Ukweli ambao kila mtu anapaswa kujua kuwa, hakuna mtu aliyeumbwa ili kuwa asiye na kitu maishani, au mwingine kuwa na kitu maishani. Kila mwanadamu ambaye amezaliwa chini ya jua, anayo nafasi ya kuboresha maisha yake, bila kujali ametoka kwenye hali gani.
Tatizo siyo kuwa umezaliwa wapi
na lini, tatizo lipo kwenye maamuzi yako ya sasa. Hakuna maana ya kulaumu watu,
au viongozi au mifumo kila siku, na wakati unayo nafasi ya kuamua kufika mahali
ambako Mungu amekusudia kukufikisha kama ukiamua kuanza.
Kila unayemuona amesimama mahali
pa juu katika haki na kweli, amepitia mchakato, na hajafika pale kama bahati au
ajali, aliamua kuwa pale alipo. Usipoamua, utaishia kuwa huyo ulivyo kila siku,
na hali mbaya zaidi kwa wanaokuja baada yako.
Hauwezi kubadili walichofanya wa
nyuma yako, lakini unaweza kubadili kuanzia hapo ulipo, na kwa ajili ya wale
watakaokuja baada yako, ni aibu kubwa sana kuamua kutumia miaka yako yote
duniani kuishia kulaumu watu, nchi, mifumo, na viongozi, na wakati wao wana
akili kama wewe, mwili kama wewe, ni wanadamu kamili kama wewe na wana masaa
24.
Kila unayemuona amekuwa juu
katika eneo fulani. Kuna maamuzi 5 aliyafanya, ambayo yamegeuza kabisa maisha
yake. Hatahivyo, usidanganywe kuwa kuwa mtu fulani ni tukio la mara moja,
pamoja na kuwa utashika hayo maamuzi, kutakuwa na mchakato wa muda fulani,
utakaokutoa hatua mpaka hatua, ili ufike pale. Kufika mahali maishani, siyo
jambo la siku moja, ni mchakato, ni safari inayohitaji kujikana, inayohitaji
uvumilivu maana usipokuwa makini maamuzi yako mwenyewe utayatupa njiani na
kuamua kufanya mambo ya kawaida, ambayo huwafanya watu kuishia kuwa wa kawaida
tu maishani.
Karibu tujifunze maamuzi hayo.
1. Amua kutafuta ufahamu wa
kule unakohitajika kuwa kiasi kwamba akili yako imemezwa na kule unakohitajika
kuwa.
Huwezi kufika mahali zaidi ya
ufahamu wako ulivyo. Ukitaka kufika mahali hakikisha kuwa akili yako imefika
hapo. Usichoweza kukimiliki kwa akili yako, kiasi kwamba akili yako
imeshawishika na kuathiriwa nacho kiasi cha kubadili hadi mfumo wako wa kusema na
kutenda, hauwezi kukimiliki mwilini.
Kila unayemuona amefanikiwa,
amewekeza kwenye ufahamu wa kule anakotakiwa kuwa. Akifahamu kuwa anatakiwa
kuwa mfanyabiashara, anawekeza katika ufahamu wa biashara, kwa kina, kiasi
kwamba, maneno yake, na matendo yake, yanakuwa matokeo ya kile anachokifahamu
kuhusu biashara au huko anakohitaji kuwa.
Kama usipofika kiwango ambacho
unachosema, na unachofanya ni matokeo ya ufahamu wako juu ya kule unakohitajika
kuwa, hautaweza kufika huko, asikudanganye mtu kuhusu bahati.
Mambo mengi ambayo Mungu alikuwa
akiwafundisha wana wa Israeli jangwani, ilikuwa ni kwa ajili ya Kanaani. Wengi
wao waliposhindwa kujenga ufahamu wao, waliishia jangwani.
Mungu hataruhusu kamwe, wewe
ufike mahali ambako akili yako haiwezi kustahimili kuishi, maana anajua
utakufa. Utabaki hapo ulipo, mpaka ukamate akili ya kule unakohitajika kwenda,
la sivyo utabaki hapo hapo.
Usipokubali kulipa gharama ya
kujifunza mambo ya kule unakohitaji kuwa, sahau kuwa kule unakohitajika kuwa.
Ndiyo maana, watu wote waliofanikiwa unaowaona na kuwasoma kwenye habari
mbalimbali, mojawapo ya siri wanayoishika kila siku ni KUJIFUNZA. Wanalipa
gharama kujifunza, kuliko kitu kingine.
Ni wale tu wanaojiandaa kufa
maskini, wasio na kitu, wasio na alama kwenye maisha ya watu, wasio na matokeo,
wasio na faida duniani, ambao hawakubali kulipa gharama ya kujifunza.
