MTU WA AINA HII NDIYE ATAKAYETAZAMWA KATIKA TAIFA MIAKA MICHACHE IJAYO

Ndugu msomaji, natumaini unaendelea vyema na maisha yako ya kila siku, na ninamshukuru Mungu ambaye amekuweka kuwa hai hadi sasa. Ni dhahiri kuwa ana mpango kamili na wewe, na anaona kuna nafasi ambayo bado unahitajika katika dunia yako. Na inawezekana hujaanza bado kufanya au unafanya, lakini hii ikutie moyo kuwa unapaswa kuendelea kufanya vitu ambavyo Mungu anafurahia ufanye.

Katika wikiendi ya leo, kama ilivyo dhamira yetu kuwa ni kukuongezea thamani kila wikiendi ili uweze kuwa na wikiendi ya thamani zaidi na kuboresha maisha yako, tutajifunza juu ya mtu unayepaswa kuwa ikiwa unahitaji kutazamwa miaka michache ijayo katika taifa la Tanzania.

Ndugu msomaji, ninaomba ufahamu kuwa, miaka kadhaa ijayo, kuna watu ambao Mungu atawahitaji zaidi kwenye nafasi mbalimbali ili watazamwe na watu. Ninapozungumza kutazamwa na watu, ninamaanisha kuwa Mungu anakuweka ili uwe msaada kwa watu kupitia nafasi fulani.

Sasa, miaka kadhaa ijayo, siyo kila mtu ataweza kupata nafasi ya kutazamwa na watu. Mungu hataruhusu hili. Kwa sababu kuna aina ya watu anawaandaa ambao watafaa katika hiyo nafasi. Unapofika wakati kama huo, siyo kila mtu atakaa, ni yule tu aliyeandaliwa.

Majira haya, ni majira ambayo Mungu anamuandaa Daudi, japokuwa Sauli yupo kwenye kiti anatawala. Mungu hatishwi na utawala wa shauri kwa sasa, kwa sababu kijana wake Daudi yupo katika pango la Adulamu, na watu mia nne, ambao na wao wana hali mbaya, lakini wanatengenezwa kwa ajili ya nafasi mbalimbali, na Daudi ni jemedari wao, ili siku akipewa nchi, basi wao washike vitengo.

Mtu wa Mungu, hii nchi inaenda kukabidhiwa kwa watu walioandaliwa tu na siyo vinginevyo. Hata kama ulikuwa umepewa maono au unabii kuwa utakuwa na nafasi katika taifa, kama usipoandaliwa, hakuna kitu utakachokuwa nacho kwenye taifa lako la Tanzania. Kwahiyo, haitoshi wewe kuwa tu na maono ambayo unaweza kuwa umeyaandika kabisa, unapaswa kuandaliwa. Daudi alipakwa mafuta ya kuwa mfalme, akiwa kijana fulani, lakini alimchukua kukaa mapangoni huko Adulamu ili aweze kuandaliwa kwa ajili ya hiyo nafasi. Haitoshi kuombewa, au kuwekewa mikono, au kupakwa mafuta na kuwekwa wakfu kwa ajili ya taifa la Tanzania. Kama haujatengenezwa, hatutapewa chochote. Rudi katika pango la Adulamu, huko utengenezwe na wengine, na uhakikishe kuwa ukipewa nafasi, ukitazamwa MUNGU WAKO ALIYEKUWEKA ANAONEKANA NA SI VINGINEVYO.

Sasa watu hawa walioandaliwa au kutengenezwa ndiyo watu watakaokuwa na kipaumbele siku chache zijazo, nazo hazitakawia. Mtu huyu ndiye atakayetazamwa na watu katika taifa lake.

Mtu huyu atatazamwa na wengi;

 

1.      Mtu aliyeamua kuacha dhambi na kuwa mtakatifu kweli kweli

Hiki ni kitu cha kwanza kabisa, kinachomjenga mtu ambaye atatazamwa na wengi katika siku chache zijazo kwenye taifa la Tanzania. Mungu ni mtakatifu na anafanya kazi katika utakatifu na anayefanya naye kazi lazima awe na tabia kama ya kwake, ambayo ni UTAKATIFU.

Kumbuka unapopewa nafasi, unapewa na Mungu, na kama unapewa na Mungu, ni Mungu anayetaka kuonekana katikati ya watu kupitia nafasi hiyo. Sasa, mtu ambaye si mtakatifu, hawezi kumfunua Mungu aliye Mtakatifu. Yaani mwizi, hawezi kumuwakilisha mtu ambaye si mwizi.

