MAMBO 7 YA KUKUSAIDIA KUWA NA ALAMA KWENYE MAISHA YA WATU

Ndugu msomaji karibu katika wikiendi nyingine njema na ya baraka sana. Natumaini kuwa wiki yako imeenda vizuri na Mungu amekulinda.

Leo tunajifunza juu ya mambo 7 ya kutusaidia kuwa na alama kwenye maisha ya watu. Kuwa na alama kwenye maisha ya watu, ni kufanya mambo ambayo kwa namna moja ama nyingine yanaongeza thamani ya maisha ya watu wengine, na kuwafanya wawe bora kuliko walivyokuwa jana. Kuwa alama kwa lugha nyingine ni kuwa kielelezo kwenye maisha ya watu, kuwa mtu ambaye wengine wanajifunza na kupata picha ya wanavyotakiwa kuwa.

Karibu tujifunze mambo haya

 

1.      Nidhamu Binafsi

Hili ni jambo la kwanza la kuzingatia kama unahitaji kuwa na alama kwenye maisha ya watu. Kama unahitaji kuwa na nafasi kwenye maisha ya watu, na kuwa kielelezo chema kinachoongeza thamani ya watu unahitaji kuwa na nidhamu binafsi.

Nidhamu binafsi inajumuisha mfumo wa kanuni na taratibu ambazo umeamua kwa hiyari yako mwenyewe, umeweka na kuamua kwenda nazo maishani ili kuamua utambulisho wako. Inamuisha mipaka uliyojiwekea na namna unavyojichukua kwenye shughuli zako zote.

Nidhamu binafsi inahusisha maamuzi ya makusudi kabisa, ya kuamua kuishi vyema na watu, sawasawa na kanuni za MUNGU ambazo zinaendesha maisha ya watu.

Nidhamu binafsi inajumuisha namna ambavyo unasimamia matumizi ya rasilimali zako. Unatumia muda kwa mpangilio, unatumia fedha na vitu vyote ulivyoaminiwa na Mungu kwa faida. Wewe ni mtunzaji. Haupotezi muda wako.

Unalinda muda kwa sababu unajua maisha yako yamefungwa katika muda, na hakuna jambo ambalo utafanya nje ya muda ukiwa hapa duniani. Kwahiyo, watu watakutazama kama mtu ambaye anatumia muda wake ipasavyo, wanaweza kuapata kwake hekima nzuri ya kutumia muda na rasilimali nyingine.

 

2.     Malengo Yanayofanyiwa Kazi

Hili ni jambo la pili, ambalo litakufanya uwe na alama au nafasi katika maisha ya watu. Kila mtu unayemuona ambaye ameacha alama, au hata sasa bila kujali yupo hai, amekuwa alama isiyofutika kwenye maisha ya watu, anaishi kwa malengo na yanafanyiwa kazi.

Kwenye hii dunia, hauwezi kuwa na alama kwenye maisha ya watu, kama utaishi kiholela bila mpangilio. Maisha yasiyo na mipangilio, hayawezi kutumika kuacha alama yenye tija kwenye maisha ya mtu. Wala hayawezi kutumika kuwa mfano wa maendeleo ya watu katika jambo husika.

Unapaswa kuwa mtu wa malengo na mikakati, uwe mtu ambaye unafanyia kazi. Haitoshi kusema una malengo, haitoshi kuandika malengo, kama haufanyii kazi malengo yako, hautakuwa na tija katika jamii yako wala dunia yako. Hakuna atakayefaidika na uwepo wako, hakutakuwapo na kumbukumbu lako uondokapo duniani, na wala huko uendako. Inahitaji kuwa mtu wa malengo.

 

3.     Mtazamo Chanya Kuhusu Maisha

Kila unayemuona duniani, ana mtazamo fulani kuhusu maisha, na mtazamo huo ndio unaomfanya awe mtu fulani katika dunia yake.

Ni ukweli kwamba, kila unachokifanya, namna unavyoongea, unavyoitikia mambo katika maisha, ni matokeo ya mtazamo au mitazamo uliyonayo katika jambo husika. Kwahiyo, kama usipokuwa na mitazamo sahihi, hautakuwa na jambo sahihi unalolifanya kwenye maisha ya watu, na usiwe na alama yoyote kwa watu.