Ukweli ni kwamba, kujifunza ni
gharama, ndiyo maana wengi wanashindwa kujifunza, wanakuwa na visingizio vingi.
Maarifa yanatafutwa, na yanakamatwa sana. Maandiko yanasema mkamate sana elimu.
Unahitaji kukamata sana mafundisho ya kule unakotaka kuwa.
Wengi wetu wanasikiliza kila
kitu, wako bize na tamthiliya, muvi, na mfululizo wa hadithi mbalimbali, na
vitu vingine, ambavyo ukiwauliza vitakupeleka mahali unakohitaji kwenda,
watakuambia hapana, na bahati mbaya wapo tu hapo hapo kila siku.
Ikiwa unahitaji kufika mahali
maishani, amua kutafuta ufahamu wa huko, na kuhakikisha kuwa, umeathiriwa
kabisa na ufahamu huo. Yaani imani yako imekomaa kabisa kiasi kwamba, unaona
kabisa sehemu hiyo, kiasi cha kubadili mfumo wako wa matendo ili kuelekea
sehemu hiyo. Inawezekana kama ukiamua.
2. Amua kukaa chini ya
malezi.
Huwezi kufika mahali maishani
bila kukaa chini ya malezi. Asiyelelewa, ni chokoraa, hawezi kuwa chochote
maishani. Ndiyo maana unaona kuna taasisi, zinawalea wale watoto wa mtaani
waitwao machokoraa, kwanini wanawalea? Wanawapa malezi kwa sababu ni mtu
anayekaa kwenye malezi tu ambaye atafika mahali maishani.
Wana wa Israeli ili kufika nchi
ya Ahadi, iliwalazimu kukaa chini ya malezi ya Musa na baadaye Yoshua.
Hautafika mahali bila kukaa chini ya malezi. Hauwezi kukwepa malezi kama
unataka kuwa mtu maishani.
Usipokubali kuwa chini ya mtu
fulani anayekuwajibisha, na kufuatilia ukuaji wako, ambaye anajua kabisa wapi
unaelekea, na umepewa mtu huyo na Mungu mwenyewe, hautakuwa mtu katika dunia
hii. Watu wengi wanajitafutia watu wao wawalee, ambao hawatawawajibisha kuwa
bora, Mungu akupe mtu wa kukulea na kukuwajibisha.
Hii ni kanuni isiyokwepeka, hata
kwa wale ambao wanatumia nguvu za giza kuendesha shughuli zao, wanalelewa na
wakuu wao. Lazima uwe chini ya malezi. Hakuna mtu mkuu asiyekuwa chini ya mtu.
Kila mkuu, ni mlelewa wa mtu fulani mkuu zaidi yake hata kama haujamuona huyo
mkuu wake.
Hautakuwa chochote kama
unajiamulia chochote, hakuna anayekuonya ukikosea, ukiamka na lolote, hilohilo
ndiyo unalo. Hakuna mtu wa kukuonya, wewe unajua kila kitu. Yaani hata kama
unajua vitu vyote, una kila kitu, na unatakiwa kufika mahali, kama haupo chini
ya malezi, huko unakotaka kwenda utaishia kusikilizia kwenye masikio na ndoto
za usiku tu.
Mungu hawezi kuruhusu mtu
asiyewajibika kwa mtu fulani kuwajibika kwa ajili ya dunia au taifa. Huyu mtu
ni sekunde chache kuwa na kiburi, ni sekunde chache kufanya maamuzi ya hovyo
ambayo yataharibu maisha ya wengi. Ndiyo maana hata kina Daudi walikuwa chini
ya walezi kama kina Nathani nabii. Siku sauli alipodharau nafasi ya Mlezi wake
Sauli, na kuona kuwa nafasi ya ufalme ni kubwa kuliko ya mlezi, ndiyo siku
ambayo, Mungu aligeuka na kumuacha, akaenda kutafuta mtu mwingine aitwaye
Daudi.
Anayekaa chini ya malezi kwa
uaminifu, anaupendeza moyo wa Mungu, na ni rahisi kuaminiwa na Mungu katika
vitu vya Mungu katika sehemu fulani. Kama kweli, moyoni mwako, unajua kuwa
Mungu anakuita kuwa mtu fulani hapa duniani, badi amua kumtafuta Mungu akuweke
chini ya malezi ya mtu fulani, na ufanye hivyo, na uwe mwaminifu hapo
3. Amua kutunza na kulinda
nafasi ya Mungu maishani mwako.
Kila unayemuona amekaa kwneye
kitu fulani kwa haki na kweli, amewekwa na Mungu, na wakati mwingine hata
wabaya wameruhusiwa kwa ajili ya ajenda fulani maalumu.