Ni jambo la kufahamu kwa upana kuwa, tunapaswa kuwa watakatifu ili kumfunua Mungu aliye mtakatifu. Na utakatifu hauigizwi, na siyo wa vipindi, na hautafutwi siku unapewa nafasi. Kama hauwezi kuwa mtakatifu leo na kuufanya utakatifu kuwa maisha yako ya kila siku, nikuhakikishie kuwa, hata kama uliombewa hautakuwa na nafasi.

Yusufu alipewa ndoto na Mungu, kuwa atakuwa mtu mkuu kati ya nduguze, lakini alilinda utakatifu wake, hakukubali kuchezea nafasi ya Mungu kwenye maisha yake. Kulinda utakatifu ni kulinda nafasi ya Mungu kwako wewe ambaye unakusudiwa kupewa nafasi fulani kwenye taifa miaka kadhaa ijayo. Potifa pamoja na cheo chake, na ushawishi wake, na kila kitu alichokuwa nacho, bado hakuweza kabisa kuzuia utakatifu wa Yusufu kubaki pale pale.

Mtu wa Mungu, kama umewahi kuwaza, au umewahi kuona maono au ndoto, au umewekewa mikono na maombi, kuwa utakuwa mtu fulani wa kutazamwa na wengi basi mojawapo ya jambo unalopaswa kuliweka kipaumbele ni UTAKATIFU. Kwako utakatifu siyo ombi, ni lazima.

 

2.     Mtu aliyejijenga kimaadili kiasi cha kuweza kusimama imara dhidi ya uharibifu wowote kwenye nafasi husika.

Mtu wa Mungu ninatamani ufahamu kuwa, kila nafasi unayoiona mtu amekalia, ina mambo yake, na kuna watu walianza vyema lakini mwisho wa siku, kwenye nafasi hizo hizo wakaharibika, ni rahisi sana kupata uharibifu kwenye nafasi.

Kama haujajijenga kimaadili mapema, ile nafasi kutokana na mambo mengi yaliyopo, na namna ambavyo itaonekana umepata mamlaka fulani, unaweza kufanya mambo ya hovyo, ambayo hata wewe mwenyewe utajiuliza siku ukitoka kwenye hiyo nafasi.

Ninaomba kukusemesha jambo moja, wale ambao unawalaumu kuwa wameharibika, na wanafanya mabaya pale kwenye kiti, ni matokeo ya kutojijenga kimaadili kwa kina kiasi cha kutoshea mambo makubwa na magumu na ya kutisha yaliyopo kwenye nafasi hiyo.

Ndugu yangu, ni bora utumie miaka hata 30 kujijenga kimaadili vya kutosha ili kuja kufanya kazi kwa miaka 3 ambayo itadumu milele kama ilivyokuwa kwa Yesu, kuliko kuwa na maadili sifuri yaliyojengwa kwa miaka mitatu, halafu ukae kwenye kiti miaka 30. Kwa sababu maadili yako, ndiyo mizizi yako.

Kama maadili yako, ndiyo mizizi yako, basi kadri ambavyo unajijenga kimaadili ndivyo ambavyo unazidi kupeleka mizizi yako chini, hivyo hata ukipewa nafasi sitakupoteza kwa sababu msingi wako una kina. Haupaswi kuwa na maadili ya nyanya, ambayo haina misingi ya kina yaani mizizi iliyoenda chini sana, kiasi kwamba, ikianza kuzaa matunda yake, lazima kuwe na mti pembeni unaoupa nguvu, nje ya hapo hamna kitu. Jifunze kuwa kama mbuyu, hata kama umebeba matunda mangapi, lakini bado uko imara.

Hatari kuu katika nafasi ambazo Mungu anawaweka watu ni kuwa, nafasi hiyo hiyo ndiyo inayoweza kukua kabisa. Inawezekana kabla hujapewa nafasi unaonekana uko salama, lakini siku ukipewa nafasi, ndiyo itajulikana umeharibika kiasi gani, na kifo chako kitakuwaje.

Ndivyo ilivyokuwa kwa Sauli, mwanzoni alionekana afaaye sana, tena akakomesha uwepo wa waganga na wachawi katika taifa, tena akaonekana kuwa anafanya sawasawa na mapenzi ya Mungu, lakini baada ya muda, kiti kikamgeuza ghafla akawa mtu wa hovyo kiasi cha kukataliwa na Mungu.