Unahitaji kufanya maamuzi ya kuacha mitazamo ya kizamani ambayo ni mibovu, mitazamo yoyote isiyofaa, mitazamo yoyote isiyokusaidia. Na hii inatokana na namna ambavyo kila siku unalipa gharama kujifunza vitu chanya.

Kwa maneno mengine, unapaswa kuangalia aina ya taarifa ambazo kila siku unajilisha. Hakikisha kuwa unajilisha taarifa chanya maishani. Epuka taarifa ambazo zitakupelekea ufanye vitu visivyo na tija na mwisho wa siku kuharibu nafasi yako kati ya watu.

 

4.     Ushirika Wako Na Mungu

Hili ni jambo la nne la muhimu sana kuzingatia kama unahitaji kuwa na alama kwenye maisha ya watu. Mungu huvuta watu kuja kwetu ili tuwaachie alama isiyofutika ambayo itakuw ana tija kwenye maisha yao.

Ukishindwa kuwa na ushirika mzuri na Mungu, yeye hatakuruhusu uwe na nafasi kwenye maisha ya watu, kwa sababu utaishia kuwa mharibifu wa maisha ya watu. Unahitaji kujenga na kulinda na kuukuza ushirika wako na Mungu kila wakati.

Ni lazima ujenge tabia ya maombi yasiyokoma, utakatifu, kujifunza Neno la Mungu kwa kina, kumtumikia Mungu kwa dhati. Ni jambo dogo sana kwa Mungu kukuletea watu maishani ili uwasaidie kama amekuona kuwa unamfaa.

Unamhitaji sana Mungu kuliko unavyodhani kama unataka kuwa na alama isiyofutika kwenye maisha ya watu. Ni muhimu kujua katika mchakato wa kusaidia watu, kuna wakati watu hao hao watageuka na kufanya vitu usivyotarajia, inahitaji neema ya Mungu kuendelea kuwasaidia yaani kutolipa mabaya kwa watu wakati wamefanya mabaya kwako.

Ukipuuzia nafasi ya Mungu kwako, utatumia nguvu nyingi sana kuacha alama kwa watu. Utatumia sana nguvu kuishi na watu vizuri. Unapaswa kufanya maamuzi ya kulinda na kuheshimu mahusiano yako na Mungu siku zote. Mungu ni namba moja.

 

5.     Kuthamini Watu

Hakuna mtu atakayempa mtu nafasi ya kuacha alama kwenye maisha yake, kama mtu huyo haoneshi thamani kwake. Inahitaji kuthamini watu ili kuwa na alama kwenye maisha ya watu.

Waone watu kwenye jicho la kiungu. Kuna namna Mungu anawatazama watu kwa uthamani mkubwa sana kiasi kwamba, akamtoa mwanae wa pekee ili kupitia yeye watu waokolewe. Thamani ya mwanadamu ni kubwa sana mbele za Mungu.

Kimsingi, kuna ufahamu ambao Mungu anao kuhusu watu, ambao sisi wanadamu hatuna kuhusu wanadamu wengine, inahitaji kupata ufahamu huo, ili kuona thamani ya watu hata wakati ambao kwa macho ya kawaida, wanaonekana siyo kitu chochote popote.

Unahitaji kufahamu kuwa kila mtu ana kitu anaweza kufanya, kuna mahali akiwekwa anaweza kufanya maajabu, ni vile pale alipo hajakutana na mazingira sahihi, watu sahihi na labda kuna ufahamu ameukosa. Unapaswa kufanyika daraja la mtu kupata vile ambavyo akivipata, vitasaidia kufunua thamani yake iliyofichika.

 

6.     Maono Yanayokimbiziwa

Kumbuka kuwa kila mtu anapaswa kuwa na kitu anachokikimbizia kwenye maisha. Unapaswa kuwa na maono ambayo unayafanya, unayafuatia kila siku na unahakikisha kuwa unasogea hatua moja zaidi. Maono uliyonayo yanahusisha watu.