Mungu hatakuweka juu kama
haujajifunza kutunza, kulinda na kuheshimu nafasi yake kwenye maisha yako. Watu
wengi wanatafuta kuwa watu fulani, halafu wanasahau kabisa kulinda nafasi ya
Mungu kwenye maisha yao.
Ukweli ni kwamba, unamhitaji
Mungu kuliko unavyodhani ndugu yangu. Hata kama unajihisi una uwezo kiasi gani,
una nguvu, una fedha, una hekima, ukimkosa Mungu hautafika popote. Ndiyo maana
kuna watu inaonekana wana kila sababu ya kuwa mahali fulani, lakini hawajawahi
kuwa hapo, hii hutokea kwa sababu Mungu hajapewa nafasi anayostahili katika
maisha ya huyo mtu.
Kuna mtu ukimsikiliza, unaona
kabisa kuwa ana kitu, na ana uwezo. Lakini tatizo, mbona kila siku yuko hapo
hapo, anapambana lakini hasogei. Ukiona haya, ujue tu kuwa huyo mtu ameamua
kwenda mwenyewe bila Mungu.
Kila wakati ambao wana wa
Israeli walisahau kutunza na kulinda nafasi ya Mungu kwenye maisha yao, mambo
yao yaliharibika, na wengine walikufa jangwani kabisa. Ukishindwa kutunza
nafasi ya Mungu, huwezi kutunza nafasi utakayopewa huko juu.
Mungu anawapandisha juu wale wanaolinda
nafasi yake kwenye maisha yao. Yusufu alikubali hata kwenda gerezani kwa kesi
ya kulazimishiwa ya kumbaka mke wa mkuu wa kitengo cha ulinzi ili tu asimkose
Mungu. Alichokuwa analinda hapa ni nafasi ya Mungu kwenye maisha yake. Na tunafahamu kuwa hii ilimfanya awe mkuu
katika taifa alilopelekwa hata kama ni ugenini.
Haitoshi kuota ndoto, Yusufu
aliota ndoto, alijua kuna mahali anaenda, lakini alihakikisha analinda nafasi
ya Mungu. Tunajifunza hili pia kwa Danieli, huyu alisimama imara kwenye kulinda
nafasi ya Mungu, na tunaona namna ambavyo aliinuliwa juu zaidi ya wengine bila
kujali alikuwa ni mgeni.
Wengi wanacheza na dhambi,
halafu wanataka kufika mahali. Wanafanya kila aina ya uchafu. Dhambi nyingine
wanazifanya kwa siri, wakidhani kuwa wanafanya kifichoni, kumbe wanafanya mbele
za Mungu, na Mungu akiwaangalia, anageuza uso wake kwao, na wanaishia kutokuwa
chochote.
Usipoazimia kuwa mtakatifu kweli
kweli na kujitenga na dhambi. Usipoamua kuishi chini ya uongozi wa Roho
Mtakatifu na maelekezo yake. Usipoamua kumuomba Mungu msaada wa kukusaidia kuwa
mtakatifu kama yeye alivyo Mtakatifu. Usipoamua kuwa mtu wa ibada ya kweli.
Usipoamua kuwa mtoaji kwa moyo mweupe na wa kweli. Usipoamua kuyatoa maisha
yako kwa Mungu, hautafika popote maishani.
4. Amua kuishi kwa tabia
zinazoeleweka ambazo utaziishi ukiwa kule juu.
Mungu mwenyewe, hakuwa anawapa
sheria wana wa Israeli jangwani kwa ajili ya jangwani, alikuwa anawapa kwa
ajili ya wao kuziishi kule Kanaani. Wakishindwa kuziishi wakiwa jangwani,
hawawezi kuziishi wakiwa nchi ya Kanaani.
Kama usipokubali leo kuanza
kuishi kanuni ambazo utaziishi kule juu, usiweke kabisa kichwani mwako kuwa
utaishi kule juu. Haipo hiyo kabisa.
Kama unajua kule juu panahitaji
uaminifu, na wewe haujifunzi na kuiishi katika uaminifu sasahivi, kamwe
hautakuwa pale juu. Kama ukijua kule kunahitaji watu wenye nidhamu na muda, na
usiwe na maisha ya nidhamu sasa hivi, hautakuwa chochote.
Kule juu hakuhitaji watu
wanaolala masaa mengi, watu wavivu, wasio na bidii, wasio na maadili, watu
wasiofanya kazi zinazoeleweka. Kule juu watu wenye bidii ndiyo wanaopata
nafasi.
Kama usipoanza leo kuishi maisha
ya bidii, ya utendaji kazi wenye akili, usitegemee kufanya hivyo ukiwa kule. Haiwezekani
ndugu yangu.