Ndugu yangu, unapaswa kujenga maadili yako. Maandiko yanasema, aliyepaa kwenda juu zaidi, ndiye aliyeshuka chini zaidi katika pande za chini za nchi. Kama kweli, ndani yako una mzigo, una moto, una kiu na shauku ya kulitumikia taifa hili katika miaka michache ijayo, basi hakikisha unajenga maadili yako sana.

Jifunze maadili ya kule unataka kwenda, na uyaishi hayo, nje ya hapo hakuna nafasi utakayokuwa nayo. Hii ni kwa sababu, watu wengi wameshapewa nafasi, lakini wakafanya mqambo ya hovyo, nje ya matarajio, sasa Mungu anatengeneza watu wake, kama uko tayari, nenda ukatengenezwe, ili miaka michache ijayo, ulifae taifa la Tanzania.

 

3.     Mtu mwenye moyo uliopondeka

Hii ni sehemu ya tatu inayomjenga mtu ambaye atatazamwa na wengi katika nafasi fulani kwenye taifa la Tanzania miaka michache ijayo. Lazima awe na moyo uliopondeka. Moyo ambao unampa Mungu nafasi ya kudhihirika na kufunua utukufu wake katika taifa la Tanzania.

Ndugu yangu, taifa la Tanzania halihitaji yeyote, limeshawahi kuwa na watu wenye mioyo yenye kiburi, ambao walifanya walichojisikia wao, ambao walijiona wao ndio miungu wa taifa hili, walifanya chochote walichofanya kwa sababu ya mamlaka yao, sasa wanatafutwa watu wenye mioyo iliyopondeka.

Mtu mwenye moyo uliopondeka, ndiye ambaye anaweza kufanya kazi na Mungu. Anaweza kumpa Mungu nafasi akafanya kazi kupitia yeye, yuko tayari kushuka na kunyenyeke mbele za Mungu, hatakuwa kama Sauli ambaye alitaka hata kumnyamazisha Samweli aliyekuwa mwakilishi wa Mungu kwake.

Mwenye moyo uliopondeka anafundishika. Ana moyo wa toba, akifanya makossa, anarudi haraka kwa Mungu, na yupo tayari kupokea maonyo na kubadilika. Ndiyo maana Mungu alimpenda Daudi. Daudi alikuwa na moyo uliopondeka, yeye hakujivunia cheo chake, yeye hakujivunia mali alizopewa na Mungu wala mamlaka yeyote, siku zote alinyenyekea kwa Mungu, na kwa watumishi wengine ambao Mungu amewaweka kwenye taifa lake.

Ukiona mtu anapita njia yake mwenyewe, hafundishiki, haonyeki, hakubali kuwa amekosea, na kukubali kubadilika. Ukijaribu kumsahihisha anakutishia kuwa yeye amepewa nafasi na Mungu, mara ameitwa, mara ana macho ya kiroho kuliko wewe, mara anajua kuliko wewe, ujue huyo mtu hata kama anaomba sana, hatatumiwa na Mungu kwa ajili ya taifa hili.

Mungu anapenda sana watu wanaoomba, na kwa kweli anawatafuta. Lakini Mungu anapendezwa zaidi na waliopondeka roho zao. Watu hawa hata kama hawana uwezo, au wanaonekana kuwa si kitu mbele za watu, Mungu atawaheshimu, atawaangalia, atavutwa kuja kwao, na kuhakikisha anakaa nao.

Mtu wa aina hii, ni vyepesi kufundishwa na Mungu, ni vyepesi kufundishwa kupitia watumishi wa Mungu, na kukubali kugeuka. Ni vyepesi kuwa tayari kufuata mapenzi ya Mungu bila kujali nani anasema nini ikiwa ni Mungu amemwambia kwa ajili ya utukufu wa Mungu.

Kama kweli unahitaji kuwa na nafasi katika hili taifa miaka michache ijayo, na unajiandaa au una ndoto ndani yako, Mungu ameweka ya kuwa mtu fulani, hakikisha unashughulikia moyo wako.

 

4.     Mtu anayejali mapenzi ya Mungu na maslahi ya wengine.

Hii nayo ni sehemu nyingine inayomjenga mtu ambaye siku moja katika siku chache zijazo, atatazamwa na wengi katika taifa hili kama jibu kwa kilio cha wengi, na kama jibu la maswali mengi ya watu maishani kwa muda mrefu.

Ndugu msomaji, Mungu anafanya kazi na watu wanaojali mapenzi yake. Mojawapo ya vitu ambavyo vilimfanya Yesu afanye kazi kubwa sana na Mungu ya ukombozi, ni kuwa alikuwa anapenda na kujali kufanya mapenzi ya Mungu. Ilifika mahali alisema chakula chake ni mapenzi ya Mungu.