Kila mtu mwenye maono, anagusa maisha ya watu. Iwe ni maono katika biashara, huduma, uchumi na mengine mengi. Kila maono yanahusu watu na yanafanywa na watu.

Ikiwa una maono ambayo unayafuatia. Ambayo yanakufanya uamke asubuhi na kuchukua hatua mbalimbali, hakika utakuwa na alama kwenye maisha ya watu. Ni lazima uamue kuyakimbizia maono.

Maono yanazaliwa na Mungu mwenyewe ndani ya mtu kwa mtu anayetokana na Mungu na yanatoka kwa shetani kwa mtu anayetokana na shetani.

Kila maono yamebeba ajenda fulani katika ulimwengu wa roho kuhusu maisha ya watu. Ajenda hiyo inaweza kuwa ya kwa Mungu au kwa shetani. Ukiamua kuwa na ukaribu na Mungu, utakuwa na maono ambayo yanahusu maisha ya watu, ambayo yamebeba ajenda ya Mungu na siku zote ajenda ya Mungu lazima iyafanye maisha ya watu kuwa chanya.

Ukitaka kuwa na alama kwenye maisha ya watu, hakikisha una maono unayoyapambania. Yanayokuweka bize kila siku. Yanayokupa sababu ya kuamka, na ulazima wa MUNGU kukulinda zaidi.

 

7.     Maamuzi Thabiti

Kila kitu maishani kinazaliwa kwa maamuzi. Hauwezi kuwa na alama kwenye maisha ya watu, au katika dunia yako kama haujafanya maamuzi thabiti. Ni ukweli kuwa kuna mambo utalazimika kuacha hata kama ulikuwa unapenda kuyafanya, hata kama unahisi ni ngumu kuacha, hata kama unaona hauwezi. Unapaswa kufanya maamuzi ya kuacha na Mungu hauyupo mbali, usisahau kumpa nafasi akusaidie.

Ni lazima ufanye maamuzi ya kujenga thamani yako, kwa sababu hauwezi kujenga thamani za watu wengine na kuweka alama kwenye maisha ya watu, kama hata thamani yako umeshindwa kuijenga. Huwezi kupenda wengine kiwango ambacho haujipendi.

Ni lazima kuamua kujifunza mambo mapya, hata kama inaumiza na kuona kuwa ni uzoefu mpya. Kuacha alama au kuweka alama kwenye maisha ya watu ni gharama. Hakuna bahati wala ndoto katika kuwa na alama kwenye maisha ya watu. Ni maamuzi ya kulipa gharama.

Ni lazima ufanye maamuzi ya kuwatumikia watu kwa niaba ya Mungu. Uwe tayari kutafuta mapenzi ya Mungu kwa ajili ya watu, ili uwape watu kitu wanachohitaji hasa maishani. Kila kitu ni maamuzi kwa sababu lazima kilipiwe gharama.

Kuna marafiki itakulazimu kuachana nao, na kuna watu itakulazimu kujiweka karibu nao kwa maelekezo ya MUNGU. Unahitaji kuamua kwa kweli.

Ndugu msomaji, ni ushauri wangu kwako kuwa, kwenye maisha unapaswa kufanya maamuzi. Mwaka huu amua kuwa mtu mwenye tija kwenye dunia yako na kizazi chako. Amua kulipa gharama. Amua kuchukua hatua, amua kuwa mtu mwingine.

Ndugu msomaji, imetosha kuendelea kuwa yule yule asiye na matokeo kila siku. Itoshe kuwa yule yule ambaye jamii yake inamuona hana tija, wengine wanamuona hana kitu cha kuipa dunia yake cha kufaa. Amua kuifunua hazina ambayo Mungu ameiweka ndani yako kwa ajili ya dunia.

Ndugu msomaji, unapomaliza wikiendi hii, amua kuzungumza na Mungu juu ya hili, muombe akusaidie na kukugeuza kuwa mtu mwingine, utakayeifaa jamii yako. Ni matumaini yangu kuwa kuna siku utanitumia ujumbe wa mabadiliko kutokana na Makala hii.

Nikutakie wikiendi njema, na Mungu akubariki sana, tukutane wikiendi nyingine.

Comments