Maisha ni utaratibu
unaopangiliwa, usipojifunza kupangilia leo matumizi ya muda, matumizi ya fedha,
na rasilimali nyingine, hautajifunza kufanya hivyo siku ukiinuliwa, ndiyo maana
wengi wana vitu lakini hawainuliwi na bado wapo hapo kila siku.
Tabia yako inaamua utakuwa wapi
kesho. Kama tabia yako ni ya hovyo, utaishia kukaa mahali pa hovyo siku zote. Amua
kujenga tabia yako leo.
Kama leo hauwezi kusimamia hisia
zako, unaendeshwa na kemikali za mwili. Usitegemee kuwa ukioa au ukiolewa
utaweza kusimamia, badala yake zitazidi kukuendesha.
Usichoweza kukitawala sasahivi,
huwezi kukitawala ukiwa juu. Kama unahitaji kufika kule juu, jifunze tabia za
kule juu, na anza kuziishi leo.
Hatahivyo, hii isikufanye kuishi
nje ya uwezo wako wa sasa, ninapomaanisha tabia, nalenga zaidi kwenye nidhamu
ya maisha kwa ujumla. Mfano kuhusu fedha, kama usipojifunza kutumia fedha kwa
nidhamu sasahivi, hautatumia kwa nidhamu kesho.
Kama hauwezi kuweka akiba, au
kuwekeza, hata kesho hautawekeza kwa sababu hauna huo msingi. Kumbuka maisha ya
watu yanaamuliwa na misingi iliyojengwa tangu huko nyuma.
Kila unayemuona leo, ni matokeo
ya misingi yake aliyoiweka au kuwekewa jana. Maisha na nafasi maishani si
ajali. Misingi mizuri itakupa nafasi nzuri na maisha mazuri.
Usipoamua kuwa mtu wa mipango na
tathmini leo, usidhani kuwa kesho utakuwa mtu wa mipango na tathmini. Usipokuwa
mtu wa maombi leo, kesho kule juu hautakuwa hivyo, na kwa sababu hiyo, haupaswi
kuwa pale juu. Amua leo kujenga tabia yako.
5. Amua kufanya kazi na watu
sahihi.
Ukweli ni kwamba, hautafanya
kila kitu peke yako. Unahitaji kufanya kazi na watu ili ufike juu. Hata Musa
alifanya kazi na Haruni, Miriamu, Yoshua, Huri, Kalebu na wazee na wengine.
Kila aliyepo juu, kuna watu
ameinuka nao, ambao anafanya nao kazi pale. Na uwe na uhakika kuwa hao watu,
ameanza nao huko nyuma.
Siyo kila mtu unapaswa kufanya
naye kazi hata kama unahisi unampenda. Wengine unapaswa kuwaweka pembeni.
Hatufanyi kazi na watu kwa sababu tu tunawapenda, tunafanya nao kazi kwa sababu
ni watu sahihi.
Hakikisha unazungukwa na watu
sahihi, ambao watakuchochea na kukuhimiza na kukufanya kila siku uwe na nguvu
ya kuendelea mbele. Mungu anafanya kazi na watu, ukiwa na watu sahihi
itakusaidia sana.
Usikubali kufanya kila kitu peke
yako, hata kama unaona kuwa unaweza kufanya, shirikisha watu ambao Mungu
anakupa. Hii itakufikisha mbali.
Kuna msemo usemao kuwa ukitaka
kufika haraka, nenda peke yako, ila ukitaka kufika mbali, nenda na watu. Msemo
huu ni wa kweli kabisa. Umbali na nafasi unayofanya, huamuliwa na watu
unaofanya nao kazi.
Yesu kuwa na kazi ambao inadumu
mpaka leo, ni matokeo ya watu aliofanya nao kazi hata kabla hajaondoka duniani.
Ameondoka, lakini bado kazi ipo kwa sababu kuna watu kadhaa aliamua kufanya nao
kazi.
Anza pale ulipo, na watu wale
ambao utaanza nao, usisubiri liwe kundi kubwa sana, anza vile ulivyo na wale
ulionao na taratibu kadri unavoendelea kuwa mwaminifu katika madogo, ndivyo
unavyoaminiwa katika makubwa zaidi.
Ukiweza kwenda na hao ulionao,
ni rahisi kwenda na wengine utakaoongezewa.
Ndugu msomaji, mambo haya 5 ni
maamuzi ambayo kila mtu mkuu aliamua kuyafanya, ndiyo maana unamuona pale
alipo. Mahali na nafasi fulani maishani si ajali, ni matokeo ya maamuzi
yaliyofuatwa kikamilifu kwa muda fulani. Unaweza kuwa yule unayepaswa kuwa,
kama utaamua kulipa gharama hiyo leo.
Mungu akubariki.
Comments
Post a Comment
Thanks for your comment, God bless you!!!