Inalazimu ufike mahali ambako unayaelewa mapenzi ya Mungu, kisha yanakuwa chakula chako. Yanakuwa kipaumbele chako cha maisha kiasi kwamba hakuna kitu cha kukutoa hapo. Mtu wa Mungu, kama haujajifunza kutembea katika mapenzi ya Mungu, usitegemee kuwa chochote katika hili taifa.

Haitoshi kuwa na ndoto, ni lazima uelewe mapenzi ya Mungu katika nafasi anayokupa ili utimize hicho. Lengo la Mungu kukuweka hapo ni kutimiza kitu fulani ambacho ndiyo mapenzi yake. Kukamilisha ajenda fulani iliyopo kwenye moyo wake.

Mapenzi ya Mungu yanahusisha mambo yote ambayo Mungu mwenyewe anayataka yafanyike katika wakati fulani. Sasa ukitaka kutembea na Mungu, lazima uyajue mapenzi yake. Lazima ujue anataka nini? Kwanini anataka anachokitaka? Kwanini anataka ufanye kwa njia fulani na siyo nyingine? Mambo hayo ni machache kati ya mengi ambayo unapaswa kuyafahamu mapema sana kipindi hiki bado hujawa kwenye nafasi, siku ukisimama pale, mambo hayawi mageni kwako.

Kuna watu wanajaribu kuanza kutafuta mapenzi ya Mungu kwa sababu wamekaa kwenye nafasi fulani. Mtu wa Mungu kama siyo maisha yako kukaa kwenye mapenzi ya Mungu, itakushinda maana itakuwa mzigo mzito usiouweza. Unapaswa kuanza leo, hivi bado kabisa, ili hapo hapo, Mungu akusaidie kutembea katika mapenzi yake, katika muda huu wa sasa, ili ikuandae kuweza kutembea na mapenzi yake katika muda ule ujao.

Kuna watu wapo kwenye nafasi mbalimbali za taifa hili, na wanafanya mambo ya ajabu ajabu tu. Wanafanya hivi kwa sababu hawajui mapenzi ya Mungu kwenye nafasi alizowapa ni zipi na kwanini? Hawajui chochote, wanachojua wao ni kuja na mipango tu fulani fulani, ambayo mwisho wa siku, wanaishia kupoteza wengi. Hakikisha kuwa unajifunza kuishi na kutembea katika mapenzi ya Mungu.

Vilevile, unapaswa kujali maslahi ya wengi. Mungu hafanyi kazi na watu wabinafasi, hafanyi kazi na watu wanaojijali wao wenyewe na familia zao. Mungu anafanya kazi na watu wanaojali mambo ya wengine, watu wanaojali maisha ya wengine kuwa salama katika hali njema. Huu ndiyo moyo wa Mungu, Mungu anajali maisha ya wengine sana kiasi kwamba aliamua kumtoa mwanae wa pekee kwa ajili ya watu. Siyo jambo rahisi.

Kutokuwa mbinafsi, ni kuwa na moyo alionao Mungu juu ya watu. Ni kuwa na upendo alionao Mungu juu ya watu. Kama hauhisi anavyohisi Mungu, haufikiri anavyofikiri Mungu juu ya watu, hauwezi kufanya naye kazi hata kidogo. Amua kwa moyo wa dhati, kubadilika, usijipendeze wewe. Yatoe maisha yako yawe sadaka kwa ajili ya wengi, katika njia iliyo haki, isiyokiuka Neno la Mungu.

Ndugu msomaji, ninatumaini kuwa umejifunza mambo mengi katika somo hili. Ukiyatazama yote haya yanamhitaji Mungu. Unapaswa kukubali kusaidiwa na Mungu. Amua kumpa Mungu nafasi ya kukutengeneza. Nakushauri kurudi kwenye chumba cha matengenezo ili akusaidie uwe vile anavyohitaji uwe na aweze kufanya kazi na wewe.

Ndugu msomaji, haya ni machache kati ya mengi. Nashauri uhakikisha upate nakala yako ya kitabu kiitwacho MTU WA AINA HII NDIYE ATAKAYETAZAMWA KATIKA TANZANIA MPYA na kama unahitaji, unaweza kutuma ujumbe wako kwa njia ya email kama unavyooneshwa katika sehemu ya mawasiliano. Mungu akubariki sana, karibu tena katika wikiendi ijayo.

 

Comments