliyo makubwa zaidi.

Mungu anapofurahi, na wewe lazima uingie katika furaha yake. Hili linaelezwa katika mfano wa watumwa waliopewa talanta na bwana wao wakazifanyie kazi, wale wote waliokuja na kitu mezani, aliaambiwa vyema mtumwa mwema, ingia katika furaha (raha) ya bwana wako. Mungu akifurahi, utashiriki furaha yake.

Kumbuka kuwa FURAHA YA BWANA ndiyo nguvu yetu. Mungu akifurahi, maisha ya aliyechochea furaha ya Mungu lazima yabadilike, inamfanya aaminiwe katika nguvu na hekima nyingi zaidi, ili azidi kuwa na matokeo mbele za Mungu.

Ndugu msomaji, hii ikupe shauku ya kumpendeza Bwana Mungu. Yeye amesema siyo wale wamwitao Bwana Bwana ndiyo watakaourithi ufalme, ni wale wayafanyao mapenzi ya Baba (Mungu). Wayafanyao mapenzi yake (matakwa yake) ndio wampendezao, na hao ndio ambao atakuwa na furaha nao. Hao atawaongezea kicheko, na hawatakuwa wanyonge katika kizazi chao.

Ndugu msomaji, ni imani yangu kuwa katika somo hili umepata mambo mengi ya kukujenga, na hakika maisha yako hatabaki kama yalivyo. Wikiendi hii ikazidi kuwa ya baraka. Mwaka huu, azimia kufanya kazi na Mungu, na uwe mtu wa matokeo. Karibu tena wikiendi nyingine.

Comments